Wajibu wa Wamiliki wa Shule za Msingi za Bweni
PICHA: BORGEN Magazine |
TUMESHAURIANA
mambo kadhaa ya kuzingatia tunapolazimika kuwapeleka watoto wadogo kwenye shule
za msingi za bweni. Kubwa zaidi ni mzazi kujiridhisha na namna shule inavyomwekea
mtoto mazingira mazuri yanayofanana na yale ya nyumbani.
Katika
makala haya, tunazishauri menejementi za shule zinazotoa huduma za bweni kwa ngazi
ya shule ya msingi. Ushauri huu
unatokana na uchambuzi wa matokeo ya tafiti mbalimbali za malezi ya watoto
wanaolelewa vituoni (institutionalized child care).
Huduma za msingi
Shule
zihakikishe huduma zinazingatia ubora kwa kuyafanya mazingira ya shule yawe na
sura ya nyumbani. Watoto wadogo wasichanganywe na watoto wa umri mkubwa katika
chumba/bweni moja.
Mtoto asichangie kitanda na wenzake; aishi na majirani wachache
chumbani wanaolingana nae kiumri; apate uangalizi wa karibu kwa mlezi mwenye
sifa na anawasiliana kwa karibu na wazazi wake.
Idadi
nzuri kwa watoto wa darasa la kwanza mpaka la saba ni watoto wanne kwa chumba kimoja
bwenini. Mlezi mmoja aangalie vyumba viwili mpaka vinne kwa watoto wa madarasa
ya awali, na vyumba vinne mpaka sita kwa madarasa ya juu. Kufanya hivi
kunawawezesha walezi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mtoto mmoja moja kama
inavyokuwa nyumbani.
Sifa za walezi
Si kila
mtu anaweza kuwa mlezi wa watoto wadogo. Ni muhimu, basi, kupata mtu mwenye
moyo wa kuwapenda, kuwajali na kuwatunza watoto bila mtoto kujisikia kusumbuliwa.
Mara
nyingi walezi wa kike ambao ni wazazi hufanya vizuri zaidi ya walezi wa kiume. Walezi
hawa wanakuwa na uelewa mzuri wa mahitaji mahususi ya watoto kuliko walezi
wasio wazazi.
Kadhalika,
walezi wasibadilike badilike mara kwa mara. Watoto wanahitaji kuwa na mtu
waliyemzoea na kumwamini, waweze kuwa huru naye. Unapobadili mlezi mara kwa
mara, unawapa kazi watoto kumzoea upya hali inayoweza kuwafanya wakakosa amani
kuona mtu waliyemwamini anaachana nao.
Pia menejimenti
zitambue kuwa uzoefu pekee hautoshi. Ni muhimu kuwaandalia walezi semina za
mara kwa mara kuwasaidia kuboresha uelewa wao kuhusu mahitaji ya watoto kiumri.
Utaratibu wa
mawasialiano
Mtoto
aliyetengwa na familia yake anapungukiwa kitu muhimu kwenye maisha yake. Ukaribu
wa kifamilia unamsaidia mtoto kujisikia salama kisaikolojia.
Shule itengeneza
utaratibu mzuri wa wazazi kuwasiliana na watoto wao mara kwa mara. Kwa watoto
wa madarasa ya awali, ni vyema wazazi wapate fursa ya kuwaona watoto angalau
mara moja kwa juma. Kufanya hivi kutawaruhusu watoto kuendelea kuwa karibu na
wazazi wao hata katika mazingira ya shule.
Sambamba
na hili, wazazi waelimishwe na kimsingi walazimike kuwatembelea watoto wao
wanaoishi bweni. Kwa kuwa wapo wazazi wanaoweza kuwatelekeza watoto shuleni kwa
miezi kadhaa, shule zinaweza kuweka kigezo cha kumtembelea mtoto kama kigezo
cha kuendelea kupata huduma hiyo ya bweni.
Mazingira sisimushi
Shule
iweke mazingira sisimushi kwa mtoto. Sambamba na vifaa vya kujifunzia vinavyopatikana
kwenye shule nyingi, ni muhimu kuhakikisha watoto wanapata muda mzuri wa
kucheza na kufurahia muda wa mapumziko. Shule nyingi zinaweka msisitizo kwenye
taaluma na kusahau michezo.
Pia katika
kuhakikisha mtoto anajenga uwezo wa kujimudu, shule iwe na ratiba ya
kuwawezesha watoto kushiriki kazi za mikono. Badala ya kuwa na watu maalum wa
kufanya kazi za nje, ni muhimu mtoto ashiriki kikamilifu. Shughuli kama kufua
nguo nyepesi, kusafisha maeneo anayoishi, kutunza bustani, kusafisha vyombo na
shughuli nyingine kama hizo.
Kama tulivyoona,
wazazi wengi wanakuwa na matarajio makubwa kitaaluma kwa watoto wao. Hali hii
inakuwa shinikizo kwa walimu kuweka msisitizo wa kitaaluma ambao wakati
mwingine haulingani na uwezo wa mtoto.
Wazazi
waelimishwe hasara za kuwa na matarajio makubwa kitaaluma kwa watoto. Hatua hiyo
inaweza kuzisaidia shule kuongeza muda wa michezo ambayo nayo ni muhimu kwa
ukuaji wa watoto.
Haya
yakifanyika, shule za bweni zinaweza kuwa na faida kwa watoto ambao kwa namna
moja au nyingine wanalazimika kuondoka kwenye mazingira ya nyumbani kwenda kupata
elimu katika shule za bweni.
Makala
haya yalichapishwa awali kwenye Jarida la Kisima cha Maarifa linaloandaliwa na
Gazeti la Mtanzania.
Maoni
Chapisha Maoni