Vigezo Vinne Unapotafuta Msichana wa Malezi
PICHA: Gumtree South Africa |
MALEZI
katika enzi tulizonazo hayafanani na vile iliyokuwa hapo zamani. Mambo
yamebadilika. Kwa mfano, zamani wazazi wetu hawakuwa na shida ya nani hasa
abaki na mtoto nyumbani. Mama alikuwepo nyumbani. Kazi yake kubwa ilikuwa malezi.
Hata katika mazingira ambayo mama hakuwepo, bado walikuwepo ndugu na jamaa
walioweza kubeba jukumu hili kwa muda.
Hivi
sasa mfumo wa malezi umebadilika. Wazazi ambao wote kwa pamoja wanalazimika
kwenda kazini, wanalazimika kuweka utaratibu mzuri wa mtoto kupata malezi
yasiyo na mama.
Ulazima wa malezi mbadala
Kwa
wazazi wengi, zipo huduma mbili mbadala za malezi. Moja, huduma zisizo rasmi za
malezi zinazopatikana katika mazingira ya nyumbani. Kwa mfano, wazazi huwaomba ndugu
na jamaa wanaoishi katika mazingira ya nyumbani kumwangalia mtoto ili
kuwaruhusu kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.
Pili,
zipo huduma rasmi zinazotolewa kwenye vituo maalum vya malezi kwa watoto kwa
mujibu wa sheria. Kupitia utaratibu huu, mama humkabidhi mwanae kwa mlezi,
aghalabu mwenye utaalamu wa makuzi, kuanzia asubuhi na humfuata mtoto baada ya
saa za kazi. Katika kituo cha malezi, wazazi huchagua huduma zinazolingana na
mahitaji yao.
Kwanza,
wanaweza kuhitaji uangalizi wa mtoto pekee bila matarajio ya elimu rasmi (day
care). Lakini wanaweza pia kuhitaji mtoto apatiwe malezi sambamba na elimu
rasmi (nursery). Aidha, ikiwa umri wa mtoto tayari unaruhusu, wazazi wanaweza
kumwanzisha shule ya msingi kwa mfumo wa kutwa au bweni.
Tutajadili
huduma hizi moja baada ya nyingine kwa kuangalia fursa na changamoto za kila
moja. Kwa kuanzia, tunaangazia huduma ya malezi rahisi kupatikana kuliko zote kupitia
wasichana wa kazi wanaoajiriwa mahususi kwa ajili ya kuwaangalia watoto.
Wanavyopatikana
Wasaidizi
wa nyumbani, maarufu kama ‘house girl’ ni watoto au vijana wadogo waliokulia
katika mazingira ya kawaida, mara nyingi kijijini, wanaoajiriwa na wazazi kwa
lengo la kuwasaidia kumtazama mtoto wakati wao wakiwa kazini. Sambamba na
malezi, wasichana hawa husaidia kazi za ndani kama vile usafi, kuandaa chakula,
kutunza nyumba na majukumu mengine kadri yanavyojitokeza.
Kwa
kawaida walezi hawa hupatikana kwa utaratibu usio rasmi unaotegemea mfumo wa
kufahamiana na ndugu, jamaa na marafiki. Ndugu hawa wanaweza kuwaunganisha
wazazi wanaomhitaji msichana anayetafuta kazi ya kufanya.
Hakuna
utaratibu rasmi unaowawezesha waajiri wenye uhitaji kuwa na uhakika na historia
yake, ujuzi wake pamoja na tabia zake kwa ujumla. Hata hivyo, kwa kubahatisha inawezekana
wazazi wakampata kupitia watu wanaofahamika.
Wajibu wao kimalezi
Kwa
ujumla, msichana wa kazi ndiye mtu anayetumia muda mwingi na mtoto kuliko mtu
mwingine yeyote kwenye familia. Ndiye anayefahamiana na mtoto kwa karibu zaidi
kwa sababu ndiye anayehakikisha mtoto anapata chakula na huduma nyingine za
muhimu wakati wazazi wakiwa kazini.
Kwa
upande mwingine, yamekuwepo matukio ya akina dada hawa kudaiwa kuwafundisha
watoto tabia zisizofaa. Matukio haya, mara nyingine, hutokea katika mazingira
ambayo binti mwenyewe hajui namna nyingine bora zaidi ya kukaa na mtoto.
Alivyolelewa yeye ndivyo anavyofanya.
Hata
hivyo, wakati mwingine, huwa ni matokeo ya visasi wanapojisikia hawatendewi haki
na waajiri wao. Kwa mfano, mara nyingi, wasichana hawa huajiriwa bila mikataba.
Malipo yao hayalingani na kazi nyingi wanazozifanya. Wengi wao huwa wa kwanza
kuamka na wa mwisho kulala. Hali ya kutokuridhika na mazingira ya kazi huongeza
uwezekano wa vitendo visivyotarajiwa.
Kwa
kuwa hakuna mzazi angependa nia njema ya kumtafuta msichana wa kazi ilete matatizo,
tunapendekeza hatua nne za kuchukua katika kuboresha huduma za malezi kupitia akina
dada hawa ambazo, kwa hakika, zinahitajika kwa wazazi wengi.
Mfahamu
kabla
Wapo
wasichana wanaotoka kwenye familia zilizokuwa na migogoro. Mazingira kama haya
huwafanya wawe wepesi kugombana, kukwazwa hata kuwa tayari kuwaumiza wengine.
Pia wapo wanaotoka kwenye familia zenye imani za kishirikina.
Fanya
jitihada za kumfahamu kabla hujafanya maamuzi. Huwezi kumfahamu mtu kirahisi
lakini ni vyema kujua ametoka wapi, aliishi vipi na familia yake, misimamo yake
na mambo mengine ya msingi. Ili hayo yawezekane, ni vizuri ukampata kupitia
watu wanaomfahamu vizuri.
Mwelimishe
ajue wajibu wake
Mitafuruku
mingi kati ya waajiri na hawa mabinti wakati mwingine inachangiwa na
kutokufahamu majukumu yao ipasavyo. Waajiri wengi huwa na matarajio makubwa kwa
akina dada hawa ingawa hawawasaidii kujua kile wanachopaswa kukifanya.
Ni
vyema mara baada ya kufanya makubaliano naye, hakikisha anajua utaratibu kamili
wa kazi. Afahamu anaamka saa ngapi, anatakiwa kufanya kipi siku nzima na kipi
hapaswi kukifanya. Ukifanya hivyo unapunguza uwezekano wa makosa ya kutokujua
jambo sahihi la kufanya.
Mtendee
haki
Mfanye
binti wa kazi awe sehemu ya familia yako. Mfanye ajisikie kupendwa kama
mwanafamilia mwingine. Mtu anayependwa huchangamka moyo na hivyo kuwa na hamasa
ya kujituma. Sambamba na hilo, epuka mahusiano yasiyo ya kimaadili na msichana wa
kazi. Makosa kama hayo hujenga mazingira ya kudharaulika. Ukidharaulika, ni
rahisi mwanao kuwa mhanga.
Aidha,
mtengenezee mazingira bora ya kazi. Kwa mfano, unaweza kufikiria kumtengenezea
utaratibu wa kujiendeleza kitaaluma. Hakikisha unaonesha kutambua kazi
anazozifanya. Kutambuliwa ni hitaji la msingi kwa kila mwanadamu. Kutambuliwa kunamjengea
ari ya kujituma.
Mfundishe
kwa vitendo
Onesha
kwa vitendo namna unavyotarajia mtoto ahudumiwe. Binti atajifunza kwa vitendo. Unapopata
muda fanya kazi za ndani kama unavyotarajia afanye yeye. Pika, tenga chakula,
fua nguo ili kuonesha kuwa unaishi matarajio yako. Unapofanya hivyo, binti atajifunza.
Kadhalika,
tambua kuwa upo uwezekano wa mwanao kujifunza tabia usizozitarajia. Unaporudi
nyumbani jua maendeleo ya mwanao kitabia. Jitahidi kuzungumza na mwanao kubaini
ikiwa yapo yasiyofaa aliyojifunza. Unapoyabaini chukua hatua za haraka
kuyarekebisha.
Maoni
Chapisha Maoni