Unavyoweza Kutumia Mshahara Kujikwamua Kiuchumi
Wapo
watu wanawakejeli wafanyakazi kwa kuajiriwa. Kwamba kama mtu asiye na elimu anaweza
‘kuosha magari mtaani’ na akakuzidi kipato kuna sababu gani kuishi maisha
magumu ofisini?
Upo
ukweli wa namna fulani. Wafanyakazi wengi wanaishi maisha ya ukata. Kazi yao
kubwa ni kupambana kuhakikisha kuwa mishahara inakutana. Katika mazingira ya
namna hii, inakuwa vigumu kupiga hatua za maana kimaisha.
Ukweli
huo, hata hivyo, hauondoi umuhimu wa kuajiriwa na kufanya kazi chini ya mtu mwingine.
Kila mtu ana wito wake katika maisha. Wapo watu wanaoweza kufanya kazi bila kuajiriwa.
Kimsingi, watu wa aina hii wana uwezo wa kubuni na kuendesha biashara zao
wenyewe. Furaha yao ni kujitegemea na kutengeneza ajira kwa watu wengine.
Lakini
pia wapo wenye wito wa kuuza ujuzi kwa wengine. Furaha yao ni kutumia ujuzi
walionao kutatua matatizo ya watu katika jamii. Kinachompa daktari utosholevu,
kwa mfano, ni kuona anaokoa maisha ya wagonjwa. Mwalimu naye anafurahi
kuelimisha jamii.
Mafanikio
ya watu hawa ni vile wanavyouza na kutumia ujuzi wao kwa manufaa ya wengine.
Unapowashauri waache kazi wakafanye biashara nyingine, kimsingi unawanyang’anya
thamani waliyonayo kwa jamii.
Pamoja
na umuhimu wa mtu kutambua na kuheshimu wito wa maisha yake, bado fedha ina
nafasi kubwa kwenye maisha. Tunahitaji fedha kutatua matatizo mengi. Kwa
kuzingatia kuwa hakuna wakati kila mtu atajiajiri, makala haya yanaangazia namna
mwajiriwa anavyoweza kujikwamua kiuchumi kwa kutumia mshahara wake.
Mafanikio hayategemei kipato
Wapo
wafanyakazi wanafikiri ugumu wa maisha wanaokabiliana nao unasababishwa na udogo
wa kipato. Kwamba wangelipwa mshahara mkubwa, basi maisha yao yangebadilika. Dhana
hii haina ukweli mkamilifu kama nitakavyofafanua.
Wapo
watu wanaolipwa mshahara mkubwa lakini haukutani na mshahara unaofuata. Kinyume
na hao, wapo wafanyakazi wanaolipwa mishahara midogo, lakini wanaweza kufanya
mambo yanayoonekana.
Tofauti
ya makundi haya mawili si kipato bali namna wanavyotumia kile wanachokipata. Unapoelekeza
kipato chako kwenye matumizi ya kila siku ni dhahiri utahitaji kiasi kikubwa
cha fedha ili ufanikiwe kuweka akiba. Maisha yasiyolingana na kile unachopata
hayawezi kukutoa kwenye umasikini.
Kwa
mfano, mtu mwenye mshahara wa Tsh milioni moja kwa mwezi anapoamua kuishi
kwenye nyumba inavyomgharimu Tsh 200,000 kwa mwezi; akatumia Tsh 200,000
kuendesha gari la mkopo; akatumia Tsh 300,000 kulipa mkopo kila mwezi mtu huyu
atakuwa anaishi maisha yasiyolingana na kipato chake. Kwa hakika ataishi katika
‘umasikini wa kisomi’ kwa muda mrefu.
Kwa
nje, kijana huyu anaweza kuonekana ‘mambo safi.’ Jamii inaweza kumheshimu kwa
sababu kwa haraka haraka mafanikio yake yanaonekana. Anaendesha gari (ya
mkopo); anaishi mitaa wa wenye hadhi; anapumzika kwenye maeneo ya gharama kubwa
lakini katika hali halisi ‘mafanikio’ hayo hayapo.
Tunasema
hana mafanikio kwa sababu mbili. Kwanza, kipato kinaishia kugharamia mahitaji
ya msingi katika maisha. Pili, kipato hicho hakiwezi kutosha kuweka akiba
itakayowekezwa kwa ajili ya kuzalisha.
Mazingira
ya namna hii yanaweza kumshawishi kukopa kwa watu (mara nyingi wenye kipato
kama chake) ili asukume maisha. Matokeo yake ni kuendelea kujididimiza kwenye
kifungo cha madeni zaidi yatakayomnyima amani.
Pia,
katika mazingira haya, mtu huyu anaweza kukosa utulivu kazini na kufanya
maamuzi ya kuacha kazi katika jitihada za kutafuta kipato zaidi. Lakini hata anapopata
kazi nyingine, maisha yanaweza kubaki kuwa yale yale kwa sababu tatizo linaweza
kuwa namna anavyotumia kidogo anachokipata.
Mbinu za kujikwamua
Tunahitaji
elimu ya msingi ya fedha ambayo pengine ni vigumu kuipata kupitia mfumo rasmi.
Fedha, kwa kawaida, inaongozwa na kanuni zake. Ukiziheshimu, unaweza kuimudu
fedha na ikakufuata. Unapozivunja kanuni hizo,unaweza kutumia muda mrefu kuitumikia
fedha.
Kinachoongoza
kanuni hizi, kwa mujibu wa wataalam wa uchumi binafsi, ni nidhamu ya fedha.
Bila kujali kiasi cha fedha unachokipata kwa mwezi, unahitaji uwezo wa
kutokukubali mtindo wako wa maisha ubalishwe na ongezeko lolote la kipato.
Ukifanikiwa
kuwa na nidhamu hiyo, kiasi chochote cha fedha kinaweza kukupa usalama wa
kipato. Hapa kuna mambo kadhaa ya kuzingatia.
Jifunze
kuweka akiba. Usifanye matumizi ya kawaida kabla hujaweka akiba. Unapopata
mshahara elekeza asimilia fulani kwenye akiba na kinachobaki kipangie matumizi.
Unapoweka akiba kwa mtindo huu, ni sawa na kujilipa ili ufanye mambo ya
maendeleo.
Pili,
punguza matumizi ya kila siku kwa kujiruhusu kuishi maisha ya kawaida kwa kipindi
fulani. Wafanyakazi wengi hutamani kutetea hadhi za ofisi wanazofanyia kazi kwa
kuishi maisha ya hadhi kubwa. Matokeo yake wanajikuta wakifanya maamuzi
yanayoweza kuwagharimu.
Mfano,
kijana anapoanza kazi anakuwa na shauku ya kujenga taswira ya mtu
aliyefanikiwa. Shauku hiyo itamsukuma kutamani kuendesha gari ili awe na hadhi inayolingana
na kazi anayoifanya. Kwa hiyo anapopata fursa ya mkopo kazini, kijana huyu kwa
haraka atawaza kununua gari.
Anaweza
kuwa na sababu nyingi za kuhalalisha maamuzi yake hayo. Labda atasema gari
itamsaidia kutatua tatizo la kuchelewa kazini. Lakini ukweli halisi ni kwamba
angeweza kuendelea kutumia usafiri wa umma kwa muda fulani wakati akijenga
misingi imara ya kiuchumi.
Changamoto
anayoweza kukabiliana nayo kijana huyu inaweza kuwa kubwa kuliko faida ya ‘kutatua
tatizo la usafiri.’ Kwanza atalazimika kulipa mkopo na riba yake kwa muda mrefu
hali inayoweza kumfanya asiweze kufanya chochote kwa miaka kadhaa. Maamuzi ya
namna hii huchangia umasikini wa wafanyakazi.
Tatu,
fikiria kuwekeza ujiongezee kipato. Tumia ujuzi wako kujiongeza kiujasiriamali.
Maarifa na ujuzi ni mtaji. Si lazima ufanye uchuuzi. Tumia ujuzi wako kufanya
kitu cha ziada. Usikae ukimlilia mwajiri akuongezee kipato. Jiongoze.
Faida
waliyonayo wafanyakazi wengi ni mikopo. Kama sio kupitia mwajiri, kuna vyama
vya kuweka na kukopa. Tumia fursa za mikopo kwa faida. Wekeza unachokopa badala
ya kununua vitu visivyokuzalishia. Hiyo ndiyo namna rahisi ya kujikwamua.
Kisingizio
cha wafanyakazi wengi ni kukosa muda wa kufanya mambo mengine. Ni suala la kubadili
mtazamo tu. Hulazimiki kuacha kazi ili ukafanye biashara. Unaweza kufikiri kufanya
kazi kwa kushirikiana na watu wanaofanya biashara tayari. Ukiwekeza hatua kwa
hatua, unaweza kupata mafanikio ukiwa kazini.
Makala haya yamechapishwa awali kwenye Jarida la Ajira na Kazi linaloandaliwa na gazeti MWANANCHI kila Ijumaa.
Maoni
Chapisha Maoni