Nidhamu ya Mtoto Bila Viboko Inawezekana
PICHA: Pinterest |
Adhabu
ya bakora ni utamaduni. Kwa wengi wetu bakora ni imani. Tunaziamini kiasi cha
kuwa tayari kuzirithisha kwa wanetu kama ambavyo na sisi tumeziridhi kwa wazazi
wetu. Kwa hiyo tunapopendekeza mbadala wa bakora kama adhabu iliyozoeleka
tunaelewa hili haliwezi kuwa jambo jepesi.
Kama
tulivyoona, wazazi tunapowachapa watoto tunaamini lengo ni kuwasaidia wawe na nidhamu.
Hata hivyo, kwa kutazama mazingira yanayoambatana na adhabu hii ni dhahiri
bakora haiondoi tatizo linalokusudiwa.
Kwanza,
hutumika kama njia ya mkato ya kujenga nidhamu ya woga ambayo hata hivyo
haidumu. Pili, mara nyingi bakora hutolewa kwenye mazingira ya hasira yasiyokwenda
sambamba na mbadala wa tabia inayoadhibiwa.
Kwa kuwa
bakora hutolewa kwa msukumo wa hasira, ni rahisi mtoto kuitafsiri kama ugomvi
binafsi kati yake na mzazi. Hali hii, kama tulivyoona, hujenga imani potofu
kuwa mabavu ndiyo namna sahihi ya kutatua matatizo. Tuone mfano wa Diana.
Ukomo wa bakora
Diana
ni mama wa watoto wawili. Frank, mwanae wa pili, ni mkorofi kuliko Salome, mwanae
wa kwanza. Salome kwa kawaida ni msikivu na Diana anampenda. Kwa Salome, Diana
anasema, fimbo si lazima. Ni mwepesi kusikia na hana ubishi anapoelekezwa
kufanya jambo.
Shida
iko kwa Frank. Kwa mujibu wa Diana, kila siku lazima angalau amtishie Frank kumlazimisha
kuoga, kumlisha na hata kumlaza. Hata nyakati za asubuhi wakati wa kumwandaa
kwenda shule, Diana hulazimika kushika fimbo kumtisha Frank achangamke
kujiandaa.
Karibu
kila anachomwambia Frank kinatanguliwa na fimbo –iwe ni kwa namna ya kitisho au
kwa kumchapa kabisa. Wazazi wengi tunaweza kuelewa hali hii. Tumeamini bila bakora
mambo hayawezi kwenda.
Ninapomwuuliza
Diana kujua kama kweli fimbo zinasaidia, jibu lake lina utata. Ingawa kwa
haraka inaonekana Frank hupata usikivu anaposhikiwa fimbo, kimsingi fimbo zimemjenga
utegemezi fulani.
Frank
anaendelea kuzoea fimbo. Kadri anavyoziona zikitumika ndivyo anavyokuwa jasiri.
Amejenga ujasiri kujilinda na maumivu ya kihisia na kimwili. Ili kukabiliana na
hali hii, Diana atalazimika kuendelea kushika fimbo kwa muda mrefu ikiwa
anataka kuendelea kutumia njia ya hofu na vitisho kama namna ya kupata usikivu
wa Frank.
Ingawa
njia hii inaweza kuonekana kuwa na ufanisi, kiukweli haiwezi kuwa na msaada wa
muda mrefu. Frank atajenga nidhamu ya woga kumridhisha mama yake. Lengo la
nidhamu hii bandia atakayoijenga Frank ni kujinasua na matatizo kati yake na
mama.
Kwa
upande mwingine, Frank anaweza kuamini katika ubabe na matumizi ya nguvu kama namna
ya kumsaidia anapokuwa na matatizo na watu. Kadri anavyokuwa mtu mzima, Frank
ataendelea kuamini maisha ni mapambano.
Ukikosewa,
ni lazima kutumia nguvu kumtisha au kumwuumiza anayekukosea. Matokeo yake Frank
anaweza kuwa mwanaume mgomvi kwa familia yake mwenyewe. Yote haya chimbuko lake
ni nguvu anazotumia Diana kumrekebisha mwanae kwa nia njema ya kumrekebisha.
Bakora
haiwezi kuwa jibu la nidhamu ya mtoto. Maumivu anayoyapata mtoto kwa bakora hayawezi
kukupa heshima yako kama mzazi. Kama tulivyoona, kumchapa mtoto huishia kuumiza
hisia na mwili wake. Maumivu ya namna hii hayawezi kumfanya mtoto awe na
msukumo wa dhati ya kukusikiliza.
Elewa kinachomsumbua
Ni
rahisi kuchukua hatua bila kujua msukumo ulio nyuma ya tabia anayoionesha mwanao.
Badala ya kumtisha na kumchapa mtoto, jaribu kumwelewa. Naam, mwelewe. Fanya
jitihada za kujua kwa nini hasikii unachomwambia. Pengine unatumia vitisho na
maumivu kama njia ya mkato kwa sababu haujawa tayari kuingia kwenye ulimwengu
wake.
Frank, kwa
mfano, hamsikilizi mama yake pengine kwa sababu mama hajawa tayari kujua namna
bora ya kuwasiliana nae. Pengine mama amemkatia tamaa Frank na anaonyesha wazi
kuwa mwanae hana usikivu. Frank naye anaamua kufanya kama mama yake
anavyoamini. Frank kichwani anafikiri, ‘kwa kuwa unaniona mjeuri, basi sina
namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuwa mjeuri kama unavyotaka.’
Vipi
kama mama yake Frank atamfanya mwanae aamini, ‘mbona kama mama ananiona
msikivu?’ Kwa nini mama yake Frank asioneshe matarajio yaliyo kinyume na kile
Frank anachokifanya?
Unapomjengea
imani mtoto kuwa unamwona kama mtu msikivu, na akakuamini kuwa kweli ndivyo
unavyomwona, inaweza kuwa rahisi kwake kubadilika na kupunguza upinzani.
Kwa
kutumia mfano wa Frank, kama ataamini mama anamchukulia kama mtu msikivu, hiyo
inaweza kubadili mwelekeo wake. Kama tulivyosema, watoto wengi wanapenda
kushirikiana na wazazi. Unapomwaminisha kuwa unamtazama kwa jicho chanya, anaweza
kabisa kukuthibitishia kuwa hujakosea kumwona hivyo. Huo unaweza kuwa mwanzo wa
mabadiliko.
Ukimheshimu, atakuheshimu
Sambamba
na kumwelewa mwanao, fanya juhudi za kumwonyesha kuwa unamheshimu kama
binadamu. Kwa mzazi mwingine, hili si jepesi kutekeleza. Wakati mwingine
tunafikiri watoto ni wadogo mno kustahili heshima yoyote ya mtu mzima. Hata
hivyo, ukweli ni kwamba unapomheshimu mwanao, na akajua hivyo, atakuwa tayari
kushirikiana na wewe.
Heshima
ni pamoja na kuepuka kuchokoza hisia za mtoto bila sababu za msingi;
kutokumdhalilisha mbele za wenzake kwa kumkemea, kumtukana na kumdhalilisha. Heshima
ni kumpa muda wako na kutokuonekana ukithamini vitu vingine kuliko yeye. Unapomfanya
mtoto aamini unamheshimu, hatakuwa na sababu ya kupambana na wewe na
ukalazimika kumchapa.
Kadhalika,
mheshimu mwanao kwa kujua msukumo ulio nyuma ya madai yake. Tulishajadili namna
kisasi, kutafuta usikivu, kukosa ushawishi na hata kujiona hawezi kuvyoweza
kuchangia utovu wa nidhamu. Mpe nafasi ya kuona anaweza kusikika. Mruhusu
kuongoza utendaji wa shughuli ndogo ndogo hapo nyumbani kulingana na umri wake.
Mpe
nafasi ya kuongoza sala kabla ya kula; mwache aongoze ibada zenu hapo nyumbani;
mruhusu kupendekeza mahali pa kutembelea; mtamkie kuwa unampenda; mkumbatie
ajisikie yu salama mikononi mwako; weka utaratibu wa kumwezesha kufanya vitu
kwa uhuru unaoweza kuudhibiti bila yeye kughamua. Ukiyaratibu vizuri mambo haya
na mengine yanayofanana na hayo, utamjenga mtazamo tofauti. Hatakuwa na sababu
ya kufanya vituko.
Maoni
Chapisha Maoni