Kujenga Uwezo wa Kufanya Maamuzi kwa Mtoto
Unajisikiaje
mzazi unapogundua mtoto ameanza kujifunza tabia zisizofaa? Inaumiza, kwa mfano,
kuona mtoto anaanza kujifunza wizi, kudanganya na hata kutokuwa na uwezo wa
kujisimamia mwenyewe bila uangalizi wa karibu.
Tafiti
za malezi zinaonesha kuwa, kwa kiasi fulani, tabia hizi huchangiwa na kutokumpa
mtoto nafasi ya kufanya maamuzi yanayohusu mambo yake mapema. Labda unaweza kujiuliza
mtoto anaweza kufanya maamuzi gani katika umri ambao hata uwezo wake wa
kufikiri bado ni mdogo?
Maamuzi ni kuchagua
Kufanya
maamuzi ni kumpa uwezo wa kuchagua mambo rahisi kabisa bila kumfanya alazimike
kufuata matarajio ya wengine ambayo pengine hayaendani na matarajio yake. Kwa
mfano, kumpa mtoto nafasi ya kuchagua kifaa kipi angependa kukitumia kuchezea
ni kumwezesha kufanya maamuzi yanayolingana na uwezo wake.
Maamuzi hujenga kujiamini
Kumfundisha
mtoto kufanya maamuzi yake humjengea uwezo wa kujiamini kungali mapema.
Kujiamini kumethibitika kumsaidia mtoto kuwa na subira hata atakapokuwa mtu
mzima. Kwa hakika, mambo mengi
tunayoyafanya kama watu wazima yanategemea kwa kiasi kikubwa sana uwezo wetu wa
kuwa na subira.
Bila subira, kwa mfano, hatuwezi kudhibiti hasira, hatuwezi
kuheshimu makubaliano na hata kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha. Kimsingi,
subira ina nafasi kuwa katika maisha yetu na kwa kweli inatokana na uwezo wetu
wa kufanya maamuzi.
Utafiti wa ‘Marshmallow’
Mwanasaikolojia
Walter Mischel aliwahi kufanya utafiti kupima nguvu ya maamuzi ya subira kwa
watoto wa miaka minne. Mischel aliwapa watoto vitu vitamu viitwavyo marshmallow
–mfano wa pipi kwa mazingira yetu –ili kuona kama watoto wangeweza kufanya
maamuzi ya kujinyima kile wakipendacho kwa hiari yao. Watoto waliambiwa wangeweza
kula pipi hizo kama wangetaka lakini kama wangesubiri mpaka atakaporudi wangepata
‘pipi’ zaidi kama takrima ya kujinyima.
Matokeo
yalionesha watoto wachache waliweza kujizuia. Wengi walikula ‘pipi’ bila
kungoja. Mischel aliwafuatilia watoto hao kwa miaka mingi baadae na kugundua wale
waliongoja walikuwa na mafanikio makubwa shuleni na hata katika maisha.
Wenzao
walioshindwa kufanya maamuzi ya kungoja hawakuwa na mafanikio na wengi
waliishia kuwa na tabia zisizofaa kama wizi, matumizi ya dawa za kulevya na
walipata matatizo katika mahusiano ya kimapenzi na kadhalika. Tafsiri rahisi ni
kwamba kujengwa kimaamuzi mapema na kuwa na subira kunahusiana kwa karibu na
mafanikio ya mtu.
Tunachoweza kufanya
Tunashauriwa
kuwasaidia watoto kushiriki katika maamuzi madogo yanayolingana na umri wao
tangu wakiwa wadogo. Kwa mfano, tunaweza kuwaruhusu watoto kuchagua nguo wanazopenda
kuvaa, kuwashirikisha kupanga ratiba za michezo yao ili kuwafanya waweze kujiona
kama watu wanaoweza kufanya maamuzi ya kujisimamia tangu mapema.
Kadhalika,
tunaweza kuheshimu hisia za watoto wetu tangu wakiwa wadogo ili kuwajengea
imani na uwezo walionao. Kwa mfano, wanaporipoti hisia za maumivu
tusiwalazimishe kuamini vinginevyo kwa lengo la kuwafanya watulie. Kuwajengea
uwezo wa kukubali hisia hasi walizonazo ni njia muafaka zaidi ya kuwasadia
kukabiliana nazo na hukuza uwezo wao wa kuamua mambo yanayowahusu tangu wakiwa
wadogo.
Kwa
hakika, upo umuhimu mkubwa wa kuwasaidia watoto kufanya maamuzi yao kulingana
na umri wao. Maisha yao ya utu uzima yatategemea sana namna wanavyofanya
maamuzi. Tunao wajibu wa kuwakuza kimaamuzi tangu wanapokuwa wadogo.
Unafahamu
njia nyingine za kuwasaidia kukuza uwezo huu?
Niandikie: bwaya@mwecau.ac.tz, 0754 870 815
Maoni
Chapisha Maoni