Ayafanyayo Mzazi Huamua Atakavyokuwa Mtoto
PICHA: Pinterest |
'Mwanangu ni mtundu
haijapata kutokea’ alilalamika msomaji mmoja wa safu hii. Sikuelewa ana maana
gani aliposema mwanae ni mtundu. Nikaomba ufafanuzi. ‘Hasikii. Jeuri asikwambie
mtu. Usipomfanyia purukushani huwezi kumwambia kitu akasikia.’ Kwa mujibu wa
maelezo yake, kuna nyakati hubidi amtishe, amwadhibu vikali na hata kumtukana
ikibidi.
‘Hao watoto unaowaongelea
sio huyu wangu. Huyu ni mkorofi. Ukisema nimsikilize kama unavyoshauri ndio
unaharibu […] Akiona fimbo ndio kinaeleweka.’ Nilitamani kujua kama mbinu hizo anazotumia
zimesaidia.
‘Kidogo. Nikimshikia fimbo
ndio tunaelewana. Ukienda hivi hivi hana anachoelewa […] Shida yake kubwa ni
utukutu. Ni mwongo sijapata kuona.’
Mzazi huyu anawakilisha
mtazamo wa wazazi wengi. Imejengeka imani kuwa watoto wanazaliwa na tabia zao.
Wapo watoto kwa ‘asili’ ni wakorofi na watundu wakati wapo pia watoto wapole na
wasikivu.
Ni dhahiri kuwa vinasaba
vina mchango wake kwenye kuumba tabia zetu.
Kama ambavyo huwezi kuamua kimo cha mwanao, huwezi pia kuamua
mustakabali wa tabia fulani za mtoto kwa asilimia mia moja.
Tunafahamu, kwa mfano, kuna
watu wana ukali usioelezeka. Pamoja na kulelewa kwenye familia yenye watu
wapole, anaweza kutokea mtu mwenye hasira kali. Ukimgusa anawaka kwa ghadhabu.
Katika mazingira kama haya, inaonekana upo uwezekano wa kurithi tabia fulani
fulani.
Hata hivyo, watafiti wa tabia
za mwanadamu wanakubaliana kuwa mazingira ya kimalezi anamokulia mtoto nayo yana
mchango mkubwa katika kuchonga tabia zetu. Hata pale inapoonekana watoto
wamerithi tabia kwa wazazi wao, kimsingi wanakuwa wanaakisi kile wanachokiona
kwa wazazi wao.
Makala haya yanaangazia
makundi manne ya tabia za watoto yanayotokana na mazingira ya kimalezi. Kimsingi,
hoja ni kuwa hulka anazokuwanazo mzazi ndizo zinazochangia kutengeneza tabia ya
mtoto. Lengo si kujenga hatia kwa wazazi bali kutusaidia kuelewa mchango wa
yale anayoyafanya katika kujenga mustakabali wa mtoto kitabia.
Mtoto mtulivu mwenye uchangamfu
Huyu ni mtoto mwenye utulivu na kwa
hakika anajiamini. Huwa ni mchangamfu kwa watu kwa sababu anapenda watu. Ukitaka
kupima upendo wa mtoto huyu kwa watu, mpe kitu. Ni mwepesi kuwapa wenzake.
Ingawa kuna umri fulani kila mtoto huwa na ubinafsi, mtoto wa kundi hili anapozidi
miaka miwili, anakuwa mwepesi kuwapa watu kile alichonacho. Sababu ni kuwa
anawaona wengine kuwa bora kama alivyo yeye.
Pia, hana ugomvi wala usumbufu. Tangu
anapokuwa mdogo, huwezi kusikia akilia lia bila sababu. Hata pale anapolia ni
rahisi kumtuliza. Kwa mfano, anapoachwa na mzazi wake, anaweza kulia kama
watoto wa makundi mengine tutakayoyaona lakini ni mwepesi ‘kusahau’ na
kuendelea kucheza. Mama anaporudi baadae, mtoto huyu humchangamkia.
Kwa ujumla, utulivu wa mtoto huyu si wa
kuzaliwa. Ni matokeo ya malezi yanayomwelewa, yanayomshirikisha, yanayomkubali vile
alivyo na yanayomweka karibu. Kisaikolojia tunasema mtoto huyu ana nafsi
iliyotulia. Anajisikia kama mtu aliyeshiba asiye na njaa ya ‘kueleweka’,
‘kushirikishwa’ ‘kukubaliwa’ na ‘kupendwa.’
Mtoto mkimya ‘asiyependa’ watu
Huyu ni mtoto anayejiamini
kama yule wa kundi la kwanza lakini ana tatizo la kujiona bora kuliko wengine. Kwa
kawaida hana tabia ya ugomvi, lakini hupenda kujitenga na watu kufanya mambo
yake. Kinachomfanya apende kuwa ‘kivyake’ ni kutokuamini uwezo wa watu wengine.
Hana imani watu wanaweza kuwa na msaada wowote kwake. Ndani yake anajiona yuko
sahihi mara nyingi, anajitosheleza na hahitaji sana msaada wa wengine.
Mara nyingi ni mkimya na
hana maneno mengi sana, ingawa wakati mwingine akimzoa mtu na kumwamini anaweza
kuwa mwongeaji. Shauri ya kupenda kuzingatia kile anachokifanya, anaweza kuwa
na uwezo mzuri kiakili wazazi wakimwelekea mazingira sisimushi.
Unaweza kumgundua mtoto wa kundi
hili tangu akiwa mdogo. Si mtoto wa kulia lia bila sababu kama yule wa kwanza,
lakini sababu yake kuu ni kutokujali ukaribu wake na watu wa karibu. Anapoachwa anaweza kulia
kama watoto wengine, lakini mama anaporudi, huwa haoenekani kujali.
Tabia hii ni matokeo ya mchanganyiko wa
malezi yasiyojali (yanayopuuza) hisia zake lakini yenye kumshirikisha kwa namna
fulani. Kwa mfano, mtoto anapokuja kukulalamikia, huonekani kujali hisia zake.
Mzazi unapokuwa huna tabia ya kuonyesha kuelewa hisia za mtoto kwa hakika
unamfanya mtoto aamini watu hawaelewi hisia zake. Mara nyingi atajijitetea kwa
kupenda kuwa kivyake vyake. Kukosa uchangamfu na watu ni lugha ya kusema kuwa watu hawamwelewi.
Mtoto ‘mpenda watu’ asiyejiamini
Huyu ni mtoto anayependa
watu kama mtoto wa kundi la kwanza. Tatizo lake ana hulka ya kuwaona wengine
kuwa bora kuliko yeye. Ndani yake anajisikia kukosa kitu fulani na anaamini
watu wengine watamsaidia kukipata hicho anachokikosa. Kwa hiyo, anapenda sana
michezo na kuwa na marafiki zake.
Mtoto wa namna hii anaweza kuonekana
mpole na mwenye haya (aibu) anapokuwa na watu anaoamini hawamwelewi. Lakini anapokutana na watu
wanaomwelewa, ni mchangamfu na mwongeaji kuliko kawaida.
Wapo wa kundi hili, hawana uwezo wa kuwachangamkia watu hata kama ndani wanatamani kuchangamka. Wanatamani marafiki lakini hawawezi kuwakaribia. Kimsingi mtoto wa kundi hili anajisikia upweke ndani yake na anajaribu kufidia hisia za upweke
ndani yake ama kwa kujichanganya na watu au kwa kutamani kujichanganya na watu.
Huyu ni mtoto aliyeathirika na tabia ya
utoro wa wazazi (wasiopatikana kimwili.) Mtoto wa kundi la pili, ana wazazi
wanaopatikana lakini hawaelewi hisia zake. Huyu wa kundi hili ni tofauti. Wazazi
wake wanaonekana kuelewa hisia zake na anajua wanampenda, lakini muda mwingi
hawapo.
Kwa sababu mtoto angependa kuwa karibu
na wazazi wake, ndani yake anajisikia kukosa kitu muhimu anachojua kinapatikana
kwa watu wengine. Hii ndiyo sababu ya yeye kupenda ‘kujichanganya’ sana na watu
wengine. Uzungumzaji na kupenda watu unamsaidia kufidia hali ya kukosa uwepo wa
mzazi.
Mtoto mkorofi na mgomvi
Huyu ni mtoto asiyejielewa. Hujiona hana thamani na wengine wanaomzunguka hawana maana pia kama alivyo yeye. Ni mtoto anayejidharau na kudharau wengine. Hana hisia na haelewi hisia za wengine na ndio sababu huwa mgomvi na mtundu.
Ukimchunguza mtoto huyu ni
kama anafurahia kuwaona wengine wakiumia. Huwachokoza wengine na hata
kuwatukana almuradi ajisikie ‘mbabe.’ Ni mchoyo hasa kama amekulia kwenye
mazingira ya umasikini na huwa ni mbinafsi.
Kimsingi huyu ni mtoto anayelelewa
kwenye mazingira ya mabavu na udhalilishaji. Mfano wazazi walevi wenye tabia ya
kupigana na kutukanana mbele yake. Pia wazazi wakali kupindukia wanaangukia
kwenye kundi hili.
Aidha, wakati mwingine wazazi
hawatambui kuwa wanawalea watoto wao kimabavu. Ndani yao mna hasira na maumivu wasiyoyatambua
na huwatumia watoto kama namna ya kufidia maumivu waliyonayo. Matokeo yake,
wanakuwa wepesi hutukana na kutumia nguvu kubwa kuwaadhibu watoto bila kung’amua
wanachokifanya.
Inaendelea
Ni kweli kabisa mwalimu, maana wazazi wengi kutumia hasira katika kuwaonya watoto, kumbe tatizo ni wao, laiti wangejua/tambua tatizo ni wao, hakika malezi mabovu ya watoto yangepungua.Ahsante maana umenifungua akili japokua zipo katika ndoa.
JibuFutaChapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.
JibuFutaChapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.
JibuFuta