Tujitathmini Kabla Hatujamhukumu Mtoto Mjamzito
Matukio ya watoto wa kike kupata ujauzito yanaongezeka.
Kwa mujibu wa Takwimu za Elimu (BEST) wanafunzi 4,718 wa sekondari kwa mwaka
2012 na 3,439 mwaka 2015 walikatishwa masomo yao kwa sababu ya ujauzito.
Takwimu kamili hazipatikani lakini kwa elimu ya msingi hali haina tofauti
kubwa. Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu
(UNFPA) linadai kwamba msichana mmoja kati ya sita wenye umri wa miaka 15 mpaka
19 wakiwemo wasiokuwepo shuleni hupata ujauzito kila mwaka hapa nchini. Ni wazi
kuwa mimba za utotoni ni tatizo kubwa katika jamii yetu.
Aidha, matukio ya mimba yanakwenda sambamba na ongezeko
la ngono holela miongoni mwa wanafunzi. Utafiti uliofanywa na Method Kazaura na Melkiory Masatu mwaka
2009, ulibaini kwamba asilimia 32 ya watoto na vijana wenye umri wa miaka 10
mpaka 19 walikuwa wanashiriki vitendo vya ngono. Wengi wao hawana
elimu ya afya ya uzazi. Jarida la African Population Studies toleo Na.29 la
2015 linathibitisha matokeo hayo.
Kwa mujibu wa Eunice Muthengi na Abebaw Ferede
waliofanya utafiti uliochapishwa na Jarida hilo, idadi kubwa ya vijana hapa
nchini wanakosa taarifa za msingi ambazo zingeweza kuwasaidia kufanya maamuzi yanayoongozwa
na uelewa. Hata hivyo, vijana hawa wanapopatiwa elimu ya afya ya uzazi mapema,
asilimia 52 wanaonekana kuweza kuchelewesha maamuzi ya kuanza ngono.
Tunaishi kwenye nyakati zenye uholela mkubwa wa
taarifa. Changamoto, hata hivyo, ni kukosekana kwa elimu na huduma za afya ya
uzazi kwa vijana. Wazazi, kwa mfano, wameendelea kuogopa kuzungumza kwa uwazi masuala
yanayohusiana na ngono kwa imani kwamba ni kinyume na utamaduni wetu. Mtoto
huyu anapokwenda shuleni anakutana na walimu wasio na ujasiri wa
kuyashughulikia mambo haya kwa uwazi. Katika mazingira haya ya uhaba wa taarifa
sahihi katikati ya uholela wa taarifa zinazohimiza ngono, ni wazi maamuzi mengi
wanayofanywa na wanafunzi yatakuwa batili.
Pia, tunafahamu watu wazima wakiwemo wazazi na
walimu wameshindwa kuonesha mfano mwema wa kimaadili. Maadili yamebaki kuwa
hotuba za majukwaani wakati maisha ya watu faraghani ni jambo jingine kabisa. Wazazi
wanaohubiri maadili hadharani, kwa mfano, ndio hao hao wanaofuga ‘nyumba ndogo.’
Walimu waliopaswa kuwaelekeza watoto njia sahihi ya kufuata ndio wanaowashawishi
wanafunzi wao kushiriki nao vitendo vya ngono. Kwa ujumla, jamii inayomzunguka
mtoto inamwaminisha kuwa ngono holela ni sehemu ya maisha.
Jambo la kushangaza ni kwamba mtoto anapoiga yale
anayoyaona na kujiingiza kwenye vitendo vya ngono jamii hiyo hiyo inamshangaa. Hukumu
inakuwa kubwa zaidi inapotokea binti amepata mimba. Huu ndio unakuwa wakati wa
kumkemea mtoto kwamba alichokifanya ni kinyume na maadili. Msichana mwenyewe wakati
huo anashangaa imekuwaje kosa lake liwe kubwa kuliko yale anayoyaona yakifanywa
na watu wazima wanaomzunguka.
Aliyempa mimba anaamini tatizo ni la binti
mwenyewe. Kwa hiyo anamkana. Wazazi, kwa upande wao, wanachukulia mimba kama
aibu mbele ya macho ya jamii. Ili kuonekana hawakuzembea, wengi wao nao humshutumu
na wakati mwingine kumtenga kuonesha kwamba hawakubaliani na uvunjifu wa
maadili uliofanyika.
Msichana huyu akiwa bado katika hali ya kushangaa
inakuwaje tumbo linaendelea kuwa kubwa, anajikuta akikabiliana na mkono wa
serikali isiyotaka kuona wajawazito wanaendelea na masomo. Watu ambao awali hawakuwa
na utaratibu wowote wa kumsaidia kuufahamu mwili wake, wanakuwa wa kwanza kumfukuza
‘ili iwe fundisho wa wanafunzi wengine wasioheshimu maadili.’
Mtoto huyu anarudi mtaani akiwa hana mtu
anayeweza kuvaa viatu vyake na kujaribu kumsaidia. Kila anayezungumzia tatizo
lake anamlaumu yeye. Wengine watasema ‘alijipeleka mwenyewe kwa wanaume.’ Wengine
watasema, ‘ni kiherehere chake kimemponza.’ Hatua zozote za kumsaidia binti
huyu zinatafsiriwa kama kuunga mkono tabia yake mbovu. Kwa kuwa hakuna anayethubutu
kuonekana hana maadili, basi kila mtu anashindana kumshambulia ili nay eye aonekane
ni ‘mlinzi wa maadili ya jamii.’
Ikiwa binti huyu masikini atajifungua salama, atakabiliana
na changamoto nyingine ya ndoa. Si wanaume wengi wanaweza kuwa tayari kuanza
maisha na mwanamke mwenye mtoto tayari. Katika mazingira kama haya, ni wazi,
mzazi huyu ataishia kuwa maskini wa kweli kweli atakayelea mtoto fukara kuliko
yeye. Kosa kubwa la binti huyu ni kukosa elimu ya afya ya uzazi ambayo
ingemwezesha kukabiliana na shinikizo la kushiriki mapenzi kabla ya wakati
wake.
Inaendelea
Ahsante Sana Mwl.Christian Bwaya
JibuFutaAhsante sana mr bwaya kwa maelezo mazuri kuhusu tatizo hili sugu kabisa hapa nchini lakini pia hujagusia upande mmoja wa mwanafunzi mwingine anaipokea hiyo elimu lakini anaiona kama naona maana au inamgandamiza na hivyo kufuata Yale anayoyaona .
JibuFutaKwa mazingira ambayo Mimi nimetokea wazazi wengi wanajitahidi sana kuwaelimisha watoto wao hasa wanapokuwa elimu ya sekondari ndio maana nikasema kuna upande wa Mwanafunz mwenyewe na anavyoipokea hiyo elimu.
Ni makala nzuri sana nasubiri kwa hamu makala inayofuata
Asante sana mwalimu
JibuFuta