Unayopaswa Kuzingatia Unapompeleka Mtoto Wako Katika Vituo vya Malezi -1
UTARATIBU
wa wazazi kuwapeleka watoto kwenye vituo vya malezi umeanza kuwa maarufu hapa
nchini. Karibu kila mji mdogo katika mikoa yote vipo vituo kadhaa mahususi kwa
ajili ya kuwatunza watoto wakati wazazi wao wakiwa kazini. Kinachofanya huduma
ya malezi ya vituoni kuwa maarufu ni changamoto za akina dada wa kazi, ambao
mara nyingi, huwa ni wadogo kiumri na hawana uwezo wala ari ya kuwalea watoto
vizuri.
Malezi ya
watoto katika vituo maalum hufanyika katika mfumo ulio rasmi kuliko ilivyo nyumbani.
Mbali na Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009, ipo Sheria ya Vituo vya Malezi
ya Watoto ya mwaka 1981 ambayo, pamoja na kutambua umuhimu wa vituo hivi,
imeweka masharti na utaratibu wa kufuata katika utoaji wa huduma hizi.
Ingawa
sheria ilitoa fursa kwa yeyote kutoa huduma hizi, masharti yalionekana kuwa
magumu kwa mashirika mengi binafsi kuwekeza kwenye eneo hili. Hata hivyo,
mashirika ya nje kama UNICEF na CARITAS yaliwahi kufadhili mradi ya vituo vya
malezi ya watoto kwa miaka ya nyuma. Bahati mbaya hapakupatikana utaratibu
endelevu kuhakikisha miradi hiyo inaendelea.
Vituo
vingi vilivyopo hivi sasa vinaendeshwa na watu binafsi na mashirika yasiyo ya
kiserikali. Lengo ni kuwawezesha wazazi wanaofanya kazi mbali na nyumbani kuendelea
na shughuli zao bila kuwa na wasiwasi na usalama wa watoto. Matokeo ya tafiti
mbalimbali yanaonesha kwamba huduma ya vitu vya malezi ya kutwa kwa watoto yana
faida kadhaa kwa watoto.
Uchangamfu wa kiakili
Tafiti
zilizofanywa katika nchi zilizoendelea zinathibitisha kuwa watoto waliopelekewa
kwenye vituo vya malezi mapema wanakuwa wachangamfu kiakili kuliko wenzao
wanaolelewa nyumbani. Katika umri wa miaka miwili, kwa mfano, watoto
wanaohudhuria kwenye vituo hivi wanakuwa wepesi zaidi kujifunza lugha kuliko wale
wanaolelewa nyumbani katika umri huo.
Sababu
kubwa ni kuwa, katika kituo cha malezi, mtoto anakuwa na fursa ya kuchangamana
na wenzake wanaotoka kwenye familia nyingine. Kucheza, kuzungumza, kuwasiliana
na wenzake ni fursa kwake kujifunza mambo mapya kwa wepesi kuliko anapokuwa
kwenye mazingira ya nyumbani.
Lakini
pia, malezi katika vituo hufanyika kwa mfumo wa shule zisizo rasmi. Mtoto
hupatiwa vifaa vya kujifunzia na kucheza vinavyolingana na mahitaji yake.
Shughuli zake hufanyika kwa kufuata mtiririko maalum tangu anapowasili asubuhi mpaka
anapoondoka. Wakati mwingine, mtoto hulazimika kuvaa sare za shule na hivyo
kujisikia yuko shuleni.
Kuzoea mazingira ya
shule
Vituo vya
malezi hujenga daraja muhimu kati ya maisha ya nyumbani na shule. Mazingira ya shule
yasiyomshinikiza mtoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu humfanya mtoto azoee
mazingira ya shule ukilinganisha na mwenzake anayebaki nyumbani.
Ingawa
baadhi ya vituo huwalazimisha watoto kuanza kujifunza kusoma, kuandika na
kuhesabu kabla ya wakati, kufanya hivi ni kinyume na utaratibu. Kwa mfano, watoto
wanaolamishwa kuanza kujifunza masomo katika umri mdogo, hukabiliwa na
uwezekano wa kujenga mtazamo hasi na mazingira ya shule.
Kumlazimisha
mtoto wa umri mdogo, mfano miaka mitatu, kufanya mahesabu ni kuzidisha
matarajio. Uwezo wake wa kiufahamu bado ni mdogo na hauwezi kumudu mafunzo
rasmi. Hata hivyo, mara nyingi matarajio makubwa waliyonayo wazazi ndiyo hasa yanayochangia
kuwafanya walezi na walimu kuweka msisitizo wa kitaaluma kwa watoto. Badala ya
watoto kutumia muda wa kutosha kucheza, kuimba na kufurahia mazingira ya shule,
wanabanwa kufanya kazi nyingi zinazochosha akili.
Jambo
muhimu ni kwamba vituo hivi vinapoendeshwa na watu wenye uelewa wa masuala ya
watoto, vinamsaidia mtoto kujiandaa vizuri na maisha ya shule. Sambamba na
hilo, humpa mzazi fursa ya kuendelea na kazi zake kwa utulivu akijua mtoto yuko
kwenye mikono salama.
Changamoto nazo zipo
Tafiti zilizofanyika katika nchi zilizoendelea
zinabainisha uwezekano wa kuzorota kwa uhusiano kati ya mzazi na mtoto
anayepelekwa kwenye kituo cha malezi tangu akiwa mdogo. Kwa mujibu wa tafiti
hizi, mtoto anayeanza kuhudhuria malezi ya vituo katika umri mdogo anakuwa
kwenye hatari ya kuwa na uhusiano hafifu na wazazi wake.
Hata hivyo, kuzorota kwa uhusiano
huu ni suala linalotegemea zaidi tabia ya mama. Utafiti mmoja ulionyesha kwamba
kuna uwezekano wa uhusiano huo kuzorota hata katika mazingira ya nyumbani. Maana
yake ni kwamba kinachozorotesha uhusiano ni umbali wa kihisia kati ya mama na
mwanae. Ikiwa mama ataweza kuwa na ukaribu na mwanae baada ya saa za kituoni,
hakuna sababu ya mzazi kuwa na wasiwasi.
Kujifunza yasiyotarajiwa
Vituo vingi hapa nchini vinakabiliwa
na changamoto ya idadi kubwa ya watoto wasiolingana na idadi ya walezi. Makundi
makubwa ya watoto humnyima mtoto mmoja moja fursa ya mahitaji binafsi
kushughulikiwa. Tunafahamu, kwa mfano, mtoto wa umri wa kati ya mwaka mmoja na
miwili huwa na madai mengi yanayoweza kuwa usumbufu kwa mlei. Mtoto wa umri huu
anahitaji mtu anayeweza kumsikiliza kwa karibu. Wingi wa watoto usioendana na
idadi ya kutosha ya walezi huweza kufanya hili lisiwezekane.
Katika mazingira ambayo mtoto
hapati usikivu wa kibinafsi wa mlezi, anakuwa kwenye hatari ya kutafuta mbadala
wa kupata usikivu kwa kulia lia bila sababu, kuwa mbinafsi na wakati mwingine
kuwa mgomvi. Kadhalika, mtoto kukaa muda mrefu na watu wengine mbali na familia
yake katika umri ambao bado hajajifunza lolote kutoka kwenye familia yake, huongeza
uwezekano wa kujifunza tabia ngeni.
Vile vile, zipo tafiti kadhaa
zinazohusianisha malezi ya vituoni na changamoto za kiafya kwa watoto. Hili,
hata hivyo, linategemea na hali ya usafi ilivyo na mazingira yasiyo na
uangalizi mzuri yanayowaweka watoto kwenye hatari ya kuambukizana magonjwa.
INAENDELEA
Maoni
Chapisha Maoni