Fahamu Namna Ajira Inavyoweza Kukoma kwa Mujibu wa Sheria
Ufanisi wa ajira unategemea uhusiano mzuri uliopo kati ya mwajiri na mwajiriwa. Mwajiri, kwa kawaida, huweka mazingira mazuri kumwezesha mwajiriwa kutekeleza kazi zake. Mwajiriwa naye, kwa upande wake, hutumia ujuzi na uzoefu alionao kufanya majukumu aliyokabidhiwa na mwajiri.
Hata
hivyo, si mara zote matarajio ya pande hizo mbili hufikiwa. Kwa mfano, mwajiri
anaweza kumlalamikia mwajiriwa kwa kutokutekeleza wajibu wake. Mwajiriwa naye anaweza
kuona mwajiri hampi haki zake. Mazingira kama haya huibua migogoro ya kazi
inayoweza kuzorotesha mahusiano ya kikazi.
Sababu
nyingi zinatajwa kuchangia migogoro ya namna hii kazini. Kubwa ni mwajiri na
mwajiriwa kutokujua au kupuuza sheria zinazolinda mahusiano ya ajira baina ya
pande hizo mbili. Mahusiano ya ajira yasiyoongozwa na mkataba wa ajira
isipokuwa kuaminiana yanahatarisha haki na maslahi ya kila upande. Hali hii
inaweza kusababisha migomo, kushitakiana na hata usitishwaji wa ajira.
Sheria
ya ajira na mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 inaainisha namna mwajiri na
mwajiriwa wanavyoweza kulinda haki na maslahi yao. Makala haya yanakuletea
dondoo muhimu za sheria hiyo. Kwa kuanzia, tunajadili mazingira yanayoweza
kusababisha ajira ikome.
Usitishaji kazi
Sheria
hii inatoa mwongozo wa mazingira yanayoweza kufanya ajira ya mwajiriwa ikome.
Kwa mujibu wa sheria hii, ajira inaweza kukoma ikiwa moja kati ya haya
yafuatayo litatokea.
Mosi,
mwajiri amesababisha iwe vigumu kwa mwajiriwa kuendelea na ajira. Mfano, mwajiri
anaposhindwa kumlipa mshahara mwajiriwa; kumnyanyasa au kushindwa kumlinda
mwajiriwa na unyanyasaji wa kijinsia katika eneo la kazi.
Sababu
nyingine ni mwajiriwa mwenye mkataba wa muda maalum anaposhindwa kuongeza
mkataba wake baada ya kuisha muda ulioainishwa kwenye mkataba. Mwajiriwa wa
namna hii anapokuwa na matumaini makubwa ya kuongeza mkataba na mwajiri
akamnyima fursa hiyo, maana yake ni kuwa ajira inakoma. Ikumbukwe zipo ajira za
mkataba wa muda maalum mfano mwaka mmoja, miaka miwili au mitatu. Muda huo
unapokwisha, ajira inaweza kukoma.
Pia,
mwajiri anaposhindwa kumruhusu mfanyakazi wake aliyekuwa kwenye likizo ya uzazi
au ya ulezi kuendelea na kazi. Vile
vile, mwajiri anaposhindwa kumwajiri tena mfanyakazi katika mazingira ambayo
mfanyakazi huyo aliachishwa kazi na wenzake waliorudishwa kazini baadae.
Ajira kukoma yenyewe
Mbali
na uachishwaji kazi, sheria hii inaainisha mazingira ambayo ajira inaweza
kukoma yenyewe. Kwa mfano, inapotokea mwajiriwa amefariki dunia au ametimiza
umri wa kawaida wa kustaafu, ajira inakuwa imekoma yenyewe. Katika mazingira
ambayo mkataba wa kazi hauainishi umri wa kustaafu, basi umri uliozoeleka utatumika.
Umri wa miaka 55 kwa hiyari na miaka 60k kwa lazima.
Kadhalika,
changamoto za kiuendeshaji anazokutana nayo mwajiri zinaweza kutengeneza
mazingira ya ajira kukoma yenyewe. Kwa mfano, mwajiri akipoteza utaalamu wa kufanya
shughuli iliyotengeneza ajira kwa mwajiriwa au inapotokea amenyang’anywa mali
zake, ajira itachukuliwa kama imekoma.
Kuachishwa kazi kwa makubaliano
Mkataba
wa kazi kati ya mwajiri na mwajiriwa unaweza kusitishwa kwa mujibu ya
makubaliano yaliyoainishwa kwenye mkataba husika. Kwa mfano, pale ambapo
mkataba ni wa muda maalum, kama ilivyo kwa waajiriwa wengi kwenye sekta
binafsi, mkataba huo utakoma wenyewe wakati muda uliokubaliwa utakapokoma
isipokuwa kama mkataba unaeleza vinginevyo.
Hata
hivyo, kama mazingira yanaruhusu, mkataba huo wa muda maalum unaweza kuongezwa
kwa makubaliano kati ya mwajiri na mwajiriwa. Katika mazingira ambayo mwajiriwa
anategemea kuongezewa mkataba wa kuendelea na ajira, mwajiri anaposhindwa
kumwongezea mkataba, hiyo itachukuliwa kama uachishwaji kazi usio wa haki.
Kama
mkataba wa muda maalumu haukuongezwa, na mwajiriwa akawa na sababu za msingi za
kusema alitegemea kuwa angeongezewa mkataba hiyo itachukuliwa kuwa ameachishwa
kazi. Kwa mfano, kama siku za nyuma mwajiri
alimwongezea mwajiriwa mkataba basi hiyo inaweza kumaanisha kuwa mwajiriwa
alikuwa na matumaini makubwa ya kuendelea na ajira hata kama mkataba wa ajira
ulikuwa ni wa muda maalum.
Mwajiri
naye anaweza kuwa na sababu za kutokumwongezea mwajiriwa mkataba. Kwa mfano, ikithibitika
mwajiriwa alishiriki kufanya vitendo viovu kazini kinyume na taratibu za kazi;
aina ya shughuli ya ajira inahitaji kufuata kikamilifu kanuni kuliko inavyoweza
kuwa kawaida na uwezo wa mwajiri hauruhusu kuongeza mkataba.
Kujiuzulu
Mwajiriwa
mwenye mkataba wa muda maalum anaweza kujiuzulu tu kama anaona mwajiri amevunja
makubaliano ya mkataba au kwa sababu nyingine yoyote. Lakini kama mwajiri
hakuvunja mkataba, mwajiriwa anaweza kuvunja mkataba kisheria kabla ya kuisha
kwa muda uliowekwa kwenye mkataba kwa kuhakikisha amekubaliana na mwajiri.
Sheria
hii pia inamruhusu mwajiriwa mwenye mkataba usio na kikomo kujiuzulu ikiwa ana
sababu za kufanya hivyo. Ili aweze kujiuzulu, mwajiriwa analazimika kutoa mapema
taarifa ya kuacha kazi kama ilivyoanishwa kwenye mkataba.
Hata
hivyo, mwajiriwa anaweza pia kuacha kazi bila kutoa taarifa ikiwa mwajiri ndiye
aliyevunja mkataba kimsingi. Kuvunja mkataba kimsingi ni kukiuka kiini cha
makubaliano ya msingi yanayoonekana kwenye mkataba. Kwa mfano, mwajiri akikataa
kulipa mshahara, akimdhalilisha mwajiriwa kwa maneno au vitendo vya unyanyasaji
wa kijinsia au ubaguzi usio wa haki kazini.
Kuacha kazi kwa kulazimika
Kulazimika
kuacha kazi kuna maana kuwa mwajiriwa anajikuta katika mazingira ambayo mwajiri
amefanya iwe vigumu kwa mwajiriwa kuendelea na kazi yake. Kwa mfano, inapobainika
kuwa mwajiri amesababisha ajira kushindwa kuvumilika na kusababisha mwajiriwa
kuacha kazi, itachukuliwa kuwa mwajiriwa ameachishwa kazi na mwajiri.
Mambo
yanayoweza kufanya mwajiriwa aonekane amelazimika kuacha kazi ni pamoja na unyanyasaji
wa kijinsia unaofanywa na mwajiri, kutokutendewa haki na mwajiri katika
mazingira ambayo amefuata taratibu za kushughulikia malalamiko yake.
Inaendelea
Mawaidha mazuri mno. Mimi ni mwalimu wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Wanafunzi wangu hapana shaka watafaidika na maoni haya.( http://kiswahili.uonbi.ac.ke)
JibuFutaJe katika suala la likizo swali lipo ivi mfanyakazi anatakiwa aende likizo kwanza ndipo aje aongeze mkataba au inakuaje
JibuFuta