Shukrani za pekee kwa Prof. Mbele kwa zawadi ya thamani!

'Africans and Americans Embracing Cultural Difference', ni kitabu kizuri nilichokisoma kwa mara ya kwanza Aprili, 2009 nilipokiona katika duka la vitabu KIMAHAMA, Arusha. Ilikuwa ni baada ya kukisikia kikisemwa na rafiki yangu mmoja. Ni miaka mitano imepita, lakini kitabu hiki hakikuwahi kuizoea maktaba yangu tangu wakati huo.
Kusoma kitabu chenye saini ya mwandishi, si jambo linalowatokea wengi. Ni muujiza ulionitokea. Picha: Jielewe

Kwanza, kwa rafiki zangu wasomaji waliofika kwangu kwa mazungumzo ya vitabu na waandishi, kitabu hiki hakikukosekana kwenye mazungumzo hayo. Na kila aliyesikia sifa zake, alipenda kuthibitisha ikiwa nilisema  kweli kwa kukiazima. Kiliazimwa na wasomi, wasafiri, waongozaji wa watalii (tour guide), wapenda maarifa, kutaja kwa uchache.

Ni bahati mbaya sana kwamba hakikuwa kinapatikana katika baadhi ya maeneo. Hivyo, kiliazimwa, na kuazimwa, tena na tena kwa muda wa miaka miwili. Mwaka 2011, kiliondoka rasmi kwenye maktaba yangu.

Nilikuja kugundua baadae kuwa aliyekiazima, naye alikiazimisha kwa mwingine, ambaye naye alikiazimisha na hatimaye hakijulikani kilipo na wala sina wa kumdai. Mie huamini kitabu hakiwezi kuibwa, kitabu husomwa. Nina hakika kinasomwa na nisiyemjua.

Namshukuru kwa dhati, mwandishi wa kitabu hiki, Prof. Mbele kwa kunitumia kitabu hiki bila malipo, tena kwa gharama zake. Si jambo linalowatokea wengi. Ni furaha iliyoje hatimaye nimekipokea leo asubuhi. Naanza kukisoma kitabu hiki kwa mara nyingine, safari hii kikiwa na saini ya mwandishi! Ni upendeleo na muujiza wa pekee kunitokea katika siku za hivi karibuni. Ni lazima nimshukuru kwa dhati. Asante sana Profesa.

Wakati mie ndio kwanza naanza kukisoma kwa mara nyingine, ningependa kukushauri, kama hujapata kukisoma kitabu hiki, fanya hima ukitafute, na ukisome. Kitakusaidia kuelewa mambo ya msingi yanayohusu tofauti za kiutamaduni kati ya Marekani na Afrika na changamoto za miingiliano hiyo ya kiutamaduni. Ni jungu kuu lililosheheni elimu kwa lugha nyepesi na yenye mvuto tena kwenye karatasi zisizozidi 101.

Maoni

  1. Kaka bwana....ni kwrli ni kitabu kizuri pia nimekisoma pamoja na Matengo Folktales kama hujasoma soma au nunua

    JibuFuta
  2. Yasinta...mzima? Ni kweli kabisa. Matengo Folktales ninacho. Ni hazina kubwa.

    JibuFuta
  3. Ndugu Bwaya, ulipoongelea waongozaji wa watalii, yaani "tour guides," umenikumbusha "tour guides" wa "Cultural Tourism Program" pale Mto wa Mbu na wale wa J.M. Tours (Arusha) ambao waliniambia kuwa wanakipenda kitabu hiki kwa kuwarahisishia mahusiano yao na watalii wa Ulaya na Marekani.

    JibuFuta
  4. Dada Yasinta, shukrani kwa ujumbe wako. Samahani nilipitiwa, ningejibu mapema zaidi. Nafurahi kuwa vitabu vyangu vimekuridhisha kiasi hicho. Mungu akinijalia uzima na afya, nitaendelea kuandika na kuchapisha vingine.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia