Gharama ya kusema ukweli inazidi gharama ya kuongopa? -1

Je, ni mara ngapi umewahi kulazimika kusema 'uongo' kwa kisingizio cha kulinda mahusiano mema na watu wanaokuzunguka? Je, ni mara ngapi umetamani kudanganywa ili ujisikie vyema? Usishangae. Uongo hapa ni pamoja na 'ukweli nusu' unaosemwa kama mbinu ya kulindwa/kulinda 'matatizo yasiyo ya lazima'.

Chukulia umekosewa na rafiki yako mkubwa mnayeheshimiana. Kwa jinsi mlivyoshibana, unahisi 'nikimwambia alivyoniudhi...atakasirika na huenda urafiki wetu utakuwa katika hatari ya kusambaratika'. Unahesabu gharama, unaishia kujipa matumaini kuwa ukweli (ambao kwa wakati huo ni kumwambia rafikiyo kuwa kakosea) una gharama kubwa mno kuliko gharama utakayoingia ya 'kumwumiza hisia zake' na pengine kumkosa. Unatabasamu na kumhakikishia kuwa 'hakuna alichokosea. It's alright!'. 'Una hakika sijakuudhi?' anauliza rafiki yako huyo baada ya kuhisi kama umebadilika uso. 'Kabisa. Niko vizuri!' unamhakikishia na kubadili kabisa mada. Moyoni unajua kabisa kwamba alichokifanya rafikiyo hakikuwa sahihi. Unaugulia moyoni.

Kwa 'hekima' ya kutunza mahusiano, unaona ni bora kujikaza kiume kuliko kuhatarisha mahusiano na rafiki yako mpendwa. Ukweli, katika mukhtadha huu, umeonekana kuwa 'mchungu mno' kuweza kusemwa, na hekima yake ni kusema uongo ili maisha yaendelee. Huu ni mfano mmoja wa maisha yetu ya kila siku yanayofunikwa na 'hekima' ya kusema uongo kama njia bora ya kuishi vyema na ndugu na rafiki zetu.

                                                           Picha: Mary DeTurris Poust

Tafiti zinaonyesha kuwa watu wengi husema uongo katika zaidi ya asilimia 20 ya mawasiliano yao na watu wengine. Kwamba angalau uongo mmoja husemwa baina ya watu wanaofahamiana kwa siku.  Nini kinasababisha watu kukwepa ukweli? Kwa nini uongo huonekana kuwa njia rahisi ya kuishi na watu kuliko ukweli?

Imethibitika kuwa uongo asili yake  ni shauku ya mwanadamu kukubalika na watu anaowathamini iwe kwa kuficha hisia au taarifa hasi zinazoweza kuhatarisha hitaji la kupendwa, kuonekana bora, wa maana na mwenye nguvu. Kinyume cha hitaji hilo ni hofu ya  kukataliwa au kudunishwa, hali ambayo ni watu wachache huweza kukabiliana nayo.

Kwamba ukweli, sincerity, ama kufunua hisia au taarifa halisi zisizoonekana au kujulikana kwa unayewasialiana naye, mara nyingine hutishia hisia za kupendwa, kukubalika au kuonekana wenye nguvu. Ndio maana, basi, pamoja na kudai kwamba tungependa kusikia ukweli, mara nyingine watu hukwepa kuusikia hasa inapotokea ukweli huo unahatarisha shauku yetu ya kuonekana watu bora, wa thamani na watendao mema kwa watu wengine. Mathalan, tunapoambiwa kuwa 'tumekosea', na kosa lenyewe lihusishwe na udhaifu wa haiba yetu, tunajisikia vibaya. Fahari yetu ya kutaka kuonekana watu wa maana au basi wenye nguvu hutishiwa. Tunaona bora kudanganywa, kuambiwa kuwa hatukukosea, almuradi fahari ya thamani ya utu wetu ilindwe.

Tafiti kuhusu tabia ya kutokusema ukweli zinaonyesha kuwa watu wasiojiona salama ndani mwao (insecure) na hivyo kujaa hofu kuhusu namna watu wengine wanavyowaona wao, ndio wanaokuwa katika hatari kubwa ya kudanganya, kusema kweli nusu, ama kutokuwa wakweli.
Kwa watu hawa, ukweli unaoakisi hisia zao hasi zao kwa watu wanaowathamini au ukweli unaoakisi uhalisi wa hisia za watu hao kwao, ni gharama kubwa mno inayohatarisha sura yao (self presentation) kwa watu hao. Njia nyepesi ya kujisikia vyema, bora na wa maana, ni kusema ukweli nusu (unaowapendelea) kwa wengine na kuficha hisia zao halisi katika jitihada za kuwafurahisha wanaowasikia.

Itaendelea...

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Pay $900? I quit blogging

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Heri ya mwezi mpya!