Unavyoweza Kumfundisha Mtoto Kuwa Mkweli
Fikiria uko jikoni ukiandaa chakula cha jioni. Watoto wako wawili wadogo
Fred na Joe wanacheza sebuleni. Salome yuko mezani akifanya kazi za shule.
Mara unasikia mlio wa kitu kuvunjika sebuleni. Unapatwa na wasiwasi. Unakwenda
haraka kujua kilichotokea. Maji yanatiririka sakafuni. Chupa ya chai imedondoka
na kupasuka. Unakasirika.
Fred, mwanao mdogo, haonekani kuwa na wasiwasi. Haraka anamsemea mkubwa,
‘Sio mimi mama…ni Joe!’ Kwa hasira unamtazama Joe. Uso wake kweli unaonyesha wasiwasi.
Kwa ukali unamwuuliza, ‘Wewe ndo’
umevunja chupa?’
Anasita. Amejaa wasiwasi. ‘Nauliza ni wewe?’ unarudia. Kwa haraka anajibu
huku akitikita na kichwa, ‘A-a-a! Sio mimi mama!’
‘Nani amevunja chupa?’ Unauliza kwa hasira kali. Mdogo anasisitiza, ‘Ni
Joe!’ Unamshika mkono kwa ghadhabu kubwa huku ukilalamika, ‘Kwa nini umevunja
chupa?’
Salome anaona aokoe jahazi. ‘Usimchape Joe mama. Aliyevunja chupa ni
Fred!’ ‘Fred?’ Unakasirika kudanganywa na mtoto wa miaka miwili. Mbaya zaidi haonekani
kujutia anachokifanya.
Hatari ya uongo
Kwa nyakati na sababu tofauti watoto wote
hudanganya. Kudanganya ni kusema uongo. Ni kutoa habari zisizo za kweli.
Uongo ni dhambi. Uongo huumiza watu.
Uongo unaharibu uhusiano wetu na watu. Mtu mwongo haaminiki. Hakuna mzazi anaweza kuvumilia kuona analea
mtu ambaye hataaminika kwa jamii.
Tabia ya uongo ikiachwa ikomae ni
hatari kwa mstakabali wa mtoto. Kama mzazi unayetamani kukuza mtoto mwadilifu
atakayeaminiwa na watu ni lazima kuushughulikia mapema.
Sababu za watoto hudanganya
Hatuzaliwi na tabia ya kudanganya.
Tunajifunza. Bahati mbaya, tunapoanza kujifunza uongo, nia huwa ni ‘njema.’ Mtoto
wa miaka miwili, kwa mfano, hajui maana ya kusema uongo. Anapodanganya, akili
yake haikusudii kudanganya.
Fred tuliyemwona hapo juu hakuwa na lengo
la kudanganya. Mazingira yalimlazimisha kudanganya. Kimsingi kwa umri wake,
hana uwezo wowote wa kutunga uongo.
Fred anatamani angechukua nafasi ya
Joe. Anajua kabisa kuvunja chupa ni kosa kwa sababu mama amekasirika. Hatamani
kuwa upande wa kumwuudhi mama yake.
Kwa sisi watu wazima Fred anadanganya.
Lakini yeye haoni hivyo. Anatumia ‘uongo’ kusema matamanio yake. Anaposema, ‘Ni
Joe’ maana yake anatamani angekuwa Joe. Hapendi matokeo ya kile alichokifanya.
Sababu ya pili, mtoto hutumia uongo
kama namna ya kulinda uhusiano wake na mzazi. Kwa mtoto, uhusiano na mzazi ni
kitu cha maana kuliko kitu kingine chochote kinachostahili kulindwa kwa gharama
yoyote.
Kufanya kosa maana yake ni kuhatarisha uhusiano
wake na mtu wa muhimu zaidi kwenye maisha yake. Kwanza, anajua matokeo ya kukiri
kosa maana yake ni kukaribisha adhabu. Ili awe salama lazima aseme kile
anachojua ndicho mzazi anachokinatarajia. Kudanganya ni kuepusha shari na mzazi
wake.
Pia mtoto mkubwa kidogo huweza kutumia
uongo kama silaha ya kupambana na wabaya wake. Hudanganya kama namna ya
kumwuumiza mtu mwingine.
Kwa mfano, anapoamini mdogo wake
anapata upendeleo, anaweza kutumia uongo kujaribu kumwingiza mwenzake kwenye
matatizo. Anachoamini ni kuwa wazazi wanapokosa imani na mwenzake, yeye anakuwa
kwenye nafasi nzuri.
Tufanyeje kuondoa tabia ya uongo kwa
watoto? Tuangazie kanuni nne kubwa.
Usimfanye akudanganye
Unaweza
kuchochea tabia ya uongo bila kujua kwa kuuliza maswali yanayoweza kumfanya
mtoto ashawishike kukudanganya. Kwa mfano, unamwona mtoto anakula
bila kuombea chakula kama ulivyomwelekeza. Usiombe akudanganye kwa kumwuuliza
kama ameshaombea chakula.
Kumbuka kuwa fahari ya mtoto ni kukupendeza wewe mzazi.
Unapomwuuliza swali kama hilo unamshawishi kukudanganya ili asipoteze sifa za
kuwa ‘mtoto mzuri kwako.’
Badala ya kuomba kudanganywa kwa maswali ya uchokozi, shughulika
na kosa moja kwa moja. Mwonyeshe kosa lake na mwelekeze afanye nini. Ikiwa kosa
linastahili adhabu fanya hivyo.
Mrekebishe anapodanganya
Kupuuza
uongo ‘mdogo’ unaoubaini kwa mwanao ni kukomaza tabia ya uongo wa makusudi
mbeleni. Shughulika nao kila unapojitokeza. Hapa kuna njia mbili.
Mosi,
kama mwanao tayari ana uelewa, zungumza nae kirafiki uelewe kwa nini amekudanganya.
Ikiwa anadanganya kwa lengo la kukupendeza, pengine shida ni namna unavyoshughulikia
makosa yake. Jifunze kumrekebisha kwa njia za kirafiki.
Pili,
ikiwa mwanao anadanganya kwa nia ya kuwakomoa wengine, mwadhibu. Jambo la
kuzingatia ni kwamba si wakati wote adhabu husaidia. Mtoto anaweza kukwepa
ghadhabu zako kwa kukudanganya. Jirekebishe.
Hata
anapokuwa amekudanganya, tumia lugha inayoonyesha kuwa bado una matarajio
chanya na yeye. Epuka kumwita majina kama ‘mwongo wewe’ ‘nilijua
utanidanganya.’ Unapofanya hivyo anaona tayari umemweka kwenye kundi la
waongo.
Usimwadhibu kwa kusema ukweli
Unafanyaje
mtoto anapokwambia ukweli unaothibitisha kuwa amekosea? Mfano, mtoto amekiri
kuwa ndiye aliyevunja sahani. Unamwadhibu kwa sababu alichofanya ni kosa?
Katika
mazingira haya unalazimika kufanya mazungumzo ya kirafiki kuliko kuadhibu.
Unapoadhibu fikiria ujumbe usiowazi unaoutuma kwake. Adhabu inaweza kuwa na
maana, ‘ni hatari kuwa mkweli.’ Siku nyingine atakudanganya kuepusha shari.
Badala
ya kutumia adhabu kama suluhisho, zungumza nae ajue kosa lake. Kisha onyesha
kuelewa kwa nini amefanya kosa na mpongeze kwa kuwa mkweli. Unapofanya hivyo
hulei makosa yake bali unampa motisha ya kuwa mkweli.
Onyesha mfano mzuri
Mtoto
hawezi kuwa tofauti na mzazi wake. Usipokuwa na tabia ya kusema ukweli hata katika
mazingira magumu, unamfundisha mtoto kudanganya. Unapoahidi jambo kwa mwanao,
tekeleza. Ikitokea umeshindwa kutekeleza, omba msamaha.
Usitumie
uongo kufunika makosa yako. Anapouliza
swali gumu, mpe maelezo rahisi ya kweli badala ya uongo ‘mzuri’ ambao, hata hivyo,
anaweza kuugundua baadae.
Kadhalika, usiwadanganye watu mbele yake. Usimpe mtu majibu
ambayo mtoto atajua ni ya uongo. Mfano, uko nyumbani umepigiwa simu na mkuu
wako wa kazi akiuliza uliko. Unaposema uko ofisini na mtoto anakusikia, mtoto
ataona uongo ni sehemu ya maisha. Usishangae akikudanganya na wewe siku
nyingine.
Asante mwalimu.Wazazi tuwe wakweli ili watoto nao watuige
JibuFuta