Ukitaka Kuaminiwa Jenga Mazingira ya Kuaminika
PICHA: PsyBlog |
“Nina mke asiyeniamini kabisa,”
aliniambia bwana mmoja hivi majuzi. “Hana imani kabisa na mimi. Juzi kati hapa nimemkuta anachunguza simu
yangu. Tuligombana sana.” Nilimwuliza kwa nini anafikiri mke wake hamwamini.
“Basi tu ndivyo alivyo. Hata ufanyaje hana imani.”
Sote, kama alivyo bwana huyu,
tuna hitaji la kuaminiwa. Tunatamani watu wasiwe na mashaka na sisi. Tunatamani
watu waamini yale tunayowaambia.
Pengine nawe, kama huyu bwana umewahi
‘kuwadai’ watu wakuamini. Umekwenda kwa rafiki, mathalani, kumkopa fedha.
Rafiki yako anasita. Hakuamini. Kutokuaminiwa
kunaumiza hisia kwa sababu, kama tulivyosema, kuaminiwa ni hitaji la kila mtu.
Hata mwongo naye anapenda watu wamwamini.
Kuaminiwa ni matokeo
Mambo mengi hayaendi bila
kuaminiwa. Kazini, wakubwa wa kazi wanapenda mtu anayeaminika. Bila kuaminika,
huwezi kupata mafanikio. Mfanyabiashara naye, anapoaminiwa na watu anakuwa
kwenye nafasi kubwa ya kupata mafanikio.
Urafiki kati ya watu wawili, hali
kadhalika, unategemea kwa kiasi kikubwa namna watu hao wanavyoaminiana. Huwezi
kuwa na urafiki mzuri na mtu kama hamuaminiani. Kuaminiwa ni msingi wa
mahusiano yoyote ya karibu na hata shughuli zinazohusisha watu zaidi ya mmoja.
Kuaminiwa, hata hivyo, si tukio
la siku moja wala haki inayoweza kuidaiwa kwa watu. Mke hawezi kudai ‘aaminiwe’
na mume wake. Mume hali kadhalika. Kuaminika ni zao la tabia zetu. Kuaminiwa ni
sawa miamala ya Benki. Unaweza kuchukua
kile ulichokiweka. Huwezi kudai zaidi. Fanya mambo matatu uaminiwe.
Sema ukweli daima
Fikiria uko mahali na rafiki yako
ukamsikia akimdanganya mwenzake kwenye simu. Hata kama aliyedanganywa ni
mwingine, kwa vyovyote vile imani yako kwa aliyedanganya inapungua. Uongo unapunguza kuaminika.
Ukitaka kuaminika, jenga tabia ya
kusema ukweli. Epuka kusema kitu usichomaanisha kwa lengo tu la kuwafurahisha
watu. Usimdanganye mtu hata kama unajua hatagundua. Ukitambulika kama mtu
mwenye tabia ya kusema ukweli unawafanya watu wasiwe na wasiwasi na maneno
yako. Utaaminika.
Timiza ahadi zako
Ni rahisi sana kutoa ahadi hasa
kama hujiamini na unatamani kuwaridhisha watu. Hata hivyo, ni vizuri kuelewa
kuwa ahadi ni kipimo cha ukomavu wako. Usipotekeleza ahadi zako watu
wanakuchukulia kama mtu asiye na ukomavu. Huwezi kuaminika katika mazingira
unayoonekana huna ukomavu.
Kuliko kutoa ahadi kwa lengo la
kumridhisha mtu, ni bora usiahidi kabisa. Punguza matarajio ya watu kwako,
kisha fanya jitihada za kuzidi matarajio hayo. Unapoahidi kufanya kitu,
tekeleza. Ukishindwa kutekeleza, kuwa mwuungwana. Omba msamaha. Kwa namna hii
watu watakuamini.
Heshimu uheshimike
Mtu asiyeheshimika ni vigumu
kuaminiwa. Wapo watu wanaaminiwa kirahisi kwa sababu tu wamejijengea taswira ya
heshima kwa jamii. Heshima ni zaidi ya vitu ulivyonavyo na namna unavyoonekana.
Heshima kubwa unayoweza kupewa na watu inategemea vile unavyowaheshimu. Ukitaka
kuheshimiwa, heshimu watu.
Unapokuwa na tabia ya kuwadharau
watu; kujiona bora kuliko wengine; watu wanakudharau. Hata wale unaowazidi wanastahili heshima. Hata
wanaokukosea na kukutendea mabaya wanastahili heshima. Ukijenga tabia ya kulipa
ubaya kwa wema utashangazwa na matokeo.
Jambo la kukumbuka ni kwamba watu
wanaweza kupoteza imani na wewe kimya kimya. Si kila mtu anaweza kukutangazia
kuwa hana imani na wewe. Linda sana tunda la uaminifu. Imani ikipotea, ni
vigumu kuirejesha. Habari njema, hata hivyo, ni kwamba kadri unavyojiwekea
mazingira ya kuaminika, ndivyo utakavyoendelea kuaminika.
Maoni
Chapisha Maoni