Tunavyoweza Kuacha Tabia ya Kuhukumu Wengine
Majuzi nikiwa kwenye mgahawa
mmoja mjini, waliingia watu wawili wanaume waliokuwa wamevalia mavazi
yanayoashiria imani yao ya kidini. Wote wawili walipamba vichwa vyao kwa
vilemba nadhifu, mmoja wao akibeba mfuko mdogo mweusi. Nyuso zao, kwa hakika
zilipambwa na tabasamu pana la kirafiki lililofanya ndevu zao ndefu ziwe na
mwonekano wa kupendeza. Miguu yao ilivaa viatu vya wazi na juu yake
zilining’inia suruali fupi mithili ya kaptula ndefu zilizojitokeza ndani ya
kanzu fupi nadhifu.
Walipokuwa wakijongea
kukaa kwenye meza mojawapo, kila mmoja aligeuka kuwatazama kwa wasiwasi. Mkahawa
ulijawa hali ya tahayaruki fulani isiyotarajiwa. Macho yote yaliwaelekea vijana
wale wawili. Ndani ya muda mfupi, wageni wasio wa-Tanzania, ambao ndio
waliokuwa wengi kwenye mgahawa huo, walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine.
Ingawa nilikuwa mmoja wapo wa waliobaki, nami kama wengine nilikuwa na wasiwasi
ya nini hasa kingeweza kutokea.
Tunahukumu kwa haraka
Wasiwasi wa sote
tuliokuwa kwenye mgawaha ule ulinifanya nijiulize masuala mengi. Kwamba pamoja
na kwamba hatukuwajua hata kidogo watu wale wawili, akili zetu zilituaminisha
kuwa tunawajua vilivyo. Kila aliyeondoka kwa wasiwasi, huenda aliwahusisha watu
wale na taswira fulani aliyokuwa nayo kabla ya kuwaona. Kwamba huenda watu wale
walishabihiana na watu waliowahi kuhusishwa na matukio fulani yasiyo ya
kawaida.
Hivi ndivyo
tunavyofanya katika maisha yetu ya kila siku. Kila tunayekutana naye tunamweka
katika kundi fulani tulilonalo tayari kichwani. Tunapokutana na mtu kutoka mkoa
wa Mara, kwa mfano, tunamlinganisha na watu wa Mara tuliowahi kukutana nao
kabla. Tunatumia kundi tunalolifahamu kumwelewa mtu huyo ambaye ndiye kwanza
kumekutana naye.
Akili zetu zinaona chochote
Ukitazama picha hii
hapa chini, unaweza kuona sura mbili. Waweza kumwona ajuza wa umri mkubwa
aliyejifunika na blanketi zito shingoni na kuzizungushia ushungi kichwani.
Lakini pia waweza kumwona binti mdogo akiangalia upande akiwa kajizungushia ushungi
upande mmoja wa kichwa. Unachokiona kwenye picha hii kinategemea ama matarajio
yako au vile akili yako inavyotafsiri kila kilichochorwa kwenye mchoro huu.
Unamwona bibi au binti? Picha: huria mtandaoni |
Kwa mfano, pua ya ajuza
yaweza kuwa mwonekano wa upande wa uso wa msichana anayetazama upande wa pili.
Jicho la ajuza laweza kuwa sikio binti. Mdomo na kidevu cha ajuza vyaweza kuwa
shingo ya msichana wakati mdomo wa ajuza ni mkufu wa binti. Hiyo ni mifano
namna akili zetu zinavyoweza kuchakata taarifa ili kupata taswira inayoeleweka.
Katika kujaribu kuelewa
kile tunachokitazama, mara nyingi akili zetu hazipendi kujitesa. Akili zetu
hazitaki kujichosha kufanya kazi ya kufahamu kitu kimoja moja kwa kukichambua chenyewe
bila kukihusisha na ama tunavyojijua tayari ama mazingira yake. Ni kama vile akili
hutafuta njia rahisi ya kupunguza kazi ya kuwaelewa wale wanaotuzunguka.
Tunajikuta tunachanganyikiwa
Matokeo ya hulka hii ya
kujaribu kuelewa kile tusichokifahamu wakati mwingine ni kutokuelewa kile
tunachotaka kukifahamu. Kwa mfano, watu wale wawili walioingia kwenye mkahawa
ule wanaweza kuwa watu wema, wacha Mungu, waliofika pale kufanya kikao cha
kujadili mambo yao mema. Tuliokuwepo pale, tulitumia taswira tulizo nazo
vichwani mwetu kuwaelewa. Ndio sababu wengine wetu waliondoka.
Katika maisha ya
kawaida, kutumia uzoefu tulionao katika kuwaelewa watu na matukio tunayokutana
nayo, hutufanya tuwe watu wa kuhukumu. Tunaamini, kwa mfano, watu wa makabila
fulani, dini fulani, taifa fulani, kuwa wanayo tabia inayofanana. Matokeo yake
ni kwamba tunawaonea watu wengi kwa kuwaweka katika mafungu ambayo wakati
mwingine hayawastahili. Kwa mazoea haya, tumewahukumu wengi isivyostahili na
wakati mwingine hata wanapofanya kinyume kabisa na matarajio yetu, bado
tunashikilia sifa tuliyowapachika kabla hatujafahamu.
Tunaweza kubadilika
Tubadili fikra zetu kwa
kuachana na mazoea ya kufikia mahitimisho haraka bila kuwa na taarifa za
kutosha. Ni makosa, kwa mfano, kulielewa jambo kwa sababu tu tunaamini tumewahi
kukutana nalo siku za nyuma. Tunahitaji kuyaona mambo katika upekee wake.
Kila mtu katika kabila,
dini na hata familia anaweza kuwa na tabia zozote zisizo na uhusiano wowote na
watu wengine wa kundi tulilomweka. Ubaya wa mtu leo, waweza kufuatwa na uzuri
wake kesho. Uzuri wa leo, waweza kufuatwa na ubaya wa kesho. Tusihukumu mapema.
Mwandishi ni Mhadhiri wa
Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa bwaya@mwecau.ac.tz na 0754 870 815
Mwanafunzi wa wanafunzi wako, nakushukuru kwa kipande hiki elimishi.
JibuFutaNi kweli, mara nyingi tumekuwa wepesi kutoa hukumu kwa mambo tusioyajua kwa undani wake. Tumeshindwa kutoa faida ya mashaka kwa tusiowajua/tusioyajua matokeo yake tunapopata fursa ya kufahamu ukweli (baada ya hukumu) tunajikuta katika maisha ya kukuta.
Ingawa katika mazingira hatarishi ni vema kuchukua tahadhari kwa kuhukumu hivyo ili mradi hukumu yako haina madhara kwa mhukumiwa. Falsafa ya askari ni kuwa tuhumu kila mmoja na usiamini hata mmoja (suspect everyone, trust no one), kwa kiasi fulani naweza kukubaliana na falsafa hii hasa katika mazingira hatarishi - mazingira ambayo usipochukua tahadhari kwa kuhukumu hivyo madhara yake ni makubwa kuliko madhara yatokanayo na hukumu yako.
Aidha, wakati flani mkuu wangu wa kazi aliniambia. Unaposhughulikia masuala ya fedha ni bora kuwa na falsafa ya kuwa kila mmoja katika kampuni/shirika ni "mwizi" na kwamba wakati wowote mtu anapoleta madai yake mezani unapaswa kuangalia madai yale kwa jicho la shauku ya kumkamata mwizi - kuwa yeyote anaweza kuwa mwizi (everyone is potentially a thief).
Sasa nikiangalia falsafa hizo mbili, nashawishika kuamini kuwa sio mara zote hukumu zetu huwa ni mbaya bali hutumika kama kinga (defence mechanism) na kama hukumu hiyo haina madhara kwa mhukumiwa ukilinganisha na madhara yanayoweza kujitokeza kwa kutojali viashiria vilivyoonekana, basi ni bora kuweka hukumu na kuchukua hadhari kuliko kuiishi hatari kwa hofu ya kutoa hukumu.
Mpaka wakati mwingine.
Maranya O'Mayengo
Ubarikiwe....tuna kasumba ya kuwaweka watu katika mkundi ambayo tayali tunaya kichwani...kuna wakati pia makundi yetu yana toa majibu sahihi ama tofaut lakini tunakataa kukubali ukweli..nini tufanye kupokea mabadiliko tunapoona utofaut na matarajio yetu???
JibuFuta