Dan Vinci Code: Ukweli unaouma?


Dan Brown mwandishi wa kitabu kinachokwenda kwa jina la Da Vinci Code, kafanya kile ambacho binadamu wengine hatuthubutu hata kukijadili. Kaamua kuchokonoa mambo ya kiimani ambayo watu tunakwepa kuyahoji, kwamba hayajadiliki. Ni dogma. Trela ya filamu yake hii hapa.

Katika Da Vinci code, Dan Brown anajaribu kuchimbua “kweli” zilizojificha nyuma ya ukristo, “kweli” ambacho zimefunikwa na kanisa ili kuwapumbaza watu waamini kwamba Jeshua alikuwa mwana wa Mungu.

Kwa kadiri ya Da Vinci Code, ukweli wenyewe ni kwamba Ukristo ulianzishwa na “nabii wa kawaida” ambaye hastahili kujidai kwamba ana uungu (divinity) wowote. Nabii mwenyewe ni Yesu Kristo. Kwa hakika, alimwoa Mariam Magdalena, ambaye baadaye ndiye aliyemchagua kuliongoza kanisa baada ya kifo chake.

Suala hili, kwa mujibu wa Da Vinci Code, liliwakasirisha sana wanafunzi wake na baada ya kusulubishwa kwake, Mariam Magadalena ilibidi atimuliwe, ndipo akakimbilia Ufaransa na mtoto wao waliomzaa na Yeshua “mume” wake.

Mwandishi anasema kwamba habari hizi hazifahamiki na wengi leo hii, kwa sababu vitabu ya injili ambavyo kwavyo pekee ndiko tunakopata simulizi za Yesu zilihaririwa kwa makini sana ili kuondoa maelezo yoyote yaliyojikita katika maisha ya “kawaida” ya Bwana Yesu. (Rejea uk. 244).

Vilevile kwa kadiri ya Da Vinci Code, biblia tuijuayo leo hii, iliwekwa sawa na Mfalme wa Rumi Constantine ambaye alikuwa ni mpagani. (Rejea uk. 231). Tafsiri yake ni kwamba wakristo wanamekubali kudanganywa na mtu amabye hata hakuwahi kuwa Mkristo.

Katika ukurasa wa 231, Leonardo Da Vinci ametoa maoni yafuatayo kuhusiana na Kitabu cha agano jipya:
“Many have made a trade of delusions and false miracles, deceiving the stupid multitude”. Halafu anaendelea, “Blinding does mislead us. O! Wretched mortals, open your eyes”. Sijathubutu kutafsiri, nikihofia kupoteza maana halisi.

Nimekisoma kitabu miezi kadhaa iliyopita, wakati tayari nimekuwa msomaji wa vitabu vingi vya Theolojia, nikijaribu kutafuta majibu ya maswali yangu mengi kuhusu imani yenyewe ya Ukristo.

Kuna suala linaitwa canonization katika Theolojia, yaani utaratibu wa kuyatambua maandiko ili kuyafanya yawe sehemu ya Biblia. Katika kitabu cha Jensen’s Survey of the New Testament, utaratibu huu ulifanyika kwa maongozi ya ziada, yaani Mungu mwenyewe. Katika ukurasa wa 22 anasema “…God gave to His people (japo hawataji) in collective sense, the spiritual perception to recognize in each of these books genuine marks of divine inspiration and authority. With the Holy Spirit’s guidance, they knew what spurious writings to reject, as well as what genuine writings to accept”.

Tatizo la masuala haya ya kidini yanapojadiliwa anatangulizwa Mungu kabla ya hoja. Matokeo yake unakuta maswali mengi yanamezwa kirahisi na majibu kwamba ni Mungu. Hivyo unakuta hofu kwamba tunajaribu kujadili mambo ya Mungu, inatutia woga wa kuendelea mbele.


Suala la kujiuliza ni kwamba ilikuwaje maandiko mengine yaonekane yanafaa na mengine yakaonekana ni ya kutupa? Tutapuuza suala hili tukienda haraka kwa kufanya kama ilivyo ada ya majadiliano ya kidini: Kutangulize imani! Pengine yanayosemwa na Dan Brown ni ukweli ambao hao tunaoambiwa waliongozwa na Mungu waliuficha! Tutajuaje kama wana-theolojia wenyewe wanatuambia hivyo?

Kwa mujibu wa Bruce, F.F katika kitabu chake cha “The books and Parchments” uk. 104-13, tunaambiwa kuwa wakati hawa jamaa wanaongozwa na Mungu (Dan Brown anasema ni pamoja na pagani Constantine) wanakubaliana kitabu kipi kiingie kwenye orodha na kipi kitupwe kapuni, kukawepo mabishano mazito kuhusu vitabu vinavyoitwa Antilegomena yaani Waebrania, Yakobo, Waraka wa 2 na 3 wa Yohana, Yuda na waraka wa 2 wa Petro. Ninashangaa mabishano yatokee wapi wakati tunaambiwa hawa mabwana Roho wa Mungu alikuwa juu yao? Sio kwamba ni hekima tu?

Ndio maana mpaka leo Wakatoliki wanabiblia yao tofauti na Wakristo wengine. Ya kwao ina vitabu ambavyo wenzao wanaviita Apocrypha, yaani Wamakabayo, Tobit na vingine!

Ukweli ulio wazi ni kwamba kuna mkanganyiko mkubwa katika zoezi zima za canonization. Mkanganyiko huu hauwezi kujibiwa kwa majibu rahisi rahisi.

Mwaka jana nimekutana na bwana moja, rafiki yangu nikataka kujadili naye Da Vinci Code, nikijua atakuwa na majibu kwa kutumia shahada ya Theolojia anayoisomea. Akaja juu. Kila nilipojaribu kudai majibu ya hoja, akawa ananituhumu kuwa sina imani na kwamba nimepotoka. “Huwezi kuuliza maswali kama haya kijana!”

Tukavutana sana mwishoni nikamwuliza umekisoma kitabu chenyewe? Kumbe wala hajakisoma. Nikamwambia usibishe kwa kusikia, kusikia sio kufahamu! Akanimbia: “Mimi nasoma theolojia naelewa biblia…najua implication ya hayo unayojadili”. Nikamwuliza swali nililolibandika juu ya blogu yangu: “Unajuaje kwamba unajua? Sio kwamba unaelewa Theolojia kwa sababu umetanguliza imani kwanza?”. Akafikiri sana, mwisho akaanzisha mjadala ambao mpaka unahitimika sikupata majibu ya maswali yangu. Nikajua jamaa yuko “biased”.

Sasa sijui anayekosea ni huyu anayejaribu kufikiri au aneyeogopa kabisa kufikiri?

Maoni

  1. Bwaya shukrani sana kwa mjadala huu mzito. Siku moja nilipita maktaba baada ya movie ya Da Vinci kutoka nikitaka nijinunulie kitabu hicho kwanza. Kilichoniudhi ni kuwa kuna mitabu mingi sana (mitabu ni kiswahili kisicho rasmi nimeandika kwa kupenda tu) ambayo kama unataka kuisoma uimalize basi kuna haja ya kufungua shahada ya Da Vinci kabisa. Kuna maswali ya muhimu kama ulivyoyaahinisha na ukweli unabaki juu ya umuhimu wa kuruhusu vichwa vyetu kufikiri kuliko kukubali kila jambo bila kufikiri.

    JibuFuta
  2. Hili swala zito Mzee!Ukiuliza maswali hukawii kuambiwa imani yako ni pungufu!Mimi nafikiri ingekuwa rahisi sana kwangu kama ningeogopa kufikiri, lakini tatizo nililonalo ni kwamba nashindwa kujizuia kufikiri

    JibuFuta
  3. Makene,

    Hatukuwezi misamiati. Leo umekuja na mitabu! Uzuri wa Kiswahili chetu mtu unaweza "kuimprovise" neno kirahisi. Halalfu bado watu wanadai oooh, kiswahili lugha ya uchochoroni!

    Ningejua mapema ningechagua kusoma Kiswahili. Sina hakika kama ninaweza sasa ila ntajaribu ili niwe "Makene".

    Kuhusu Da Vinci, ni kweli kama unavosema kuna haja ya kuwa na Kozi inayojitegemea. Maana ina mambo mengi mengi ya kiudadadisi. Tatizo jamii yetu haipendi kujisomea, sembuse kujadili mambo kama haya!

    Manake kuna watu wamefugwa kwenye kiboksi cha mawazo ambacho Kitururu anasema amekibomoa siku nyingi.

    JibuFuta
  4. Huyo bwana aliyekuwa anabishana nawe kuhusu kitabu ambacho hajasoma simshangai. Ni sawa na mkristo anayekwambia kuwa kurani sio kitabu cha mungu. Unamuuliza, "Je umekisoma?" Anasema hajakisoma. Sasa amejuaje? Hivyo hivyo kwa Muislamu anayesema biblia ni kitabu cha uongo huku hakakisoma, pengine kamsikiliza Mazinge!

    Tuna tabia ya kujenga mtazamo juu ya mambo kwa kufuata hisia tu.

    Napenda Bwaya unajadili masuala ya dini maana watu wetu wengi huamini kuwa ni kosa kujadili na kuhoji masuala haya. Eti wanasema, "Mambo ya dini yaache yalivyo." Viongozi wa dini wanapenda sana wenye mitazamo kama hiyo. Ndio maana walishtuka sana na kuchukia alipotokea Martin Luther na mistari ile 99 akihoji kanisa linaloongozwa na wanaume, Katoliki.

    Simon: nakubaliana nawe kuhusu kufikiri. Mtu anaweza kukunyang'anya haki zako zote, ila haki ya kufikiri na kuwa na fikra zako hawezi kuitwaa.Labda wakupige sindano uwe mwendawazimu...lakini wendawazimu nao wana fikra zao ingawa ni tofauti na zetu tunaodhani tuna akili timamu.

    JibuFuta
  5. Ni mkweli Ndesanjo, mambo yetu yetu mengi yanakwenda kwa hisia. Na mara nyingine hata hisia hakuna, basi tu tunafanya kushukilia masimulizi ya wengine ambao nao sio kwamba wana hakika na wanachokisema, hapana. Wanaongozwa na hisia.

    Lakini tunapofanya hivyo tuwe tayari kuonekana ni mahayawani. Askofu Milingo katimuliwa kwa kuhoji kwa nini "mabrother" hawaoi wakati fundisho hilo halina mashikio kwenye biblia!

    Karugendo naye nadhani mpaka leo anauguza majeraha ya kuhoji "dogma".

    Hata hivyo, ni muhimu tuhoji na kuhojia. Maana uhuru huo tunao.

    JibuFuta
  6. Mijadala ya dini NDIYO. Dini ni kitu gani? MUNGU ni NANI?/ MUNGU ni NINI? Je, kuna Mungu? Je, ni dini ipi ETI ni ya kweli? Je, Kristo alianzisha dini? Je, kuna Mungu mmoja au Miungu wengi? Je, Afrika haikumjua Mungu kabla ya kuja kwa wageni (Waarabu na Wazungu)? Je, ni sahihi kwa dini nyingi kuongozwa na viongozi wanaume zaidi kuliko wanawake?

    Kuhusu dini na imani mtu unaweza kuuliza maswali mengi sana. Na daima sidhani kama kuna jibu lililo sahihi zaidi kuliko jengine. Da Vinci ameandika aliyoandika. Nimesoma kitabu chake. Nimesoma pia Decoding the Da Vinci. Mwisho wa yote bado mtu unabaki na maswali yaleyale. Hakuna hatua ya maana unayopiga.
    Labda aliloeleza ndugu yetu hapo juu kuwa yeye kaamua kuwa 'neutral' ndiyo jibu? Sina hakika. Ijumaa watu wanakwenda misikitini. Wakitoka huko wanarudi katika maisha yao ya kila siku. Walio wezi wanakwenda kuiba. Walio malaya wanakwenda kujiuza. Wanafiki wanaendelea na unafiki wao. Wanyanyasaji wa kisiasa wanaendelea na unyanyasaji wao. Wenye mabavu wanawatwanga wasio na mabavu kwa risasi za kichwa. Hivyohivyo, wale wanaokwenda makanisani siku za Jumamosi na siku za Jumapili. Matendo yao hayatofautiani na ya hao niliowataja hapo juu. Je, Ukristo na Uislamu vimeleta nini zaidi ya maumivu kwa ubinadamu. Soma historia. The Crusades. The Jihads. Hivi, mbona dini ya Ukristo haikusaidia watu wasiuane kule Rwanda mwaka ule wa 1994? Je, si asilimia 90 kule ni Wakristo? Vipi kuhusu Somalia, kwa nini Uislamu usilete mtengemao na amani pale? Je, si asilimia 98 ya Wasomali wote ni Waislamu?
    Kumbe nini jamani? Inawezekana dini ni 'trade just like any other trades?' Kwamba kuna watu wanapata mkate wao wa kila siku kwa kupitia dini? Kwamba waumini ni hasa wateja? Kwamba kupigana madongo kwa dini hizi ni harakati za dini fulani kujiongezea wateja zaidi? Je, turudi kwenye dini zetu za asili? Dini tunazoziweka chini ya mvungu? Huku tunaapa kwa Biblia ama Kurani kushika nafasi ya urais au nyingineyo na huku tumevaa hirizi tuliyopata Bagamoyo ndani ya mavazi yetu?

    Dini. Dini. Dini. Ni nini wewe? Ni nani wewe Dini?

    Ciao!

    JibuFuta
  7. Nimesoma Kitabu cha dan na DVD yake. Sasa huyu Bwana kifupi amesoma historial ya kweli, nayajua majina ya mahali, majina ya magombo ya kihistoria na kwa kuwa majibu sahihi hana akajenga hekaya yake maana kama hakuna majibu bayana basi wengine huona ruksa kujenga nadharia yako hapo ingawa ni sahihi kabisa kila mtu kutoa tafsiri yake juu ya swali-wazi.

    Kwa kujenga hekaya juu ya vitu hivyo Dan ametunga riwaya iliyojiuza sana.

    Mashaka aliyojengea yametokana na vitabu viitwavyo "Injili zilizopotea" Hizi injili inasemekana ziliandikwa na Petro "injili ya petro", Injili ya Filipo", Injili ya mariamu madgalena" Injili ya Tomaso" na kadhalika. Katika injili hizo ambazo hazikuwekwa katika Biblia zinazusha gumzo kuhusu Uungu wa Yesu, au Utu wa Yesu, Uongozi wa wanaume, Mariamu magdalena kuwa na uhusiano wa karibu sana na Yesu, Kuzaliwa kwa yesu, Kuteswa na kufa kwa Yesu na kufufuka kwa Yesu. Haya ni mambo ya msingi sana katika imani ya Kikristo tangu enzi hizo na hata leo.

    Kanisa la mwanzo walieleza habari za Yesu kwa neno la mdomo maana walifikiri Yesu atarudi karibuni sasa walipoona wanazeeka na wanaanza kufa ndiyo wakaona umuhimu wa kuandika mambo waliyoyashihudia kwa macho au kusikia. Hivyo kulikuwa na maelezo mbalimbali kutoka kwa waandishi mbalimbali. Hata haya maswali anayouliza Dan Brown yalikuwepo enzi hizo.

    Viongozi wa dini wa enzi hizo walipiga marufuku baadhi za hizi injili maana nyinginezo zilikuwa hazikidhi haja au nyingine zilijaa stori za kusikia zaidi ya ushuhuda wa macho au nyingine zilikuwa haziendani ma imani zao kwa sana. Shida ya Dan amejaribu kuegemea upande wa utata na kutunga nadharia itoayo majibu anayoyapenda au yatakayouza kitabu chake maa kumbuka kitabu cha Da Vinci ni riwaya kabisa ya kumpatia chakula kwa miaka mingi.

    Sasa sipendi kueleza kirefu hapa niwachoshe, kwa hiyo kama kukiwa na muda wa kutosha tunaweza kuchambua baadhi ya mambo ambayo ni mengi labda ukweli utajitokeza katika mijadala yetu.

    JibuFuta
  8. Nilikuwa natafuta darchat kwenye google,nikakutana na blogu yako,kwa kweli inavutia sana,mijadala yenu ni mizito inabidi mtafute jinsi ya kuwafikia watu wengi zaidi.

    JibuFuta
  9. my friends it is not possible for a normal human being to write a book like davince code never. we should be aware that some of the people are agents of satan

    if yoou dont trust the bible by history, fine but the bible it self is not bound by history but according to what is happening and what will happen in the future as everything is predicted before and it happen as how it was foretold in the bible
    the problem is you people want to forge loopholes in the bible by which you can exercise your wickedness
    someni vitabu vya unabii
    mtapata habari zenu .

    JibuFuta
  10. Mwidimi,

    Asante sana kwa mchango wako.

    Ipo nadharia moja inayodai kutowapo kwa uwezekano wa kufikia kitu kinachoitwa hitimisho sahihi katika jambo lolote. Sababu ni kwamba ni vigumu kuzipata taarifa (data) sahihi na toshelevu kuwezesha mchakacho wa kufikia hitimisho sahihi. Kwa sababu taarifa zinazohitajika hutofautiana baina ya wanadamu (ambao hutumia vyanzo tofauti tofauti kujipatia taarifa hizo) basi hutokea kila mmoja akawa na hitimisho lake sahihi. Usahihi huo huo ukitizamwa kwa miwani ya lensi na wengine huleta majibu mengine kabisa.

    Hoja anazotoa Dan kimsingi ni mawazo yake yaliyotokana na taarifa chache alizofanikiwa kuwa nazo. Na kwa sababu ya uchache wa taarifa hizo alizokuwa nazo, hatutazamii awe na majibu sahihi. Na ndivyo ilivyo kwetu nasi kwamba hatuwezi kuwa nayo Tunachokifanya ni kuangalia hoja zake na mashikio yake kihistoria na kadhalika.

    Injili "zilizozimwa" ndiko alikoanzia Dan. Sasa ni vizuri tukajiuliza: Injili hizi kwa nini zilipigwa marufuku na viongozi wa dini ambao pengine walitumia masimulizi.

    Sasa kama hivyo ndivyo, kwa nini Injili zingine zitupwe kapuni? Kwa sababu ziliandika maisha ya kawaida ya Yesu jambo ambalo halikuwapendeza viongozi wa dini walikuwa wanataka Yesu aandikwe wanavyotaka wao na kwa mujibu wa mafundisho yao?

    Isije ikawa historia ya Yesu ilibinuliwa na watu fulani kwa maslahi yao, kiasi kwamba akitokea mtu kuifunua tunamlaani kwa nguvu zote.


    Simbadeo,

    Maswali yako ni ya msingi sana katika kuelewa mambo haya yanayohusiana na imani zetu. Tunawajibika kama binadamu wenye uhuru wa mawazo kupata majibu sahihi ya maswali uliyoyauliza.

    Je, kuna Mungu? Niongeze kidogo: Je, tunajuaje kama yupo? Tunawezaje kuwasiliana naye? Haya maswali si ya kupuuza.

    Hata hivyo, mijadala ya dini na imani inakuwa na ugumu wake kwa sababu kila mwenye imani/dini yake anavutia upande wake hata inapobidi kutumia mabavu. Lakini mimi nafikiri tunaweza kuwa na mahitimisho mazuri na sahihi zaidi kama tutaondoa upendeleo wa kidinia na kiimani.

    Kwa hakika, tukiwa wazi na wakweli, dini zetu zimeleta hasara zaidi kuliko faida kwa jamii. Ipo mifano mingi katika hili. We chukulia waumini wanaoamini kuwa kuwatoa roho watu wasio na dini kama yao ati ni kujipatia thawabu kwa Mungu. Ninachojiuliza: Mungu huyu ni wa aina gani anayeweza kuhalalisha kuuawa watu kwa kisingizio cha utetezi wa kidini? Ndio maana ninadhani miungu ipo mingi. Haiwezekani mungu huyo aseme hivi kwenye dini A, halafu maagizo hayo yahitilafiane na ya kwenye dini B.

    Dini za asili ndio utatuzi?

    JibuFuta
  11. Mada hii ni muhimu sana kuijadiri kwa sababu kitabu hiki cha da vince code,elimu yake ime kwisha enea karibu ulimwengu mzima na lengo kubwa la kitabu hiki si kuleta ufahamu bali kurejesha ulimwengu ulio aribiwa kwa gharika kipindi cha nuhu na pia kitabu hiki kinalengo la kutafuta watu watakao ujenga mnara mnara wa baberi upya wa Baberi.
    Hapo juu nimetumia lugha ya picha lakini lengo langu ni kwamba "kitabu cha Da Vince Code kinatafuta watu watakao jitoa kueneza Imani ya kuupotosha Uungu wa Yesu ili kujenga mnara yaani Dini itakayo kuwa na misingi ya kitabu hiki ulimwenguni kote"

    TAMBUA KWAMBA;
    Tangu mwanzo wa huduma ya Yesu Kristo mpaka alipokufa na kufufuka katika wafu kisha akapaa mbinguni, wanafunzi
    wake walikuwa wakimpa heshima ya uungu, sawa na Mungu kama alivyojitambulisha kwao yeye mwenyewe. Kwa hiyo,
    kabla ya hata ya mfalme Constantine kuitisha mkutano wa Nikea, wakristo walikuwa wakimwabudu Yesu kuwa ni Mwokozi
    na Mungu.

    Hata hivyo, mnamo karne ya nne, aliibuka mzushi mmoja jina lake Arius aliyeanzisha kampeni ya kile alichokiita kutetea
    umoja wa kuwa ni nafsi moja na akaanza kufundisha kwamba Yesu hakuwa Mungu, bali naye ni kiumbe, japokuwa ana
    hadhi zaidi ya malaika, lakini si Mungu. Lakini Athanasius na viongozi wengi wa Kanisa walisimamia vikali kuwa Yesu
    alikuwa ni Mungu katika mwili.

    Mfalme Constantine akitaka kusuluhisha mgongano huu ili kuleta amani katika himaya yake na kuondoa mgawanyiko
    kati ya Mashariki na Magharibi, mnamo mwaka 325 B.K. aliitisha mkutano wa Maaskofu 300 huko Nikea waliokusanyika
    kutoka kila mahali duniani.

    Kwa hiyo, kama nilivyokwisha kudokeza huko nyuma kwamba wanafunzi wa Yesu waliamini kwamba Yesu ni Mungu
    badala ya kuwa kiumbe. Hii ilitokana na mtume wake wa kwanza kuandika vitabu na nyaraka za kwanza kuhusu maisha
    ya Yesu zikimtaja Yesu ni Mungu.

    Tunaporejea madai ya kitabu cha ‘The Da Vinci Code’ kinachodai kwamba madai ya uungu wa Yesu yalitengenezwa na
    kuingizwa katika maandiko mnamo karne ya nne, ndipo tunapogundua kwamba siri ya kashfa dhidi ya imani ya Kikristo
    imelenga kupinga moja kwa moja uungu wa Yesu.

    Mwandishi wa kitabu hicho, Bw. Brown anatetea uzushi wa Arius. Aidha, Bw. Brown hakutaka kusema ukweli kwamba
    katika mkutano wa Nikea, tamko la kuendelea kukiri uungu wa Yesu liliungwa mkono na Maaskofu 318 na kwamba ni
    wawili tu ndio waliokataa kukubaliana na maamuzi ya kikao hicho. Wakati Arius aliendelea kuamini kwamba Nafsi ya
    Baba ndiyo ilikuwa ni Mungu peke yake na kwamba Yesu alikuwa kiumbe wake mkuu, Baraza la Maaskofu wengine
    walishikilia msimamo wa Nafsi tatu za Mungu ambazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hii inadhihirika katika tamko la
    imani ya Nikea linapotetea uungu wa Yesu pamoja na Roho Mtakatifu.

    Kuzaliwa kwa Yesu na Mariamu si mwanzo wa kuwepo kwake

    Habari za Yesu kujulikana kuwa ni Mungu zililetwa na Malaika Gabriel kwa Mariamu. Katika ufafanuzi malaika Gabrieli
    aliweka bayana kwamba huyo ambaye angezaliwa duniani ni Mwana wa Mungu aliye juu: “Tazama utachukua mimba na
    kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana
    Mungu atampa kiti cha Enzi cha Daudi, Baba yake.” (Luka 1:32).

    Mtu wa pili kutaja habari za uungu wa Yesu ni Yohana Mbatizaji aliyetangulia kutabiri habari za kuja kwake. Hii
    inadhihirishwa na pale ambapo Yesu alipotaka kubatizwa na Yohana alitaka kukataa akisema hastahili kumbatiza:
    “Lakini Yohana alitaka kumzuia, mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? (Mat.3:14).
    Wapinzani wa uungu wa Yesu hujikwaa katika historia ya kuzaliwa kwa Yesu katika mwili, wakidhani huko ndiko mwanzo
    wa kuwepo kwake. Lakini maandiko yanadhihirisha kwamba kabla ya Kristo kuja duniani, alikuwepo kabla! Ndiyo maana
    wakati Yesu anajadiliana na Mafarisayo kuhusu habari za Ibrahimu ambaye walimwamini kuwa ndiye baba wa imani
    kwao, yeye akasema alikuwepo kabla ya Ibrahimu hajakuwepo: “Yesu akawaambia, Amin amin nawaambia, yeye
    Ibrahimu asijakuwapo, mimi niko.” (Yoh.8:58)

    Ushahidi kamili ni jinsi Yohana alivyoanza kuandika habari za Yesu. Tofauti na Waandishi wa Injili za Mathayo, Marko na
    Luka, Yohana alianza kwa kuandika kuwepo kwa Neno ambaye hatimaye anataja alikuwa ni Mungu: “Hapo mwanzo
    kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
    Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. (Yoh.1:1-13)

    Aidha, Yohana ndiye anayefunua kwamba huyu Neno ambaye alikuwa Mungu na alihusika katika uumbaji wa vitu vyote,
    ndiye alikuja duniani na kufanyika mwili: “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake kama
    wa Mwana pekee atokaye kwa Baba amejaa neema na kweli” (Yoh.1:14)

    Mwisho kabisa, tunasoma habari za Yesu alipomtokea Yohana huyu huyu, alipokuwa ametupwa katika kisiwa cha Patmo
    kama mfungwa wa dini. Hapo ndipo Yesu anajitambulisha kwake tena kwa sifa ya Mungu mwenyewe: “Mimi ni Alfa na
    Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.” (Ufu.1:8)

    Yesu hakuoa kwa sababu alikuwa Mungu;

    Katika kuhitimisha makala haya, naweza kusema kwa ujasiri kwamba Yesu hakuja duniani kuoa na kuzaa, kwa sababu
    hakuwa binadamu kwa asili. Alivaa mwili wa binadamu kwa sababu ya ukombozi wa binadamu kutoka katika dhambi.

    Na hii ndiyo inamtofautisha Yesu na manabii au mitume wa dini zote duniani. Yeye alikuwa Mungu kabla, ni Mungu hata
    sasa na ataendelea kuwa Mungu milele. Wazushi wote waliotangulia na wanaoendelea mpaka sasa akiwemo Brown na
    kitabu cha ‘The Da Vince Code,’ wametumiwa na Ibilisi kutaka kumfanya Yesu kuwa binadamu wa asili. Nia ni kuwafanya
    binadamu waondoe imani yao kwake wasimwamini kuwa ni Mungu mwokozi wao. Hakuna uongo mpya kwa sababu Ibilisi
    ambaye ni baba wa uongo hajabadilika.

    Mwisho, ningependa kusema kwamba uungu wa Yesu si wa kupewa, bali ndiyo asili yake. Kila mwenye kutaka
    kuthibitisha uungu wake anaweza kukutana naye binafsi akajitambulisha kwake kama alivyojitambulisha kwa wanafunzi
    wa kwanza. Maana Yesu ni yeye yule jana, leo na hata milele.

    JibuFuta
    Majibu
    1. UBARIKIWE kwa ufufunuzi mzuri ''wapinga Kristo wapo wengi sana kuwapotosha watu, lakini KWELI ITABAKI KUWA KWELI MILELE

      Futa
  12. Sasa mwinjilisti, una hakika gani kuwa nukuu hizo ulizotupa zina uungu na sio falsafa za watu wa kawaida?

    JibuFuta
  13. kabla ya kujibu swali la mjumbe aliyepita ninapenda kwanza alitafakari swali aliloliuliza kwa maana swali lake lina zaa swali jingine la upande mwingine kwamba kati ya "Da Vince Code" na "Biblia" ipi ni falsafa ya binadamu wa kawida.
    Lengo la swali hilo kuzuka ni kuweka usawa kati ya vitabu vyote viwili jambo ambalo mjumbe aliye uliza swali hakulizingatia.
    TAMBUA;
    Ili kuweza kutambua kati ya Da Vince Code na Biblia ipi ni falsafa ya watu wa kawaida, ni vyema kwanza sisi sote tutafute maana kamili ya neno falsafa ndipo tuta kapo tambua kwamba ipi ni falsafa ya watu wa kawaida.
    FALSAFA ina maana ya itikadi,mbiu,ekima yenye lengo lakuleta mabadiliko katika jamii usika,mabadiliko hayo yana weza kuwa mazuri au mabaya kwa mfano "azimio la Arusha" lililo anzishwa na Hayati Baba wa taifa lilikuwa ni falsafa kwa maana lilikiwa na mbiu ndani yake yenye lengo lakutaka watu waishi maisha ya ujamaa.kuna watu wengi ambao nikiandika habari zao na falsafa zao ili kuweka sawa tafsiri hii nina weza kuchukua muda mwingi sana,mfano hitler,mobutu,mandela na wengineo,tambua katika hao kuna wengine falsafa yao ilileta matokeo mabaya,kwahiyo kwa vile falsafa ni hekima,mbiu na itikadi ina weza kuleta migogoro mingi katika jamii,kwasababu kabla ya kuwasilisha falsafa yako nilazima utambue kwamba kila jamii ina falsafa yake na bila falsafa, hakuna maendeleo kwa hiyo kama falsafa yako itapingana na jamii husika ni lazima patatokea matokeo mabaya.
    ELEWA KWAMBA
    Falsafa ya mtu ndiyo inayo mtambulisha mtu kama ni mwema au ni mbaya kwakuliangalia kusudi la hiyo falsafa(mwisho na matokeo ya hiyo falsafa)

    Nitamalizia kesho muda wangu hautoshi

    JibuFuta
  14. Sijui kwamba mimi ndio sijaelewa ama ni Mwinjilisti.

    Ninavyodhani, mjumbe aliyepita anataka ufafanuzi wa ikiwa kuna ushahidi kuwa biblia ni maneno ya Mungu. Alivyomwelewa si sahihi. Hakuwa akitaka kulinganisha kipi ni kitabu cha mungu kati ya biblia na Da Vinci. Kwanza inaeleweka kuwa Da Vinci ni novo tu, ama mawazo kama haya ninayoandika hapa, na wala hajadai kuandika mambo kutoka kwa Mungu.

    Lakini biblia inadaiwa kuwa ni kitabu cha Mungu na ndio maana Minjilisti anakinukuu kama tulivyoona. Sasa swali ni kuwa tutaaminije kuwa nukuu hizo ni za Bwana? Namba kufafanua. Endelea Mwij.

    JibuFuta
  15. Kabla ya kuendelea,na sehemu niliyoishia
    Kwanza, nina penda kuweka sawa kwamba kitabu cha Da Vince Code ni kitabu kinachopinga uungu wa Yesu na akuna kitabu kingine kinachozungumzia Uungu wa Yesu isipokuwa Biblia, na kihistoria Biblia ni ya kwanza Kujitokeza,kwanamna hiyo Mtunzi wa Da Vince Code alitunga kutokana na mawazo yake hasi kuhusu Biblia Haswa maisha ya Yesu.
    Pili;Da Vince Code ni hadithi iliotungwa na mtu wa kawaida na kuwekwa kwenye kitabu kwa mfumo wa noval,yenye lengo la kukanusha Uungu wa Yesu kwa kumtumia maria Magdalene ili kuleta kashfa kwa imani husika (ukristo)

    Tatu, kitabu cha Da Vince Code kina wafuasi kamili na kinaendelea kupata wafuasi kila kukicha, kwa mfano nchini Marekani Kumezuka dini inayo tumia falsafa ya Da Vince Code na kuna kanisa linaloendea kutumia falsafa hii kukusanya watu nchini humo,

    JIULIZE KWANZA
    Kama vitabu vyote vina wafuasi je wewe upoupande gaini ?
    Kwa hiyo atakama Da vinc Code ni Noval ya kawida ni lazima tutambue kwamba ina wafuasi wanayoiamini na kamwe hawawezi kukichukulia kama kitabu cha kawaida,hii ndiyo sababu nilisema kwamba "kitabu cha Da Vince Code kinatafuta watu watakao jitoa kueneza Imani ya kuupotosha Uungu wa Yesu ili kujenga mnara yaani Dini itakayo kuwa na misingi ya kitabu hiki ulimwenguni kote",kwa hiyo nita muhubiria mfuasi wa Da vince Kama nitakavyo fanya kwa wenye imani ya hindu ,uislamu na wengineo, kwa maana wote wanamzungumza Yesu kwa njia wanayo ijua wao na wote wana vitabu wanavyo viamini,
    Kwahiyo ninapojibu swali la mjumbe aliyepita ninajibu akiwa mtu anaye kiamini kitabu cha Da vince na mimi nikiwa naamini Biblia na Uungu wa Yesu.ili niweze kumsaidia ni lazima tuangalie umuhimu wa vitabu vyote viwili pande zote za imani kama ninavyofanya kwa waumini wa dini zingine.
    Kwa jinsi hiyo anayo haki ya kujibiwa swali lake kwa maelezo ya kutosha.kwa maana nina heshimu maamuzi yake na maswali yake,hii ndiyo sababu siku ficha jina langu kwa wote.
    nitaendelea na swali la mjumbe nita kapo kamilisha taarifa ya kutosha ili kunielewa vizuri.

    JibuFuta
  16. Furaha yangu ni kuona wasomaji wakishiriki mijadala kwa kuacha maoni yao, badala ya kusoma na kuondoka.

    Mwinjilisti Okuku, nakukaribisha kwenye mjadala huu. Nafurahi kwa sababu naamini, kwa kule kuwa mwinjilisti, maana yake ni kwamba wewe ni mtetezi wa Yesu moja kwa moja, na kwamba tutarajie majibu ya kina kutoka kwako hasa yanayohusiana na biblia.

    Nitachangia baada ya kusoma mchango wako ulioahidi kutupa.

    Itapendeza tukijenga utamaduni wa kujadiliana kwa kupambanisha hoja tofauti tofauti. Tukubaliane kuwa sote tunahitaji kujifunza. Sote tunayo machache tunayoyafahamu na hivyo mengi hatuyafahamu. Ndio maana tunahitaji kujifunza.

    Najua si wasomaji wote wanao mtazamo wa kiinjilisti.

    Hata hivyo, naamini kuwa mwinjilisti maana yake ni kwamba unao uzoefu huo wa kueleweshana na watu mnaotofautiana mtizamo.

    Naheshimu mawazo ya wasomaji wasiopenda kujulikana majina yao. Wapo watu hujisikia huru zaidi wasipofahamika wao ni akina nani. Tuwaache watumie haki yao. Muhimu ni hoja zao.

    Hivyo, ninaamini kuwa mwinjilisti pamoja na wengine wenye mtizamo kama wa kwako, hamtasita kuyatolea ufafanuzi wa kila masuala yatakayokuwa yakijitokeza.

    Tuendelee kujadiliana. Tujielewe. Tuko pamoja.

    JibuFuta
  17. mimi ni mfuasi wa kristo na Yesu Kristo ni Mungu Kweli kwa Mungu Kweli' Yeye ni Alfa' na Omega na ufalmwe wake si wa dunia hii hi bali watoka kwa Baba. Kama alivyosema Mwinjilisti ukisoma Biblia Takatifu Kitabu cha Yah.1:1-14 inajieleza vizuri uwepo wa Kristo Yesu Kama Neno aliyekuwepo kwa Baba tangu kale
    Atukuzwe Baba, Mwana,na Roho Mtakatifu Amina.

    JibuFuta
  18. Bado najiuliza nakipata wapi kitabu hiki in swahili...

    Nitumien link plz kama kuna sehemu..

    matiahyera9@gmail.com

    JibuFuta
  19. Kiukweli nimesoma kitabu hiki Mara mbili lengo langu kupata uelewa wa kutosha ambao Mr Brown amependa tujifunze toka kwake,ukweli usio pingika kuwa mwanadamu ni mkubwa kuliko hizi dini tunazo zifuata leo hii,mwanadamu uko huru kujiuliza maswali ya msingi hili kujijua na kujielewa wewe ni nani,umetoka wapi na kwa nini uko duniani na mwisho unaenda wapi mara baada ya kufa? Bwana Brown ametufungua jicho la tatu kwa kufichua mambo yaliyo fichwa na kutaka tuyafuatilie na tuyajue. Imani ni jambo gumu sana kwani ata definition yake ni tata kuihoji na kuelewa kwa ufasaaa.

    JibuFuta
  20. Mimi ni Black Rambo kutoka Grammy, ninafanya kazi katika Kambi ya Grammy, mke wangu alifariki mwaka 6 iliyopita na tangu nimekuwa nikimtunza mwanangu pekee aitwaye Clinton, rafiki yangu wa ushauri wangu wa kumtafuta mke, kwenye upekuzi wangu nilikutana na Jennifer alikuwa na mwanamke wa Kiingereza, Nilimpenda sana kiasi kwamba ningeweza kumpa kila kitu alichokuwa na umri wa miaka 37, baada ya muda fulani wa uchumba nilikuwa na mapenzi sana naye, tulikuwa na kutokuelewana, na alivunja na mimi na ninamsihi arudi mwanangu aitwaye alisema Hapana, kwamba amempata mtu mwingine, na tunapendana sana baada ya siku kadhaa nilisoma makala kuhusu jinsi Dk Lomin anaweza kusaidiana , Niliamua kutoa jaribu, nawasiliana na Dk Lomi kwa msaada aliniambia nini cha kufanya ili kumrudisha mpenzi wangu niliyefanya, alifanya maombi na Jennifer alikuwa nyuma ananipenda na kunithamini zaidi sasa, na tuna wakati mzuri wa maisha yetu, Dk Lomi pia kuandaa baadhi ya mimea ya asili ambayo imenifanya niwe na nguvu na afya tena sasa nahisi kama kijana niliyemridhisha vizuri sana sisi sote tuna furaha, wasiliana na Dk Lomi kwenye WhatsApp namba +2349034287285 au barua pepe yake kwenye lomiultimatetemple@gmail.com ANA SULUHISHO BORA KWAKO.

    JibuFuta
  21. Maisha yangu Maajabu yanashangaza ushuhuda, Jinsi nimepata kisanduku chenye nguvu sana ambacho sasa ni pesa yangu mara mbili kutoka mia hadi elfu ya pesa ndani ya masaa 24, na pia jinsi nimerudisha mpenzi wangu wa zamani, sababu kuu niliwasiliana na Dk Lomi kwa msaada mimi kumrudisha mpenzi wangu wa zamani, basi ananisaidia ni nguvu kubwa ya kumrudisha mpenzi wangu wa zamani, na ananipenda na ananithamini sasa, basi mimi na Dr Lomi tukawa marafiki, baada ya mazungumzo kadhaa namuuliza ikiwa kuna njia anaweza kuniganga ili nipate pesa, hapo ndipo aliponiambia juu ya sanduku hili la uchawi, akaniambia kuna aina na saizi tofauti ya sanduku, aliniambia aina zote za sanduku, ningeweza kumudu ndogo tu ya sanduku, baada ya maombi muhimu anayofanya kwenye sanduku, ananipeleka kupitia huduma ya kujifungua, aliniambia niweke pesa ndani, niliweka ndani ya sanduku 100 euro baada ya masaa 24 nikagundua ilikuwa elfu 10 euro ndani, na nimekuwa nikitumia sanduku kwa miezi 7 sasa, mimi na mchumba wangu tunaishi maisha bora, ikiwa unahitaji b ack mpenzi wako au pesa spell wasiliana na Dr Lomi kwa barua pepe: lomiultimatetemple@gmail.com au WhatsApp namba +2349034287285 unaweza pia kumwandikia kupitia Jina la Mtumiaji la Snapchat: drlomi20 atakusaidia nje, asante kwa kusoma,

    Kwaheri Gerd Ulrich

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?