Wajibu wa Mzazi kwa Mtoto Kisheria
Tumeshuhudia matukio mengi katika jamii yetu ya
watoto kunyanyaswa na kudhalilishwa na watu wazima wakiwemo walezi na hata
baadhi ya wazazi wasio waadilifu.
Imekuwa kawaida kusikia watoto yatima wakitendewa
vitendo vya uonevu baada ya wazazi wao kufariki. Ndugu na jamaa, bila haya,
wamekuwa wakifanya maamuzi yanayowahusu watoto bila kuzingatia maslahi na haki
za watoto.
Unyanyasaji wanaofanyiwa watoto, wakati mwingine
unafanyika kwa sababu wazazi, walezi na hata jamii kwa ujumla hawafahamu wajibu
walionao kwa mtoto kisheria. Kutokujua namna mtoto anavyolindwa kisheria kunaweza,
kwa namna moja au nyingine, kuchochea vitendo hivi.
Katika [blogu] hii kila Alhamisi, tunakusudia kukuletea
dondoo muhimu kama zinavyoainishwa kwenye sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009
iliyotungwa kwa minajili ya kulinda maslahi na ustawi wa mtoto.
Sheria hii ilitungwa na serikali yetu kukidhi
matakwa ya mikataba ya kimataifa inayomhakikishia mtoto haki zake za msingi.
Kwa mhutasari, sheria hii inalenga kumwekea mtoto mazingira
ya kukua na kustawi katika nyanja zote za kimaisha bila kudhalilishwa, kuonewa
na kunyanywaswa na jamii ikiwemo familia yake. Ingawa msisitizo ni kumlinda
mtoto zaidi, sheria hii pia inafafanua wajibu wa mtoto kwa familia na jamii kwa
ujumla.
Labda tuanze na tafsiri ya mtoto. Mara nyingi
tumetumia neno ‘mtoto’ kumaanisha mambo mengi kwa wakati mmoja. Kwa mfano,
unaweza kushangaa mzee wa miaka 55 anajitambulisha kama ‘mtoto’ wa tatu katika
familia yake. ‘Mtoto’ huyu wa tatu, naye anaweza kuwa na ‘watoto’ kadhaa wenye
umri wa utu uzima.
Hapa mtoto maana yake ni nini? Mtoto, katika
mazingira hayo, ni mtu aliyezaliwa na mtu mwingine bila kujali umri wake.
Tafsiri hii inazingatia uhusiano wa mzazi na mwanae bila kujali umri.
Kadhalika, unaweza kusikia mtu mwenye miaka 40
akidaiwa kufanya mambo ya kitoto. Utoto, kwa mazingira hayo, ni kufanya vitendo
visivyoakisi uwezo wa mtu mzima anayejitegemea. Jamii inakuwa na matarajio
fulani kwa mtu anayejitambulisha kama mtu mzima. Anatarajiwa kufikiri kwa namna
fulani, kufanya vitu kwa namna fulani na hata kuonekana kwa namna fulani.
Inapotokea mtu mzima huyu anashindwa kukidhi
matarajio hayo, watu humtazama kwa jicho la ‘utoto.’ Utoto ni sifa mbaya kwa
mtu mzima.
Lakini, kidini tunaambiwa ‘msipokuwa kama watoto
wadogo hamuwezi kuurithi uzima wa milele.’ Mtoto, katika mukhtadha huu, si sifa
mbaya. Tabia za kitoto kimsingi ni sharti muhimu la kumpa mtu sifa za kuuona
ufalme wa mbinguni.
Hata hivyo 'mtoto' huyu anaelekezwa kuendelea kukua na kuongezeka ili awe na sifa ya kujitegemea na kuwategemeza wengine. Haifai kuendelea kuwa 'kama watoto wachanga' wanaoendelea kuwategemea wengine. Jambo hili linaelezwa kisaikolojia pia.
Kisaikolojia mtoto anaweza kuwa mtu yeyote bila kujali umri wake ambaye bado anaendelea kukua kiakili, kimwili, kiroho na kimahusiano. Hata hivyo, mtu mwenye miaka pungufu ya 12 ana nafasi kubwa ya kuwa na sifa hizi.
Kisaikolojia mtoto anaweza kuwa mtu yeyote bila kujali umri wake ambaye bado anaendelea kukua kiakili, kimwili, kiroho na kimahusiano. Hata hivyo, mtu mwenye miaka pungufu ya 12 ana nafasi kubwa ya kuwa na sifa hizi.
Sababu kubwa ni kuwa katika umri huo, mtu huyu bado anaendelea kukomaa na
kupevuka kiakili, kimwili, kiroho na kimahusiano. Ndio kusema mtu ambaye bado hawezi kujitegemea
kimwili, kiakili, kiroho na kijamii, ana sifa za kuitwa mtoto.
Kwa kuwa tafsiri za ‘mtoto’ na ‘utoto’ zinaweza kuwa
na mkanganyiko mkubwa kama tulivyouona hapo juu, sheria hii imetumia kigezo kimoja
cha umri kumtambua mtu mwenye sifa za kuitwa mtoto.
Mtoto, kwa mujibu wa sheria hii, ni mtu yeyote
mwenye umri wa chini ya miaka 18. Haijalishi amepevuka akili kiasi gani, maadam
ana umri usiozidi miaka 18 mtu huyo bado ataendelea kutambuliwa na sheria hii kama
mtoto.
Mtu anayekidhi sifa hii amepewa haki na wajibu kisheria
kama tutavyobainisha katika makala yanayofuata.
Inaendelea
Fuatilia Safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa mjalada huu.
asante kwa uchambuzi mzuri
JibuFuta