Madhara ya Kumpeleka Mtoto Shule ya Bweni

PICHA: Daily Maverick


Moja wapo ya sababu nyingi zinazowasukuma wazazi kuwapeleka watoto wadogo kusoma shule za bweni ni mafanikio ya taaluma. Mazingira ya shule yanaaminiwa kuwa bora zaidi katika kuwasaidia watoto kufanya vizuri zaidi kuliko wanapokuwa nyumbani.

Pia, imekuwa ikiaminika kwamba anapopata uzoefu wa maisha ya bweni anakuwa kwenye nafasi ya kujifunza stadi za maisha vizuri zaidi kuliko anapoishi na familia yake.

Hata hivyo, wanaopinga shule hizi kwa watoto wanadai pamoja na ufaulu, watoto wanaoishi bweni wanakuwa kwenye hatari ya kujifunza tabia mbovu zinazoweza kuathiri maisha yao ya baadae.

Ili kuondoa mkanganyiko huo wa kimtazamo, katika utafiti wangu, niliwalinganisha watoto wanaosoma shule za bweni na wale wanaosoma kwa kutumia utaratibu wa kurudi nyumbani baada ya saa za masomo. Maeneo matatu yaliyotumika kuwalinganisha watoto yalikuwa ni uwezo wa kitaaluma katika hesabu na lugha; uwezo wa kushiriki kazi za mikono; na uwezo wa kuhusiana na watu wanaowazunguka.

Watoto walioshiriki utafiti huu ilikuwa ni sharti watoke kwenye shule ile ile. Kila shule iliyoshiriki ilikuwa ni lazima iwe na makundi mawili ya watoto. Kundi la kwanza ni wale wanaokaa bweni na kundi la pili ni wale wanaorudi nyumbani baada ya saa za masomo.

Pia, ilikuwa ni lazima watoto wote wawe na umri wa miaka sita na saba wanaosoma darasa la kwanza na pili, mtawalia. Watoto walioshiriki utafiti huu walikuwa na wazazi wote wawili.

Uwezo wa kitaaluma

Matokeo yalionesha kwamba watoto wa bweni walikuwa bora zaidi ya watoto wa kutwa kitaaluma. Tofauti hiyo, hata hivyo, haikuonekana kuwa kubwa kwa watoto wa darasa la pili.

Wataalam wa elimu wanatuambia kwamba mazingira ya kujifunzia yanachangia kuchochea mafanikio ya mtoto kimasomo. Shule za bweni zilizokuwa na watoto wanaofanya vizuri zaidi, kwa mfano, ziliwawekea watoto ratiba inayoeleweka inayowalazimisha kusoma kuliko walivyofanya wazazi wa watoto wa kutwa. Wakati mtoto aliyerudi nyumbani baada ya masomo hakupata msaada wa kukamilisha kazi za shule jioni, mwenzake wa bweni alikuwa na mwalimu wa kumfuatilia kwa karibu hata baada ya saa za masomo. Tofauti ya ufuatiliaji inaonekana kuchangia kuwatofautisha watoto wa bweni na wale wanaorudi nyumbani.

Jambo la kujiuliza, hata hivyo, ni kama kuna ulazima wowote wa kumpeleka mtoto bweni ili akafaulu masomo. Je, mzazi hawezi kuweka mazingira rafiki yatakayomwezesha mtoto kujifunza akiwa nyumbani? Hakuna majibu ya moja kwa moja kwa sababu hilo linategemea mtazamo na uelewa wa mzazi. Mzazi akiweza kuweka mazingira ya kitaaluma nyumbani, ni wazi mtoto anayerudi nyumbani anaweza kufaulu kama mwenzake anayeishi bweni.

Suala la pili la kujiuliza ni kama mafanikio ya kitaaluma yanatosha kuwa kipimo cha ukuaji wa jumla ya mtoto.  Je, ufaulu usioambatana na tabia njema na stadi za maisha unamsaidia mtoto? Je, kuna sababu ya kusisitiza taaluma kupita kiasi hata kama kwa kufanya hivyo tunadumaza maeneo mengine ya kimakuzi?

Stadi za maisha

Kinyume na imani ya wengi wetu, watoto wa kutwa waliwazidi wenzao wa bweni katika uwezo wa kujimudu na stadi za maisha. Kwa mfano, watoto wa kutwa walikuwa na uwezo mzuri zaidi wa kufua nguo nyepesi, kuoga, kupiga mswaki, kujitawadha baada ya kujisaidia kuliko wenzao wa bweni.

Pia, wengi wao walishiriki shughuli ndogo ndogo kama kuosha vyombo, kumwagilia bustani, kufagia, kusafisha vyoo kutaja kwa uchache.

Mazingira ya malezi katika shule za bweni yalisisitiza taaluma kuliko stadi nyingine za maisha. Shughuli karibu zote za mikono zilifanywa na watu maalum. Ingawa lengo linaonekana ni kuwafanya watoto waelekeze juhudi zaidi kwenye taaluma ili kukidhi matarajio ya wazazi, kwa kiasi kikubwa, matokeo yake yalikuwa ni kudumaza uwezo wa watoto kujitegemea na kujifunza stadi za maisha.

Swali la kujiuliza, mtoto anayekulia kwenye mazingira kama haya yanayomjenga kuamini kuwa watu wengine ndio wenye wajibu wa kufanya kazi kwa niaba yake, atakuwa raia bora baadae?

Niliongea na Fransisca Mushi (sio jina lake halisi) mwanafunzi wa Chuo Kikuu aliyesoma shule ya bweni tangu akiwa darasa la tatu. Aliniambia: “Kazi za kufua na kuosha vyombo nitaajiri watu wa kunisaidia kuzifanya. Hiyo sio kazi ya muhimu kwa mwanamke.” Hata hivyo, jamii inatarajia mwanamke aliyefunzwa vyema afanye kazi hizo. Ikiwa Fransisca atashikilia mtazamo wake huo ni dhahiri anaweza kupata changamoto atakapoingia kwenye ndoa.

Uhusiano mzuri na watu

Eneo la tatu nililochunguza ni mahusiano ya mtoto na watu wanaomzunguka. Kwa kawaida, ili uweze kuishi vizuri na watu ni lazima ujiamini na uwaamini wengine, ushirikiane nao, kutaja kwa uchache.

Matokeo ya utafiti yalionesha kwamba watoto wa bweni walikuwa na matatizo mengi ya kitabia kuliko wenzao wa kutwa. Kwa mfano, tabia kama vile upweke, kukosa nidhamu kwa wakubwa, uongo na hasira zilionekana zaidi kwa watoto wa bweni. Mlezi mmoja alinipa uzoefu wake: “[Watoto] hawa wa bweni wanasumbua sana. Wengi wana kiburi na ni wagomvi. Sio wote lakini kweli ni wasumbufu.”

Familia ni eneo muhimu kwa mtoto anayeendelea kukua. Mazingira yanayomweka mbali na watu wake wa karibu yanaweza kumfanya akajisikia kutelekezwa. Usumbufu huu tuliouona kwa watoto unaweza kuwa matokeo ya kukosa ukaribu na watu anaowaamini.

Aidha, umbali na familia ulichangia kuwafanya watoto wa bweni wawaamini watu wengine zaidi kuliko wazazi wao. Kwa mtoto wa bweni, mtu wa muhimu zaidi alikuwa ni mwalimu, mlezi na rafiki anayemtetea. Maana yake ni kwamba kukaa mbali na wazazi kulilegeza imani ya watoto kwa wazazi wao.

Ushauri kwa wazazi

Kama tulivyotangulia kuona, wakati mwingine familia huwa na changamoto kubwa zaidi kuliko mazingira ya bweni. Uangalizi hafifu, migogoro baina ya wanafamilia, unyanyasaji na udhalilishaji ni baadhi ya sababu zinazoweza kufanya shule ya bweni iwe uamuzi nafuu zaidi. Katika mazingira kama hayo, ni vyema kujiridhisha na ubora wa huduma zinazotolewa shuleni wakati wa kufanya maamuzi. Ubora wa walezi, utaratibu wa malazi, fursa za michezo, mawasiliano ya mara kwa mara na mtoto ni mambo ya kuzingatia.

Hata hivyo, familia bado ni eneo bora zaidi la kimalezi. Kadri inavyowezekana, wazazi wajitahidi kutatua changamoto zilizopo na kuboresha mazingira ya kujifunzia nyumbani ili mtoto mwenye umri pungufu ya miaka 12, akae karibu na wazazi.


Maoni

  1. Pliz naomba munipe disadvantages za bweni

    JibuFuta
  2. faw99 เป็นเกมออนไลน์ ที่ สามารถ โปรโมชั่น PG ที่เล่นแล้วได้เงินจริง เครดิตฟรี เล่นแล้วร่ำรวยทำให้ท่านมั่งมีขึ้นได้ เพียงแต่คุณร่วมบันเทิงใจกับ สล็อต ต่างๆที่มีให้เลือกเล่น

    JibuFuta
  3. heng 999 หาประสบการณ์การเล่นเกมส์ออนไลน์ที่น่าตื่นตาตื่นใจและก็ได้โอกาสชนะเงินโบนัสจริง คุณไม่สมควรพลาด pg slot แล้วก็บริการที่ครบวงจรอื่นๆที่มีเสนอให้ท่านใส่ใจ Wallet

    JibuFuta
  4. fun88 เว็บไซต์พนันออนไลน์ที่ได้รับความนิยมเปิดให้บริการโดยตรงลงทะเบียน pgslot ด้วยโปรโมชั่นที่น่าสนใจ การชำระเงินรางวัลเร็ว ความปลอดภัยสูง บริการส่งเสริมลูกค้าอย่างมือโปร

    JibuFuta
  5. pg slot เว็บตรงอันดับ 1 เมื่อพูดถึงความบันเทิงออนไลน์ ไม่สามารถที่จะไม่พูดถึงสล็อตออนไลน์ได้ PGSLOT เกมสล็อตได้กลายเป็นหนึ่งในเกมคาสิโนที่นิยมและเป็นที่นิยมมากที่สุดในยุคปัจจุบันนี้

    JibuFuta
  6. ทางเข้า pg เฮง 99 มือที่ครบครันเกี่ยวกับประตูท่ามกลางการผจญภัยเกมออนไลน์ที่ไม่เหมือนใคร PGSLOT บทความนี้จะให้ความรู้จากผู้เชี่ยวชาญ คำถามที่พบบ่อย และข้อมูลมีค่าเพื่อเพิ่มประสบการณ์

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Uislamu ulianza lini?

Kama sio utumwa ni nini hiki?