Ni kweli Israel haikosei kwa Mkristo kama ilivyo Hamas kwa Mwislam?

JUZI nikiwa katika pita pita zangu katika mitaa ya mjini, nimebahatika kukutana na bango kubwa sana barabarani. Bango lenyewe lilikuwa na ujumbe wa kuhamasisha maandamano ya siku ya Quds kupinga 'Masaibu ya Wapalestina' yatakayofanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 25 Julai, 2014. Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa umma, maandamano hayo yataanza saa 3 asubuhi, kuanzia kituo cha Boma, Barabara ya Kawawa, jijini Dar es Salaam. Bango hilo lina picha ya msikiti.

Tutakumbuka kwamba Israel imekuwa ikiwashambulia vikali Wapalestina kwa siku za hivi karibuni, hali ambayo kwa kweli inasikitisha. Mamia ya Wapalestina wamepoteza maisha yao wakiwemo watoto. Ni hali ambayo inatia simanzi. Maandamano kadhaa tayari yameshafanyika kuishutumu Israel kwa mashambulio hayo. Israel kwa upande wao, wanadai wanachokifanya ni kulipiza kisasi kwa uchokozi wa Hamas. Siandiki kutafuta kujua nani anafanya vizuri na yupi anakosea katika mgogoro huo wa enzi na enzi. Hayo si ya leo.

Bango lililoko maeneo ya Mikocheni, Picha: Jielewe
Ukifuatilia mwitikio wa dunia kwa hali hiyo inayoendelea mashariki ya kati utaona kuwa, wapo wanaochukulia kirahisi sana yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza. Ni kama hakuna linalotokea. Ukiwaauliza kwa nini hawaguswi na hali hiyo, wanakwambia, 'Israel wamechokozwa, wanajibu mapigo.' Ni kama wanaiunga mkono Israel kwa yale inayoyafanya. Wanasema, lolote linalofanywa na Israel lina mkono wa Mungu. Haturuhusiwi kuhoji. Wanaenda mbali kwa kusema, ukijaribu kuilaani Israel, unajitafutia matatizo yasiyo ya lazima. Mambo ya Israel waachiwe wao, ndio wanaoyajua vizuri. Hawaguswi na  na 'Masaibu ya Wapalestina'. Lakini ndio wa kwanza kulaani wakisikia Al Shabaab wanaua raia wasio na hatia Mombasa. Ndio wa kwanza kukilaani kikundi cha Boko Haram kinapotekeleza vitendo vibaya vya kikatili nchini Naijeria. Kwao, ni vigumu kuvitenganisha vitendo hivyo vya kigaidi na Uislam. Hakuna mjadala.

Upande mwingine, wapo wanaonesha kuguswa vikali na yanayoendelea Mashariki ya kati hivi sasa. Tunajua wapo wengi, wenye dini na wasio na dini. Lakini ni wazi kuwa Waislam ndio wanaowajibika vilivyo kuhakikisha 'udhalimu wa Israel' unalaaniwa kwa uzito wake. Ndio hawa ambao sehemu kubwa wameandaa maandamano niliyoyataja awali hapa nchini. Wanalichukulia kwa uzito wa kutosha suala hili. Hata ukifuatilia wachambuzi wengi wa siasa za mashariki ya kati, utagundua kuwa dini inaweza kukufanya ubashiri mwelekeo wa maoni ya anayechambua. Biases.

Lakini hawa hawa, wanaolaani 'udhalimu' unaofanywa na Israel kwa Wapalestina, huwezi kuwasikia wakilaani kwa dhati kabisa matendo ya hovyo yanayofanywa na Magaidi wa Al Shabaab, Boko Haram na Al Queda. Na wakilaani, hawaandamani kama wanavyofanya inapotokea ukanda wa Gaza ukiathirika. Na wakilaani, zinafanyika juhudi za kutenganisha 'Uslam' unaotumiwa na magaidi na Uislam halisi. Wakati huu, wenzao waliokuwa wazito kulaani yanayofanywa na Israel, ndio wanakuwa mstari wa mbele 'kuwaanganisha' Waislamu wote na vitendo vya kigaidi. Sijui kama nimejieleza ipasavyo.

Sasa swali, kwa nini hali huwa hivi? 

Kisaikolojia, kinachofanyika hapo si kitu cha ajabu hata kidogo. Ni juhudi za binadamu kujiridhisha kwamba imani yake, dini yake, ndiyo sahihi wakati huo huo imani ya mwingine, dini ya mwingine haiwezi kuwa sahihi kama ilivyo yake. Nitaeleza.

Kama binadamu, tunalo hitaji kubwa la kujitambulisha na makundi yetu. The need to belong. Katika vikundi vingi tunavyoweza kujitambulisha navyo, dini ni moja wapo. Dini ni namna rahisi ya kukutana na hitaji letu la kujitambulisha. Dini ni gundi inayotugandamiza pamoja kirahisi.

Na kwa sababu tunapenda kuwa sehemu ya utambulisho fulani, ili kujitambulisha na kundi fulani, hubidi kwanza tujipambanue kwa kuwatenga watu wa nje ya kundi, outgroup, na kujifungamanisha na watu wa kundi letu, ingroup. Kigezo hapo, kwa mfano, huwa dini. Tunafungamana na wale wanaoamini kama sisi, na kutengana na wale wasioamini kama sisi.

Ili kupata furaha ya moyo, tunalazimika kuamini kuwa kundi letu lina wema ambao haupatikani kwenye makundi mengine. Hatuishii hapo. Tunaamini kwamba watu wa kundi letu ni wema, na bora kuliko watu wa makundi mengine. Na inapotokea hali inayokinzana na imani hiyo, kwa mfano mmoja wa watu wa kundi letu anapofanya tendo lisilokubalika na linaloweza kuhatarisha sura ya kundi letu, haraka tunajipa advantage kwamba watu wa kundi letu wanatofautiana. Kwamba, hata hivyo si kwamba sote tunafanana. Wapo wenye matatizo yao 'binafsi', yatengwe na kundi zima.

Kwa watu wa kundi jingine, sivyo tunavyofanya. Kwao, tunawaona kama watu wasio na wema tulionao sisi, na kwamba wote wanafanana kwa ubaya. Inapotokea mmoja wao akakosea, tofauti na tunavyofanya akiwa wa kundi letu, haraka tunajumuisha kosa hilo kuwa sehemu ya udhaifu wa kundi zima. Kwa kufanya hivyo, tunajisikia amani kwamba tuliko sisi ni mahali sahihi, na waliko wengine ni mahali palipopotoka.

Hii ndio sababu Mwislamu anaposikia kuna Mwislamu kajilipua Naijeria, hawezi kukubali kuwa huo ni Uislamu. Hatajisikia vizuri. Akikubali, hiyo itamaanisha kupingana na imani aliyonayo kuwa dini yake ni sahihi. Kwa hiyo, ni lazima umsikie akisema aliyefanya kitendo hicho ana matatizo yake na kamwe yasihusishwe na Uislamu. Anapofanya hivyo, huwa anajibu hitaji lake la kisaikolojia kwamba yuko katika kundi sahihi, ambalo hata hivyo linaweza kuingiliwa na 'wehu' wachache. Mkristo, kwa upande wake, hawezi kumtenganisha Mwislamu huyo aliyejilipua na dini yake. Atajitahidi kukiunganisha kitendo hicho na dini 'iliyopotoka', tena kwa haraka. Kisaikolojia kufanya hivyo, kunampa kuridhika kwamba dini yake ndiyo sahihi.

Nitoe mfano mwingine. Chukulia namna jamii inavyopokea taarifa kwamba Padre anatuhumiwa kumdhalilisha mtoto kijinsia. Kwa Mwislamu au Mkristo wa sect nyingine, ni rahisi kuamini tuhuma hizo kwa haraka sana. Kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwamba Padre amefanya kosa hilo. Hahitaji hata ushahidi. Ni hitaji la kisaikolojia kwamba, 'niliko mimi ndiko penye usahihi... angalia mambo yanayofanywa na Mapadre.' Lakini mwitikio wa Mkatoliki utakuwa tofauti. Kwake, atasubiri sana kupata ushahidi wa kutosha, na hata ukipatikana, atafanya juhudi za kumtenganisha Padre 'mdhalilishaji' na Ukatoliki. Ni hitaji lile lile la kisaikolojia kwamba, niliko mimi ndiko kwenyewe, hata kama kuna wakosefu wachache'.

Tufanyeje ili tujitambulishe na makundi yetu bila kuyafanya haya?

Hili ni swali gumu kidogo. Kadri unavyokuwa na hitaji kubwa la kujitambulisha na imani yako, na dini yako, na kikundi chako, utaendelea kuyafanya hayo tuliyoyaona hapo juu. Na kadri unavyokosa hamasa ya kujitambulisha na kundi lako, ndivyo unavyoweza kupunguza kufanya hayo tuliyoyajadili. Sasa ufanyeje ili uendelee kujitambulisha kwa hamasa na imani yako bila kulazimika kuwashambulia watu wa makundi mengine?

Kwanza, tambua kuwa unachokifanya ni kutaka kupata uhalali wa kidini kisaikolojia kwa kutumia mazoea yaliyojikita kwenye ufahamu wako bila hata wewe kujua. Kupunguza hali hiyo, tumia muda wa kutosha kuelewa misingi halisi ya imani yako, kundi lako, dini yako, bila kutegemea nguvu ya wengine. Kama tulivyoona, kani kutoka nje, yaani hitaji la kujitambulisha na wengine, ndilo mzizi wa tatizo. Usitegemee msukumo wa kundi ili kujitambulisha nalo, bali tegemea msukumo wa ndani. Na ukifanya hivyo, utapunguza kutegemea usahihi wa watu wa kundi lako, na makosa ya watu wa makundi mengine.

Pili, elewa kwamba hakuna kundi linaloweza kuwa na watu wanaofanana katika hali zote, na kwa wakati wote. Watu hutofautiana. Hivyo usijenge mazoea ya kuji-reward kwa kuwaweka watu kwenye mafungu ya pamoja kitabia, kimwenendo na kadhalika kwa sababu tu wako kwenye kundi moja. Badala yake, kila mmoja achukuliwe kama mtu anayeweza kufanya lolote kwa hiari yake, bila msukumo wa utambulisho wa dini au kundi lake. Maana yake, usijisikie kukosea na kuhukumiwa, anapokosea wa kundi lako, wala kufurahi anapokosea wa kundi lisilo lako.

Tatu, elewa kuwa utambulisho wa kundi lako hautegemei ubaya wa kundi la mwingine. Unaweza kabisa kujitambulisha vizuri na ukajisikia kuridhika kuwa kwenye kundi lako, bila kulazimisha wengine kuwa wakosefu. Mnaweza wote kuwa sawa ila kwa sura tofauti. Ukatoliki hauwi sahihi kwa sababu Uprotestanti umepotoka au kinyume chake. Kuwa chanya.

Mwisho, jenga mazoea ya kuwa objective. Yaani kitazame kitu kwa macho ya haki yasiyo na misingi ya upendeleo, bias. Udhalimu haigeuki kuwa 'upigania haki' ukifanywa na mtu wa kundi lako. Kosa ni kosa. Na haki ni haki. Iite haki hata kama imefanywa na mtu wa kundi usilolipenda. Hiyo haitapunguza hadhi ya kundi lako. Na uite udhalimu kwa jina lake, hata kama umefanywa na vinara wanaolitambulisha kundi lako. Hata kama kufanya hivyo kunatishia uhalali wa kundi lako, bado, udhalimu unabaki kuwa ni udhalimu.

Vinginevyo, kwa kuhakikisha kuwa haki haiwi haki mpaka ifanywe na watu wa dini yako, au udhalimu hauwi udhalimu ukifanywa na watu wa dini yako, basi, aliyesema kwamba dini ni bangi, anaweza kuendelea kuwa sahihi mpaka utakapofanikiwa kubadilika. Jielewe.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi