Hatua za Kuchukua Unapojisikia Kuchoka Kazi
Kutokuridhika na kazi ni hali ya
kujisikia hufikii matarajio yako kikazi. Matarajio yanaweza kuwa kiwango cha
mshahara, kujisikia unafanya kazi ndogo kuliko uwezo ulionao, kazi kutokuendana
na vipaji ulivyonavyo au hata kutokupata heshima uliyoitarajia.
Kila mtu kwa wakati fulani hujisikia kutokuridhika. Kuna
sababu kadhaa. Moja, ni kuwa na matarajio makubwa kuliko uhalisia wa kazi. Lakini
la pili, kujilinganisha na watu wasiolingana na kazi unayoifanya. Unapoona
wenzako wanafanya kitu tofauti na kile unachokifanya wewe inawezekana ukajisikia
kuachwa nyuma hata kama kimsingi pengine unafanya vizuri.
Vyovyote iwavyo, zipo nyakati unaweza kujikuta huridhiki na
kazi unayoifanya. Makala haya yanaangazia vichocheo vinne vya kuchoka kazi na hatua
za kuchukua unapojikuta katika hali kama hiyo.
Huridhiki
na mshahara
Ulipokuwa mwanafunzi uliota ndoto za kufanya kazi yenye mshahara
mnono. Uliamini maisha yako yangebadilika ndani ya muda mfupi. Baada ya kupata
kazi, unashangaa mambo ni kinyume. Unacholipwa hakilingani na matarajio yako.
Hapa sababu inaweza kuwa kukosa subira. Hakuna mafanikio
yanayokuja kwa njia ya mkato kama vijana wa siku hizi wanavyoamini. Mafanikio
katika mazingira ya kazi yanafuata hatua fulani. Unahitaji kuwa mvumilivu.
Lakini vile vile huenda kuna maslahi usiyoyaoona. Hata kama
mshahara ni mdogo, pengine mwajiri wako anakupa usafiri kwenda na kurudi kazini;
amekulipia nyumba; amekuweka mpango wa bima ya afya; anahakikisha unapata
chakula cha mchana ukiwa kazini.
Mbali na mshahara huo mdogo, labda mwajiri anakupa fursa ya kwenda
masomoni na pia unapata muda wa ziada kufanya mambo mengine. Haya yote unaweza
kuona ni madogo lakini ukiyabadilisha kuwa fedha yanaweza kuwa nusu ya mshahara
unaoutamani.
Ujuzi wako
hautumiki
Moja wapo ya mambo yanayopunguza ari ya kazi ni kujisikia
ujuzi ulionao hautumiki ipasavyo. Unalipwa vizuri lakini moyo wako hauridhiki
na kazi unayofanya.
Labda una Shahada ya Biashara na Masoko, lakini majukumu
yako ya kila siku ni yale yale na hayakupi changamoto. Kazi yako ni kupokea
barua za wateja na kuzigonga muhuri. Unaichukulia hali hii kama udumavu na
unatamani ungefanya kazi inayokupa changamoto.
Katika hili unahitaji kutafuta fursa nyingine za kutumia
ujuzi wako kazini. Pengine kampuni ina shughuli nyingi za ziada ambazo ukiweza
kuwa tayari unaweza kuzifanya.
Vipi kama ukianzisha wazo la chama cha akiba na kukopa? Kazi
hiyo inaweza kukufanya ukatumia muda wako wa ziada kutumia maarifa yako ya
Biashara na ukajisikia kuridhika.
Kadhalika, unaweza kuamua kufanya kazi nyingine za ziada
zisizoathiri utendaji wako. Kuna fursa nyingi za ujasiriamali zisizokulazimu
kuacha kazi na zikakufanya utumie vizuri zaidi ujuzi ulionao.
Lakini pia kuna suala la uzoefu. Unaweza kuamua kuwa
mvumilivu ukaweza kupanda ngazi hapo kazini. Kubadilisha kazi kila baada ya
muda mfupi, kunakufanya uendelee kuwa mtu asiyeweza kuaminiwa kwa nafasi za uandamizi.
Huoni
fursa ya kukua
Umefanya kazi kwa miaka mitano kwenye kampuni kubwa
inayokulipa vizuri lakini hujioni ukikua kiujuzi. Huwezi kwenda masomoni ukiwa
kazini na pengine kampuni haina mpango wa kukusaidia kujiendeleza kiujuzi. Hali
hii imekufanya ujisikie kuchoka, unajisikia kudumaa na huna hamasa tena ya
kufanya kazi. Ufanyeje?
Tafakari kitu gani hasa kilikufanya ukapenda kazi
unayoifanya hivi sasa. Kitu gani kilikuwa kinakuvutia kwenda kazini mwanzoni
mwa ajira yako? Nini kimebadilika leo?
Unapokuwa katika mazingira kama haya ni rahisi kumlaumu
mwajiri wako. Kumbuka mwajiri halazimiki kufikiri namna ya kukuendeleza na
kukupa hamasa ya kujiendeleza. Hiyo ni kazi yako.
Kwa kuwa fursa ya kujiendeleza kimasomo mbali na ofisini
haipo, fikiria kujiunga na masomo ya masafa. Jiandikishe kufanya masomo yako
kwa njia ya mtandao; jiunge na vyuo vya karibu vinavyotoa masomo ya jioni au
mwisho wa juma. Kwa namna hiyo unaweza kuendelea na kazi huku ukikuza ujuzi
wako.
Kadhalika, jenga utamaduni wa kujisomea vitabu vinavyoendana
na fani yako. Maarifa yanabadilika kwa kasi. Vijana wa leo wanaoingia kwenye
ajira wanajua mambo mengi ambayo pengine wewe mkongwe hukujifunza. Usiposoma
utaachwa nyuma na utendaji wako unaweza kuanza kupwaya.
Una ndoto
za kazi nyingine
Inawezakana kazi unayoifanya leo hailingani na masomo
uliyosomea. Ulikuwa na ndoto za kuwa mwanasheria lakini mazingira yalikulazimu
kusomea Sayansi ya Siasa. Ingawa unafanya kazi kwa sasa, lakini moyo wako bado
uko kwenye sheria.
Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba si wakati wote tunapata
kile tunachopanga. Si mara zote watu hufanya kazi zinazolingana na fani
walizosomea. Unaweza kusomea Sayansi ya Siasa ukajikuta ukifanya kazi ya Ofisa
Raslimali Watu. Unaweza kusomea Biashara na Masoko ukajikuta unafanya kazi ya
Ualimu. Mambo hubadilika.
Ukweli ni kwamba elimu ya chuo hutupa maarifa ya jumla
yanayoweza kutumika kwenye eneo zaidi ya moja. Mwalimu, kwa mfano, anajifunza utawala,
siasa, mipango, uandishi wa miradi na maarifa mengine anayoweza kuyatumia
kwenye eneo tofauti na Ualimu.
Mbali na maarifa na ujuzi mahususi, miaka unayotumia
darasani inakufundisha ujuzi wa ziada ambao hatuufanyii mtihani. Mfano, namna
ya kuwasiliana na watu, kutatua migogoro na watu msioelewana, uandishi wa
nyaraka, nidhamu ya muda na ujuzi mwingine mwepesi.
Kila tunachokisoma kinatunufaisha kwa namna moja au
nyingine. Hakuna ujuzi usio na maana yoyote hata kama huoni ukiutumia moja kwa
moja. Pengine ni wakati wa kukubali kuwa mambo yamebadilika. Ulichotaka
kukifanya sicho unachokifanya. Ndivyo maisha yalivyo.
Hata hivyo, kama umejaribu kukuza ujuzi wako; umejiendeleza
ukiwa kazini; umefanya jitihada za kujiongezea kipato na bado huridhiki na
mazingira ya kazi, pengine ni wakati wa kujaribu kwingine.
Maoni
Chapisha Maoni