Kwa Nini Tunapenda Kusikia Habari Mbaya?

Umewahi kujiuliza kwa nini habari tunazofuatilia kwenye vyombo vya habari mara nyingi ni matukio mabaya? Kwamba ili iwe habari yenye kuvutia watu wengi mara nyingi hulazimu iwe habari ya jambo lisilotarajiwa. Kwa mfano, habari za mbunge kulala wakati kikao cha bunge kikiendelea inaweza kuwa na mvuto kuliko habari ya namna mbunge huyo huyo alivyotekeleza wajibu wake kabla ya ‘kupitiwa na usingizi.’


Kadhalika, matukio yasiyofurahisha huwa yana nguvu kubwa ya kufunika mazuri mengi tuliyowahi kukutana nayo. Ni rahisi, kwa mfano, unaporudi nyumbani ukajikuta ukielezea tukio moja baya ulilokutana nalo kazini kuliko mambo mazuri uliyokutana nayo siku hiyo. Tukio la mfanyakazi mmoja kukukosea, linakaa kichwani zaidi kuliko mazuri mengine yote uliyokutana nayo.

Si hivyo tu. Hata tunaposikia mambo ya wengine, tunavutwa kusikia habari hasi (mbaya) kuliko habari zao njema. Ukisikia mtu fulani amefanya kosa fulani, ni rahisi kuvutiwa kujua kulikoni, kuliko pale unaposikia mtu huyo huyo amefanya vizuri. Huu ni ukweli usiopendeza wa maisha yetu ya kila siku. Kwa nini inakuwa kama vile fahamu zetu zinatafuta kujua mabaya kuliko mazuri?

Hofu ya Yasiyotarajiwa

Hofu ndiyo sababu kubwa inayotufanya tuvutwe na mabaya yasiyotarajiwa. Linapotokea tetemeko la ardhi, kwa mfano, ni rahisi tukio hilo baya kufuatiliwa kwa karibu na watu kwa sababu si tukio lililotarajiwa na kwa kweli linatishia uhai wetu. Kwa kawaida, mambo yanayotishia uhai wa mwanadamu ni yale hasi na ndiyo hayo tunayoyafuatilia kwa karibu ili tuweze kujihami na madhara yanayoweza kutupata siku zijazo. Tunafuatilia mambo mabaya kujilinda na uwezekano wa madhara.



Vilevile, hofu ya kushindwa kufikia malengo yetu hutufanya tuguswe na matukio machache tusiyoyatarajia pengine kuliko mafanikio mengi tuliyonayo. Kukemewa na bosi, kwa mfano, hujenga hofu ya kupoteza hadhi yako, jambo ambalo, katika hali ya kawaida, usingependa litokee. Ili kufanikiwa kazini, unaamini unahitaji hadhi fulani.

Huzuni kwa kiasi kikubwa huchangiwa na mazoea yetu ya kutarajia mabaya PICHA: blackprssusa.com 

Shauri ya hofu hiyo ya kupoteza hadhi waweza kujikuta ukichukulia kwa umaanani karipio hilo kuliko hata pale unaposifiwa na kila mtu ofisini kwako.  Katika mazingira hayo, hofu ya kupoteza ulichonacho inakufanya upuuze sifa nyingi ulizonazo kwa sababu tu umechukulia kwa uzito yale unayohisi yanahatarisha kupoteza heshima/hadhi yako.

Kadhalika, wakati mwingine tunapenda habari mbaya za wengine kwa sababu ya kushindana sisi kwa sisi. Kwa kawaida unaposhindana unatamani wale unaoshindana nao washindwe. Kwa hiyo tunapokuwa watu wa mashindano ni rahisi kujawa hofu ya kushindwa pale tunaposikia mazuri yao na hivyo tunavutwa zaidi na habari zao hasi kuliko yale mazuri wanayoyafanya. Mabaya yao yanatufanya tuwaone kama watu wanaoelekea kushindwa.


Athari za Kutarajia Mabaya

Mwanadamu anahitaji kiwango fulani cha hofu ili aendelee kujibidiisha kufikia malengo yake. Pasipo hofu, huenda tusiweze kuwa na nguvu ya kuwa waangalifu katika mambo yetu. Mwanafunzi, kwa mfano, anahitaji kuwa na kiwango fulani cha hofu ya kuanguka katika mtihani ili aweze kusoma kwa bidii. Bila hofu atajiamini kupindukia na hatasoma. Matokeo yake yanaweza kuwa mabaya.


Kijana anayetaka kuanzisha familia anahitaji kiwango fulani cha hofu ili awe mwangalifu katika maamuzi yake. Mfanyakazi naye, hali kadhalika, anahitaji hofu ya kufutwa kazi ili afanye kazi kwa bidii na kujituma. Maana yake ni kwamba kwa namna fulani tunahitaji hofu kama motisha ya maisha. Na kama tunahitaji hofu, kwa namna fulani ni muhimu kutarajia mabaya ili kuchukua hatua stahiki kabla mabaya hayo hayajajitokeza. 

Hata hivyo, hofu inapozidi kiwango, ni hatari. Hutufanya tukose nishati ya kujiamini. Ndio kusema, hofu inayotusababisha tufuatilie sana mambo hasi yaweza kuwa sumu katika fikra zetu na yaweza kuwa nishati ya kuturudisha kwa mwendo wa kinyume nyume. 

Ni kweli kufuatilia sana mambo mabaya yaweza kuonekana kuwa jambo la kawaida. Kama tulivyoona, mara nyingi ndivyo ilivyo. Akili zetu zina kawaida ya kupekua mambo mabaya. Tunayatafuta. 

Pamoja na hayo, upo ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa hisia zetu hutokana na kile tulichokiingiza katika fahamu zetu. Kwa hivyo, mazoea ya kujaza akili zetu taarifa mbaya muda wote hujenga matarajio mabaya yanayoondoa utulivu wa moyo.  Huwezi kuwa na nafsi iliyotulia kwa kutarajia mabaya.

Wakati mwingine tunaweza kujikuta tukikosa amani na furaha katika maisha na tunashindwa kujua kwa nini inakuwa hivyo. Kumbe hofu ambayo wakati mwingine haina msingi wowote huwa tunaijenga sisi wenyewe. Tunajikuta tukikosa amani, tunajawa hasira, tunakata tamaa, tunatarajia mabaya yasiyokuwepo na matokeo yake tunakuwa na msongo wa mawazo usio na sababu. Chanzo cha haya yote ni mazoea ya kufuatilia mabaya yanayotokea.

Tunaweza Kubadili Mazoea Haya

Ingawa ni kweli fahamu zetu zinatuelekeza kutarajia mabaya na wakati mwingine kuyatafuta, tunaweza kabisa kubadili mazoea. Tunaweza kufanya jitihada kujenga upya fikra zetu. Tunaweza kulazimisha fahamu zetu kufikiri mambo chanya hata kama mambo hayo hayatarajiwi.

Kwa mfano, badala ya kutarajia kwamba utaharibu kazi, kwa nini usitarajie utafanya vizuri? Kwa nini iwe rahisi kufikiria kuharibu kazi na kujiongezea hofu inayoweza kuathiri utendaji wako badala ya kufikiria unavyoweza kufanya vizuri?

Kwa nini, kwa mfano, unapotafakari siku yako ilivyokwenda usiilazimishe akili yako kufikiria mazuri uliyokutana nayo siku hiyo hali inayoweza kukuongezea ujasiri na kujiamini badala ya kutafakari mabaya machache yaliyojitokeza?

Tunaweza kabisa kujenga utamaduni mpya mgumu wa kutafuta mambo chanya katika mazingira yetu yanayotuongezea ujasiri wetu badala ya yale hasi yanayotujengea hofu isiyo na sababu. Tunaweza, na kwa kweli, ni muhimu kuyapa nafasi mambo chanya katika fikra zetu ikiwa kweli tutajitambua. 



Soma gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa mada kama hizi kwenye safu ya Saikolojia.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?