Namna Bora ya Kuwasiliana na Wafanyakazi Unaowaongoza
Maisha ya kazi kwa kiasi kikubwa ni
mawasiliano. Karibu kila tunachokifanya kazini ni kuwasiliana. Tunawasiliana na
wateja. Tunawasiliana na wakubwa wa kazi. Tunawasiliana na walio chini yetu.
Kwa ujumla kazi ni mtiririko wa mawasiliano.
Pamoja na umuhimu mkubwa wa
mawasiliano kazini, tafiti zinaonesha kuwa wengi wetu hatuwasiliani
ipasavyo. Kwa mfano, tunapoongea na watu
tunaowaheshimu tunakuwa makini kuliko tunapowasiliana na watu wasio na hadhi.
Kadhalika, tunapowasiliana na mtu tunayemfahamu
vizuri, mara nyingi, tunaamini tunawasiliana vizuri kuliko pale tunapoongea na
mtu tusiyemfahamu. Lakini katika hali halisi tunafanya kinyume chake kama watafiti
wa Chuo Kikuu cha Chicago walivyobaini.
Kwenye
utafiti wao, watu wanaofahamiana walikutanishwa waongee na baadae watu hao hao
walikutanishwa na watu wasiowafahamu kuona wanavyowasiliana. Matokeo yalionesha
kuwa watu wasiofahamiana waliweza kuwasiliana vizuri kuliko watu wanaofahamiana.
Tunapowasiliana
na watu tunaowafahamu mara nyingi tunafikiri tunajua kile wanachokihitaji na
hivyo hatujishughulishi kuwaelewa. Fahamu zetu zinatuaminisha kuwa tunawaelewa
na hivyo hatuna haja ya kufanya jitihada za kuwaelewa. Lakini tunapoongea na
wageni tunakuwa makini zaidi kujaribu kuwaelewa.
Mawasiliano ni kumwelewa mwenzako
Mawasiliano
yenye ufanisi ni yale yanayolenga kumwelewa mtu mwingine kwa kumsikiliza na
kumpa nafasi ya kufafanua mtazamo wake. Kadhalika, kuwasiliana ni uwezo wa
kueleza mtazamo wako katika namna ambayo msikilizaji anayelengwa ataielewa kirahisi.
Kimsingi,
mawasiliano ndiyo shughuli kubwa ya kiongozi. Huwezi kuwa kiongozi kama huna
uwezo wa kuwasiliana nyema na watu unaowaongoza. Mawasiliano bora yanagusa moyo
wa mtu mwingine. Mtu mwenye uwezo wa kuwasiliana vizuri na watu hujiunganisha
na hisia za watu kwa kuzungumza moja kwa moja na mahitaji ya watu anaoongea
nao.
Mbinu hizi nne zinaweza kukusaidia kujenga uwezo
mzuri zaidi wa kuwasiliana na watu hasa wa chini yako.
Kujali
hisia za watu
Hatua ya
kwanza ya kuwasiliana na watu ni kujali hisia zao. Binadamu ni kiumbe
anayeheshimu hisia zake. Ukigusa hisia zake, iwe kwa kumkwaza au kumfurahisha, atachukulia
kwa uzito. Hisia hazisahauliki. Usiweza
kugusa hisia za mtu hutaweza kuwasiliana naye ipasavyo.
Ili uweze
kugusa hisia za mtu lazima uondoe kiambaza kinachoweza kukutenganisha naye.
Kiambaza kimoja wapo ni cheo. Unapokuwa na cheo, ni rahisi sana kupuuza hisia
za walio chini yako katika jitihada za kulinda heshima yako. Madaraka yanakuwa
kikwazo cha mawasiliano.
Sambamba
na hili, nafasi yako inaweza kukufanya usifikike. Walio chini yako wanaweza
kushindwa kusema mawazo yao ama kwa kukwambia wanayojua unapenda kuyasikia au
kwa kukwambia wasiyoyaamini ili kutetea nafasi zao.
Unaweza
kukabiliana na changamoto hii kwa kutokujali sana nafasi yako. Jifunze kuongea
kama mtu wa kawaida anayejali zaidi utu kuliko hadhi na madaraka. Unapofanya
hivyo, unagusa hisia zake na atakusikiliza.
Huna
sababu, kwa mfano, humfanya mtu ahisi uko juu yake. Ukiweza kuongea na mtu kwa
namna isivyoonyesha namna unavyomzidi kwa hadhi, utakuwa na nafasi kubwa ya kueleweka
vyema kuliko unapozungumza kama mtawala.
Kusikiliza
kuliko unanyoongea
Mara nyingi
tunapozungumza tunatamani kusikilizwa. Tunaamini sisi ndio watu wenye taarifa
na uelewa sahihi kuliko wanaotusikiliza. Ukishaongeza na madaraka, shauku ya
kusikilizwa inakuwa kubwa zaidi. Unaanza kuyachukulia mawasiliano kama haki
yako ya kusema mawazo na maamuzi yako kuliko kuwasikiliza walio chini yako.
Ukishaamini
una haki ya kusikilizwa, hata katika mazingira unayoonesha kusikiliza, kimsingi
unakuwa ukingoja zamu yako ya kuongea. Unafikiria utasema nini baada ya hapo.
Tatizo ni kuwa kadri unavyotamani kusikilizwa ndivyo unavyomfanya anayepaswa
kukusikiliza ajione hathaminiki. Kutokuthaminika humfanya ajenge umbali wa
kihisia na hivyo kukosa ari ya kukusikiliza.
Jenga
mazoea ya kusikiliza watu kwa makini. Hapa hatuzungumzii kusikiliza
kinachosemwa pekee, bali namna gani kinasemwa, kitu gani hakisemwi wazi na kipi
kimejificha. Ili hili liwezekane, lazima uwe na uzingativu kuonesha unaheshimu
mazungumzo ya mtu.
Kuonyesha
unafuatilia
Kumfanya mtu ajisikie anaheshimiwa na kusikilizwa ni
sehemu muhimu ya mawasiliano. Unahitaji kujifunza kuonyesha kuwa unazingatia
mazungumzo kwa namna kadhaa. Kwanza, epuka kumkatisha mtu anapoongea au
kumalizia sentensi yake. Mtu anapoona unaingilia maneno yake anahisi tayari
unaamini unajua anachotaka kusema. Unamkatisha tamaa.
Pili, itikia anachokisema mwenzako kumtia moyo
kuwa unajali na kufuatilia mazungumzo
yake. Itikia kwa kutikisa kichwa, kumwangalia machoni, maneno kama ‘mmh-mh!’
Tatu, rudia anachokisema kwa maneno yako. Kwa mfano,
baada ya maelezo yake, mwambie, ‘Kwa hiyo unachokisema ni kuwa maamuzi
tuliyofikia jana yanahitaji kufikiriwa tena, sio?’ Kufanya hivyo kunamsaidia
anayeongea kujiridhisha kuwa unaelewa.
Nne, uliza maswali kupata ufafanuzi. Unapomwuuliza
mtu maswali kiungwana, anaona unajali. Kumbuka, wakati mwingine, watu wa chini
yako hawana ujasiri wa kukwambia kitu vile kilivyo. Unapohisi kuna hoja fulani
haijawekwa wazi vya kutosha uliza kumwonyesha mzungumzaji kuwa unaelewa lugha
inayotumika.
Mkutanoni
zungumza na mtu
Kama kiongozi, sehemu kubwa ya majukumu yako ni kufanya
vikao au mikutano na watu zaidi ya mmoja. Katika mazungumzo ya namna hii, ni
rahisi kutoa hotuba ya jumla isiyolenga kumgusa mtu mmoja mmoja. Hali hii hufanya
kila mtu kujiona hahusiki.
Kiongozi bora anajua namna ya kuongea na watu wengi
kama anavyoongea na mtu mmoja moja. Kwa mfano, unapoongelea kosa au tabia ya
mfanyakazi mmoja mbele ya watu wengine hata bila kumtaja jina, unawafanya
wengine waone hawahusiki. Kila mtu atajiondoa kwenye mazungumzo hayo akijua
hahusiki.
Unahitaji kujifunza mahitaji ya watu wanaokusikiliza
ili ujua namna ya kuyagusa moja kwa moja. Tengeneza ujumbe wako kwa namna
inayojibu matarajio yao badala ya kutumia lugha ya mafumbo kuwasema baadhi ya
watu mbele ya hadhara.
Maoni
Chapisha Maoni