Namna ya Kuutambua Wito wa Maisha Yako
PICHA: Baha'i Blog |
Umewahi kufanya kazi
zenye heshima lakini hujisikii ridhiko ndani yako? Unapata kipato kizuri na
watu wengine wanatamani kufanya unachokifanya lakini wewe mwenyewe hufurahii.
Unakuta umesoma vizuri lakini
huoni thamani ya kile ulichokisoma. Zaidi ya kutaja chuo ulichosoma na ngazi ya
elimu uliyofikia huoni namna gani elimu yako inakusaidia kutoa mchango kwa
jamii.
Lakini pia inawezekana umejitahidi kupenda hicho ulichokisoma. Ni kawaida ukifanya kitu kwa muda fulani akili inaweza
kukulazimisha kukipenda. Shida ni ubunifu. Unapofanya kitu ambacho sio wito
wako huwezi kuwa na ubunifu zaidi ya kukariri kile ulichofundishwa na mwalimu
wako. Unakuwa kama umefungwa na nadharia.
Katika maisha mazingira
yana nafasi kubwa ya kutulazimika kufanya kisichotoka ndani. Tunajikuta
tukifanya mambo yasiyoendana na wito wetu. Tunakuwa wepesi sana kusikiliza
maoni ya watu wengine kuliko kujua kile kilichojificha ndani yetu.
Matokeo yake tunaishi
maisha ya wengine. Tunawaiga wale tunaodhani wanaheshimika kwenye jamii. Tunafanya
tunachofikiri watu wanakitarajia kwetu. Tunasoma kozi fulani kukidhi matakwa ya
watu. Tunajikuta tunataka kufanya kazi zinazotarajiwa na jamii. Tunaishi wiito
ya watu wengine.
Tunasahau kuwa
mwanadamu ni mtu wa pekee. Wewe unayesoma hapa ni mtu wa pekee. Mungu ameweka
vitu vya pekee ndani yako. Unahitaji kuvijua ili vikuongoze kufanya maamuzi ya
msingi katika maisha.
Tufanye nini kutambua
vitu alivyoviweka Mungu ndani yetu? Kuna mambo mengi ya kuzingatia. Hapa
naleta kwako maswali matatu unayohitaji kuyajibu.
Una vipaji gani?
Kila mtu ana vipaji
vyake. Unaweza usikifahamu kipaji chako lakini hiyo haimaanishi huna.
Tunapoongelea kipaji usifikiri vitu vikubwa ukachanganyikiwa.
Kipaji ni ule uwezo wa
kufanya vitu kwa namna rahisi ambayo watu wengine hawawezi. Ni ule ujuzi
unaokuwa nao bila hata kufundishwa sana.
Kwa mfano mwimbaji.
Hahitaji kwenda kusomea ili ajue namna gani aimbe. Ni uwezo wa kuzaliwa nao.
Akienda shule kujinoa zaidi inakuwa vizuri. Lakini elimu inakuwa kama inajazia
kitu ambacho tayari anacho tayari. Asiye na kipaji anapokwenda kusomea kitu
inakuwa kama kumfundisha sungura namna ya kupaa angani kama kunguru.
Tafakari vipaji
alivyokupa Mungu. Pata nafasi ya kujikagua ndani yako. Una kipaji gani? Je, ni kuwashawishi
watu? Kuchora? Mbunifu? Fundi? Mwandishi? Mwalimu? Biashara? Tambua kipaji
chako.
Kitu gani kinakuvutia?
Pengine kujua kipaji
inaweza kukuwia vigumu kwa sasa. Najua si kazi rahisi na wakati mwingine
inahitaji muda. Lakini angalau kila mmoja wetu anaweza kujua kile anachopenda
kukifanya. Nikikuuliza unavutiwa na nini kwenye maisha huwezi kupata shida.
Kila mtu ana vitu vinavyomvutia.
Ndivyo hata wewe ulivyo. Kuna vitu vinakuvutia. Unapenda kuvifanya vitu fulani kwenye
muda wako wa ziada. Mfano mimi hapa napenda kuandika. Nikiwa kwenye mapumziko kuandika.
Ndiyo furaha yangu kujieleza. Kuandika ni moja wapo ya vitu vinavyovipenda.
Kipimo kuwa unapenda
kitu fulani ni utayari wako wa kukifanya bila malipo. Unaridhika tu kukifanya hata
bure. Nikijitolea mfano mwenyewe, sisubiri kulipwa ili niandike. Navutiwa na maandishi.
Mwimbaji hali kadhalika maisha
yake ni kuimba. Huhitaji kumlipa ili aimbe. Mwalimu naye huhitaji kumlipa ili
akuelekeze kitu. Kufundisha ndiyo maisha yake. Wewe unavutiwa na nini? Lazima ukifahamu.
Kusema hivi
haimaainishi tusilipwe kwa sababu tu tunapenda tunavyovifanya. Hapana. Tunachokisema
ni kupenda kitu kwa dhati kabisa.
Labda mpaka hapa bado
huelewa unavutiwa na nini. Nikupe kipimo kingine. Hebu fikiria watu maarufu wanaokuvutia. Nani
unampenda? Mimi nawapenda wengi. Mmoja
wao anaitwa Rick Warren. Nimejifunza vingi kwake. Mwingine Stephen Covey.
Nimesoma mawazo yao mengi.
Usiishie kusema
nampenda fulani. Nenda hatua moja mbele. Tafuta sababu kwa nini unawapenda watu
hao. Kwa mfano mimi hao jamaa niliokutajia nawapenda kwa sababu ya misimamo yao kwenye maisha. Kila
nikisoma na kusikiliza mawazo yao kuna kitu wanachokisema hakibadiliki. Kinanivutia kwao.
Na wewe lazima ujiulize
kwa nini unavutiwa na hao uliowafikiri hapo juu. Hicho kinachokuvutia chaweza
kuwa ndio ni sehemu ya kitu unachokipenda kwenye maisha. Huo ndio wito wako.
Maamuzi gani yanakupa kuridhika?
Kwa kuwa zipo sababu nyingi
zinaweza kukufanya ukavutiwa na kitu lazima kuongeza kipimo cha kupima udhati wa
msukumo ulio ndani yako. Hapa tunaongelea kuchukua hatua ngumu lakini zinazokupa
kuridhika.
Kuridhika ni kujisikia
utoshelevu na kitu unachokifanya. Hapa
hatuongelei utoshelevu wa kuwaridhisha watu. Hatuongelei kuamua kufanya kitu
fulani unachojua kuna watu wanatarajia ukifanye. Hatuongelei msukumo wa
kuridhisha watu unaowapenda.
Tunaongelea msukumo wa
kimaamuzi unaoanzia ndani yako kukushawishi kufanya vitu unavyodhani ni vya
muhimu kwako bila kuangalia wengine wanasemaje. Hiki ndicho kipimo cha juu cha
wito wako. Utayari wa kulipa gharama za kuutumikia wito wako.
Maamuzi haya mara nyingi ni yale yatakayobadili maisha
yako. Mfano kuacha kazi na kubadili fani uliyosomea. Si jambo jepesi. Inahitaji moyo. Fikiria mtu anayeweza kuamua kuacha kazi. Lazima awe na sababu kubwa kiasi cha kutokuwa na woga na changamoto zinazoweza
kuambatana na maamuzi yake.
Maamuzi haya yanaweza kuwa na changamoto kadhaa. Changamoto ya kwanza ni
kupishana na hata kuachana na baadhi ya watu wa muhimu kwenye maisha yako. Mara nyingi si kila mtu atauelewa wito wako. Watu hawataelewa mantiki ya unachokifanya. Watu wanakuona kituko. Lakini ndani yako unajua unafanya kitu sahihi.
Hata hivyo si mara zote unapouendea wito wako mambo yatakuwa mepesi. Unakumbata na changamoto nyingi. Lakini kama umeupambanua wito wako vizuri hutarudi nyuma
hata kama mambo yatakuwa magumu namna gani. Utaendelea kusimama imara huku
ndani yako ukiwa na amani.
Kama bado hujaweza
kufanya maamuzi mazito kwenye maisha yako; kila mtu anaelewa kile unachokifanya; unapend kufanya kitu kwa sababu tu wengi wanakipendekeza; unafanya kufanya kitu usichokipenda au
unajaribu kufanya vitu vingi kwa wakati moja, inawezekana kabisa bado hujautambua wito
wako.
Rudi ndani yako tafakari wito wako. Jielewe. Fanya maamuzi ya kuufuata wito wako. Ukifanya kitu ulichopaswa kukifanya, utakuwa mtu mwenye utoshelevu mkubwa.
Rudi ndani yako tafakari wito wako. Jielewe. Fanya maamuzi ya kuufuata wito wako. Ukifanya kitu ulichopaswa kukifanya, utakuwa mtu mwenye utoshelevu mkubwa.
Daah nimeipenda hii article asante sana mwl
JibuFutaThanks
JibuFuta