Namna ya kuifanya huduma ya 'day care' imfae mwanao

TULIJADILI kwa kifupi sana hitaji la huduma ya malezi yasiyo ya mama (non-maternal child care). Anzia hapa kama hukuisoma. Tulisema, sababu kubwa ni kwamba akina mama wa kileo wanatafuta kipato nje ya nyumba, hali inayosababisha changamoto ya kimalezi. Tuliona pia kwamba katika jamii yetu, huduma isiyorasmi ya malezi ndiyo inayotumika zaidi. Changamoto yake kubwa kuliko zote ni ukweli kuwa akina dada hawa wengi hawana uelewa wa kutosha wa malezi. Ni kweli kuwa hata akina mama wengi hawana uelewa huo unaoitwa wa kutosha. Lakini angalau, tunafahamu kuwa mama anaweza kujibiisha kuhangaika na mahitaji ya mtoto kuliko house girl, ambaye wakati mwingine hata hatumjui vizuri, yeye mwenyewe, wala familia yake, wala undani wa tabia yake.

Shauri ya changamoto hizo, pamoja na nyinginezo, familia zenye uwezo kidogo zinachagua kutumia huduma za malezi rasmi ya watoto. Day care. Mtoto mara nyingine wa miezi kadhaa hadi wa umri wa kuanza shule, hupelekwa kwenye vituo vinavyotambulika ili alelewe kwa muda ambao mama atakuwa kazini. Tofauti na huduma zisizo rasmi za malezi, huduma hii inatumia watu wenye ujuzi wa malezi ya watoto, waliofunzwa namna bora ya kumhudumia mtoto kulingana na umri wake. Vile vile, mtoto hulelewa kimakundi, kwa maana ya kulelewa akiwa na wenzake wa umri wake na mara nyingine wa umri tofauti na wake.

Aina ya huduma rasmi za malezi ya mtoto
Huduma za day care, kama tulivyogusia kwenye makala iliyopita, zinatofautiana kulingana na umri wa mtoto. Katika umri wa kuanzia mtoto anapozaliwa mpaka miaka miwili, huduma kuu huwa ni sawa na ile inayotolewa na mama. Yaani kukutana na mahitaji ya msingi ya mtoto kihisia, kimahusiano, kimwili na kiakili. Hakuna msisitizo wa mtaala wa elimu. Kisha kuanzia miaka 2 au mitatu, walezi huanza kudokeza kidogo mambo ya elimu kumkuza mtoto kiufahamu.


Watoto wakifurahia michezo, Arusha . Picha: soschildrenvillages.org.uk
Na baadae, miaka minne hadi sita, vituo hivi huanza kufahamika kama shule, kwa maana ya kwamba pamoja na kukutana na mahitaji ya msingi ya mtoto, lengo kuu linakuwa elimu. Kumwandaa mtoto na elimu ya msingi. Kwa hiyo watoa huduma huwa ni walimu. Kuanzia miaka sita na kuendelea, malezi yanaweza kufanyika kwa mtindo wa mtoto kulala shuleni kabisa, mbali na nyumbani, akilelewa na walimu na kufundishwa.

Huduma hizi hazikuwa maarufu sana siku za nyuma, lakini kwa sasa zimeanza kupatikana. Jijini Dar es Salaam, kwa mfano, vituo hivi vya aina zote hizo tulizozitaja vipo katika maeneo mengi. Miji mingine kama Arusha na Moshi, huduma hizi zinapatikana, na wazazi wanazitumia. Kwa miji kama Arusha na Moshi, shule za msingi za kulala, ni maarufu sana. Watoto wanaanza darasa la kwanza wakiwa 'boarding'. Lengo? Well, kwa wazazi wengi ni kumpa mtoto elimu bora. Kwa upande mwingine, ni kuwapa wazazi nafasi ya kujikita na kazi zao kwa bidii zaidi.

Watafiti wa ukuaji wa mtoto wamekuwa na wasiwasi na huduma hizi kwa muda mrefu. Zimefanyika tafiti kwa mamia, kujaribu kuchunguza uwezekano wa madhara, kama upo, wa huduma hizi. Moja  wapo ya taasisi zilizofanya kazi hii kwa kina ni Taasisi ya Taifa ya Mtandao wa Afya ya Mtoto na Maendeleo ya ya Utafiti wa Malezi ya Watoto (NICHD) ya Marekani. Maswali makuu yaliyoulizwa na watafiti wengi wa huduma hizi ni 1) Je, kuna uhusiano wowote wa huduma za day care na mahusiano ya kihisia kati ya mama na mtoto (emotional attachment).
2) Je, kuna uhusiano wowote kati ya huduma hizi na uwezo wa kiakili wa mtoto? 3) Je, kuna uhusiano wowote kati ya wingi wa masaa anayokaa mtoto kituoni na mahusiano ya kihisia kati ya mama na mtoto? 4) Je, ubora wa huduma zinazotolewa na kituo unaweza kusaidia kuboresha mahusiano hayo ya kihisia kati ya mtoto na mama? Kwa mwendo wa pole, tuangalie kipengele kimoja baada ya kingine.

Uhusiano wa huduma hizi na emotional attachment
Watafiti karibu wote, isipokuwa wachache, wanakubaliana kuwa huduma za malezi kituo kwa kiasi fulani zinaathiri mahusiano ya mama na mtoto. Watoto hawa wanakuwa insecure. Utakumbuka tulishajadili uhusiano uliopo kati ya emotional attachment na tabia za mtoto mbeleni. Ingawa wapo watoto ambao hawaonekani kuathirika na huduma hizi, lakini namba kubwa ya wanufaika wa huduma hizi walionekana kuathirika.

Mfano, imeonekana kuwa watoto wanaopata huduma hizi wanakuwa kwenye hatari ya kuwa wabishi, hasira, wagomvi, na hawawi rafiki sana na mama. Ingawa, pia inaonekana watoto hawa wanafanya vizuri kwa upande wa kuhusiana na watoto wenzao, bado mbeleni, wanakuwa na matatizo ya hapa na pale ikiwamo ubinafsi.

Uhusiano wa huduma hizi na uwezo wa kiakili wa mtoto
Habari njema ni kwamba imethibitika pasipo shaka kuwa huduma hizi, zinapofanywa na  walezi wenye kujituma na utaalamu, ukuaji wa watoto hawa kiakili unakuwa mkubwa kuliko wenzao wasiohudhuria malezi haya. Mfano, kuanza kujua kuhesabu kabla ya wakati, kuwa na uelewa na mambo mapema na kadhalika. Wapo wanaosema, uelewa huu wa mapema si faida sana, kwa sababu hata watoto waliochelewa kuchangamka kiakili, huwakuta mapema tu wanapokuwa shuleni.

Wingi wa masaa ya kukaa kituoni una madhara?
Kuhusu wingi wa masaa anayoyatumia mtoto kituoni, imethibitika kwamba masaa yanayozidi 20 kwa juma, yanaweza kumwathiri zaidi mtoto. Sababu ni kwamba mama anapokosekana kwa zaidi ya masaa matano kwa siku, mtoto hujisikia kupuuzwa na kuachwa (neglegence) na hivyo kupunguza imani na mama yake. Tatizo jingine linalojitokeza ni mama anaporudi nyumbani, hali akijua kabisa kwamba mtoto amemkosa mchana kutwa, huweza kujikuta akimbana sana (overcontrol) na hivyo kupunguza uwezo wa mtoto kujitegemea na kujiamini. Upungufu wa masaa, unapunguza athari za kihisia anazozipata mtoto kwa kuwa kituoni.

Ubora wa huduma unaboresha mahusiano ya mama na mtoto?
Habari njema kwa wazazi wanaotumia huduma hii ni kwamba, imethibitika pasipo shaka kwamba ubora wa huduma, huondoa kwa kiasi kikubwa madhara ya huduma hii. Ubora una maana kuu nne: 
1) Uwiano mzuri kati ya walezi na watoto.
Kwa mtoto mwenye miezi 6 hadi mwaka 1½ uwiano wapaswa kuwa watoto angalau watatu kwa mlezi mmoja, mwaka 1½ mpaka 2 uwiano uwe watoto wanne au watano kwa mlezi mmoja, na kwa miaka 2 mpaka 3, uwiano unaweza kuwa watoto saba kwa mlezi mmoja. Ikiwa mzazi atalazimika kumpeleka mtoto mwenye umri usiofika miezi sita, Wills & Ricciuti wanashauri kila mtoto awe na mlezi wake.
2) Ukubwa wa makundi ya watoto unaokubalika. 
Kwa mtoto mwenye  miezi 6 hadi mwaka 1½ yapaswa kuwa watoto sita kwa kundi mmoja, kwa maana ya walezi wawili. Mwaka 1½ mpaka 2, watoto nane kwa kundi, kwa maana ya walezi wawili. Na kadhalika.
3) Mafunzo kwa walezi. 
Lazima walezi wawe wamejifunza makuzi na mahitaji ya mtoto ili kuweza kujua namna ya kuitikia mahitaji ya mtoto kwa wakati (sensitivity) na kuelewa kwa usahihi namna ya kuwasiliana na kuhusiana na mtoto. 
4) Mazingira ya malezi yawe rafiki kwa mtoto. 
Vifaa vya kuchezea vinavyokuza uelewa kwa kulingana na umri, michezo inayoendana na umri, chakula kinachofaa, na kadhalika.

Yanapokuwepo hayo manne, ukichanganya na uelewa na uwajibikaji wa mama mwenyewe, tunaambiwa, ni wazi kuwa hapatakuwa na matatizo tuliyoyaona hapo juu.


Namna gani huduma ya day care inaweza kumfaa mwanao?
Hakikisha kuwa kituo kina ubora unaotakiwa. Mambo manne makuu tuliyoyaona hapo juu yawepo. Sasa, ilivyo ni kwamba kadri kituo kinavyozidi kuwa bora, kwa maana ya kutimiza vigezo hivyo hapo juu, ndivyo gharama zake zinavyozidi kuwa juu. Hiyo ni kusema kwamba, hata kama inawezekana kituo kisifike viwango hivyo, jaribu kuchunguza kuona kama angalau kuna ubora unaokaribia huo.
Mlezi akitoa huduma zenye ubora FUN 'N'LEARN, DSM. Picha: bongopedia.com
Nimetembelea vituo kadhaa hapa nchini. Na ukweli ni vipo vituo vyenye ubora wa kuridhisha. Lakini pia vipi vituo ambavyo kwamba ubora wake unatia shaka. Mlezi mmoja, asiye na mafunzo ya maana, anaweza kuhudumia watoto wengi wenye umri mdogo kuliko anavyoweza kuwamudu. Matokeo yake, watoto wanakosa mtu wa kuwasikiliza na kujibu mahitaji yao. Mazingira ya malezi pia yanaweza kuwa ya wasiwasi, na hivyo kuhatarisha afya ya mtoto.

Pili, punguza muda wa mtoto kukaa kituoni. Tumeona kuwa kadri mtoto anavyokaa kituoni muda mwingi, ndivyo anavyopata athari kihisia na kimahusiano. Kwa mtoto mwenye umri wa mpaka miaka 3, ni vyema kuangalia namna anavyoweza kukaa muda mfupi iwezekanavyo. Hapa kuna mambo ya sera za kazi kuwa rafiki na malezi. Kwa nini mama asipewe ruhusa ya miaka miwili abaki nyumbani kulea mtoto? Denmark wana utaratibu huo. Mwaka mzima mama anaruhusiwa kubaki nyumbani kulea mtoto! Kama tunaweza kumpa mfanyakazi ruhusa ya kwenda masomoni kwa miaka mitatu, minne kadhalika, kwa lengo la kutafuta elimu, tunashindwaje kuweka mazingira rafiki kwa mama angalau basi ahudhurie nusu siku kazini kwa muda wa miaka mitatu?


Tatu, mama mwenyewe anawajibika kujifunza namna ya kuhusiana na mtoto kwa upendo, kila anapopata muda. Ni kazi bure kutafuta malezi ya kituo yaliyo bora wakati mama mwenyewe halichukulii kwa uzito suala la malezi. Unafanya nini unapokutana na mwanao baada ya kazi? Unampa muda wako wa kutosha? Una matatizo gani ya kihisia yanayoweza kumwathiri mwanao? Tafuta msaada. Ukiwa na frustration zako, ni rahisi sana kuzihamishia kwa mtoto, na ukaongeza matatizo.

Je, tunalo tumaini katikati ya changamoto?

Ndiyo. Lipo tumaini. Tunaweza, tena kwa ujasiri, kusema kwamba huduma hizi za malezi nje ya nyumba zetu, ukiacha shule za kulaza watoto shule, zinaweza kufaa zaidi ukilinganisha na malezi ya akina dada wa kazi, ikiwa zitatolewa katika ubora unaotakikana. Hakuna haja ya kuogopa. Maana inaeleweka pia kuwa wapo akina mama wa nyumbani wanaokaa na watoto wao muda wote nyumbani na hawawatendei haki watoto wao. Je, malezi ya mama wa nyumbani yasiyo na viwango, yanaweza kufananishwa na malezi ya kituoni yasiyo na ubora? 
Akina dada wa kazi, nao tunaweza kuwajengea uwezo wa kuwalea watoto wetu vyema. Hilo linawezekana kama tutawapa mafunzo yasiyo rasmi na yale rasmi ya namna ya kuwasiliana na watoto wetu vizuri. Tunahitaji watu wanaoweza kuanza kutoa huduma hizi kwa jamii. Kuwafunza akina dada hawa A Be Che za malezi. Yatasaidia. 
Vile vile, tunahitaji sera za kazi zinazowezesha akina mama kutimiza wajibu wao kwa watoto wao. Kuna ubaya gani kutoa likizo ya angalau miaka miwili kwa mama, ili aweze kuwekeza vya kutosha katika kukuza kizazi kujacho? Wakati sera hizo hazijaja, je, yupo mama anayeweza kuchagua kumlea mwanae kwa muda wa kutosha, kwa gharama ya kuacha kazi yake? 

 Shule za awali/msingi za boarding?

Kwa kweli, pamoja na kwamba wazazi wengi hupeleka watoto wao kwenye shule za msingi za kulala, wakiamini wanafanya hivyo kwa faida ya mtoto, tafiti nyingi zimeonyesha kinyume chake. Watoto wanaohamishwa nyumbani na kuanza maisha mengine nje ya familia zao, na kulelewa kimakundi shuleni wanaathirika sana kihisia. Katika umri huu, ndio kwanza, mtoto anahitaji kujengewa misingi imara ya tunu, maadili, imani na wazazi wenyewe. 

Kumpeleka mtoto wa miaka sita, saba mpaka kumi na tatu boarding, ni kumwonea. Huko hakuna atakayekabiliana na matatizo ya kibinafsi ya mtoto. Huko mtoto anakutana na marafiki wengine mapema zaidi na juu ya uwezo wake. Huko mtoto anajifunza values na tabia zinazomzidi yeye, na anakuwa hana base/msingi wa kulinganisha nao. Kwa maana nyingine, the child is socialized too soon! Matokeo yake, nafasi ya wazazi, baba na mama, kwenye maisha ya mtoto inapotea. Mbaya sana. Lakini kwa kuwa siku hizi fedha na tulivyo navyo vinatupa fursa ya kufanya tupendavyo, hakuna wa kutusaidia. Tunasomesha watoto wadogo shule za kulala. Uchaguzi ni wako. Chagua.

Kwa habari zaidi kuhusu vituo vya kulelea watoto jijini Arusha tembelea tovuti hii na jijini Dar es salaam, tembelea tovuti hii.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?