Gharama ya kusema ukweli inazidi gharama ya kuongopa? -3

TUMEJARIBU kuonyesha sababu za watu kutokuwa tayari kusema ukweli kama ulivyo. Sababu zote zinafungwa kwenye fungu moja: Hofu ya kukataliwa. Hofu ya kushusha hadhi. Faida ya ukweli huonekana pale ambapo ukweli wenyewe utatusaidia sisi kukubaliwa na watakaousikia. Mume awapo mkutanoni, mahali panapomsaidia kuonekana anawajibika kwa familia yake na mwajiri wake, hawezi kudanganya. Kusema yuko mkutanoni kunamsaidia isipokuwa kama ukweli huo unaweza kuhatarisha heshima yake. Katika mazingira ambayo ukweli hauwezi kusaidia kulinda heshima yetu, hatuwezi kuwa tayari kuusema. Hapa ndipo tunapojikuta tukiusema ukweli nusu nusu au kwa lugha nyingine uongo.

Katika kujua gharama ya ukweli, waweza kutazama hata namna ambavyo viongozi wa dini wanaohubiri umuhimu wa ukweli wanapojikuta nao wakishindwa kuusema ukweli halisi pale ambapo ukweli huo unahatarisha usalama wao binafsi au wa taasisi wanazoziongoza.  Ni nadra kwa mfano kumsikia kiongozi wa dini aliyetoa kauli yenye ukakasi kuhusu suala fulani, kukiri kuwa kakosea. Kukiri kosa, ndio ukweli anaouhitaji ingawa unakwenda kinyume na hitaji lake la kulinda hadhi na heshima yake. Katika mazingira hayo, si ajabu kumsikia akijitetea kwa kosa lililo wazi, maadam tu, anajua kuukiri ukweli ni hatari kwa heshima yake. Hapo tunaweza kuona kuwa ukweli una bei ya juu kwa wengi wetu kukubali kuilipa.

Ingawa kwa juu juu ukweli waweza kuonekana kuwa na gharama kubwa, hasa unapokuwa unahusu uhalisia hatarishi kama tulivyosaili, ni muhimu kutambua kuwa gharama hiyo huwa ni ya muda mfupi sana. Uongo ambao huonekana kuwa njia ya mkato ya kujilindia heshima na kujihakikishia hitaji la kukubaliwa, una gharama kubwa na ya muda mrefu zaidi. Nitaeleza.

Kama tulivyoona, ukweli 'mchungu' waweza kukufanya uonekane huna maana kwa muda mfupi. Na inawezekana wanaotusikia tukiusema ukweli 'mchungu' wakatushangaa. Faida yake ni kuwa ukweli huo huwafanya wanaokusikia ukiyasema mapungufu yako hadharani, wakuamini zaidi. Fikiria unamsikia mtu uliyedhani hawezi kuwa na nyumba ndogo, mchepuko, anakwambia wazi pasipo shinikizo kuwa anajutia kitendo chake cha kuwa na mwanamke mwingine asiyefahamika na mke wake. Unamchukuliaje mtu huyo? Kwa hali ya kawaida, ni rahisi kumwamini zaidi mtu huyo katika mazingira mengine ya maisha kwa wakati mwingine. Ukweli hujenga kuaminika zaidi kwa wanaousikia.
Inawezekana kusema ukweli kama ulivyo. Picha theinsuranceproblog.com

Pande mbili za shilingi hutuhamasisha kumsikiliza na hata kumkubali msemaji. Upande wa pili wa shilingi huongeza uhalali (credibility) wa anayeusema. Hata katika hoja. Anayeeleza hoja zinazopendelea upande wake tu na kuzipuuza hoja zinazomnyanyasa, hukosa kuaminiwa na wanaomsikiliza. Hukosa uhalali. Hatushangai kumsikia Mbowe akiisifu CHADEMA na mazuri yake. Lakini ukimsikia Mbowe akiyataja mema ya CCM, unamwamini zaidi hata atakapoisifu CHADEMA yake. Kadhalika, watu wasiotaka kubainisha upande mwingine wa maisha yao, upande unaohatarisha heshima yao, hadhi yao na hivyo kukubalika kwao, wana nafasi ndogo sana ya kuaminiwa. Tabia ya kutaka kusimamia hadhi yatu kwa gharama za kudanganya, ina msaada wa muda mfupi sana.

Tunapofanya juhudi za kutaka kuonekana watu wenye heshima zetu, ni vyema tukumbuke kusema ukweli hata pale ukweli huo unapogharimu heshima ya muda mfupi. Ukweli 'mchungu' kutusaidia kujenga kuaminika zaidi. Mke humwamini mumewe zaidi pale mume huyo anapokuwa mwepesi wa kusema ukweli hata ule unaomwumiza. Ukweli mchungu. Mkuu wa kazi anayeelewa kazi yake vyema, humwamini mfanyakazi wake anayekiri mapungufu yake.

Ingawa ni kweli mara nyingi kuubaini uongo huwa si kazi nyepesi, lakini zipo nyakati uongo huo hubainika. Tunaambiwa njia ya mwongo ni fupi, na mbio za sakafuni huishia ukingoni. Maana yake upo uwezekano wa uongo huo unaopendeza leo kufahamika kesho. Na wakati huo, hiyo kesho, ukweli halisi unapofahamika, ile faida ya muda mfupi tuliyokuwa tukiitafuta, hugeuka kuwa shubiri. Hadhi tuliyokuwa tukiisaka kwa gharama yoyote huporomoka.

Imesemwa tangu kale kuwa ukisema kweli hutakuwa na haja ya kukumbuka ulichowahi kusema. Ukweli hukuweka huru. Nilifurahi wakati fulani kusoma mahala simulizi la rafiki yangu aliyekuwa na matatizo yake binafsi. Aliamua kuandika bandiko kwenye blogu linalosimulia hali yake. Nikapenda mtazamo huo wa kusema upande wa pili wa maisha yetu. Maana tumezoea kusoma maandishi ya watu wanaojisifu. Watu wanaosema ukweli unaowapendelea. Lakini kwa rafiki yangu yule, ukweli ulikuwa ni ukweli hata kama ungemgharimu  heshima yake kwa wasomaji. Ukweli ulimweka huru.

Ni watu wanaojisikia usalama wa nafsi pekee ndio wanaothubutu kusema ukweli bila kuuchagua. Hawajali matokeo ya ukweli huo. Hawaogopi kukataliwa, hawaogopi kupoteza heshima ya muda mfupi. Husema ukweli kwenye Facebook. Hawaogopi maoni hasi kwenye hoja zao. Hawafurahii mrejesho chanya pekee. Wanajua kuwa kwa kuwa tayari kuusikia ukweli 'mchungu' kuhusu maisha yao, wanakaribisha kupewa mrejesho wa maana zaidi wenye ukweli (genuine) utakaowasaidia kwenye kazi zao na maisha yao  kwa ujumla. Wanajua kutokutaka kusikia ukweli 'mchungu' hutufanya tuambiwe yale ambayo watu wanajua tunatamani kuyasikia. Na bahati mbaya hayatusaidii.

Si kazi rahisi. Nilianza kujenga tabia ya kuvumilia kusikia upande wangu wa pili wa shilingi. Mwanzoni ilikuwa ngumu sana. Unapata mrejesho unaokunyong'onyeza. Inauma. Lakini taratibu, kwa kujikaza kusikia ukweli kama ulivyo, bila kujali namna unavyonisaidia kulinda heshima yangu, nilifungua milango kwa watu wa karibu kuwa wakweli kwangu. Ninaweza kusoma maoni hasi kwenye ukurasa wa Facebook, bila kujenga ukuta na aliyeandika. Nikagundua kuwa kuambiwa ukweli hata tusioutaka, kunatujenga zaidi. Kunanipa fursa ya kujikagua kihalisia zaidi. Sijafika bado. Maana ukweli si mwepesi kuubali.

Nimejifunza kusema mambo yangu hasi ya moyoni kwa ninaowaamini. Kusema kushindwa kwangu. Kusema kuogopa kwangu. Kusema hofu zangu. Kumenisaidia. Kwa haraka ninaonekana dhaifu. Maana wakati mwingine haitarajiwi kusema tunavyoshindwa. Watu wanatarajia kusikia tunavyoweza. Hata hivyo, nimeona faida. Sisemi ukaseme mabaya yako njia panda, yawasaidie hatawapita njia. Hapana. Najua nafasi ya marafiki wa karibu. Najua nafasi ya kusema hata yale yasiyopendeza kusema kwa walio karibu.

Lakini kujenga picha hadharani kuwa kila kitu kiko sawa wakati moyoni unaugua, hakutasaidia kwa muda mrefu.
Kuigiliza maisha fulani kwenye mitandao ya kijamii wakati unajua kabisa kihalisia, uko vingine, ni kujidanganya.

Tufike pahala tuweze kusema pande zote. Tusimulie kushindwa kwetu. Wanaotusikiliza watajifunza zaidi kuliko tunapoigiliza ukamilifu usiokuwepo.

Tafuta usalama wa nafsi. Hutalazimika kusema uongo ili kuwa salama. Kila la heri unapoushikilia ukweli bila kujali kama unakupendelea au la.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi