Mambo Yanayokuza Motisha kwa Wafanyakazi
Pengine umewahi kufanya kitu kwa sababu tu ulilazimika kukifanya.
Moyoni hukusikia msukumo wowote isipokuwa hofu ya kushindwa kufikia matarajio
ya mtu mwingine. Lakini pia inawezekana umewahi kufanya kitu bila kusukumwa
wala kufuatiliwa. Ndani yako unakuwa na furaha na msukumo unaokuhamasisha
kutekeleza jambo si kwa sababu ya hofu iliyotengenezwa na wengine bali shauku
ya kufikia kiwango kinachokupa kuridhika.
Ndivyo ilivyo kazini. Wapo
wanaofanya kazi kwa sababu wanamwogopa kiongozi wao. Jitihada yao kazini
inategemea sheria na vitisho kutoka kwa kiongozi. Inapotokea kiongozi huyo
hayupo karibu, watu hawa hukosa msukumo.
Kwa hakika utendaji kazi wa namna hii hauwezi kuleta tija. Kwanza,
mtu anayetegemea msukumo wa nje kufanya kazi hawezi kujituma. Atafanya kazi kwa
mazoea. Pili, ni vigumu kuwa mbunifu. Huwezi kuwa na uwezo wa kutafuta majibu
ya matatizo kama huna msukumo unaoanzia ndani yako.
Hata hivyo, kiongozi anaweza kuweka mazingira yanayowapa
wafanyakazi motisha ya kutekeleza majukumu yao kwa kujituma bila kutegea.
Motisha ni hamasa inayomsukuma mtu kufanya jitihada za kufikia malengo. Mtu
mwenye motisha hahitaji uangalizi wa karibu kutekeleza wajibu wake.
Makala haya yanaangazia matano yanayosaidia kukuza motisha ya watu
wanaofanya kazi chini yako wewe kama kiongozi.
Mazingira bora ya kazi
Hamasa ya kazi inaanzia kwenye namna unavyomwezesha mfanyakazi kutekeleza kazi yake bila vikwazo. Utendaji wa kazi, kwa mfano, unategemea upatikanaji wa vitendea kazi vya msingi. Hakikisha vitendea kazi anavyovihitaji mfanyakazi wako vinatosheleza.
Pia, weka mazingira yanayomwezesha mfanyakazi kutumia vipaji vyake ipasavyo. Moja wapo ya sababu zinazoongeza motisha ya kazi ni mtu kuona mamna gani anaweza kutumia uwezo alionao kikamilifu. Weka mazingira yanayompa fursa hiyo.
Kadhalika, maslahi mazuri yanampa mfanyakazi utulivu wa nafsi. Mfanyakazi mwenye msongo wa mawazo wa namna atakavyoendesha maisha yake, hawezi kuwa na hamasa ya kufanya kazi kwa kujituma. Mlipe mfanyakazi wako kiwango kinacholingana na makubaliano mliyojiwekea.
Baadhi ya viongozi wana tabia ya kuzuia stahili za mfanyakazi kwa sababu zisizoeleweka. Mwisho wa mwezi unapofika ndio kwanza wanajifanya wako na mambo mengi kiasi cha kuchelewesha mishahara. Haipendezi. Mpe mtu kile unachojua ni haki yake. Kama huna sababu ya msingi, lipa madai yoyote ya haki kulingana na kazi aliyoifanya.
Kuaminika na kuheshimika
Kila binadamu analo hitaji la kuaminiwa. Unapokuwa na uhakika mtu
unayemheshimu anakuamini unakuwa na motisha ya kufanya vizuri zaidi kukidhi
imani yake. Kama kiongozi kazini, unahitaji kuwa na tabia ya kuonyesha unaamini
utendaji wa watu wako pasipo kuwaingilia bila sababu.
Unaweza kuonyesha imani kwa namna nyingi. Kwa mfano, badala ya
kumfuatilia mtu kwa karibu mno, mpe kiasi fulani cha uhuru wa kufanya kazi kwa
namna anayoona inafaa muhimu asiharibu kazi. Hitaji kuona matokeo ya kazi
badala ya kudhibiti kila kinachofanywa ikiwa si lazima.
Kadhalika, kuwaamini wafanyakazi kunakwenda sambamba na
kuwaheshimu. Heshima kwa watu walio chini yako –iwe ni kwa maneno na vitendo
vyako –inakutengenezea mazingira ya kuheshimiwa. Epuka kuonekana unawadharau
watu kwa kuwatendea kama watoto.
Hata pale wanapokuwa wamekosea onyesha staha kwa namna
unavyoshughulika makosa yao. Kwa mfano, huna sababu ya kumfokea mtu kwa sababu
tu una madaraka. Jifunze kudhibiti hasira hata pale unapokuwa na sababu ya
kuhalalisha kuudhika mbele ya kadamnasi.
Kutambuliwa na kushirikishwa
Kutambuliwa ni kuonyesha kuelewa nafasi ya mfanyakazi wako kwenye
ofisi, idara, kampuni au taasisi. Unapomtambua mfanyakazi, unamfanya
ajisikie kuthaminiwa. Kwa mfano, kufahamu jina na kumtambua kwa nafasi
aliyonayo inatuma ujumbe kuwa unathamini uwepo wake.
Kadhalika, namna bora ya kuthibitisha kuwa unawatambua wafanyakazi
wako ni kuwafanya wajione ni sehemu ya taasisi au kampuni yako. Washirikishe
kwenye maamuzi hata kama unajua wewe ndiye mwenye sauti ya mwisho. Omba mawazo
ya watu waliochini yako. Onekana ukiandika mawazo unayoyapokea. Kile
kinachowezekana kufanyiwa kazi, kitekeleze. Unapofanya hivi kwa dhati watu
watakuwa na ari ya kazi.
Kueleweka kwa malengo
Moja wapo ya mambo yanayofanya watu wakose ari ya kazi, wakati
mwingine ni kutokueleweka kwa malengo ya taasisi. Hali hii hufanya kila mtu
ajikute anafanya kile kinachomjia kichwani ili naye aonekane anachapa kazi.
Fanya jitihada wafanyakazi wajue kampuni au taasisi inalenga
kufika wapi. Malengo ya muda mrefu na ya muda mfupi yaeleweke. Kwa mfano, kama
ni kampuni, ifahamike mnataka kupata mafanikio gani katika kipindi cha mwaka
mmoja. Kila mmoja aelewe mwelekeo wa pamoja.
Lakini ili malengo hayo ya kitaasisi yawe na maana, lazima
uhakikishe kila mmoja anajua anapaswa kufanya nini. Ainisha majukumu ya kila
mfanyakazi kuepusha mwingiliano usio na sababu. Kila mmoja afanye kazi yake
bila kuingilia majukumu ya mwenzake.
Kadhalika, ni vyema na wewe kama kiongozi ukatabirika. Hakikisha
waliochini yako wanajua kwa hakika unatarajia nini kwao. Kutabirika kwako kama
kiongozi kunarahisisha kazi ya watu kukidhi matarajio uliyonayo.
Usalama wa ajira
Watu wanapenda kuwa na uhakika na kesho. Hofu ya kufutwa kazi,
kuonewa, kudhulumiwa, inaondoa motisha kazini. Ukitaka kuongeza ari ya kazi kwa
wafanyakazi wako, wafanye wajisikie wako salama.
Njia ya kwanza kumhakikishia mtu usalama wake ni kumpa mkataba.
Hili ni sharti la kisheria na kisaikolojia. Mfanyakazi anapokuwa na mkataba
anaouridhia anakuwa hana sababu ya kuwa na wasiwasi na kesho.
Sambamba na hilo, jitahidi kuaminika. Epuka kuonekana mtu mwenye
tabia ya upendeleo wa namna yoyote ile. Makundi ya wafanyakazi ‘vipenzi’ si tu
yanawavunja moyo wasio ‘vipenzi’ lakini pia yanazalisha misuguano inayoweza
kufubaza ufanisi wa kampuni, idara au taasisi unayoiongoza.
Maoni
Chapisha Maoni