Watoto waliolelewa kidini, wamegundulika kushindwa kutofautisha uhalisia na mambo ya kufikirika

MIAKA miwili iliyopita, 2012, Justin L. Barret alionyesha kwamba binadamu wote huzaliwa na hitaji la asili la imani na kutambua nguvu zisizoonekana na kwamba imani haitokani na jamii kama wanavyodai watu wasio amini uwepo wa Mungu. Kwa Barret, imani za kidini ni sehemu ya 'maumbile' ya asili anayozaliwa nayo mtu.

Hoja zake kuu katika kitabu chake ni mbili 1) kwamba watoto wana uwezo wa asili wa kuamini nguvu za kimungu zisizoonekana kwa sababu ya, pamoja na mambo mengine, huamini uwepo wa miungu iwezayo yasiyowezekana kibindamu kabla hata ya kufikia hatua ya kujua kuwa watu wazima wanajua zaidi ya watoto 2) kwamba watoto sio madodoki ya kunyonya utamaduni unaowafanya kuwa waumini wa dini kwa sababu imani, hata hivyo, hutofautiana kati ya mtu na mtu, mahali na mahali na kadhalika. Soma pitio la kitabu Barret kiitwacho Born Believers: the science of children's religious belief.

Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni unapingana na hayo aliyoyasema Barret miaka ipatayo miwili iliyopita. Kinyume chake, inaonekana kwamba imani hutokana na jamii anamokulia mtoto. Kwa maana nyingine, mazingira ya makuzi ya mtoto ndiyo kichocheo cha imani yake.

Je, mafundisho ya kidini yanaathiri uelewa wa kawaida? Picha:faithgateway.com
Kathleen H. Corrieveau na wenzake, siku chache zilizopita wamechapisha matokeo ya utafiti wao kuonyesha kuwa watoto wadogo wanaolelewa katika misingi ya kidini hawana uwezo wa kutofautisha ukweli na masimulizi ya kufikirika.

Katika utafiti wao, watoto wa kati ya miaka mitano na sita wa makundi mawili makubwa:  wasiokwenda kanisani na wanasoma shule zisizo za kdini na wale wanaohudhuria makanisani au wanasoma kwenye shule za kanisa walitumika.

Washiriki hao wa makundi hayo mawili walipewa hadithi za aina tatu, 1) hadithi za kidini, 2) hadithi za kufikirika na 3) hadithi za kweli na kutakiwa kung'amua ikiwa hadithi hizo zina mambo yasiyowezekana katika hali halisi. 


Matokeo yalionesha kwamba theluthi mbili ya watoto wanaolelewa na wazazi wanaosisitiza mafundisho ya kidini, hawakuwa na uwezo wa kugundua mambo yasiyo ya kawaida yaliyokuwa kwenye hadithi hizo ambayo kwa hali ya kawaida hayawezekani. Kwa mfano, watoto hao walionekana kutumia miujiza inayoonekana kwenye biblia ili kuelewa hadithi za kufikirika na hivyo kujikuta wakifanya mahitimisho yasiyokuwepo. Wakati wenzao wasiolelewa kwenye misingi ya kidini walielewa kwa haraka mambo yasiyowezekana yaliyokuwa yamechomekwa kiufundi na watafiti kwenye masimulizi hayo.

Na katika masimulizi ya kufikirika, watoto hawa [waliolelewa na wazazi wanaoamini dini] hawakuweza kabisa kuelewa wahusika waliotumika katika masimulizi hayo kuwa ni wa kufikirika na kwamba kihalisia, hawapo. Ni sawa na kusema, katika hadithi za akina Sungura na Fisi, watoto waliolelewa katika misingi ya kidini, waliamini kweli kuwa Sungura huongea na ana tabia kama za binadamu. Lakini wenzao wasiolelewa katika misingi ya kidini, walionekana kung'amua kuwa wahusika waliotumika katika hadithi hizi ni wa kufikirika, na kwamba katika hali halisi hawapo.

Watafiti hao wanatafsiri matokeo hayo kuwa  mafundisho ya kidini, hasa hasa masimulizi ya miujiza  kwenye biblia, huwafanya watoto wawe wepesi kuamini mambo yasiyokuwepo na ambayo kwa hakika hayana uhalisia na hali halisi.

Hali hii ikiota mizizi kwa mtoto, pamoja na kweli kuwa ni muhimu sana katika kukuza imani ya mtoto, inaweza kuathiri vibaya uwezo wake wa kuelewa tofauti ya mambo katika maisha halisi, na kwamba ikawa rahisi sana kudanganyika na kujiingiza kwenye imani za hatari ikiwa ni pamoja na ushirikina na uaguzi ili kutatua matatizo yake kwa njia za mkato.

Je, matokeo haya yanaweza kuwa na maana yoyote  kwa wazazi wa Kiafrika ambao asilimia kubwa wanaamini dini, na wangependa watoto wao wafuate nyazo zao? Je, tunawezaje, kama wazazi tunaopenda wanetu wawe waumini wa dini tunazoziamini sisi, kufanya hivyo bila kuwafanya watoto hao wawe watu wanaoamini mambo yasiyokuwepo?

Je, kuna uwezekano wa kumkuza mtoto kimaadili na kiimani pasipo kumwingizia misingi ya kidini pasipo hiari yake? Kama mzazi, unajisikiaje ikiwa mtoto wako ataamua kuchagua kufuata imani anayodhani inamfaa yeye zaidi kuliko inavyokufaa wewe?

Imeandaliwa kwa kutumia taarifa zilizochapishwa kwanza kwenye jarida la  Huffington Post

Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini