Kumsaidia Mtoto Kujifunza, Kumudu Lugha -2
Makala
yaliyopita yalipendekeza njia nne za kumsaidia mtoto mdogo kujua kuongea.
Kadhalika, tuliona hatua kuu anazopitia mtoto katika kujifunza lugha. Katika
makala haya, tunamtazama mtoto anayejua kuongea na tunaangalia mapendekezo
kadhaa ya kumsaidia kuwa mtumiaji mahiri wa lugha katika mawasiliano yake ya
kila siku.
Mazingira yahamasishe lugha
Ni
muhimu kuweka mazingira yanayompa mtoto nafasi ya kukuza uwezo wake wa lugha. Mazingira
hayo ni pamoja na kumruhusu kucheza na wenzake kwa muda maalum. Kucheza ni fursa
nzuri ya mtoto kuwasiliana na wengine kuhusu kanuni za michezo husika, kujadiliana
pale wanapohitalifiana na kadhalika, na hivyo kukuza uwezo wake wa kujieleza.
Vile
vile, kadri hali inavyoruhusu, ni vizuri kumtafutia mtoto CD za katuni (mfano
Ubongo Kids), nyimbo na mafundisho mengine na ikibidi kumruhusu mtoto kutazama
vipindi vya televisheni vyenye maudhui yanayoweza kumpanua uelewa wake. Vyote
hivi, mbali ya kupanua uelewa wa mambo ya kawaida, humsaidia kukuza msamiati
wake na hata kujifunza mambo mengi asiyoyasikia katika mazungumzo na watu
wengine nyumbani.
Anapoanza
kujifunza kusoma, vitabu vyenye picha zinazomvutia kujifunza zaidi vina nafasi
kubwa ya kumsaidia kuelewa mambo mbalimbali yanayoendana na umri wake. Hivyo, ni
vyema kuhakikisha mazingira ya nyumbani yanampa nafasi mtoto kujifunza lugha.
Ongea nae
Mazungumzo
ya kirafiki na mtoto pia yanamhamasisha kujifunza matumizi sahihi ya lugha. Kuongea
naye, kunampa nafasi ya kuiga na kujifunza maneno ya kiutu uzima. Maneno haya
yanamwongezea mtoto msamiati mpya wenye kubeba mawazo mapana zaidi ambayo kwa
hali ya kawaida pengine asingeisikia kwa watoto wa umri wake.
Unapoongea
nae, hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha lugha inakuwa rahisi, wazi na ya moja
kwa moja. Lugha ngumu isiyoeleweka kirahisi haimsaidii kujifunza.
Mawasiliano ya karibu kama haya yanasaidia watoto kujifunza lugha kwa urahisi. Picha: Mitandao |
Mwulize maswali yanayofikirisha
Maswali
yanayohitaji kufiria kwa kina yanamsaidia kukuza uwezo wake wa lugha. Badala ya
kumwuliza maswali yanayohitaji majibu ya ndio na hapana, au yale yenye majibu
mafupi, mwuulize maswali yanaitaji maelezo marefu kidogo. Kwa mfano, maswali
kama ‘kwa nini unafikiri hivyo?’ yanamfanya afikirie zaidi kile ambacho
angeweza kukijibu kirahisi kwa jibu la ndio au hapana.
Kadhalika,
maswali yenye kumwuuliza njia aliyoitumia kufanya mambo fulani, maswali
yanayomfanya afikirie zaidi ya alichokifanya yanamsaidia kujifunza kutumia
maneno anayoyafahamu tayari katika kujieleza vizuri zaidi.
Mpe nafasi ya kukusimulia
Vile
vile, kumpa nafasi ya kukusimulia mambo anayokutana nayo kunamsaidia kujenga
uwezo wake wa kujieleza. Imethibitika kwamba watoto wanaopata fursa ya
kusimuliza mambo yao kwa wengine, wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuijua
lugha zaidi ya wale wasiopata fursa hiyo. Mtoto anapolazimika kueleza mambo
yake kwa maneno yake, hujifunza kuelewa namna ya kuelezea hisia zake kwa kutumia
maneno sahihi na kwa wakati sahihi.
Kwa
mfano; unaweza kumwomba kusimulia anayoyaona kwenye televisheni, michezo
aliyocheza mchana, mambo mazuri aliyojifunza shuleni/kanisani/madrasat, nani
alimfanya afurahie siku yake na mambo kama hayo. Kusimulia mambo haya hukuza
uwezo wake wa kuelezea mambo.
Kwa
ujumla, ukaribu wa mzazi na mtoto ndio msingi mkuu wa mtoto kumudu lugha. Kadri
unavyokuwa nae karibu, ndivyo anavyopata usaidizi wa kukuza uwezo wake wa
kujieleza na kuwa mtumiaji mahiri wa lugha.
Fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamis kwa makala kama hizi. Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz
Maoni
Chapisha Maoni