Aina za 'Emotional attachments' kwa watoto wenye umri hadi miaka mitatu



TULIGUSIA namna mahusiano ya awali kabisa kati ya mtoto na mama yanavyojenga muunganiko wa hisia za usalama kati ya mama na mtoto. Soma utangulizi huo hapa. Tuliona kwamba mhusika mkuu wa attachment (muunganiko wa kihisia) anaokuwa nao mtoto, ni mama. 

Kwa kweli ni sahihi kusema kwamba katika umri wa miaka miwili ya mwanzo, mtoto huwa na mradi endelevu wa ama kuwaamini watu au kuwatilia shaka. Na ni bahati mbaya kuwa haya yote hutokea mapama na katika umri mdogo ambao wazazi wengi hudhani watoto ni wadogo mno kuweza kuelewa yanayoendelea. Kwa ufupi, katika umri huu, wa miaka miwili, mama anaweza kabisa kufanya jaribio dogo la kujiridhisha ikiwa mwanae amejenga attachment naye au la.

Watafiti wa mahusiano ya kihisia kati ya mama na mtoto wakiongozwa  na Anne Ainsworth, kwa kufanya tafiti za kutosha kwa vichanga (infants) wamewagawanya watoto katika makundi mawili makubwa ya kihisia: La kwanza ni watoto wanaojisikia salama kihisia (securely attached infants) na watoto wasiojisikia salama kihisia(insecurely attached infants).
Hatua ya kwanza kujenga attachment. Picha imetumiwa kwa ruhusa

Watoto wanaojisikia salama kihisia

Hawa ni watoto wasio na wasiwasi na mahusiano. Usalama huu unaanzia katika kunyonyeshwa vya kutosha na kwa wakati. Ni watoto wenye bahati ya kuwa na ukaribu wa mama au yaya (caregiver) usiobadilika badilika. Kwa maana nyingine, watoto hawa hawachanganywi na kubadilika badilika kwa walezi wao. Hawa wana furaha kwa kuwa wanayo imani na watu na hawana sababu ya kuwa hofu na mashaka. Hawalii bila sababu, na hata wakilia, hulia kuwasiliana tu na sio kwa hasira hivyo ni wepesi kunyamazishwa. Hawaogopi nyuso ngeni, na hata wakionyesha wasiwasi na nyuso ngeni hasa baada ya kuvuka umri wa miezi sita ya mwanzo, ni wepesi kuzizoea na kuzikubali.

Ukitaka kujua ikiwa mwanao ni wa kundi hili, tizama anavyochukulia kuondoka kwako, na anavyokupokea unaporudi. Ikiwa unapomwacha mwanao kwa muda kwa sababu yoyote, na ikiwa ni wa kundi hili, anaweza kuonyesha upinzani kwa kulia. Hii ni hasa kwenye umri wa miezi saba na kuendelea. Lakini kwa kawaida, hawaendelei kulia kwa muda mrefu. Tofauti kubwa na watoto wasio wa kundi hili, unaporudi, hawana matatizo. Humchangamkia mama na kuonyesha wazi kuwa walisubiri ujio wake. Urafiki huendelea kama kawaida, na kwa kawaida kumbukumbu ya kuachwa haipo. Kama mwanao ni wa kundi hili, hongera sana, ni mwanzo wa mahusiano ya mwanao na watu baadae. Tutaeleza huko mbeleni.

Watoto wasiojisikia salama kihisia

Ukiwaacha hao, lipo kundi la watoto wasiojisikia salama kihisia. Hawa kwa ujumla tunaweza kusema hawana imani na mama. Ni watoto ambao si wepesi kuridhishwa hivyo ni watoto wa kulia lia na ni vigumu kuwanyamazisha walianza kulia. Huwa na mashaka sana na wageni wanapokuja nyumbani na si rahisi kuzoea nyuso mpya.  Kwa ujumla wao, hawapendi kuachwa kama wenzao wa kundi la kwanza, wanaojisikia salama kihisia, ingawa wapo wasiojali mama anapoondoka.

Tafiti zimewaga watoto wa kundi hili katika makundi madogo madogo matatu kwa kuchunguza mwitio wao, ama wanavyompokea mama mara anaporudi.


Watoto wakwepaji (Avoidant insecure infants)

Hawa ni nadra kulia mama anapoondoka, na mara nyingi hawajali kuachwa na mama zao. Kama mwanao wa kundi hili, hata unapoondoka asubuhi kwenda kazini, haonyeshi kujali. Unaporudi nyumbani baadae mtoto wa kundi hili huwa haonyeshi kujali. Haonyeshi kusisimshwa na kurejea kwa mama na wakati mwingine anaweza hata kuendelea na michezo yake na hata kumkwepa mama. Tunategemea kuwa tukio la kurudi kwa mama liwe na msisimuko, lakini kwa mtoto wa kundi hili, sivyo. Kurudi kwa mama si tukio la kusubiriwa kwa shauku. Ni namna yao ya kusema kuwa hawana mahusiano mema na mama zao. Zipo sababu nyingi zinazosababisha hali hii. Iliyo kubwa malezi yasiyojali (negligence), yasiyoelewa na yenye kupuuza (ignore) mahitaji halisi ya mtoto.

Watoto wagomvi (ambivalent insecure infants)

Kama walivyo wenzao wa makundi mengine, watotot hawa hawapendi kuachwa na mama zao kwa kulia. Kulia kwao ni kwa huzuni ya kuona hawatendewi haki. Ni kilio cha uchungu kinachozidi kile cha kuonyesha kutaka kuwa na mama. Ikiwa mwanao ni mgomvi, mara unaporudi nyumbani, mwanao hukupokea kwa kulia kwa kiasi cha kukuwia vigumu kumnyamazisha. Utachukua muda mrefu kumfanya atulie. Maana yake ni kusema mama hajaweza kupatikana kwa kadri mtoto anavyohitaji mtoto (inconsistent care giving), kubadilisha namna ya kujibu mahitaji yake kwa muda usioeleweka na katika mazingira ambayo ni vigumu mtoto kuyaelewa. Kutokueleweka kwa mama husababisha hisia za hasira na kisasi cha utoto kinachotokana na hisia za kutokutendewa haki.

Watoto wasiotabirika (disorganized infants )

Hawa huonyesha tabia zisizoeleweka yaani mchanganyiko wa tabia za watoto wa makundi mawili madogo tuliyoyaona kwa ufupi hapo juu. Kimsingi hawatabiriki, wanaweza kulia mama anapoondoka, au wasilie. Wanaweza kulia mama anaporudi, au kupuuza ujio wa mama kulingana na mazingira yenyewe. Lililo kubwa kwao ni kuwa na wasiwasi na hofu muda mwingi. Hawa ni watoto waliolelewa na mama mwenye matatizo ya kihisia ambayo yanayomsumbua yeye mwenyewe. Mfano mama aliyeumizwa na mwenye hasira ya kudumu lakini wakati huo huo akiamini kuwa yampasa kuonyesha upendo kwa mwanae. Matokeo yake hujikuta haeleweki ni lini ana upendo na mwanae na lini hasira zake huchomoza kwa mtoto. Kiujumla, kama mwanao ni wa kundi hili, wewe ni mama mwenye hasira, unakemea zaidi kuliko kueleza unachotaka. Namna fulani ya frustration.

Ni muhimu kuelewa kuwa aina ya usalama wa kihisia anaokuwa nao mtoto hadi mwaka wa pili, ni msingi wa mahusiano yake na watu kadri anavyokua. Kwa maana nyingine, makosa yanayofanyika katika kipindi hiki cha hadi miaka miwili, huwa msingi wa makosa mengine kwa miaka inayofuata.  Na ni bahati mbaya kuwa hisia hizi hujengeka mapema sana, katika umri ambao wazazi wengi huamini mtoto bado hafundishiki. Hapa ndiko ule usemi maarufu kuwa mtu mzima ni mtoto mzazi unapoleta maana. Ndio kusema, wakati wa utoto ndio determinant halisi ya haiba ya utu uzima kama tutakavyoendelea kuona hapo mbeleni.

Katika makala yanayofuata, tutajadili sababu zinazoumba aina hizi za emotional attachments na tutapitia implications zake kwa tabia katika hatua mbalimbali za ukumbwani.

Kumbuka kuwa hata wazazi nao wana insecurities zao, ambazo huzihamishia kwa watoto wao bila wao kupenda.

Itaendelea…

Maoni

  1. Kaka Bwaya ahsante sana nimejifunza pakubwa

    JibuFuta
  2. Karibu sana Fadhy. Nimenelea vyema kurudi kwenye vijiwe vyetu vilnavyopoozwa na #micro-blogging.

    JibuFuta
  3. Lazima kieleweke kwakweli.
    Tuko pamoja kaka

    JibuFuta
  4. Ha ha! Rama. Kitaeleweka kwa kweli. Namisi ule msisimuko wa enzi za blogu miaka ya 2005/6. Ah, nyakati kweli hupita. Hata hivyo naelewa, Facebook, Twitter na micro-blogging sites zimekuwa sababu kubwa ya kuporomoka kwa umaarufu wa blogu nchini kwetu. Nimeamua kukomaa. Tukomae. Kitaeleweka tu. Pamoja sana!

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?