Malengo Yanavyoweza Kubadili Tabia ya Mtoto
Mwanangu wa miaka saba alikuwa na
tatizo la kupenda sana kununua vitu vitamu. Kila siku alikuwa ombaomba wa
chochote kinachomtosha kwenda dukani. Sikupenda tabia hii.
Mbali na kuharibu meno yake, kulikuwa
na tatizo la kutokujizuia. Ilifika mahali tunagombana kwa sababu tu hajapata
chochote kukidhi hamu yake ya kununua ‘ice cream’, ‘chocolate’ na vinavyofanana
na hivyo. Jitihada za kubadili tabia hii ya kupenda vitu visivyo na faida kwake
hazikuzaa matunda.
Nikaona nijaribu mbinu nyingine. Siku
moja jioni nikamrushia swali: ‘Ungekuwa
na hela zako mwenyewe ungetaka kufanya nini mwezi wa 12 mwakani?’ Swali gumu.
Aliomba ufafanuzi. Nikafafanua. Hatimaye akasema anachotaka. Nikaona ni lengo
dogo. Nilitaka awe na lengo kubwa la kufanyia kazi. Katika umri wake, fahari ya
kufikia malengo ni motisha tosha.
Nikamsaidia kuona zaidi: ‘Hivi unajua
unaweza kabisa kujilipia ada ya shule ukiamua?’ Ikaonekana naongea ‘mazingaombwe.’
Baada ya maswali yake kadhaa tukafikia muafaka kuwa inawezekana.
Nikaamua kupanua lengo lake: ‘Ungependa
kwenda wapi mwezi wa 12 wakati wa Chrismas ijayo?’ Macho yake yakachangamka kwa
furaha. Nilikuwa nimegusa jambo muhimu kwake.
‘Sasa nataka nikupe mtihani
utakaokuwezesha kufanya yote hayo kwa hela zako mwenyewe.’ Akasisimka.
Nikamweleza mpango ulivyo: ‘Tunataka kuwa na kiasi kitakachokutosha kulipa ada
yako, kwenda kufurahia Christmas kule ulikochagua na kununua mahitaji yako
uliyonitajia.’
‘Nitakuwa nakupa kazi za kufanya na
ukizikamilisha mwisho wa wiki nitakulipa.’ Naelewa hatari ya kutumia fedha kama
motisha kwa mtoto. Hata hivyo, lengo langu lilikuwa kumfanya ajione anawajibika
na kipato chake na wakati huo huo afikie malengo aliyojiwekea.
‘Hela utakazopata, utaziweka kwenye
kibubu. Kila wiki utaweka kiasi cha fedha kinachoonekana kwenye karatasi hii ya
mtihani.’ Nikamwonyesha katarasi iliyokuwa na utaratibu wa kuweka kiasi fulani
cha akiba kwa wiki. Kiasi hicho kinaongezeka mara mbili kila wiki inayofuata.
‘Ukishaweka fedha yako kwenye kibubu,
unatiki hapa.’ Nikamwonyesha kisanduku cha kutiki mbele ya tarakimu
zinazoainisha kiasi cha fedha atakachoweka kila wiki.
‘Una swali lolote?’ Maswali mengi.
Nikamwelewesha. Hatimaye akauliza swali la mwisho, ‘Tunaanza lini?’ Nikamwambia,
‘Utakapokuwa tayari aniambie tukatengeneze kibubu.’ Hapo nilikuwa napima uwezo wake
wa kufuatilia mambo ya msingi.
Kesho yake sikusikia akiongea suala la
kibubu. Wiki moja ikapita sisikii habari za kibubu. Nikapatwa na wasiwasi. Ikabidi
nimwuulize kulikoni.
‘Baba nilikuwa bado nafikiria utakuwa
unanipa kazi gani hizo mpaka unilipe?’ Nikaelewa hoja yake. Tukaliweka hilo
vizuri.
Kesho yake akanikumbusha kibubu.
Nikajua somo limeeleweka. Tukamwomba mama yake atutengenezee. Nikamkabidhi
karatasi inayomwongoza kiasi cha kutumbukiza kwenye kibubu. Nikamwomba aeleze
shughuli nzima itakavyokwenda. Nikagundua anaelewa. Kazi ikaanza.
Nilichokiona kimenifunza. Wiki ya 10
sasa mtoto haombi tena hela ya kwenda kununua ‘chocolate’ wala ‘ice cream.’ Kila anachokipata, anakitumia
kupunguza deni kwenye mtihani wake wa ‘kibubu.’ Inavyoonekana lengo lililokidhi
mahitaji yake limebadili tabia yake.
Kilichonifurahisha zaidi, sasa hivi
anaomba ‘kazi’ za kufanya ili apate fedha za kupunguza ‘deni’ lake la ‘kibubu.’
Uombaomba wa hela za kwenda kutumia, umepungua kwa asilimia kubwa. Binti yangu
anaonekana kuhakikisha lengo lake limetimia. Kama kuna jambo umejifunza, bado
hujachelewa. Kwa msaada wako, mwanao anaweza kusimamia malengo.
Maoni
Chapisha Maoni