Thamani Yako Inategemea Namna Unavyowasaidia Wengine
KUNA ukweli kwamba katika harakati za
kutafuta mafanikio, unahitaji kuwa na uhusiano mzuri na aina fulani ya watu. Hawa
ni watu wanaokuzidi kile unachotaka kukifanya na kwa namna moja au nyingine wanaweza kuwa msaada kwako
kwa kukupa mtaji wa kutekeleza wazo lako, kukunganisha na nafasi za ajira
zisizotangazwa hadharani au kukusaidia mawazo yatakayokupeleka mbele kimaisha.
Pamoja na uwezo mzuri wa kufanya vitu,
vipaji na elimu, bado unahitaji msaada wa watu wengine kukufikisha kule unakotaka. Hata
hivyo, kujenga uhusiano wenye tija na watu unaowahitaji si jambo linalokuja
hivi hivi. Unahitaji tabia fulani zitakazowafanya watu wajione wanalo deni la
kukusaidia. Usipozielewa tabia hizo, utajikuta katika mazingira ambayo
unafahamiana na watu wengi wasiokuchukulia kwa uzito wowote.
Vijana wengi, hasa wanaoanza biashara
na pengine wanaotoka kwenye familia zisizo na majina, wanatamani kupata watu
wanaoweza kuwa msaada kwao. Wafanye nini ili kujenga mtandao imara na watu
wanaoweza kuwa msaada kwao?
Jambo la kwanza ni kuelewa tabia za
ubinafsi alizonazo binadamu. Sote kwa namna moja au nyingine tunajali zaidi
maslahi yetu binafsi kuliko maslahi ya watu wengine. Hata pale tunapoonekana
kuwajali wengine, ndani yetu, inawezekana kuna faida fulani tunayoipata.
Aidha, ubinafsi
huo huo ndio unaotufanya binadamu tusipende shida. Hakuna mtu anapenda kuwa
kwenye mazingira yanayomwuumiza. Hii ni kweli hata kwenye uhusiano wetu na
watu. Kila binadamu hujilinda asijikute
kwenye mazingira ya kutumiwa na watu wengine bila faida. Kinachojenga
urafiki wa karibu, kwa mfano, ni vile watu wawili wanavyosaidiana kupunguziana
shida badala ya kuumizana.
Kwa hivyo, ukitaka
kuwa na uhusiano imara na watu, hasa wale wanaokuzidi, epuka kuonekana
unawaongezea shida kwenye maisha yao. Usimfanye mtu akajihisi anatumiwa zaidi
kuliko anavyopata kwako. Ukifanya kosa hilo utaonekana mzigo.
Kuna mambo mengi
unaweza kuyafanya bila wewe kujua na ukaanza kuonekana mzigo kwa watu. Mfano,
ni kuwa mtu wa kulalamika. Unapolalamika maana yake huna majibu ya matatizo
unayoyaongelea. Watu waliofanikiwa, hawapendi kusikia mtu anayetumia nguvu
nyingi kuongelea shida badala ya ufumbuzi.
Pia, unapokuwa
na tabia ya kutaka kupata misaada na vitu kwa watu kuliko vile unavyochangia
kutatua changamoto zao, watu hawatatamani kukutana na wewe. Sababu ni kwamba
wanapokuona hawakuoni wewe, bali wanaona mzigo. Hakuna mtu anapenda mizigo.
Kwa bahati mbaya, binadamu huwa tunavutia watu wanaofanana na sisi. Kwa mfano, unapokuwa na uso wenye tabasamu, ni rahisi watu unaokutana nao kukuonesha tabasamu. Unapokasirika, unawafanya wanaokuzunguka wakasirike pia. Ndivyo ilivyo hata kwenye mambo mengine. Unapoonekana huna mwelekeo, utawavutia watu wasio na mwelekeo. Ukiwa mzigo, utavutia mizigo mingine. Wale unaotamani wakusaidie, watakukimbia.
Ukitaka kuaminiwa na watu wa muhimu wanaokuzidi, unahitaji kuanza kuwa tofauti kwa lugha na matendo yako. Kwanza, onekana kama mtu wa maana kwa mavazi, lugha yako, na mwenendo wako. Ni habati mbaya binadamu tunapokutana na watu wapya, tuna tabia ya kukadiria thamani zao kwa kutumia vigezo vinavyoonekana. Hakikisha unaonekana mtu nadhimu, timamu, anayeaminika.
Pili, jitahidi uwe na kitu unachoweza kuwapa watu badala ya
kusubiri ufanyiwe. Kwa mfano, unapoongea na watu wa muhimu, wape nafasi
wakuambie mambo yao zaidi kuliko unavyowaeleza mambo yako. Watu wenye hadhi ya
juu wanapenda kufahamika kwamba wanaheshimika. Wape nafasi hiyo.
Kadhalika, usiwe na haraka ya kutaka misaada. Kila inapowezekana,
onesha namna unavyoweza kutumia kile ulichonacho kuwa jibu la matatizo ya watu.
Thamani yako ni vile vitu unavyoweza kuwapa watu. Uwezo
ulionao wa kutatua matatizo yanayowakabili watu wanaokuzunguka. Thamani yako ni
ujuzi ulionao, maarifa na busara ambayo watu wengine wanaweza kunufaika nayo.
Maoni
Chapisha Maoni