Attachment: How secured is your infant?



KAMA lipo hitaji kuu na la msingi kabisa kwa mwanadamu ni usalama. Kujisikia upo katika mazingira yenye usalama. Security. Leo hii wageni wengi wanaogopa kwenda Mogadishu shauri ya hisia za kukosekana usalama. Al Shabab wanatishia usalama wa watu.


Kisaikolojia usalama ni zao la dhana inayoitwa kwa kimombo attachment ambayo ni muunganiko wa kihisia ambao mtu, aghalab mtoto, huutengeneza na mtu mwingine. Ni matarajio na imani za jumla anazokuwazo mtoto kuhusu wanaomzunguka.  Papalia na wenzake wanauona muunganiko huu kama uhusiano baina ya mtoto na mama, ambapo kila mmoja huchangia katika uhusiano huo. Ingawa zipo sababu nyingi zinazosababisha mahusiano haya ya kihisia, lakini watafiti wengi wanakubaliana kuwa mama ndiye mhusika mkuu.

Tafiti zinaonesha kwamba muungamaniko huu wa kihisia ni msingi wa uwezo wa mtoto kuelewa na kuhusiana na watu wengine. Attachment humwezesha mtoto kuuelewa ulimwengu unaomzunguka na kumfanya ama auamini kuwa unaaminika na unabashirika na hivyo kumfanya mtoto kuwa na ujasiri. Muunganiko huu wa kihisia unaonyeshwa kwa tabia kama kutabasamu, kucheka, kulia, kutambaa na kadhalika, tabia ambazo humleta mama kwa mtoto au mtoto kwa mama na hivyo kuwaleta karibu. 


Kujengeka kwa muunganiko huu wa kihisia

Tafiti nyingi (Howe, 1999; Berk, 2003; Ainsworth, 1973 & Bowlby, 1979) zimeonyesha kuwa attachment hufuata hatua nne kubwa: matayarisho (pre-attachment), msingi (attachment in the making), kuimarika (clear cut attachment) na mahusiano yanayoeleweka (formation of reciprocal relationship). 

Kipindi cha matayarisho huanzia kuzaliwa hadi miezi miwili. Ni wakati kichanga kinafurahia mahusiano na wanaokizunguka hata kama bado hakina uwezo wa kutofautisha hisia. Kichanga kinatabasamu, kufurahia mahusiano katika kipindi hiki. Na tunaambiwa na Berk (2003) kwamba kinafurahia kuona nyuso zenye furaha kuliko kitu kingine chochote. Akina mama wengi hutumia kipindi hiki kucheza na watoto wao.
 
Misingi (pre-attachment) huanzia miezi 3 mpaka 6, na hapa kichanga huanza kutambua sura ngeni kwa kutabasamu au kulia. Kina uwezo wa kuelewa mwitikio wa watu wengine kwa uzuri zaidi. Kinatabasamu kuonyesha kufurahia mahusiano, na kulia kunyesha kinyume chake.  

Kuimarika kwa muunganiko (clear cut attachment) ni kati ya miezi 7 hadi miaka 2 mpaka 3. Hapa kichanga kinaanza kuchagua nani wa kuhusiana nae na nani wa kukaa mbali nae. Ndipo hapa kinapojenga mahusiano ya karibu na mama au yaya. 

Kisha mahusiano yanayoeleweka (reciprocal relationship) huanza kwenye umri wa miaka 3 ambapo mtoto tayari anaelewa anataka nini na tabia halisi ya mama yake.  Mfano, mtoto hujua kabisa anahitaji kupendwa na huelewa ikiwa mama au wazazi wake wanao upendo huo anaouhitaji ama la.

Inakuwaje?

Ilivyo ni kuwa kupitia ukaribu wa kumnyonyesha kichanga tangu saa ya kwanza ya kuja duniani, kichanga hicho hujenga mahusiano ya karibu sana na mama. Hili tunalifahamu vyema tulio wengi. Kwamba kule kukumbatiwa na mama hukitia joto kichanga kujisikia salama.

Kichanga cha siku 3 kinajua mahitaji yake. Picha: Sayuni Philip
Kadri kinavyokua kiumri, siku zinavyokwenda, kichanga hiki huanza kuelewa mazingira yake kwa ufasaha. Huanza kusaili ikiwa dunia kinayoishi inaaminika na hivyo kutegemewa au kinyume chake. Kichanga hiki tangia mwanzoni kabisa mwa maisha yake, huanza ama kujenga imani na mazingira yake au kushindwa kabisa kuyaamini.

Mama ndiye hubeba jukumu la kwanza la kukifanya kichanga hiki kijenge imani katika dunia inayotabirika kwa maana ya kuaminika, kutokubadilika badilika na hivyo kueleweka. Mama mwenye wepesi wa kuelewa mahitaji ya kichanga hiki kimwili na kihisia, mama mwenye sensitivity na ushirikiano na kichanga chake, hukifanya kichanga chake kijisikie kuwa katika mikono salama. Tutalitazama suala hili vyema katika makala yajayo.

Inavyokuwa ni kwamba kichanga hulia kikitegemea kujibiwa mahitaji yake. Mama anapoyaelewa kwa ufasaha mahitaji hayo na kuyajibu kwa wakati, kichanga hicho hujenga imani. Hujenga picha kuwa wanaomzunguka wanaaminika na wanaweza kutegemewa. Ili hili lifanikiwe, mama hupaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kuelewa maana ya madai ya kichanga chake kimwili, kihisia na kijamii  kupitia kulia, kutabasamu, vitendo vya mwili na kadhalika. 

Erickson, miongoni mwa wazee wa mwanzo kabisa kutafiti namna tabia zetu zinavyojengwa, aliamini kuwa hatua ya awali kabisa katika kujenga haiba ya mtu ni kumridhisha mtoto kwa maziwa ya mama. Mama anayemnyonyesha mwanae vya kutosha na kwa wakati hutuma ujumbe kwa mwanae kuwa wapo wanaoweza kujibu mahitaji yake kwa wakati. Hii humfanya mtoto awe na imani na mazingira.

Sasa unaweza kujiuliza inakuwaje kichanga kielewe yote haya katika umri mdogo? Ukweli ni kwamba kichanga kinazaliwa kikidai mahusiano na wengine, hitaji linalokifanya kiwe makini sana kuona namna watu wanaokizunguka wanavyojibu mahitaji hayo.

Ndio maana akina mama wasiojali mahitaji haya ya wanao, kwa kudhani kuwa hawaelewi lolote, hujikuta wakiwa na watoto ambao pamoja na matatizo mengine tutakayoyajadili mbeleni, hulia muda mwingi. Kulia huku kwingi ambako mara nyingi hakunyamazishwi kirahisi ni sawa na kusema kuwa mahitaji ya msingi hayajaweza kujibiwa kwa wakati. Hivi ni vichanga visivyonyonyeshwa kwa wakati, visivyoonyeshwa kupendwa na akina mama zao, visivyopata joto la mama zao. Ni watoto walionyimwa haki ya kueleweka. Deprived infancy

Katika makala yanayofuata, tutajadili jaribio la kujua ikiwa mwanao mwenye umri wa miaka isiyozidi miwili anakuamini kwa maana ya kujisikia kuwa salama au tayari ameshaanza kujenga hali ya kutokukuamini na hivyo kuwa na mashaka na usalama wake.

Itaendelea….

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi