Jifunze Namna Bora ya Kumrudi Mtoto

PICHA: IT News Africa

Tunapojadili mbadala wa adhabu ya bakora tunatambua changamoto kadhaa. Kwanza, ni wazi bakora zimekuwa sehemu ya malezi yetu. Kwa wazazi wengi, unapozungumzia nidhamu ya mtoto, maana yake unazungumzia bakora. Imejengeka imani kwa watu kuwa bakora ndiyo nyenzo kuu inayoweza kumrekebisha mtoto.

Pili, pendekezo linalokwenda kinyume na imani hiyo lazima likutane na upinzani mkali. Wanaopinga wanafanya kwa nia njema wakiamini huwezi kumuadabisha mtoto bila bakora. Hili ni jambo la kawaida. Mwanadamu anapoamini jambo kwa dhati ni vigumu kumbadilisha.

Hata hivyo, katika maisha zipo nyakati tunalazimika kubadilika. Mambo mengi yana kawaida ya kubadilika. Imani tulizonazo zinabadilika kama ambavyo utamaduni nao hubadilika.

Kusema hivi haina maana ‘tunajifanya wasomi wanaopuuza utamaduni wetu.’ Hapana. Ni kuelewa nafasi muhimu ya kujifunza mambo mapya yanayotusaidia kufanya mambo yetu kwa namna bora zaidi.

Itakumbukwa, kwa mfano, zamani vipigo vilikuwa sehemu ya mahusiano ya ndoa. Akina mama wengi walipigwa na waume zao kwa imani kuwa haiwezekani mwanamke kumheshimu mumewe bila kupigwa. Wanawake wengine walifurahia vipigo kwa imani kuwa  anayekupenda lazima akupige.

Lakini kidogo kidogo mambo yalibadilika. Sasa tunaelewa kuwa inawezekana kupata heshima na upendo bila kichapo.

Umuhimu wa adhabu

Hata katika malezi, wazazi tunaweza kubadilisha mtazamo. Kwa mfano, tunao ushahidi kuwa pamoja na ‘faida’ zake, bakora zina athari nyingi kwenye imani, mtazamo na tabia atakazojenga mtoto baadae. Sambamba na hilo, pia misukumo iliyo nyuma ya utovu wa nidhamu anayoionyesha mtoto inafahamika.

Mzazi unapojifunza kuelewa misukumo hii, inakusaida kuchukua hatua muafaka za kurekebisha mambo kabla hujalazimika kutumia bakora. Kilicho muhimu unapochukua hatua, ni kujaribu kuvaa viatu vya mtoto na kuelewa kwa nini amefanya alichokifanya.

Kumwelewa mtoto, hata hivyo, haimaanishi tunashauri usimwadhibu mtoto. Kuna umri lugha anayoweza kuielewa vizuri zaidi mwanao ni adhabu. Unapomfanyia kile asichokipenda kama matokeo ya kufanya kisichotakiwa, unamsaidia kuelewa ubaya wa alichokifanya. Katika mazingira haya, adhabu ndiyo sauti anayoweza kuisikia kwa ufanisi zaidi. Usipomwadhibu hatajifunza.

Maana ya adhabu

Adhabu ni hatua zozote anazochukua mzazi kwa lengo la kupunguza uwezekano wa mtoto kurudia tabia isiyokubalika. Hatua hizi, mara nyingi, ni kumtendea mtoto kinyume na kile anachokipenda kama matokeo ya yeye kufanya kisichokubalika.  Kwa mfano, unapomnyima mtoto kile alichozoea kukipata, hiyo ni adhabu kwa sababu unamfanya ajisikie vibaya.

Katika mazingira hayo ya kujisikia vibaya, inakuwa rahisi kwake kuhusianisha kile alichokifanya na matokeo yake. Kwa kuwa angependa kupata kile anachokitaka, inakuwa  rahisi kwake kuachana na kile alichokifanya.

Ili adhabu ya namna hii iwe na maana, lazima kwanza kujua kitu gani mtoto anakithamini. Ukishajua mtoto anapenda kusomewa hadithi, kwa mfano, unaweza kuahirisha kufanya hivyo kumwadhibu. Kutokumsomea hadithi kutamshawishi kubadilika ili umsomee siku nyingine.

Kadhalika, adhabu inaweza kuwa na sura ya kumtendea mtoto kile asichokipenda. Tofauti na kumnyima anachokipenda, adhabu ya namna hii inalenga kumsababishia maumivu ya kihisia yanayomfanya ajisikie vibaya.

Mfano, mtoto wa miaka miwili anadeka na kulia bila sababu ya msingi. Ili kumwadhibu unaamua kumkemea, kumwonya au kuonyesha kutokufurahishwa na alichokifanya. Lengo ni kumkatisha tamaa ya kuendelea kukosea na badala yake afanye vile unavyotarajia afanye.

Kanuni za kuadhibu

Kanuni ya kwanza, adhabu ni lazima ianze mapema. Mtoto anapoanza kuwa na ufahamu, anza kumpa adhabu zinazolingana na umri wake. Usimcheleweshe.

Katika umri mdogo mtoto hufanya makosa bila kujua. Usipomsaidia kuelewa mapema kuwa amefanya makosa, utakomaza tabia itakayokupa shida kuiong’oa baadae.
Kama unamwita mtoto haitiki, hakikisha anatambua kosa lake. Usipuuze kosa kwa kisingizio kuwa mtoto bado ni mdogo. Mwelekeze. Asiposikia, mkemee. Akiendelea kufanya vile vile, tumia mbinu ya kumnyima anavyovipenda.

Pili, toa adhabu mara tu kosa linapofanyika. Usiache muda mrefu upite ndipo uadhibu. Kwa mtoto mdogo wa mpaka mwaka mmoja, mathalani, adhabu iwe pale pale. Anapofanya kosa, mwambie mara moja.

Unaponyamazia makosa hata yale unayoona ni madogo kwa kuamini utayashughulikia baadae, unatengeneza hatari ya mtoto kuamini –kwa muda –kuwa anachokifanya ni sahihi. Unapokuja kuibua kosa hilo baadae, unamchanganya mtoto.

Tatu, uwe na msimamo usiobadilika dhidi ya kosa. Usibadilike badilike utamchanganya mtoto ashindwe kujua kosa kwako ni nini na kilicho sahihi kwako ni kipi. Kwa mfano, kama ulimwadhibu kwa kutokwenda ulikomtuma, usiache kumwadhibu akirudia kosa hilo.

Msimamo unamsaidia mtoto kukuelewa unataka nini. Anapokuwa na hakika na msimamo wako, uwezekano wa kurudia makosa yale yale unapungua. Lakini pia inapotokea amerudia kosa lile lile mara kwa mara, itakusaidia kuamua aina ya adhabu inayoweza kumfaa.

Nne, toa adhabu bila kumdhalilisha. Heshimu utu na hisia za mwanao. Epuka kumwadhibu kwa namna inayomfedhehesha. Kwa mfano, huna sababu ya kumkemea mtoto mbele za wenzake, kuadhibu ukiwa na hasira kali, kumtukana au kumshambulia kwa maneno yasiyo na staha na hata kutumia nguvu kubwa isiyo na lazima.

Kosa la mtoto –bila kujali ukubwa wake– lisikufanye ukashawishika kumvunjia heshima. Mstahi hata pale anapokukosea. Hatua zozote za kumdhalilisha hujenga kisasi ndani yake kitakachofanya atamani kukukosea.

Kuna umri mtoto hupenda heshima zaidi. Mfano anapokuwa kwenye umri wa kupevuka kimwili. Jitahidi kumtendea kama mtu mzima. Mheshimu. Usifanye kosa la kumpa adhabu mbele ya wenzake kama si lazima. Anapokosea, mwite faraghani mshughulikie kwa staha.

Tano, adhabu itanguliwe na mazungumzo. Unapojiridhisha kuwa mtoto anaweza kuelewa unachomwambia, jenga utaratibu wa kuongea nae kabla hujamwadhibu. Msaidie kujua kosa lake ni nini na alitarajiwa kufanya nini.

Baada ya kumwadhibu mtoto, fanya jitihada za kurudisha uhusiano wenu. Msamehe. Usimwonyeshe mtoto mfano mbaya kwa kuendelea kumkumbushia kosa mlilokwisha kulimaliza. Msamaha ni motisha ya kufanya anachojua unakitajia.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia