Kukosa Ajira Kusikufanye Ukose Kazi
Inakadiriwa
kuwa kati ya watu 800,000 na 1,000,000 hapa nchini wanaingia kwenye soko la
ajira kila mwaka. Hawa ni vijana wanaomaliza masomo yao kwa ngazi mbambali za
elimu au wale wanaokosa nafasi ya kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa
elimu.
Mfumo
wetu wa elimu unachuja wanafunzi kwa kuangalia sifa za ufaulu wa mitihani. Ili
mwanafunzi aweze kuendelea na masomo kwa ngazi inayofuata, analazimika kupata
sifa mahsusi. Anapopungukiwa sifa hizo, hulazimika kurudi mtaani kutafuta namna
anavyoweza kuendesha maisha yake.
Bahati
mbaya kwa kundi hili kubwa linalochunjwa ni kwamba ajira nyingi rasmi
zimeendelea kutumia elimu kama kigezo muhimu. Mwajiri anapotangaza nafasi za
kazi kitu cha kwanza anachokiulizia ni cheti. Hata kwa kazi za ufundi
zisizohitaji taaluma kubwa, bado mwombaji anaweza hulazimika kuwa na sifa
fulani za kitaaluma ambazo wakati mwingine hazisaidii kuboresha kazi.
Hali si
tofauti sana kwa wale wateule wachache wanaobahatika kuhitimu ujuzi rasmi
unaotambuliwa na vyeti. Uwezo wa uchumi wetu kutengeneza nafasi mpya za ajira
zitakazokidhi mahitaji ya vijana hawa bado ni mdogo. Serikali ambayo ndiye
mwajiri mkuu, kwa mfano, haijaweza kuajiri kwa miaka miwili. Pia, tunaambiwa
biashara nyingi katika sekta binafsi zinafungwa.
Katika
mazingira kama haya, ni dhahiri tatizo la ukosefu wa ajira litaendelea
kuwaathiri watafuta ajira wengi hapa nchini bila kujali ikiwa wanao ujuzi rasmi
ama la.
Makala
haya yanalenga kuwasaidia watu ambao, kwa sababu moja au nyingine, wanatafuta
ajira na bado hawajafanikiwa kuzipata. Tunaangazia jitihada kadhaa wanazoweza
kuzitafanya kutatua tatizo badala ya kusubiri ‘mfumo’ uwatafutie majibu. Swali
kuu litakalotuongoza ni, unapokosa ajira maana yake ni nini?
Nafasi za ajira hazitoshi
Tuanze na
dhana ya soko la ajira. Soko ni utaratibu wa kuuza na kununua. Mwajiri
anapotafuta mtu mwenye ujuzi wa kumsaidia kutoa huduma zake, ni mnunuzi.
Mwajiriwa anayetafuta mtu wa kununua ujuzi wake, anakuwa muuzaji sokoni. Hawa
wawili wanategemeana. Mmoja anazo raslimali, aghalabu za fedha, kumwezesha
kununua ujuzi na mwingine anao ujuzi anaofikiri unahitajika.
Kwa
bahati mbaya, uhusiano huu kati ya muuzaji na mnunuzi wa ujuzi una ukomo wake.
Kama tulivyotangulia kuona, uwezo wa waajiri kutengeneza nafasi za ajira hautoshelezi
mahitaji halisi sokoni. Hali hii husababisha ushindani mkali ambao mara zote huliathiri
kundi kubwa litakaloachwa bila ajira.
Waathirika
wakubwa kwenye ushindani huu mkali wa soko, ni watu wanaoamini hawawezi kuishi
bila kuuza ujuzi wao kwa waajiri. Suluhisho ni kubadili mtazamo. Badala ya
kufikiri namna ya kuuza ujuzi wako kupitia ajira, jaribu kufikiri namna ya
kuutumia ujuzi wako kufanya kazi itakayosaidia kuendesha maisha yako.
Kutokuajirika kwa watafuta kazi
Upande wa
pili wa mjadala wa ukosefu wa ajira ni ukosefu wa sifa miongoni mwa watafuta
kazi. Madai ya waajiri wengi ni kwamba watafuta kazi wengi hawakidhi vigezo vya
kazi. Kwa mfano, zipo nafasi zinazotangazwa mara kadhaa, na usaili unabaini
hakuna mwenye sifa kati ya walioomba.
Wakati
mwingine baadhi ya waajiri hulazimika kutafuta watu kutoka nje ya nchi kujaza
nafasi ambazo zimeshindikana kuzajwa na kundi kubwa la watafuta kazi wanaodaiwa
kukosa sifa.
Suluhisho
la kutokuajirika, ni watafuta kazi kufanya jitihada za kukuza ujuzi badala ya
kufikiria ubora wa vyeti na ufaulu wa darasani. Upo ukweli kwamba vyuo vyetu vinazalisha
wahitimu wenye nadharia zisizo na uhusiano wa moja kwa moja na ufumbuzi wa
matatizo yanayoikabili jamii yetu.
Huu ni
ushauri kwa wanafunzi. Badala ya kufikiria kupata alama za juu kwenye mitihani,
ipo haja ya kuanza kufikiri namna gani utaweza kutumia maarifa hayo unayojifunza
darasani. Ukiweka kuweka bidii kwenye ujuzi badala ya maarifa, utajiweka kwenye
nafasi nzuri ya kufanya kazi bila kulazimika kutafuta ajira.
Fursa za kazi haziishi
Kila tatizo
linaloikabili jamii yetu ni fursa ya kazi. Ukiweza kuwa na ujuzi unaokusaidia
kutatua tatizo fulani unaloliona kwenye jamii, unajiweka kwenye nafasi ya
kupata kazi.
Bahati mbaya
ni kwamba jamii yetu inakabiliwa na kila aina ya matatizo yanayoendelea
kuzalishwa kila uchao. Matatizo haya ni fursa za kazi zisizo na kikomo kwa kila
anayetafuta kazi.
Changamoto,
hata hivyo, ni uwezo wa kutazama namna unavyoweza kutumia ujuzi ulionao kutatua
matatizo. Fanya ujasiriamali wa ujuzi kama umebahatika kupata ujuzi rasmi.
Endesha semina kwa jamii kuwasaidia watu kupata majibu ya changamoto
walizonazo. Hiyo ni kazi ambayo hakuna mtu anaweza kukunyima.
Pia
unaweza kutoa huduma zinazohitajika na watu wanaokuzunguka. Fikiria, kwa mfano,
mtu aliyeanzisha wazo la vyoo vya kulipia mjini. Alitazama tatizo, akaona
fursa. Huo ndio unaitwa ujasiriamali na inaweza kuwa njia ya uhakika kuelekea
kwenye mafanikio makubwa kuliko kutafuta ajira.
Kisingizio
cha vijana wengi ni mtaji. Ukweli, hata hivyo, ni kwamba fedha hufuata mtaji wa
wazo na sio kinyume chake. Ukiwa na wazo linaloeleweka, wenye mtaji wa fedha watakuunga mkono.
Tumia vipawa ulivyonavyo
Kila
binadamu amewekewa vitu vya pekee ndani yake. Hata kama hujafahamu kipaji ulichojaliwa
na Mwenyezi Mungu, hiyo haiondoi ukweli kwamba ndani yako umebeba raslimali
muhimu ya mafanikio yako.
Kiwango
cha elimu ulichonacho hakiamui kiwango cha mafanikio utakayoyapata. Elimu isiyokwenda
sambamba na kukuza vipaji ambavyo tayari unavyo, inaweza kuishia kutukatisha
tamaa.
Aidha, soko
la ajira linapokuamulia mwelekeo wa kazi unayopaswa kuifanya, tatizo la ajira haliwezi kukoma. Mahitaji ya
soko yakibadilika, watu wanajikuta hawana kazi. Kuna umuhimu elimu ijenge
kwenye msingi wa vipaji vya watu ili kutatua tatizo la ukosefu wa ajira.
Ushauri kwako
uliye kijana. Ukiweza kuvibaini vipaji ulivyonavyo, ukaelekeza nguvu zako
kuvitumia, hutakosa kazi hata katika mazingira ambayo nchi inakabiliwa na
ukosefu mkubwa wa ajira. Kazi yako inaishi ndani yako. Usiitafute nje.
Sina zla zaidi Bali niseme asante
JibuFutaSina zla zaidi Bali niseme asante
JibuFutaAsante sir bwaya
JibuFutaAsante Stephen Mligo na Richmal Vibes kwa kuwa wadau muhimu wa blogu yetu. Proud of you!
JibuFutaTunashukuru sana Sir Bwaya
JibuFuta