Wajibu wa Mzazi kwa Mtoto Kisheria -2
SHERIA ya Mtoto Na. 21 ya 2009 inamtambua mtoto kama
mtu yeyote mwenye miaka pungufu ya 18. Sheria hii ilitungwa kukidhi matakwa ya
makubaliano na mikataba ya kimataifa inayolenga kulinda haki, maslahi na ustawi
wa mtoto.
Kimsingi sheria hii inaainisha wajibu walionao
wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kwa mtoto na inatoa mwongozo pale
yanapojitokeza mazingira yanayohatarisha ustawi wa mtoto.
Kwa mujibu wa sheria hii, maslahi na ustawi wa mtoto
ndio msigi mkuu wa maamuzi yoyote yanayofanywa na mtu, taasisi, mahakama ama
vyombo vyovyote vya kimaamuzi.
Ndio kusema wazazi na jamii kwa ujumla wana jukumu la
kuhakikisha mtoto analindwa dhidi ya namna zote za uonevu, udhalilishaji
kijinsia, kikabila, umri, dini/imani, lugha, maoni ya kisiasa, ulemavu, afya,
hali ya uchumi, anakotoka na hata ukimbizi.
Katika makala haya tunaangazia haki ya kwanza
aliyonayo mtoto kisheria. Hapa tunazungumzia haki ya mtoto kupata utambulisho
wake binafsi unaoeleweka.
Jina
Jina ni hatua ya kwanza ya kumpa mtoto utambulisho
wake. Mara baada ya kuzaliwa, wazazi au walezi wanawajibika kumpa jina
litakalomtambulisha kama binadamu aliyekamilika.
Sheria haijafafanua zaidi kuhusu jina la mtoto. Hata
hivyo, ni dhahiri kuwa jina analopewa mtoto litakuwa sehemu ya maisha ya mtoto
kwa muda mrefu. Ni busara jina hilo likazingatia maadili, staha na utu.
Uraia
Kadhalika, mtoto anayezaliwa na m-Tanzania ana haki
ya kutambulika kama raia halali wa Tanzania. Njia moja wapo ya kumhakikishia
haki hiyo, ni kumwandikisha kwenye mamlaka zinazotambuliwa kisheria ambazo
ndizo zitakazompatia cheti cha kuzaliwa.
Kwa kutokuelewa, wazazi wengi hawajishughulishi
kuhakikisha mtoto anapata cheti cha kuzaliwa. Ni vyema kuelewa kuwa mtoto
atalazimika kuwa na cheti ili kupata haki zote anazostahili raia wa Tanzania
kama vile elimu, huduma za afya, hati ya kusafiria na vitambulisho mbalimbali.
Wazazi
Utambulisho wa mtoto ni pamoja na kumwezesha kuitambua
familia yake. Sheria hii inampa mtoto haki ya kuwafahamu watu waliomzaa. Ndio
kusema, mtu yeyote anayemlea mtoto kwa sababu yoyote ile ana wajibu wa kisheria
kumjulisha mtoto nani hasa ni mzazi/wazazi wake.
Inafahamika kuwa wapo akina mama waliowapata watoto
wao katika mazingira yenye utata. Wakati mwingine wasingependa watoto
kuwafahamu baba zao. Lakini fikiria unaishi bila kufahamu kwa hakika baba yako
ni nani. Ni adhabu fulani ya kisaikolojia. Sheria hii imelizingatia hilo.
Kwa mujibu wa sheria hii, na bila kuingilia sheria
nyinginezo, mtu yeyote hana haki ya kumficha mtoto baba/mama yake wa kumzaa.
Kumfahamu baba na mama yake ni haki yake.
Familia
tandaa
Sambamba na kuwafahamu wazazi wake halisi, mtoto pia
ana haki ya kuitambua familia tandaa. Familia tandaa ni ndugu wa pande zote
mbili, yaani upande wa baba na mama.
Ndio kusema mzazi au mlezi ana wajibu wa kuhakikisha
mtoto anafahamu ukoo wake vizuri kama sehemu ya kulinda utambulisho wake. Mtoto
awafahamu bibi, babu, shangazi, wajomba na ndugu wengine wa ukoo.
Kisaikolojia, mwanadamu anajiamini zaidi anapowafahamu
ndugu zake. Fikiria unaishi na wazazi wako lakini hujui ndugu zako. Unaweza
kuwaza mengi. Ni vyema kila
inapowezekana wazazi kufanya jitihada za kuwaunganisha watoto na ukoo wao. Kuna
leo na kesho.
Inaendelea
Maoni
Chapisha Maoni