Hatua Tano za Kuandaa Wasifu Utakaokupa Ajira
Moja wapo ya
sababu zinazochangia watu kukosa ajira wanazoomba ni uwezo mdogo wa kujenga
wasifu wao katika maandishi. Wasifu ni
maelezo binafsi yanayolenga kumshawishi afisa mwajiri kuwa unazo sifa za
kutosha kupata ajira unayoomba.
Vyuo vyetu,
kwa bahati mbaya, haviweki msisitizo katika ‘mambo madogo’ kama haya. Matokeo
yake watu wengi wazuri wenye ujuzi wanashindwa kuonekana kwa waajiri.
Katika makala
haya tunaangazia maeneo matano unayohitaji kuyazingatia unapojenga wasifu utakaoutumia
kuomba kazi.
Imarisha utambulisho wako
Maafisa waajiri makini wana tabia ya kwenda mbele ya kile kilichondikwa.
Lengo ni kukufahamu vizuri. Swali kuu unalohitaji kulijibu kwa ufasaha kupitia
wasifu wako ni, ‘Wewe ni nani hasa?’
Siku hizi teknolojia inawasaidia maafisa waajiri kukufahamu
kirahisi sana. Mbali na maelezo mazuri unayoyaweka kwenye wasifu wako, mwajiri
anaweza kukutafuta kwenye mitandao ya kijamii.
Kupitia taarifa unazoweka na kuzisambaza (share) kwenye kurasa
zako za mitandao ya kijamii, afisa mwajiri makini anaweza kuamua mtazamo na
uelewa wako ulivyo.
Maana yake ni kwamba yale unayoyafanya kwenye mitandao ya
kijamii ni sehemu ya uandishi endelevu wa wasifu wako wa kazi. Hakikisha
unapatikana mtandaoni na unaweka mambo yanayojenga utambulisho wako.
Lakini pia kuliko kuonekana wewe ni mpenzi wa masuala mepesi na mpiga
porojo zisizo na tija mitandaoni ni bora kutokupatikana kabisa mitandaoni.
Mbali na mitandao ya kijamii, mtandao wa inteneti inafanya iwe
rahisi kutuma maombi yako kupitia tovuti zinazosaidia kusambaza maombi ya kazi
kama LinkedIn.
Hata hivyo, iko hatari ya taarifa zako ulizowahi kuzituma
kwingine kupatikana kirahisi na yeyote anayetafuta taarifa zako mtandaoni. Hakikisha taarifa unazotuma mitandaoni hazijichanganyi. Hata
kama ni kweli kunaweza kuwa na tofauti ndogo ndogo, bado ni muhimu utambulisho
wako ubaki kuwa ule ule.
Eleza uzoefu ulionao
Kwa kawaida, afisa mwajiri hutafuta mtu mwenye uzoefu unaokidhi
nafasi ya kazi iliyotangazwa. Lazima ufanye kazi ya kumhakikishia kuwa wewe ni
mtu sahihi.
Kazi kubwa unayohitaji kuifanya ni kuhusianisha sifa
zilizotangazwa na mwajiri na uzoefu ulionao. Jiulize, ninakidhi vipi sifa
zinazohitajika? Je, uzoefu wangu unatosha kuomba kazi ninayoitafuta?
Inawezekana uzoefu ulionao hauendani moja kwa moja na ule
unaohitajika kwa kazi hiyo. Jambo la kukumbuka ni kwamba wakati mwingine,
unaweza kuwa na uzoefu unaoweza kuhamishika kwenda kwenye eneo jingine.
Kwa mfano, kama ulifanya kazi ya kujitolea kama mchambuzi wa
data (data analyst) na kazi unayoomba haijataja uzoefu huo, bado unayo fursa ya
kuhusisha uzoefu huu na mahitaji ya kazi unayoomba.
Kama unavyoona, kujitolea kunaweza kukusaidia kupata uzoefu hata
kama hujaajiriwa. Usiache kutafuta fursa ya kujitolea zikusaidie kupata ujuzi
bila ajira.
Onyesha ujuzi wako
Sambamba na uzoefu wa kazi, mwajiri makini anahitaji kuona una
ujuzi upi unaoweza kuwa na tija kwenye kazi atakayokupa. Ujuzi ni zaidi ya
maarifa. Mtu mwenye ujuzi hutumia maarifa yake kufanya kitu kinachoonekana.
Hakikisha wasifu wako unasimulia hadithi ya ujuzi ulionao.
Achana na porojo za kuorodhesha majukumu uliyowahi kuyafanya mahali fulani.
Mfano, ‘Katika nafasi hiyo kazi yangu ilikuwa kuandaa taarifa ya fedha kwa
kipindi cha kila robo mwaka.’ Maelezo kama haya ni mazuri lakini hayaonyeshi
ujuzi.
Kadri inavyowezekana, fikiria namna ulivyoweza kutumia vipaji,
uzoefu wako na ari ya kazi kuleta mabadiliko kupitia majukumu uliyowahi kupewa.
Mfano, kama ulikuwa afisa masoko kwa mwajiri wako aliyepita,
eleza ulivyofanikiwa kuongeza mauzo ya bidhaa. Mwajiri anapoona uwezo huu
kwako, anakuwa na shauku ya kukuita kwa usaili.
Jambo la kuzingatia ni kwamba maelezo yako ni lazima yaonyeshe
ushahidi kuwa una uwezo wa kupunguza matatizo na hivyo kuongeza tija kwa
mwajiri.
Fupisha maelezo yako
Muhimu kukumbuka kuwa afisa mwajiri hana muda wa kusoma maelezo
marefu yasiyo ya lazima. Wingi wa maombi yanayopitia mezani kwake hufanya
achoshwe na aya ndefu zenye maelezo mengi.
Lazima kujifunza namna ya kumvutia bila kumchosha. Ili hilo
liwezekane, jifunze kuchagua nini cha kusema na kipi uachane nacho na bado
ujumbe wako ubaki na nguvu ile ile.
Inashauriwa utumie sentensi fupi fupi zisizotengeneza aya ndefu.
Kama una maelezo ya ziada, tumia mtindo wa dondoo.
Pia hakuna kanuni ya upi ni urefu sahihi wa wasifu. Lakini kwa
mtu ambaye ndiye kwanza amemaliza chuo na anatafuta ajira yake ya kwanza,
kurasa mbili za karatasi ya A4 zinatosha.
Tengeneza mtandao wa ajira mapema
Vijana wengi hutumia muda mwingi kusoma lakini wanasahau
‘kujiongeza’ nje ya wigo wa darasa. Pamoja na kusoma, bado usisahau kazi kubwa
na muhimu ya kutengeneza mtandao mzuri wa watu wanaokuamini sasa na baadae.
Usitarajie kuwa kazi zitakufuata kirahisi rahisi. Wakati
mwingine waajiri hutafuta watu sahihi kupitia watu wanaowaamini. Unapokuwa na
watu wengi wanaoufahamu uwezo wako inakuwa rahisi kupata taarifa
zitakazokusaidia kupata kazi.
Mtaji wa kwanza wa watu ni makundi ya kijamii uliyonayo tayari.
Kuna wanadarasa wenzako, watu mnaoabudu mahali pamoja na hata timu za michezo.
Lakini pia, unahitaji kukutana na watu wapya kadri
inavyowezekana. Wasiliana na watu ambao tayari wanafanya kazi unayoitafuta.
Kama unatafuta kazi ya karani wa benki, kutana na makarani wa benki. Kama
unatafuta kazi ya uandishi wa habari, lazima kujenga mtandao wa watu ambao
tayari wanafanya kazi hiyo.
Jambo la kuzingatia
Unapowasiliana na watu hawa,
onyesha uwezo wako badala ya kuwa ombaomba wa misaada. Thamani itakayoonekana
kwako ndiyo itakayokuwekea mazingira ya kuaminika. Mtu anayekuamini
atakukumbuka anapokutana na habari za kazi unayoihitaji.
Asante sana Mr. Bwaya. Ni kweli fact hii niliwahi kuipata mahali. Sio kwamba ajira hazipo, na tuna wasomi wengi wa darasani, ila wengi tunashindwa kubadili knowledge kuwa skills. na matokeo yake unabaki usomi wa vyeti yaani cheti, stashahada, shahada na shahada za juu. Wengi wanakosa hata mbinu za kuonyesha kuwa ni kweli wanajua hasa kwenye mahojiano, na kukosa uzoefu.
JibuFutaNi madokezo mazuri sana!!
JibuFuta
FutaJinsi ya Kujifunza
Bila shaka, unaweza kunufaika kwa kujua kazi za mikono iwe unajifunza kazi hizo ili kujiruzuku au kutumia ustadi huo nyumbani. Unaweza kufunzwa kazi hizo shuleni. Au labda, unaweza kujifunza kazi hizo nyumbani. Jinsi gani? Kwa kufanya kazi za nyumbani. Dakt. Provenzano, aliyetajwa mapema, anaandika hivi: “Kazi za nyumbani huwafaidi hasa vijana kwa kuwapa ustadi muhimu sana ambao utawanufaisha watakapokuwa wakiishi mbali na wazazi.” Hivyo, uwe macho ili uone kazi zinazohitaji kufanywa. Je, kuna nyasi zinazohitaji kukatwa au kiti kinachohitaji kurekebishwa?
Badala ya kukushushia heshima, kufanya kazi za mikono kutakunufaisha sana. Usiepuke kazi za mikono! Badala yake, jitahidi “kuona mema” kwa ajili ya kazi yako ngumu, kwani Mhubiri 3:13 husema kwamba “hiyo ndiyo zawadi ya Mungu.”(jw.org/sw)