Gharama ya kusema ukweli inazidi gharama ya kuongopa? - 2
Tuliona katika sehemu ya kwanza ya makala haya kwamba mwanadamu ana mazoea ya kuongopa kuliko kusema kweli. Tafiti zimeonyesha hivyo. Kuongopa hapa kuna maana ya kule kushindwa kusema ukweli kama ulivyo, na badala yake kupinda pinda mambo yalivyo bila kujali malengo ya kufanya hivyo. Imesemwa tangu zamani, uongo ni uongo pasipo kujali nia ya anayeongopa. Tuligusia kwamba watu wenye hisia za uduni na kutokuwa salama nafsini mwao huwa katika hatari kubwa zaidi ya kudanganya kuliko wenye kujiamini na kujisikia salama katika nafsi zao. Katika sehemu hii ya pili, tutajaribu kusaili sababu kuu zilizothibitishwa kusababisha watu kutokusema kweli.
Mosi, ni woga wa kukosa kukubalika. Hapa tunazungumzia hitaji kubwa la mwanadamu la kukubalika na watu. Kujisikia sehemu ya mahusiano mema na watu wengine. Unajisikiaje kama watu unaowahitaji wanakukwepa au hawakukubali? Maana yake ni kwamba kama wanadamu, tunapenda kujisikia kuwa watu wengine wanatupokea na kutuona kama watu wanaostahili heshima. Hali hii ni msingi wa kutokusema ukweli unaohatarisha usalama wa heshima yetu. Nitaeleza.
Fikiria unampa mtu wako wa karibu mrejesho hasi utakaomfanya atafakari mwenendo wake na kuurekebisha. Mfano kwamba mfanyakazi mwenzako aliye rafiki yako hukupoteza muda mwingi uwapo kazini kwa mazungumzo yasiyo kwenye orodha ya majukumu unayopaswa kuyatekeleza kazini. Unajua anakosea, na ndani unajisikia vibaya lakini kwa hofu ya kumpoteza, yaweza kuwa kazi ngumu sana kuusema ukweli kama unavyouona moyoni mwako. Na badala yake waweza kujikuta ama ukiamua kuendelea kuuvumilia udhaifu huo unaowakwamisha nyote wawili kuongeza ufanisi kazini, au kuusema ukweli nusu nusu ili kuufikisha ujumbe kupitia banda la uani ili uendelee kudumisha urafiki wenu. Ingratiation. Kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa ili basi tu mahusiano yaendelee kudumu.
Wangapi tunaweza kuwaambia rafiki zetu makosa yao kwa uwazi pale wanapokosea hata kama kwa kufanya hivyo kutamaanisha kuhatarisha mahusiano yetu? Wangapi tunaweza kuwatazama watu tunaowaheshimu na kuwahitaji machoni pao na kuwaambia makosa yao wazi wazi pasipokupinda pinda? Si kazi rahisi hasa katika mazingira ambayo sisi wenyewe tunajiona chini, duni na dhaifu kuliko tunaotarajiwa kuwaambia makosa yao.
Sababu ya pili ni wasiwasi wa kushusha hadhi na heshima unayodhani unayo kwa kuusema uhalisia unaoanika udhaifu wako. Kama tulivyosema, mwanadamu analo hitaji kubwa la heshima, kuonekana bora na wa maana. Hakuna mtu anayependa kuonekana mwenzangu na mie asiye na maana katika jamii. Tunapokuwa kwenye mazingira ya kutoa taarifa zinazoweza kuhatarisha heshima yetu kwa wanaotusikiliza, tukiamini kuwa kwa kuujua udhaifu wetu wanaweza kututeremsha kwenye ngazi ya heshima na hadhi, basi uongo hufanyika njia nyepesi ya kutunza heshima hiyo.
Hali hii yaweza kuonekana sana kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, ambapo watumiaji hujitahidi kudhibiti taarifa zao hasi ili kujenga mwonekano wanaoutaka wao. Jitihada za kudhibiti taarifa wasizotaka zifahamike, mara nyingi hudai kukuza mno taarifa chanya zitakazosaidia kukuza hadhi ya mhusika wakati huo huo zikidai uongo wa hapa na pale kwa lengo lilelile. Hata katika maisha halisi mitaani, watu hufanya yayo hayo ili wakubalike.
Hali kadhalika, ukweli pia hukumbana na kikwazo cha wanaotusikiliza kutokupenda kuambiwa udhaifu wao. Hatupendi kusikia udhaifu wetu -tunaouficha sana- ukifahamika. Udhaifu ni kero. Hatuupendi japo tunajua tunao. Tunapenda watu wasikie habari zetu njema. Hatupendi ukweli unaoyataja makosa yetu usemwe nasi tukisikia.
Ukisoma vitabu vya maisha binafsi vinavyoandikwa na watu maarufu utaliona hili. Kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho, watu hawa hufafanua mazuri yao kwa bidii. Namna walivyoleta mabadiliko katika jamii, mashirika yao au hata kwenye familia zao. Watu hupenda kuhusishwa na mazuri hata kama yaliwapata kwa bahati. Lakini linapokuja suala la udhaifu, jitihada za makusudi hufanyika kuutenga na mhusika. Kwamba ni hali na mazingira ndiyo yaliyosabisha udhaifu huo uonekane na sio wao wenyewe. Ni sababu hiyo ya kutokupenda kusikia udhaifu, hutufanya tushindwe kuwaambia ukweli 'mbaya' watu tunaowaheshimu na tunaojua tunawahitaji.
Fikiria umechangia maoni katika mkutano, na ukaamini kabisa ulichokisema ndio chenyewe, kisha baada ya mkutano mtu mmoja anakufuata na kukuambia njinsi ulivyokuwa umepotoka kwenye hoja zako! Lah! Inakuharibia kabisa siku yako, shauri ya kuona kuwa hadhi uliyodhani unayo, haionekani.
Kwa hiyo, kwa kutambua kuwa masikio ya binadamu hupenda kuambiwa mema yao, watu wengi hukosa ujasiri wa kutosha kuwaambia watu madhaifu yao hata kama ni ya kweli. Matokeo yake, hujikuta wakiwapaka watu kwa mafuta ya mgongo wachupa, kwa kutokusema ukweli halisia ili tu wakubalike.
Tazama namna watu wanavyotoa maoni kwenye mitandao ya kijamii. Hata katika mazingira ambayo mwanzisha mada na mchangiaji wanafahamiana vizuri, na ikatokea kuwa mchangiaji hakubaliani na mwanzisha mada, ni mara chache sana, mtoa maoni huthubutu kusema anachofikiri hata kama mtoa mada asingependa kukisikia. Najua kuwa ni kawaida sana kwa wachangiaji wengi hukosoa na hata kutukana yaliyoandikwa na aliyeanzisha mjadala. Lakini mara nyingi hili hufanyika katika mazingira ya kutokuwepo kwa mahusiano yoyote kati ya anayeanzisha hoja na anayechangia. Hiyo ni kusema kwamba katika mitandao ya kijamii, ukweli husemwa pasipokuwepo mahusiano.
Mpaka hapa tunaweza kukubaliana kuwa ukweli unayoutaja udhaifu wa anayeusikia unatishia heshima. Hatupendi kusikia ukweli unaotushushia hadhi tunayoihitaji hata kwa gharama za uongo. Tunapenda kusikia mema yetu kwa gharama yoyote hata ikibidi kudanganywa. Lakini yote hayo huwa kwa watu wasiojiamini. Watu wasiodhani kuwa udhaifu ni sehemu ya heshima tunayoitamani. Kwa watu hawa ukweli uliokamilika si jambo jema sana.
Itaendelea...

Gharama ya urafiki mara nyingine ni kubwa. Picha money.howstuffworks.com |

Kitabu kama hiki hakitarajiwi kueleza mabaya ya mwandishi. |

Maoni
Chapisha Maoni