Adult attachment: Unaangukia kundi lipi katika haya manne?

ZIMEFANYIKA tafiti nyingi mno kuchunguza asili ya matatizo mengi ya kitabia tunayokabiliana nayo kama jamii.  Hapa tunazungumzia tabia katika upana wake kwa maana ya vipengele vyake vitatu: 1) ufahamu na imani zilizojengeka na kufungamana na akili zetu, 2) mitazamo na nia (attitude) zetu kuhusu masuala, watu, na kadhalika, na 3) matendo yetu yanayoonekana kwa wengine ambayo kimsingi hutekeleza  mawili ya mwanzo kwa maana kilichojengeka akilini na mitizamo uliyonayo.

Chukulia mfano wa tabia za ubaguzi wa kikabila, kidini au rangi. Tabia hii huanzia kwanza kabisa kwenye namna tunavyokuchukulia mambo kwa ujumla jumla na kuyahukumu kwa kutumia tunachokijua tayari kama short cut ya kuyaelewa mambo kwa wepesi (stereotype). Uelewa huu unakolezwa na imani ya jumla kuwa kundi unalokuwa wewe ni bora na linastahili mema kuliko makundi mengine. Mfano dini yangu ni bora kuliko za wengine, na hivyo kila muumini wa dini yangu anastahili mema. Ni mkakati tu wa kisaikolojia wa kukufanya ujisikie uko kwenye kundi sahihi, upate amani ya moyo.

Pili, imani hiyo hujenga mitazamo hasi kwa watu wa makundi mengine (prejudice) kwamba hawastahili haki ambayo watu wa kundi lako wanayo na/au wanastahili kuipata. Mfano Mkristo kuamini kuwa Mwislam amepotoka na Mwislam kuamini kuwa Mkristo amepotea na hivyo kuamua moyoni kuwapuuza kiimani watu wa upande wa pili japo dhamira hiyo yaweza isionekane wazi wazi. Hizi ni attitude hasi kwa watu wa makundi mengine, zenye nia ya kutufanya tujihakikishie usalama wa moyo.

Kisha mitazamo hiyo hasi kuweza kupanda ngazi na kuwa tabia inayoonekana, yaani matendo halisi yaliyotokana na 1) imani ya upendeleo na 2) mtazamo na nia ya kupendelea kundi lako. Katika hatua hii ndipo mtu huweza kuchukua hatua kabisa za kuwanyanyapaa watu wasio wa kundi lake kwa namna inayoonekana. Huu ndio ubaguzi wa kidini unaonekena wazi wazi. Discrimination. Hayo matatu yameunda tabia ya ubaguzi.

Kwa ufupi kabisa, kila tabia inatokana na namna tunavyofikiri kwa maana ya namna tunavyojichukulia sisi, tunavyowaona na kuhusiana na watu wengine na dhamira ya kutenda inayofuatiwa na matendo yanayoonekana. Nitarejea katika mjadala huu huko mbele ya safari.

Pamoja na ukweli kuwa kuna namna tofauti za kutafsiri matokeo ya tafiti nyingi zinazotafuta kujua chanzo hasa za tabia zetu, njema kwa mbaya, kwa vipengele tulivyovionyesha hapo juu, lakini jambo moja ni wazi. Kwamba matatizo mengi ya kitabia, yana historia ndefu katika namna tulivyojenga usalama wa nafsi zetu (socio-emotional security). Nitaeleza.

Tangu kuzaliwa, kama tulivyoona katika sehemu zilizopita, mwanadamu anahusishwa na mradi mmoja mkubwa na muhimu sana ambaoo yeye mwenyewe anaweza asiwe na habari kuwa unaendelea ndani ya fahamu zake. Mradi wenyewe ni kujenga hisia za usalama au kinyume chake. Na usalama huu, kama tulivyoona, unatokana na mfungamano wa kihisia kati ya mtoto na watu wengine hususani wazazi ambao tuliiuita attachment.

Ilivyo ni kwamba kutegemeana na unavyokuja kuwa, shauri ya mahusiano yako na caregivers, ndivyo unavyoweza ama kuwa salama (secure) au kujikuta katika mazingira ya kujiona uko kwenye hatari ya kisaikolojia (insecure). Security ndiyo msingi wa yote tuliyoanza kuyazungumza tangu mwanzo.

Kwa mfano. Tujiulize kwa nini jambo lile lile, mtu yule yule, au hali ile ile yaweza kumfanya mmoja akasirike kiasi cha kupigana, wakati mwingine achukulie hayo hayo kwa namna ya kawaida? Jibu ni tofauti ya namna wawili hao walivyo secure. Mtu mgomvi maana yake anaona threat ya usalama wake (heshima, hadhi) na hivyo katika kujisikia salama, anaamua kumuumiza mwingine, kwa maneno au vitendo ili ajisikie salama. Wakati asiye mgomvi, huoni threat ya usalama wake (ambao anao) na hivyo hana haja ya kumuuza mwingine ili ajisikie salama. Ndio kusema kuwa mtu secure haoni shida kushuhudia mema yakipata mtu mwingine, na kwa kweli husikitika mabaya yakitajwa kwa mtu.  Mtu mwenye insecurity zake hutamani mabaya yampate mtu mwingine na ikiwezakana, mema yamkwepe ili yote yawe yake peke yake na watu wake.

Katika kuelewa implication ya aina za attachment tulizoziona katika makala hii iliyopita, kwa ujumla tunaweza kujiuliza swali kuu lifuatalo: Je, tunaweza kubashiri tabia za baadae za watoto walio katika makundi hayo manne tuliyoyajadili? Jibu ni ndiyo. Zimefanyika tafiti za kuwafuatilia kwa makini watoto hawa kwa muda mrefu na kubaini tabia zao kadri umri unavyosonga.Hebu tuone.

Securely attached infants

Watoto hawa wamethibitika kuwa na uwezo mzuri wa kupenda wengine kwa sababu wanajikubali. Wako salama, na hawaoni tishio la kuwafanya wengine wajisikie vizuri. Katika umri wa shule, watoto hawa wameonekana kuwa na uwezo mzuri wa kujenga mahusiano na wenzao bila shida, kwa sababu hawana kiburi, hasira, visasi, wivu na tabia nyinginezo zenye kuumiza wengine. Hawana matatizo na kuheshimu mamlaka.

Umeshikwa, umeshika, au mmeshikana? Picha: Debra Kaplan
Wanapofikia umri wa kubalehe, ambao kwa kawaida mahusiano na wazazi na mamlaka hupitia kipindi kigumu kidogo, watoto hawa wameonekana kuendelea kuhusiana vyema na wazazi ikiwa mazingira ya malezi yataendelea kuzingatia mambo manne tuliyoyataja ambayo ni 1) sensitivity, kuelewa mahitaji kwa ufasaha na kuyajibu kwa wakati 2) upendo wa dhati usitolewa kama zawadi ya kuwa mwema 3) imani katika uwezo binafsi wa mtoto (kutokumbana mtoto/control kulikopita kiasi) na 4) kuendelea kwa quality time na wazazi wao. Kimsingi wana uwazi kwa wazazi wao, hawako desperate na kupendwa, wanajiamini pia, na hivyo si rahisi kutapeliwa kimapenzi.

Kwenye ndoa, watu wa kundi hili wanapenda bila ubinafsi, wanajitoa vya kutosha katika kuwafanya wapenzi wao wawe na furaha, hata ikibidi kwa gharama ya furaha yao. Wanajua kutatua migogoro inapojitokeza, wawajibikaji (proactive) wasiolaumu, hawana wivu wala tabia ya kuwa-manipulate wenzi wao. Wana uwezo mzuri wa kulea watoto kwa condition nne tulizozitaja. Kila mtu angetamani kuwa na mwenza wa kundi hili. Una bahati kama uko kundi hili na mwenza wako yuko humu.

Avoidant infants

Hawa kama ambavyo hawana mahusiano mazuri na wazazi hawawezi kuhusiana vizuri na wengine. Unakumbuka sababu? Tafiti zinaonyesha kuwa katika umri wa mpaka miaka 10, watoto hawa huwa na matizo ya hasira, ghadhabu, ugomvi na wenzao katika michezo. Hawana mahusiano mazuri na watoto wenzao, ni wachoyo, wabinafsi, wanalaumu kuliko wanavyowajibika na mara nyingine ni wakimya sana shauri ya woga na wasiwasi wa kinachoweza kutokea. Wanakwepa mahusiano na watu wengine shauri ya kutokuwaamini watu. Kanuni ya watu hawa ni 'dunia haina haki, usimwamini mtu, huwezi kujua litakalotokea'.

Katika kipindi cha bahele ni wagumu mno kupokea maelezo kwa wazazi ambao kwao, wanawakilisha mamlaka zisizotenda haki. Mamlaka zinazotesa na kunyanyasa watu. Kwa hiyo uwezekano wa kuasi ni mkubwa na hivyo ugomvi na wazazi si jambo la ajabu.

Katika mahusiano ya kimapenzi, ni vigumu sana kwao kujenga mahusiano ya kweli na watu. Ni waoga wa mahusiano na hata wakiwa nayo huwa hayadumu. They are too insecure kuwafanya waridhike. Too demanding na wana wivu uliozidi kiasi kwa sababu hawaamini kuwa mtu anaweza kumpenda mtu mwingine kwa uaminifu kwa sababu wao wenyewe hawana uwezo huo. Kabla ya kuoana na mtu wa jinsi hii, au ikiwa wewe mwenyewe ni wa kundi hili, fikiri mara mbili, na tafuta msaada wa kushungulia insecurities zenu kwanza. Maana hata anapooana na mtu secure, huleta mchanganyiko unaofanya maisha kuwa handaki.

Ambivalent infants 

Hawa ni wagomvi wakiwa na umri wa shule. Wana shida kubwa ya kutokujiamini na hawaamini uwezo wao binafsi, na ndio maana suluhu kwao ni kugombana kufidia utupu wanaojisikia ndani. Wanawaona wengine kuwa wenye uwezo kuliko wao hivyo ni wepesi kuwaamini wengine kuliko wanavyojiamini wao. Hisia za kutokutendewa haki au kudharaulika (kujihisi hisi) huwafanya wawe na kisasi. Hawana msamaha. Hukuza mambo. Hawana msimamo kimaamuzi. Wanatumia popular idea kuamua mambo yao. Na nyakati nyingine huwa wakosoaji sana kama mbinu ya kupambana na udhaifu wanaohisi wanao.

Katika mahusiano ya kimapenzi watu hawa wana aina ya mahusiano iitwayo pre-occupied attachment style. Wanaamini watu kupita kiasi kama mbinu ya kufidia udhaifu wanaouona kwenye maisha yao wenyewe. Hawa ndio wale watu wanaosemekana kupenda mpaka wanaboa. Wamepachikwa majina ya ving'ang'anizi maana wanakuwa kama watumwa wa mapenzi kwa jinsi wanavyojua kuwa obssessed. 

Wakati wa balehe, hawashikiki na hawaambiliki. Ni kama makinda ya ndege yenye njaa. Akitokea 'mpenzi feki' hawana muda wa kuchunguza. Ni wepesi sana kuchanganywa kimapenzi shauri ya pengo la mapenzi lilishindwa kujazwa na wazazi. Wana ukame wa mapenzi. Ni rahisi kutapeliwa na kuumizwa.

Shida yao kwenye mahusiano hawajiamini kwa hiyo ni wepesi kushuku kuachwa, na kwa kweli hawana amani na mahusiano yao. Wanahisi wanaweza kuachwa na hivyo wanatumia nguvu nyingi sana kulea mahusiano. Ukidhani watakufaa, usidanganyike. Hawa hawakupi muda wa kupumua sio kwa sababu wanakupenda sana (japo kweli wanaweza kuwa wanakupenda sana), bali ajenda kuu kuhakikisha huwaachi. Bahati mbaya ndio wahanga wakuu wa majanga ya kimapenzi.

Disorganised infants

Wakiwa shule, wanajiamini kiasi chake. Wanaamini wana uwezo fulani ndani mwao ambao hauonekani kwa wengine. Kwa hiyo kuna aina fulani ya kiburi hivi na majigambo ya hapa na pale. Tabu yao kubwa ni kupuuza au kudharau wengine. Kujiamini kupita kiasi huwafanya waweze kuwa wenyewe bila rafiki wa karibu na wasione shida. Wakimya fulani hivi ila ndani mwao wanajikweza sana.

Kwenye mahusiano, wanakuwa dismissing, kwa maana ya kuwa hawaoni haja kubwa ya kuhusiana na watu wengine. Hawana haja na urafiki. Ndio watu ambao ukitaka kujenga urafiki nae hana wepesi. Anakuona kama unamwingilia sana faragha yake, maisha yake. Si rahisi sana akawa rafiki yake wa karibu  kama hajaona faida yako kwake. Hana muda na mahusiano yasiyo na maslahi kwake. Yuko kwenye hatari ya kuumiza wengine katika mahusiano. Hana commitment na ameridhika.

Akiwa mzazi, hana tabia ya kujali sana mambo ya mapenzi, hana muda wa kufuatilia sana maendeleo ya watoto wake kihisia. Anadhani akitoa fedha na mahitaji ya kimwili, kama akikumbuka, basi imetosha. Ukizungumza lugha ya kuutoa moyo wako, muda wako, hisia zako kwa ajili ya mke/mume au watoto wake, haelewi unamaanisha nini. Anaweza kuona umuhimu wa kukaa na familia yake lakini kwa sababu za nje sio zinazotoka ndani. Artificial.

Hitimisho

Kwa kuhutimisha, tumeona kuwa attachment ya utotoni ni msingi wa kwanza, mahusiano yetu na nafsi zetu na kisha  mahusino na wengine. Attachment ya utotoni inayojengwa na mazingira ya malezi, ndiyo msingi wa tabia za utu uzimani kama tulivyoona kwa muhtasari.

Watafiti wameanza kuwa na mashaka na saikolojia ya temperament kwa maana ya aina za haiba anazozaliwa nazo mtu.  Hoja kuu ni kwamba, haiba haichangiwi pakubwa na genes (vinasaba) kama watu wengi walivyoaminishwa. Uthibitisho unaoendelea kupatikana kisayansi unaonyesha kuwa tabia zetu zinaathiriwa zaidi na aina ya malezi tunayoyapata tangu tukiwa watoto wachanga. Kila mmoja anaweza kuwa na haiba yoyote kulingana na aina ya malezi anayoyapata. Tabia zetu, kuanzia imani, mtazamo na vitendo hutokana na msingi uliojengwa tangu tukiwa wadogo.

Maana ya haya yote, ni kuwakumbusha wazazi nafasi waliyo nayo katika kuamua hatma ya maisha watakayoishi watoto wao baadae. Na ni bahati mbaya sana kuwa hata aina ya uzazi ambao watoto hawa watakuwa nao wakiwa wazazi baadae, nayo huchangiwa na aina malezi waliyoyapata wao wenyewe. Habari njema, pamoja na yote hayo ni kwamba bado unaweza kushughulikia insecurities zako ukishazibaini na hivyo ukafanya uamuzi sahihi wa kuwekeza kwenye malezi ya watoto wako kwa usahihi na ufanisi.

***makala haya yanaendelea kuhaririwa. Samahani kwa makosa ya hapa na pale.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia