Mabadiliko ya Kijamii Yanavyoathiri Malezi -1
PICHA: The Conversation |
TUNAISHI katika nyakati ambazo maarifa kuhusu
malezi ya watoto vinapewa umuhimu. Sambamba na ongezeko la mijadala ya malezi
katika majukwaa mbalimbali, malezi yamevutia hisia za watafiti wengi kuliko
ilivyopata kuwa. Kila siku, kwa mfano, zinachapishwa tafiti nyingi kuchunguza
changamoto za malezi ya watoto.
Jambo hili linaweza kumtia wasiwasi
mfuatiliaji makini wa mambo. Unaweza kuhoji, ‘Kulikoni msisitizo huu mkubwa
katika malezi?’ ‘Mbona wazazi wetu hawakuelimishwa namna ya kulea na hawakushindwa
kutulea vizuri?’
‘Kwa nini pamoja na kuwepo kwa kila namna ya
maarifa ya kimalezi kwa wazazi wa kisasa bado tumeendelea kushuhudia kuporomoka
kwa maadili kwa watoto wetu?’ Maswali haya ni ya msingi na hayawezi kuwa na majibu
mepesi.
Hata hivyo, lililo dhahiri ni kwamba jamii
yetu inapitia mabadiliko makubwa ya kijamii yanayoathiri mfumo uliozoeleka wa malezi.
Tutazame mabadiliko kadhaa na namna yanavyodai gharama kwenye eneo la malezi.
Wazazi
kutokuishi pamoja
Tunaishi kwenye nyakati za mabadiliko makubwa
ya mfumo wa maisha. Mtindo wa maisha tunayoishi
hivi leo unaathiri kwa kiasi kikubwa namna tunavyolea watoto wetu. Kwa mfano, siku
hizi ni jambo la kawaida kwa wazazi kutumia muda mrefu mbali na familia zao.
Kazi zinachukua muda mrefu wa wazazi kuliko ilivyopata kuwa hapo zamani.
Wakati zamani katika familia nyingi za
kawaida baba na mama waliishi sehemu moja, siku za leo ni kawaida, kwa mfano, kusikia
mume anaishi Dar es Salaam, wakati mama anafanya kazi mkoani Singida.
Katika mazingira haya, wazazi hawa wanaweza
kukutana kwa nadra na hata kuchukua miezi kadhaa kabla mzazi mmoja hajapata
muda wa kwenda kusalimia familia yake inayoishi mbali nae. Jambo hili
halikuwahi kuwa sehemu ya maisha ya familia katika siku za nyuma.
Kadhalika, ndoa nazo zimekuwa na mitikisiko
kuliko ilivyokuwa zamani. Misukosuko ya ndoa inafanya watoto ama waishi na
mzazi mmoja au wazazi wawili wasioelewana.
Ajira
kwa wanawake
Siku za nyuma mama alikuwa ndiye mlezi mkuu.
Katika familia nyingi za kawaida, wanawake walioolewa waliitwa ‘mama wa nyumbani.’ Kazi yao kubwa ilikuwa kubaki
nyumbani muda mwingi kulea watoto. Wanawake wengi, kwa kawaida, hawakuwa na
kazi nyingine zaidi ya kuwatunza watoto.
Kazi ya kutafuta kipato iliachwa kwa wanaume.
Watoto walilelewa kwa karibu sana na mama tangu wakiwa wadogo mpaka walipofikia
umri wa kuondoka nyumbani na kujitegemea. Hapakuwa na changamoto ya nani abaki
nyumbani kuwaangalia watoto.
Mambo yamebadilika hii leo. Akina mama
wameondoka nyumbani kuungana na wanaume kuongeza kipato cha familia. Dhana kuwa
mwanamke ni ‘mama wa nyumbani’ inafutika. Akina mama wanafanya ujasiriamali,
wanajihusisha na shughuli ambazo hapo zamani zilionekana kama haki ya wanaume.
Mwanamke kufanya kazi, kwa hakika si jambo
baya. Jitihada za kuwasomesha watoto wa kike zinaenda sambamba na fursa ya
kiajira sawa na mwanaume. Ndio kusema, kama mwanaume anaweza kuajiriwa, haileti
maana kufikiri kuwa mwanamke anapaswa kubaki nyumbani kufanya kazi za ndani
kama ilivyokuwa imezoeleka hapo zamani.
Katika ajira wanawake wameonesha uwezo wa kumudu majukumu yao sawa na wanaume. Karibu kila sekta hivi sasa wapo akina mama. Wanawake wanaonesha uwezo mkubwa. Wanashika madaraka makubwa makazini na wanafanya vyema, tena mara nyingine, kuliko wanaume.
Hata hivyo, mafanikio haya ya akina mama
kikazi yametikisa maeneo mengineyo ya kijamii. Malezi ni eneo moja wapo kubwa
lililokumbwa na tetemeko kubwa tangu akina mama walipoanza kuondoka nyumbani
kuelekea makazini.
Kufifia
kwa familia tandaa
Katika baadhi ya makabila, mwanamke ndiye
aliyekuwa na jukumu la kuitunza familia. Ingawa mwanamke hakuwa na ajira rasmi,
bado alitarajiwa kujituma katika shughuli zinazoingiza kipato cha familia. Mwanamke
alishinda shambani akilima na pia alitafuta soko la mazao ya kilimo ili aweze
kuilisha familia.
Hata hivyo, shughuli hizi za mwanamke
hazikuathiri wajibu wake mkuu wa malezi. Kulikuwa na familia tandaa, ndugu wa
ukoo, waliomsaidia kufanya majukumu ya nyumbani wakati yeye akiendelea na
shughuli zake nyingine mbali na nyumbani.
Wakati mama akisafiri kwenda kuuza mazao
mjini, kwa mfano, nyumbani walibaki ndugu waliomwangalia mtoto. Mama hakuwa na
wasiwasi na usalama wa mtoto kwa sababu alijua amemwacha mtoto wa baba mkubwa,
binamu au shangazi waliomjali mtoto wake kama ndugu.
Haya mawili, yalifanya suala la malezi kuwa
jambo lisilo na changamoto kubwa. Kwamba baba akiwa kazini, mama alikuwepo
nyumbani. Ikitokea mama naye anawajibika kufanya kazi nje na nyumbani,
ilikuwepo familia tandaa kuhakikisha mtoto analelewa ipasavyo. Hata hivyo,
ukaribu huu wa familia tandaa unaendelea kufifia. Kwa sababu kadhaa, imeanza
kuwa nadra kuishi na watoto wa ndugu.
Upatikanaji
holela wa taarifa
Ninakumbuka mara ya kwanza kuangalia televisheni.
Wakati nakua, hatukuwa na fursa ya kutazama vipindi vya televisheni zaidi ya
maigizo ya kwenye Radio Tanzania. Mambo ya mtandao wa intaneti hayakuwepo. Kwa
vijana wadogo waliopenda ‘udaku’ yalikuwepo magazeti ambayo hata hivyo
yaliishia kuchekesha. Hapakuwa na magazeti yanayoanika taarifa ambazo zingeleta
usumbufu kwa vijana ambao umri wao ulikuwa bado.
Katika mazingira kama haya, mzazi
hakulazimika kuzungumzia mambo fulani fulani kwa vijana wanaobalehe. Hapakuwa
na shinikizo kubwa la mzazi kuwa karibu na kijana wake kuratibu taarifa
zisizostahili. Mambo mengi yalifahamika katika umri husika tofauti na ilivyo
sasa.
Sasa hivi mtoto mdogo anayejua kusoma na
kuandika anaweza kuwa ‘Facebook’, ‘Whatsapp’ bila mzazi wake kujua. Humo, mtoto
anaweza kukutana na taarifa zinazomzidi umri. Upatikanaji holela wa taarifa
umeibua changamoto mpya ya malezi kwa wazazi wachanga. Katika mazingira yenye
mchanganyiko wa changamoto kama hizi, wazazi wanatumia muda mwingi kupanda
ngazi za mafanikio wakiamini watoto wako salama.
INAENDELEA
Maoni
Chapisha Maoni