Kujikataa, kuikataa hali yako kwaweza kuwa kichocheo cha muhimu kujielewa

HUENDA umekutana na watu wanaoshauri ujikubali. Na huenda na wewe ni mmoja wao. Unajikubali. Kwamba ili kufanikiwa, ni busara ujipokee vile ulivyo na vyote ulivyonavyo kwa shukrani. Msingi mkuu, inasemwa, bila kujikubali na kujipokea huwezi kuwa na amani. Na amani na furaha, huenda, kama sio ndivyo ilivyo, likawa ndilo kusudi kuu la maisha ya mwanadamu. Purukushani zote tunazoziona, kukusanya mali, elimu, kuwa na familia bora, madaraka makubwa, umaarufu na kadhalika mwisho wa siku ni kutafuta furaha. Utoshelevu. Ridhiko la moyo.

Watu wasiojikubali, tunaambiwa hawana amani na maisha yao. Wanavyojiona sivyo vile wanavyotaka wao. Matokeo yake, ndio hao wanajichubua wafanane na sura wanavyoitaka wao. Sote tumesikia maisha ya yule mwanamuziki maarufu mweusi aliyejigeuza afanane na wazungu. Matokeo mabaya ya kutokujikubali.

Wengine tunasikia wakidanganya wasifu na elimu zao. Ulaghai. Lakini ukweli ni kwamba wanaona wasifu walio nao haufanani na vile wanavyotaka wao kuwa. Inabidi kudanganya. Kutapeli identity. Wengine tunaambiwa, shauri ya kutokujikubali, wanalazimika kutumia madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na pombe. Wanaona walivyo, hawatoshi. Inabidi kujipumbaza kwa vilevi.

Tofauti na hawa, wapo wenzao wanaoamini wanajikubali. Hawa 'wanaamini' vile walivyo ndivyo walipaswa kuwa. Wameridhika na utambulisho wao, na maana yake basi hawaoni shida na walivyotokea kuwa. Kwa hiyo, hadanganyi kama wenzao. Wanao ujasiri wa kusema na kufanya wanachofanya. Hawageuzi mwonekano wao kama wenzao 'wasiojikubali'. Maana wameridhika. Wanajikubali.

Huwezi kukubali usichokijua

Ninachotaka kukifanya ni kujaribu kusaili dhana hii ya kujikubali kwa mwendo wa pole. Swali kuu, pamoja na utangulizi huo likiwa: Je, kujikubali ni nini? Je, ni kweli kuwa kujikubali kuna faida zaidi ya hasara? Je, kujikataa, kwa maana ya kinyume cha kujikubali, hakuna faida zaidi ya hasara?

Kabla hatujafanya shughuli ya kutafsiri mipaka ya neno kujikubali katika makala haya, hebu kwanza kwa mwendo wa pole tujiulize swali hili muhimu, 'mimi ni nani?' Maana huwezi kujikubali au kujikataa bila kujiuliza swali hilo, 'wewe ni nani?' Unakubali unachokijua.

Kwa wengi, 'mimi' maana yake ni majina waliyopewa na wazazi wao, au wanayojiita wao. Wanasahau kuwa mimi alikuwepo kabla hajapewa jina. Siku ulipozaliwa, huenda hukupewa jina mara, ila ulikuwa wewe. Ulipewa jina ili wanaoishi na wewe wawe na kazi nyepesi ya kukutambua kati ya watu.  Jina ni sawa tu na anuani ya kukupata wewe. Ni nambari ya simu ya kukufikia wewe. Hiyo ikiwa na maana wewe ni zaidi ya tunavyokuona. Ni zaidi ya jina lako. Wapo wanaoamini kuwa majina hubeba haiba na tabia ya mtu. Wasichotujibu ni ikiwa nina majina mawili, rasmi na lisilo rasmi, lipi hubeba haiba yangu? Vipi nikibadili jina? Ni imani.

Basi. Katika kumtambua 'wewe', ambaye angalau tunakubaliana kuwa hana kabisa uhusiano wowote na majina uliyoyaandika kwenye vyeti wala vitambulisho vyako, ni vyema kuelewa kuwa 'huyo wewe' ndiye hasa anayehusika na vile unavyojisikia, unavyohusiana na nafsi yako, unavyohusiana na wengine na kadhalika. Ndiyo nafsi yako. Self.

Namna kuu za kijielewa wewe ni nani

Utaniuliza, 'mimi ni nani basi?'. Unaweza kujielewa kwa namna kuu mbili. Kwanza, kujifikiria wewe ni nani kama sehemu ya wanaokuzunguka. Kujipambanua na wanaofanana na wewe. Hapa tuna maana ya kujilinganisha na wenzako wanaofanana na wewe. Wenzako wa kundi lako. Swali kiongozi ni: Una nini ambacho wenzio wa kundi lako hawana? Una kipaji gani wasichonacho wenzako?

Sasa pamoja na ubora wa namna hiyo, bado yapo mengi usiyoyaona, na huenda unayaona kwa macho ya upendeleo. Wenzako wanayaona uzuri kama yalivyo kuliko wewe. Maana yake, namna ya pili ya kumtambua 'wewe' ni kujiuliza, wanaonizunguka wananionaje? Wafanyakazi wenzangu, wanafunzi wenzangu, ndugu zangu, na wengine ninaohusiana nao, wananionaje? Faida yake ni kusikia yale ambayo kwa kawaida wewe huyaoni. Wanaokuona, ukiwapa nafasi, wanaweza kukupa mrejesho sahihi. Hata hivyo, upungufu wa njia hii ni kwamba si mara zote wanaokuzunguka watakuelewa. Lakini tukubaliane kuwa wanaweza kukupa dondoo zitakazokusaidia kujisaili mwenyewe.

Ili kujisaili mwenyewe, unachofanya ni kujinganisha vile ulivyo hivi sasa na vile ulivyokuwa siku za nyuma. Lengo ni kuelewa ulivyo sasa hivi. Yepi hukuweza kuyafanya siku za nyuma, na sasa unaweza kuyafanya? Nini hukuwa nacho na sasa unadhani unacho? Ni uwezo na si vitu. Kwamba siku za nyuma, ulikuwa na wasiwasi na mashaka. Sasa unadhani unao ujasiri. Hiyo maana yake ni kwamba katika vingine alivyo navyo 'wewe', ujasiri ni moja wapo. Tatizo la namna hii ya kujielewa, ni pale unapogundua kuwa ulivyo ni pungufu ya ulivyokuwa siku za nyuma, na hivyo kujikuta ukifunga tathmini mara moja ili kubaki na amani.

Aidha, unapojitazama kama sehemu ya kundi lako kwa kulinganisha kundi unalojitambulisha nalo na makundi mengine yasiyofanana na kundi lako, unaweza kupata dondoo za wewe ni nani. Kuna ukweli kuwa kundi haliwezi kuwepo bila kinachowaunganisha. Makundi yanayokutambulisha yako mengi. Hicho kinachokufanya uwe sehemu ya kundi, ni sehemu ya utambulisho wako. Swali muhimu katika kulinganisha kundi lako na mengine ni: Je, kipi kwenye kundi langu kisichopatikana kwenye makundi mengine?. Hapa kuna makundi mengi. Dini. Imani. Siasa. Elimu/Majukumu/Kazi.

Philip Zimbardo alifanya utafiti ulioonyesha kuwa majukumu tunayopewa hutufinyanga kuwa sawa ama kufanana-fanana na majukumu hayo. Alitengeneza gereza la maigizo, ambapo washiriki walipewa majukumu tofauti tofauti. Wapo waliokuwa maafisa magereza, kwa hiyo ikawabidi kuwa wakali na watoa amri. Wapo waliokuwa wafungwa na kadhalika. Wote kwa ujumla walitakiwa kuvaa uhusika. Zimbardo alishangazwa namna washiriki walivyoanza kuwa halisi kadri siku zinavyokwenda. Yaani uhusika waliolazimishwa kuuvaa kimaigizo, uliwaingia na wakageuka kuwa ndivyo walivyoigiza. Maana yake, kazi na majukumu tunayoyatekeleza siku kwa siku yanatugeuza kutufanya tufanane na matakwa ya kazi husika.

Namna gani mtu hujikubali au kujikataa?

Mpaka hapo, bila shaka, tunakubaliana kuwa sisi ni zaidi ya majina yetu. Utambulisho wetu unavuka mipaka ya majina. Ndio kusema kwamba wewe u tofauti na wengine wote ikiwamo walio kwenye kundi unalojitambulisha nalo. Huwezi kufanana na wengine kwa vigezo vyovyote ikiwa utajielewa. Kila mmoja yu na upekee wake hapa duniani.

Sasa tuelekee kwenye kijibu swali lifuatalo: Je, unawezaje kujikubali au kujikataa? Ili kuelewa jibu la swali hilo, ni vyema basi tuelewe kuwa huyo 'wewe' uliyemtambua kwa namna tulizozigusia hapo juu, anazo sura tatu kubwa. Sura ya kwanza, ni 'wewe wa sasa'. Huyu ni wewe kama unavyojiona hivi sasa. Uwezo ulionao unaokufanya ufanye unachokifanya hivi sasa. Mfano wewe ni mwandishi kwa kazi yako. Unaandika. Hutarajii kuwa mwandishi. Ndivyo ulivyo. Iwe ulitaka kuwa mwandishi au umejikuta mwandishi si sababu. Lililo kubwa, wewe u mwandishi. Ndivyo ulivyo sasa.

Sura ya pili ni 'wewe mtarajiwa', wewe yule unayemtarajia kesho na kuendelea. Huyu ni wewe asiyekuwepo, lakini anayetarajiwa kufikiwa siku za mbeleni. Ndiye ndoto na maono yako. Ndiye kichocheo cha mafanikio yako. Kichocheo cha utoshelevu.  Ni kule kuwa unavyotaka uwe, lakini sivyo ulivyo. Ili kujielewa ipasavyo, yakupasa kumlinganisha 'wewe wa sasa' na huyu 'wewe anayetarajiwa'. Je, wanafanana? Kama hawafanani, kuna uwezekano wa kufanana?

Sura ya tatu ni 'wewe anayepaswa kuwa'. Huyu ni wewe anayetarajiwa na wale wanaokuzunguka. Watu wanategemea uweje. Mfano kama sehemu ya familia, baba na mama wanayo matarajio yao kwako. Kaka na dada zako, wana namna wanategemea utakuwa. Namna gani unafanana na 'wewe huyo wanayemtarajia wao' ni suala jingine. Fikiria mtu anapofikia umri ulionao wewe katika jamii yako, watu unaowathamini wanatarajia uweje? Huyo anayetarajiwa, ndiye tunamwita 'wewe unayepaswa kuwa'.

Sasa, inavyokuwa ni kwamba, anayejikubali maana yake, alivyo, ndivyo anavyodhani alivyopaswa kuwa, na ndivyo anavyotarajiwa kuwa. Huyu ana amani. Karidhika. Haoni haja ya kuwa vingine. Faida kubwa, ni kwamba ana amani kwa sababu alichokiota, alichokipanga, ndicho alichonacho. Anachokifanya, ndicho alichoamini alipaswa kukifanya. Majukumu aliyonayo anaona yanamfaa. Na ndiyo aliyoyataka. Kwa maana hiyo, huyu ni mtu mwenye amani na mwenye  kuridhika na maisha.

Bahati mbaya ya huyu ni kwamba huenda hajajisaili ipasavyo. Anadhani alipaswa kuwa alivyo, lakini kiukweli hajafikiri kwa bidii. Matokeo yake anadumaa kwa kutokuelewa na hajui kama anadumaa. Ni sawa na mtu anayedhani kamba aliyo nayo yeye ina mita mbili. Na karidhika. Lakini kumbe angeichunguza kidogo zaidi angegundua mkononi anazo mita 50 asizozitambua.

Wakati mwingine, huenda huyu hajatofautisha alivyo, na alivyotaka kuwa. Matokeo yake, anadhani anacho kila anachokitaka ili kumwezesha kufikia anakotaka kuwa. Lakini kihalisia ni kwamba hajafika bado. Uzuri wake, huyu anaweza kuwa mtu mwenye furaha sana ingawa kuna uwezekano pia akakosa nguvu au kichocheo cha kumfanya akue.

Unakubali unachokiona? Picha: thinwithin.org
Asiyejikubali kwa upande mwingine, maana yake ni kuwa anaona vile alivyo sasa, sivyo alivyopaswa kuwa, na sivyo anavyotaka kuwa. Haridhiki na alivyo ama kwa sababu anachokiona mbeleni sicho alichonacho, au alichonacho sicho kinachotarajiwa na watu wa kundi lake. Kwa hiyo ana deni. Kama ni mwonekano wa mwili, huyu anadhani hakutaka kuwa hivyo alivyo. Ana hitaji kubadilika. Kama ni ajira, huyu anadhani kazi anayoifanya haijautumia wala kuutambua uwezo wake ipasavyo. Hailingani na anachokitaka. Kama ni uwezo alionao, huyu anaona kuwa bado hajaupata ule anaouona mawazoni. Hivyo anajisikia deni la kujijengea uwezo ili kutekeleza anachodhani hajakitekeleza.

Huyu, anaweza kuwa na bidii ya kutafuta kuwa vile anavyotaka kuwa. Hiyo ni endapo ataweza kugundua raslimali alizonazo zinazoweza kumsaidia kufikia anakokutaka yeye. Kwa maana hiyo anaweza kwenda mbele kwa urahisi.

Ni bahati mbaya kuwa wakati mwingine mtu huyu asiyejikubali anaweza kugundua kuwa alivyo sivyo anakokutaka na hana namna ya kufikia kule anakokutaka. Matokeo yake ni ama hujigeuza kuwa asivyo au kukata tamaa na kuishi na msongo wa mawazo.

Tunayo mifano halisi. Watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii kuishi maisha ya dhahania sababu wanagundua maisha waliyoyatarajia siyo maisha wanayoyaishi. Wanaamua kuigiza. Matokeo yake wanaishi maisha yasiyokuwepo. Sikiliza machekibobu wa mjini wanaozungumza kama mamilionea, vijana waliofanikiwa, lakini ukweli ni kwamba sivyo walivyo. Wanajikuta wanajitesa kuishi maisha yasiyo yao, yafanane na masimulizi ya ndoto zao. Wanaoshi maisha 'yatarajiwayo'. Wana furaha kuwa bandia, lakini wanajidanganya.

Wengine wa kundi hili wameuona uhalisia. Wameamua kukubaliana na ukweli kuwa hakuna namna ya kufikia wanakokutarajia pamoja na ukweli kuwa hali iliyopo hawajayakubali. Matokeo yake wanaishi maisha yaliyojaa msongo wa mawazo. Na mara nyingine, kwa kutafuta kuikataa hali halisi, wengine, tunaambiwa wanaamua kulewa. Madawa ya kulevya. Lengo ni kusahau uhalisia waliougundua na ambao kwa bahati mbaya hawawezi kuubadili.


Je, ni vyema kujikubali au kutokujikubali?
 
Tulichojaribu kukionyesha hapa ni kwamba kujikubali maana yake ni 1) kutokuona tofauti ya vile ulivyo na vile ulivyotaka kuwa, au ulivyotarajiwa kuwa 2) kuikubali tofauti ya vile ulivyotaka au kutarajiwa kuwa na vile ulivyo sasa iwe kwa faida au hasara.

Kutokujikubali, kwa upande mwingine ni kuona tofauti ya vile ulivyo na vile ulivyotaka kuwa na kisha kutokuikubali tofauti hiyo iwe kwa faida au hasara.

Sasa ili kuhitimisha, tuone kisa kimoja. Wanaosoma biblia, wanamkumbuka mwana mpotevu. Huyu kijana, chekibobu wa mjini, baada ya kuponda raha akidhani hayo ndiyo maisha, mambo yalibadilika. Hali aliyokuwa nayo haikulingana na hali aliyowahi kuwa nayo. Hali kadhalika, 'yeye wa sasa' hakufanana na 'yeye aliyetarajiwa'. Ni kama tulivyoonyesha hapo juu.

Mwana mpotevu, tunaambiwa, akarudiwa na fahamu zake. Akasononeoka. Akajiuliza maswali mengi ya msingi yaliyomsaidia kujielewa.

Je, nilivyo, ndivyo nilivyopaswa kuwa?
Je, nijikubali na kuikubali hali hii? Mbona kuna uwezekano wa kujikataa na nikasonga mbele?

Tunaambiwa, hatimaye, mwana mpotevu alijikataa. Akakataa kuyakubali mazingira yake pamoja na 'yeye wa sasa'. Akagundua kazi anayoifanya haimpi utambulisho aliuoutaka. Haina manufaa. Inamdanganya. Tafakuri hiyo ya kujikataa, ilimpa wakati mgumu na kwa lugha ya leo, tungesema, alipatwa na msongo wa mawazo. Unajua msongo wa mawazo mara nyingi ni hatua ya kujielewa. Ukiutumia vizuri, msongo wa mawazo, unaweza kugeuka kuwa fursa. Kichocheo cha kuyaendea yaliyo mema.

Baso hatimaye, tunaambiwa, mwana mpotevu akakata shauri: Nilivyo, sivyo nilivyopaswa kuwa. Mwanampotevu akajielewa. Tunajua kilichofuata na faida yake.

Wakati mwingine, si sawa kujikubali. Unaweza kukubali hali duni ukidhani ni bora. Kumbe ukweli ni kwamba hujajielewa. Ungejielewa zaidi kidogo tu, na kukubali kulipa gharama ya kujielewa, yangekukuta ya mwana mpotevu. Alifikia mafanikio yake: alichokitaka, ndicho kilichokuwa.

Abraham Maslow anaweza kusisitiza haya tunayoyasema. Maslow alionyesha namna binadamu anavyohamasishwa kutafuta mahitaji asiyonayo. Maslow anasema, kupata mahitaji ya kawaida ulivyonayo, yaani kujihisi umefika ulikokutaka, huwa ni kichocheo cha kutafuta mahitaji yasiyokuwepo. Kila unapopata hitaji moja, linakupa furaha na ari ya kutafuta hitaji la juu yake. Kila unapopata hitaji fulani, baada ya muda, hitaji hilo hugeuka kuwa kichocheo cha hitaji jingine. Kujikubali hakufiki.

Kumbe kwa lugha nyingine, na kwa mipaka ya mjadala huu, kujikataa, kukataa hali uliyo nayo, kunaweza kuwa kichocheo cha kukufanya uende mbele zaidi. Ni sawa na mwana mpotevu aliyejikataa katika hali yake. Akakubali msongo wa mawazo kama gharama ya kweli mbele. Na kweli alikwenda. Angeridhika, kwa kadri ya Maslow, angejitengenezea kikwazo cha kwenda mbele. Angedumaa akilisha nguruwe wake, tena kwa furaha.

Je, kuna hali gani katika maisha yako, unadhani unahitaji kuikubali? Unafanya hivyo kuufunika ukweli ili uwe na furaha au unamaanisha kuikubali kwa dhati? Unadhani hitimisho la kujikubali umelifikia kwa kuelewa au kutokuelewa? Je, ni maeneo yepi ambayo, kama mwana mpotevu unadhani unawajibika kuyakataa, na kwa maana hiyo, kujikataa, ili kusonga mbele? Uko tayari kulipa gharama za kujisikia umepotea kwa muda, ili hatimaye uelewe pa kwenda? Au kikwazo ni watu, ambao ungependa mara zote wakuone uko kwenye njia sahihi? Tafakari, ujielewe.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?