Sababu zipi hufanya tofauti za attachments kwa watoto?


KATIKA mfululizo wa makala haya, tumeeleza namna watoto tangu wanapozaliwa,wanavyoungamanishwa na mama zao kwa kihisia. Tulitumia neno attachment kuelezea mahusiano baina ya mama na mwanae, mahusiano ambayo kimsingi ndiyo huamua mtoto anakuwa na tabia gani huko mbeleni kama tutakavyoeleza. Vile vile, tulieleza namna tunavyoweza kubaini usalama wa kihisia walio nao watoto kwa kuangalia namna wanavyoitikia kuondoka kwa mama, na kadhalika wanavyoitikia kurudi kwa mama. Tafadhali fuatilia makala haya hapa, kabla hujaendelea zaidi.

Katika makala haya, kwa ufupi, tutatazama sababu zinazochangia sana hisia hizo za usalama anazokuwa nazo mtoto. Tutazungumzia sababu tatu pekee: Ubora wa malezi ya mama, mazingira ya familia na maumbile ya mtoto mwenyewe.

Ubora wa malezi ya mama

Msomaji atakumbuka kuwa tumegusia kidogo wajibu wa mama katika kumfanya mwanae ajenge mahusiano naye. Kimsingi, tunapozungumzia ubora wa malezi ya mama, kwa mujibu wa magwiji wa masuala haya kama vile Belsky & Rovine na Ainsworth kuna masuala makubwa manne ya kutazama.

Moja, uelewa sahihi wa ishara za mahitaji ya mtoto. Hapa tunazungumzia sensitivity, yaani, kwa jisni gani mama anaweza kuyatambua, tena kwa ufasaha, mahitaji ya mwanae. Hili tulilieleza kidogo. 

Pili, upendo wa mama kwa mtoto unaoonyesha kumpokea mtoto vile alivyo. Hapa tuna maana ya namna mama anavyoweza kuonyesha kumpokea mwanae bila kujali alivyo. Tuna maana ya hata kama mtoto ni msumbufu, mliaji na kadhalika, mama awe na uwezo wa kumkabili kwa upendo bila hasira na ugomvi. 

Tatu, uelewa na hitaji la kujitegemea kwa mtoto kwa maana ya kumpa nafasi mtoto kupumua. Kutokumbana mno mtoto ajione mtumwa wa matakwa ya mtu mwingine. Nne na mwisho ni upatikanaji wa mama kwa mtoto. Kwamba mama yupo au ana tabia ya kutoweka nyumbani na kumwacha mtoto chini ya uangalizi wa watu wasiofahamika.
Cha kuongeza na kusisitiza hapa ni kwamba aliyoyapitia mama katika utoto wake yana mchango mkubwa sana kwa namna anavyohusiana na mwanae. Kwa maana nyingine usalama wa kihisia au kinyume chake ndivyo vinavyoamua aina ya mahusiano kati ya mama na mwanae.

Mazingira ya familia 

Tafiti zinaonyesha kuwa mazingira anamokulia mtoto nayo yana nafasi kubwa ya kuathiri anavyojisikia kisaikolojia. Hapa tunazungumzia masuala kama misuguano ya ndoa, matatizo ya fedha, misongo ya mawazo inayosababishwa na maisha yote hayo yanayoingilia namna wazazi wanavyoweza kuhusiana na wanao.

Tunajua kuwa pilika pilika za maisha zinafanya wazazi wakose muda na malezi. Ugomvi kati ya wazazi, kwa maana ya afya duni ya mahusiano ya wazazi wenyewe, huathiri moja kwa moja namna wanavyowekeza muda wao kuwakuza watoto katika njia ipasayo.
Mzazi mwenye msongo wa mawazo, anayejisikia kutokuwa salama yeye mwenyewe hawezi kuhangaika kumtafutia mtoto usalama asiokuwa nao.

Maumbile ya mtoto mwenyewe 


Upo ukweli kuwa watoto wanatofautiana kihaiba (temperament). Wapo watoto wepesi kuhusiana nao tangu kuzaliwa na wapo walio wagumu kuwaelewa wanataka nini na kwa nini hasa kwa wazazi wachanga na wanaodhani kulea ni automatic
Watafiti wanakubaliana kuwa maumbile ya mtoto nayo yana nafasi kwa kiasi fulani katika kuleta changamoto ya malezi kwa mama ingawa imethibitisha kuwa kila mtoto anayo nafasi sawa ya kuwa salama hikisia ikiwa watapata mazingira yanayowasaidia kuwa hivyo.

Katika kuhitimisha sehemu hii, tunakubaliana kuwa mazingira ya malezi yana nafasi kubwa zaidi kuliko maumbile ya kuzaliwa mtoto. Kila mzazi anaweza kumfanya mwanae kuwa salama (secure kihisia).

Katika sehemu zinazofuta, tutajadili implication ya attachment hizi tulizojadili kwa tabia ya mbeleni kwa mtoto.

Itaendelea...

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi