Kuuishi Wito Wako, Unahitaji Nidhamu ya Kujifunza



PICHA: findingmastery.net/


Nimekutana na vijana wengi wanaotaka niwaonyeshe njia ya mkato ya kufanya kazi za ndoto zao. Wanafikiri kupata kazi inayoendana na vipaji na tabia zao ni jambo la siku moja.

Ingawa huwa ninawasaidia kujiuliza maswali ya msingi yanayowachochea kugundua hazina iliyolala ndani yao, bado husisitiza umuhimu wa kuwa na mtazamo mrefu wa kuona yasiyoonekana kwa macho.

Nitatumia mfano wa Robert Green, mwandishi nimpendaye aliyeandika vitabu maarufu vya ‘The 48 Laws of Power, ‘Mastery’ na ‘The Art of Seduction.’

Ingawa tangu akiwa mdogo aligundua alitaka kuwa mwandishi, Robert hakuwa na uhakika anataka kuandika masuala gani.  Baada ya kumaliza chuo, Robert alianza kufanya kazi kama mwandishi wa habari.

Kazi hiyo, hata hivyo, haikumwendea vizuri. Mhariri wake alimshauri, ‘Tafuta kazi nyingine ya kufanya. Wewe si mwandishi. Hujui kupangilia mawazo yakaeleweka. Nakushauri ukatafute maisha mengine.”

Robert anasema alijisikia vibaya kwa sababu uandishi ndicho kitu ambacho alikiota kukifanya tangu akiwa mdogo. Maumivu ya kusikia hawezi kufanya kitu alichokipenda yalimfanya aanze kuranda randa kutoka kazi moja kwenda nyingine ili maisha yaende.

Katika kazi nyingi alizowahi kuzifanya, ni pamoja na kuwa fundi ujenzi, mhudumu wa hoteli, mwongozaji wa watalii, alifundisha Kiingereza na baadae akawa mwandaaji wa vipindi vya televisheni, Brixton.

Wakati wote huo akihangaika na maisha, Robert Green anasema, aliendelea kuandika kama burudani. Mbali na kuandika makala nyingi ambazo hata hivyo aliishia kuzichana kwa sababu hakuna gazeti lilizikubali, Robert aliandika miswada kadhaa ya vitabu.   

Baadae,  anasema, ilibidi aende Los Angeles ambako ndiko alikozaliwa na kuanza kufanya kazi kwenye shirika la upelelezi. Kisha, Robert alifanya kazi kama msaidizi wa mwaandaji wa filamu, kazi ambayo ilimfanya awe mtafiti, mtunzi na mwandishi wa filamu. Robert anasema alifanya kazi za hapa na pale zaidi ya 50.

Mwaka 1995 akiwa na miaka 36, wazazi wake walianza kuwa na wasiwasi na maisha yake. Alionekana kama kijana asiyejitambua, anayemanga manga kutoka sehemu moja kwenye nyingine. Lakini kwa maelezo yake mwenyewe, Robert anasema, ingawa wakati mwingine alijisikia kuwa na wasiwasi, lakini hakuwahi kujiona kama mtu aliyepotea.

Robert alitumia muda wote huo kujifunza mambo mapya. Aliendelea kuandika bila kuchoka. Hapa tunajifunza kuwa ukiwa na kitu ndani yako, usikipuuze kwa sababu tu unafanya kazi tofauti. Endelea kukichochea hata kama bado muda wake haujafika.

Mwaka huo huo, Robert akiwa Italia, kufanya kazi nyingine, alionana na bwana mmoja jina lake Joost Elffers, aliyekuwa mchapishaji wa vitabu. Katika mazungumzo yao, Joost alitokea kumwuuliza kama ana wazo lolote la kuandika kitabu.

Robert akakumbuka vitabu vingi vya historia alivyovisoma. Fikra zake zikatuma kwenye hulka ya watu kupenda kuwa na ‘mamlaka’ juu ya wengine. Hulka hii ya watu kupenda ‘kuwatawala’ wengine huwafanya wacheze na akili zao ingawa kwa juu juu wanaonekana watakatifu wanaotaka kuwaokoa wananchi.

Kwa hiyo, Robert akamwambia Joost kuwa kama angepata nafasi basi angeandika kuhusu ‘mamlaka.’ Joost  akashawishika na wazo hilo. Kwa kuwa alikuwa na uzoefu na uchapishaji, Joost aliamua kumpa Robert Green msaada aliouhitaji ili aweze kuandika kitabu hicho.

Robert anasema hapo ndipo uzoefu wake wa kazi zaidi ya 50 alizowahi kuzifanya ulianza kuleta matunda yanayoonekana. Kila kazi aliyowahi kuifanya, ilimsaidia kwa namna fulani kuelewa karibu kila namna za michezo ya kisaikolojia inayofanywa na watu wanaotaka kuwa na ‘nguvu’ katika jamii.

Tunachojifunza hapa ni kwamba, ukiweza kuwa makini, chochote unachokifanya leo kinaweza kuwa na msaada baadae. Jambo hili pia linajitokeza kwenye masimulizi ya Dk Ben Carson aliyeandika kitabu cha ‘The Gifted Hands.’

Ukweli ni kwamba binadamu tunapenda kuyatazama mambo kwa macho haya yanayoonekana. Tunapotazama maisha ya watu waliofanikiwa tunafikiri wamefikia hapo walipofika kibahati.

Wakati mwingine tunafikiri tukikutana na watu kama Joost basi maisha yetu yatabadilika. Tunafikiri mafanikio yanategemea sana aina ya watu tunaokutana nao na pengine ufadhili wa kifedha tunaoweza kuupata.

Tusichokijua ni kwamba mabadiliko yanayoweza kuwa kichocheo cha kuuelewa wito wa maisha yetu yana tabia ya kuanzia ndani yetu na hayaonekani kwa macho.

Tunachokihitaji, anashauri Robert Green, ni kujiandaa hatua kwa hatua kwa kukusanya maarifa na ujuzi, kubadili tabia zetu na kujenga uvumilivu hata pale wanapotokea watu wanaotukosoa. Maandalizi haya mara nyingi huwa hayaonekani kwa nje.

Mabadiliko yanayoonekana kwa nje, mara nyingi, ni matokeo ya jitihada za muda mrefu kujiandaa na mafanikio yanayoonekana baadae. Hili ni somo muhimu kwako mzazi au kijana unayesoma mambo ambayo pengine huoni faida yake kwa sasa.

Bahati mbaya jamii yetu haithamini mabadiliko haya yanayoanzia ndani yetu. Tunatafuta njia za mkato ili tubadilike kuanzia nje. Tunajaribu kuiga kwa watu tunaofikiri wamefanikiwa, tunatafuta ushauri kwao, na matokeo yake tunashindwa kufanyia kazi vile vitu ambavyo Mwenyezi Mungu ameviweka ndani yetu.

Hali hii, wakati mwingine hutufanya tuwe watu wa kukata tamaa pale tunapoona wenzetu wanafanya vizuri. Kumbe jibu la mafanikio yetu ni kufanya kinyume.

Badala ya kutarajia mabadiliko ya haraka yanayoanzia nje, tunahitaji kujifunza kujikusanya kidogo kidogo. Hatua hizi ndogo za mabadiliko kuelekea mahali sahihi ni msingi wa mafanikio ya watu wengi waliofanikiwa. Maana yake ni kwamba kila tunachojifunza hata kama hatukipendi, kina maana kubwa katika maisha yetu.

Inawezekana unasoma hapa kwa sababu kile unachokisoma hakifanani na yale unayotamani kuyasoma. Huenda unafanya kazi isiyokidhi matarajio yako. Jifunze kwa Robert Green.

Kwanza, kuwa na uhakika unataka nini bila kujali hali halisi hairuhusu. Jambo la pili, elekeza nguvu kupata uzoefu kupitia hicho unachokifanya. Kuwa tayari kujifunza kwa bidii kama sehemu ya maandalizi yako kuyafikia mafanikio yako.

Makala haya yalichapishwa kwenye safu yetu ya ELIMU NA MALEZI ya Jarida la MAARIFA linaloandaliwa na Gazeti la Mwananchi.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?