Je, ni kweli lugha huathiri namna tunavyofikiri?

MJADALA wa nafasi ya lugha katika namna tunavyofikiri na kuyaelewa mazingira yetu una historia ndefu. Kwa ujumla kumekuwepo na pande mbili kuu. Upande wa kwanza unashikilia kuwa lugha, ama mawasiliano ayafanyayo mtu na wengine, iwe kwa maneno, ishara, alama au vitendo haina uhusiano wowote na namna mtu anavyofikiri. Ushahidi wa madai haya ni namna watoto wadogo wanavyoweza kufikiri uzuri bila hata kujua lugha. Na ni kweli pia kwamba kwa mtoto fikra au uelewa hutangulia uwezo wa lugha. Kwamba hawezi kusema wala kuonyesha kusikia kinachosemwa, hiyo haimaanishi kuwa mtoto hafikiri. Na ndio maana wakati anajifunza lugha, mtoto huweza kutumia neno moja kumaanisha mambo mengi. Anaelewa kuliko anavyotumia lugha.

Vile vile, inasemekana, watu wenye ulemavu wa kutumia maneno kuwasiliana na wenzao, bubu kama tunavyowaita, wana uwezo mzuri wa kufikiri kama watu wengine. Kwamba watu hawa hawana tatizo la kuyatambua na kuyaelewa mazingira yao kwa ufanisi ule ule tunaouona kwa watu wasio na ulemavu huo, maana yake ni kwamba fikra, mawazo na chochote kinachoendelea akilini, hakina uhusiano wowote na lugha.

Na isitoshe, huko kichwani hakuna lugha. Mule kuna mfumo usiotegemea lugha katika kuwakilisha (represent) kinachoonekana katika mazingira. Hata ukielewa lugha saba, kichwani haziingii kama lugha husika, bali mfumo fulani unaojitegemea na kufanya kazi bila kujali kilichoingia kimeingizwa kwa kutumia lugha gani.

Wapinzani wa mtazamo huu wanadai bila lugha hakuna fikra. Fikra ndio lugha yenyewe kwa sababu lugha ni zana (tool) ya kukusaidia kuuelewa ulimwengu. Kwamba haiwezekani mtoto kujua kitu bila kukihusianisha na lugha ambayo  si lazima iwe kwenye maneno. Tangu awali kabisa, akili zetu hufanya kazi ya kujenga picha ya tunavyoviona na kuvihusianisha na lugha hivyo haiwezekani kuyaelewa mazingira yetu pasipo lugha katika upana wake.

Mfano, inasemwa, kukua kwa uelewa kunakotokana na kukua kwa ubongo, hakuwezekani pasipo lugha. Mtoto anayekosa uwezo wa kutumia lugha, anakuwa na wakati mgumu kuielewa dunia yake na hivyo uelewa wake huathirika. Kwa maana nyingine, ili fikra zikue, lugha inahitajika katika kukusanya yanayoingizwa akili na kuyapangilia katika utaratibu mzuri ili kurahisisha kumbukumbu baadae. Bila lugha, ni sawa na kuwa na maktaba yenye vitabu maelfu visivyopangiliwa kwa utaratibu unaoeleweka, na unaoweza kurahisisha upatikanaji wake pindi vinapohitajika. Lugha, kwa maana hii husaidia zoezi la kupangilia yanayoingia kichwani kupitia milango mikuu ya fahamu, na kuyaweka katika utaratibu unaotuwezesha  kupata uhusiano kati yake na hivyo kutengeneza dhana zinazotumika katika kufikiri.

Unasemaje ndugu msomaji. Una msimamo gani kuhusu pande hizi mbili?  Kwa nini? Wakati ukiendelea kutafakari hayo, nikupe mfano mwingine wa mtazamo.

Lera Boroditsky anaendelea kufanya tafiti kujaribu kuona namna lugha zinavyoathiri au kubadili jinsi tunavyofikiri. Unaweza kusoma muhtasari wa anachokifanya hapa. Kwa mujibu wa Boroditsky, watu wanaozungumza lugha tofauti, wanafikiri kwa namna tofauti. Kwa mfano, watu wa jamii ya Aboriginal, Australia, wanaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kutumia dira katika kufikiri kwao, shauri ya lugha yao. Hawa jamaa tunaambiwa, lugha yao inawadai kujua uelekeo ili kueleza karibu kila kitu. Mathalani, ili kumwelekeza mtu mahali kilipo kitabu, kwa lugha nyingi maelekezo yangekuwa, "angalia kabatini kulia (au juu ya) faili". Ni tofauti kwa Aboriginal. Kwao maelekezo yangekuwa, "kitabu kiko kusini mashariki mwa faili, kaskazini magharibi kidogo mwa ilipo rasimu ya katiba."

Watoto wa Aboriginal wanafikiri tofauti na wewe? Picha na gva.be
Boroditsky anatuambia kwamba dira na welekeo ni hitaji la msingi la lugha hiyo, hali inayoathiri kabisa namna ya kufiri kwa wazungumzaji wa lugha hiyo. Matokeo yake, watu hawa, huwa makini sana na dira na uelekeo kokote wanakokua. Akili zao zinatumia sana dira katika kuelewa, kupangilia na kukumbuka dhana.

Australia ni mbali. Singida, kwa Wanyaturu hali si tofauti sana. Mnyaturu yuko makini sana na dira. Kokote anakokua ni lazima aelewe mashariki ni wapi, kama ilivyo kaskazini na kadhalika. Sababu ni kwamba, maelekezo mengi yanafanyika kwa kutumia dira na uelekeo. Badala ya kusema, 'Mto uko kulia mwa barabara', Mnyaturu anakwambia, "Mpemwei", yaani magharibi kidogo. Kwa hiyo Mnyaturu, sawa na wenyeji Aboriginal, wanafikiri kwa kutumia dira zaidi. Athari ya lugha.

Mfano mwingine anaoutoa Boroditsky ni jinsi lugha inavyoathiri sana kumbukumbu. Anasema, mzungumzaji wa Kiingereza anatakiwa kujua mtendaji kwa kila sentensi. Mfano, 'Masanja amevunja kikombe'. Lugha inadai kumkumbuka mtendaji wa kitendo husika. Wakati kwenye lugha nyingine, kama Kihispania na Kijapan, mzungumzaji halazimiki kujua aliyefanya kitendo, na hivyo sentensi inaweza kuwa sawa na 'Kikombe kimejivunja,' kwamba si rahisi kumkumbuka mtendaji. Kwa maana nyingine, mzungumzaji wa Kijapani na Kihispania hakumbuki sana waliotenda kuliko mzungumzaji wa Kiingereza. Athari ya lugha.

Alexander Guiora sawa na Boroditsky anasema lugha kama Kiebrania zinasisitiza zaidi kujua jinsia ya watu. Na wakati mwingine hata vitu vinapachikwa jinsia. Kwa hiyo, mzungumzaji wa Kiebrania anajikuta akilazimika kuanza kujua jinsia mapema zaidi ya wazungumzaji wengine.

Je, lugha inaweza kuwa inaathiri namna tunavyofikiri kama tulivyoona? Je, lugha ndiyo inayoathiri kufikiri kwetu au kufikiri ndiko kunakoathiri lugha? Je, ukijifunza lugha ya pili zaidi ya ile ya mama, unaanza kufikiri tofauti?

Uzuri watu kama Profesa Boroditsky wako kwenye mtandao wa Twitter. Mfuatilie hapa.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini