Unahitaji Nidhamu ya Fedha Kujikwamua Kiuchumi
PICHA: usaa.com |
Juma
lililopita tuliongelea uwezekano wa mfanyakazi kujikwamua kiuchumi. Kubwa ni
nidhamu. Unapokuwa na nidhamu ya mshahara, unaongeza uwezekano wa kuwa na
usalama wa kifedha.
Swali
linaweza kuwa, ‘Kinachomfanya mfanyakazi akose nidhamu ya fedha ni nini?’ ‘Inakuwaje
mchuuzi mdogo wa bidhaa awe na nidhamu ya fedha kuliko Afisa wa Serikali?’
Majibu
ni mengi. Moja ni uhakika wa kipato. Kwamba [mfanyakazi] una uhakika wa kupata
mshahara mwisho wa mwezi hilo pekee linaweza kutosha kukuondolea nidhamu ya
fedha.
Mjasiriamali/mchuuzi anaweza asiwe na uhakika huu. Kutokuwa na uhakika na kipato kunamwongezea
umakini wa kutumia vyema kile anachokipata. Kwa mfano, lazima ahakikishe kile alichonacho kinazalisha
kumpatia faida itakayomsaidia kuendeshea maisha yake.
Hapa
ndipo ilipo tofauti baina ya wafanyakazi na wajasiriamali. Mfanyakazi unaweza
kutumia kila senti unayopata kwa matumaini ya kupokea mshahara mwisho wa mwezi.
Mchuuzi
hawezi kuthubutu kufanya hivyo. Kwake, kile alichonacho ni mbegu ya kupanda
kumpa uhakika wa kesho.
Kwa
hiyo utaona mazingira ya kazi uliyonayo mfanyakazi hayakulazimishi kuwa na
nidhamu. Ili uweze kujenga nidhamu hiyo unahitaji kufanya kazi za ziada. Usipofanya
maamuzi ya dhati, ongezeko lolote la mshahara haliwezi kukupa unafuu wa maisha.
Makala
haya yanapendekeza mbinu nne unazoweza kuzitumia kukabiliana na ukosefu wa
nidhamu ya fedha. Mapendekezo haya manne yanadai mabadiliko makubwa ya tabia.
Ishi kwa bajeti
Kuishi
kwa bajeti ni kufanya matumizi yaliyopangwa kabla. Kinyume chake ni ufujaji.
Mtu ‘mfujaji’ hutumia kadri mahitaji yanavyojitokeza. Hapangi namna gani atatumia
fedha zake.
Ni
dhahiri ‘kufuja’ ni kazi rahisi kuliko mipango. Maisha yanayoongozwa na bajeti yana
gharama ambayo si wengi tunaweza kuwa tayari kuilipa. Lakini kwa kuwa unataka
kuona tija ya mshahara wako, lazima uwe tayari kulipa gharama hiyo.
Pangilia
mwelekeo wa mapato yako kabla hujayapata. Jenga utaratibu wa kuweka kumbukumbu
ya mapato na matumizi yako kila mwezi. Tabia hii inaitwa nidhamu. Mtu mwenye
nidhamu huweka utaratibu mzuri wa kujiwajibisha.
Unapokuwa
na utaratibu wa kujua wapi fedha zako zinaelekea na nini ufanye kurekebisha
mwelekeo, huo unaitwa uwajibikaji.
Ongozwa na sera ya fedha
Niliwahi
kukutana na bwana mmoja aliyeniuliza swali gumu, ‘Sera gani inaongoza matumizi
ya fedha zako?’ Nilidhani anatania. Nilifikiri mtu binafsi hawezi kuwa na sera
inayotawala fedha zake. Baadae nilijifunza somo muhimu.
Sera
ya fedha ni mwongozo wa matumizi ya fedha zako. Unapokuwa na sera unarahisisha
kazi ya kuainisha kipaumbele cha mapato yako.
Bila
kuainisha kipaumbele chako itakuwa vigumu kwako kujua namna gani unaweza
kutumia kile kidogo ulichonacho kukamilisha malengo unayojiwekea.
Kwa
mfano, unaweza kuwa na sera ya kuhakikisha matumizi yako ya kawaida (chakula,
mavazi, nauli, burudani) hayachukui zaidi ya asilimia 20 ya mapato yako kwa
mwezi.
Kadhalika,
kulingana na kipato chako, unaweza kuamua asilimia 30 ya mapato yako lazima iekezwe
kwenye akiba wakati asilimia 10 ikielekea kwenye sadaka au hisani kwa wenye
shida. Vyovyote iwavyo kulingana na kipato chako, asilimia hizo zinaweza
kuongezeka au kupungua kukidhi mazingira uliyonayo.
Pia,
kwa kuwa tunaishi kwenye jamii inayotegemeana, unaweza kuwa na sera ya kutumia
si zaidi ya asilimia 10 kuwasaidia ndugu na jamaa katika nyakati za shida na
raha. Huu ni mfano wa sera binafsi ya fedha unayohitaji kuiandaa kulingana na mazingira yako.
Ondokana na madeni
Kukopa,
kwa hakika, si jambo baya. Huwezi, kwa mfano, kufanya biashara kubwa bila kutumia
fedha za mkopo. Ndivyo wanavyofanya wafanyabiashara wakubwa.
Tofauti
na wafanyabiashara, wafanyakazi walio wengi hukopa kugharamia mtindo wa maisha
ya kila siku. Kinachokopwa kinatumika kufanyia manunuzi ya vitu vya kawaida, kisha
mshahara unatumika kulipia deni lisilozalisha chochote.
Kwa
namna hii, wafanyakazi wengi wamejikuta wakigeuka kuwa watumwa wa mzigo mzito
wa madeni. Huwezi kupiga hatua za maana bila kujikwamua kwenye madeni ya namna
hii.
Ikiwa
unaishi na madeni mabaya, weka mpango wa kuondokana na madeni haraka
iwezekanavyo. Sambamba na hatua hiyo, epuka kujiingiza kwenye madeni yasiyo na sababu. Utaratibu wa kuweka ukomo wa matumizi kabla hujapata kipato chako unaweza kukusaidia kuepuka madeni.
Wekeza kuongeza kipato
Kilio
cha wafanyakazi wengi ni kukosekana kwa mtaji unaotosha kuwekeza. Hata hivyo,
wapo waajiri huwadhamini wafanyakazi wao kupata mikopo kwenye taasisi za fedha. Kama una fursa hiyo, tumia mkopo kufanya uwekezaji mdogo kujiongezea kipato.
Lakini
hata kama fursa hiyo haipo, bado unaweza kutumia kanuni ya kuweka
akiba inayoweza kukutengeneza mtaji. Tuchukulie mfano mshahara wako ni Sh
600,000 kwa mwezi. Ukiamua kutenga kiasi cha Sh 50,000 tu kwa mwezi utakuwa na
Sh 600,000 baada ya miezi 12.
Lakini
pia unaweza kuboresha kanuni ya kuweka akiba kwa kuongeza kiasi fulani kisichobadilika
kwa kila mwezi unaofuata.
Kwa
mfano, baada ya kufanikiwa kuweka Sh 50,000 mwezi huu, unaongeza Sh 10,000 kwa mwezi ujao na
kufanya kiasi utakachokitenga kiwe Sh 60,000. Mwezi unaofuata unaweka Sh
70,000, Sh 80,000 na kuendelea.
Ukiufuata
utaratibu huu kwa miezi 12 utakuwa umejiwekea akiba ya Sh 1,260,000. Hiki si
kiasi kidogo kwa mshahara wa Sh 600,000 kwa mwezi. Ikumbukwe kwa mshahara huo
unaweza kujibana na kuweka akiba zaidi.
Kikwazo
kingine kwa wafanyakazi ni woga wa hasara na aina ya biashara wanayoweza kufanya.
Mambo mawili hapa. Kwanza, buni huduma inayoweza kutatua tatizo la watu
wanaokuzunguka. Mahitaji na changamoto za watu wanaokuzunguka ndiyo fursa kwako.
Pili, usiogope kushindwa au kuibiwa. Vaa ujasiri uwe tayari kujifunza kwa kushindwa. Tunajifunza
kwa makosa.
Ni somo zuri sana watu wengi kweli wanakosa nidhamu ya pesa na wengine wanakuwa na woga wa kula hasara ila kuna mtaalamu mmoja (Robert Kiyosaki) anasema kwamba wasomi wengi wanakuwa na woga wa kufeli kutokana na jinsi walivyokuwa wamepitia mafundisho ya walimu wao kwamba walikuwa wakiambiwa usiposoma utafeli ,basi imekuwa hivyo hata katika maisha yao wanaogopa kufeli na yule ambae hajasoma sana anakuwa na nidhamu ya pesa kwa sababu hana ile dhana ya kufeli katika Saikolojia take.
JibuFutaAhsante San Mr Christian Bwaya kwa makala hii
JibuFutaAhsante San Mr Christian Bwaya kwa makala hii
JibuFutaMaoni haya yameondolewa na mwandishi.
Futaasante sana kwa makala hii
JibuFutaasanteh sana nitafwata ushauri wako
JibuFutaSafi Sana! Nimekutana na somo hiliimenifunza mengi,hasa kuhusu kupanga bajeti kabla ya kupata mshahara/kipato,pia uwekaji wa akiba.
JibuFutaAsante Sana kiongozi SoMo zuri Sana hili mungu akutangulie
JibuFutaSoMo zuri Sana hongera Kwa elimu yako umetufumbua macho wahanga wengi ni wafanyakazi kwani elimu tunayosoma darasani imetuingia tofauti kisaikolojia kuwa kufeli ni kosa
JibuFuta