Unataka Kumjua Rafiki Atakayekusaliti? Soma hapa


PICHA: Recycle Coach


Katika nyakati kama hizi za Pasaka, mara nyingi, tunasikia marehemu Yuda Iskariote akijadiliwa kama jitu ovu lisilo na maadili lililokuwa tayari kumsaliti Bwana wetu Yesu Kristo.

Binafsi naamini, pamoja na ubaya wake, usaliti wa Yuda ulikuwa muhimu katika kuwezesha mpango wa Mungu kwa wokovu wetu. Wakati mwingine Mungu hutumia mabaya kuwezesha mazuri.

Hata hivyo, kwa maoni yangu, Yuda hakuwa na nia mbaya kivile. Kwanza, alikaa na Yesu kwa muda wa kutosha na hivyo alifahamu Yesu hakuwa mtu wa hivi hivi anayeweza kuchezewa kienyeji.

Yesu alifanya miujiza mingi na Yuda alishuhudia. Yesu alitembea juu ya maji. Yesu alifufua wafu. Si mara moja. Tena kuna wakati Yesu alimfufua mtu aliyekuwa kazikwa siku tatu. Unamkumbuka Lazaro. Aidha, kuna nyakati washikadini na wanafiki walitaka kumshughulikia Yesu, wakashindwa kwa sababu Yesu aliwaponyoka. Yuda aliyafahamu yote haya.

Kama baadhi yetu tunavyofanya leo, Yuda aliutazama uwezo huu wa Yesu kama fursa ya ‘kutoka.’ Akili ya kiujasiriamali ilimtuma kuona angeweza kutumia chuki ya Mafarisayo kwa Yesu kama fursa. Hii inasadifu ushauri wa watoto wa mjini, ‘Kuwa na macho ya kuiona Fursa. Kamata fursa kwa mbele!’ Kosa kubwa la Yuda.

Ubinafsi na tamaa vilimfanya Yuda aamini angekula fedha za maadui wa Yesu na hakuna kitu wangemfanya. Yesu mwenye uwezo aliokuwa anaujua Yuda, asingeuawa kienyeji vile. Lazima angechomoka na bado yeye angekuwa ‘keshatoka kiuchumi.’

Kinyume na matarajio yake, mambo yakawa kinyume. Yuda akashangaa Yesu kakamatwa kweli. Hakuwaponyoka wabaya wake. Yesu akasomewa mashitaka, hukumu ikatoka, safari ya kwenda Goligotha ikaiva. Yuda hakuamini kile alichokiona. Hatia ikaanza kumtafuna. Sasa akajiona msaliti kweli.

Kama binadamu wengine wema, Yuda akajaribu kutafuta namna ya kujinasua. Ikabidi arudi kwa wabaya wa Yesu Kristo arudishe ile rushwa. Pengine alifikiri akirudisha alichopokea, damu ya mwana wa Adamu isingekuwa juu yake. Ingempunguzia hatia.

Jamaa wakamgomea. Mpango ukafeli kwa mara nyingine. Hata ungekuwa wewe, lazima ungepatwa na sonona. Mara nyingi unapojikuta kwenye mazingira kama haya, unajiona huna kingine unachoweza kufanya tena. Hatia ya kuhusika na mauaji ya mtu asiye na hatia, aibu ya kumsaliti mtu wake wa karibu, haikumpa uchaguzi mwingine zaidi ya kujimaliza.

Je, hujawahi kufanya kama Yuda? Mara ngapi umewatumia watu kwa manufaa yako mwenyewe? Mara ngapi umewatumia marafiki zako kukidhi mahitaji yako binafsi?

‘Jamaa ana hela yule. Ngoja nikamkope lakini sitamlipa. Hela zote zile? Wala hatapata hasara na vihela kidogo vile.’ Unamwona mwenzako kama fursa. Unaenda kumkopa anakusaidia, lakini unamtapeli. Huna tofauti na Yuda.

Mara ngapi unatumia uwezo fulani alionao mwenzako kumfanyia vituko? Unajua kabisa mume/mke/rafiki yako sio mtu mgomvi. Unatumia sifa hiyo njema kwa manufaa yako. Unafanya vituko kwa siri ukijiaminisha hatagundua na hivyo hataumia. Huna tofauti na Yuda –unawatumia watu kama mtaji wa kumaliza shida zako.

Kwa hiyo, hoja yangu ni kuwa tumezungukwa na watu wasio na tofauti sana na Yuda. Wapo kila mahali. Wengine ni wafanyakazi wenzetu, marafiki zetu, waumini wenzetu, majirani tunaoishi nao na wengine ni jamaa zetu wa karibu. Pengine ni muhimu kujua namna ya kuwabaini. Hapa napendekeza mbinu tano za kukusaidia.

Mosi, lazima kwanza ujifunze kuwa mwaminifu kwa watu. Huwezi kutarajia watu wengine wasikusaliti wakati wewe mwenyewe ni msaliti wa wengine. Unavuna upandacho. Heshimu makubaliano yako na watu. Ukisema nitafanya, hakikisha umefanya. Bila kujali hadhi ya mtu, ukaribu mlionao, jisikie kuwajibika kumlinda kama binadamu anayestahili heshima. Ukiifanya hii ikawa tabia, utajikusanyia watu wengi watakaokuwa upande wako.

Pili, usifurahie sana unapokuwa kimbilio la watu. Usichukulie kuhitajika kama ishara ya kupendwa. Chukua tahadhari. Kuna watu watakuja kwako sio kwa sababu wanakupenda sana kama unavyofikiri isipokuwa wameona fursa. Inaweza kuwa fedha, upendeleo, umaarufu, fursa na kadhalika. Ukiwa mtu wa kutoa na kusaidia sana  bila utaratibu si tu utategeneza utegemezi usio wa lazima, lakini pia utawavuta akina Yuda wengi watakaotumia ulichonacho kama fursa. 

Inapobidi kuwa jasiri na sema hapana. Ukweli kuna watu huomba vitu sio kwa sababu wanavihitaji sana ila basi tu kwa sababu wanajua unavyo. Hawa utawagundua kirahisi sana ukiwanyima kile walichokifuata –watavunja urafiki, watakusema,  watakusengenya, watageuka kuwa maadui.

Lakini pia, unaweza kupima uaminifu wa mtu kwa kumwaminisha kuwa unamwamini. Unaweza, kwa mfano, kumpa mtu unayempima taarifa inayoonekana ni siri yako lakini unajua haina madhara yoyote kwako.

Chukulia unataka kujua kama mfanyakazi mwenzako ni mwaminifu. Unaweza kumsimulia tatizo lisilo na ukweli wowote au basi lenye ukweli usio na madhara yoyote kwako. Kama mtu huyu si mwaminifu na ana tabia ya kusema sema, baada ya muda mfupi unaweza kukutana na habari hizo koridoni. 

Iko hivi: Mtu mwenye historia ya kusaliti kwa jambo lisilo na madhara anaweza kusaliti kwa jambo lenye madhara. Ni sawa na msichana 'anayetembea' na kijana anayemsaliti msichana mwingine. Msichana huyu anaweza kufurahia kuolewa na kijana huyu lakini ni suala la muda tu na yeye atakuwa muhanga wa usaliti.

Kadhalika, kadri inavyowezekana, jifunze kuonekana mtu wa kawaida. Ishi maisha ya chini kidogo na uhalisia wa mambo. Huna sababu ya kujionesha kuwa unavyo. Huna sababu ya kutangaza uwezo ulionao. Kwa kufanya hivyo, akina Yuda wengi hawataona fursa ya moja kwa moja kwako. Watakaokufuata wanaweza kuwa watu sahihi zaidi kwako.

Saa nyingine tengeneza mazingira ya kuonekana mhitaji. Ni kweli hatupendi kuonekana watu wenye shida. Hata hivyo, ukitaka kuwafahamu watu ulionao, kuwa jasiri, omba msaada. Wahenga walisema, akufaaye wakati wa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Mtu anayekukimbilia unapokuwa navyo, lakini anakukimbia vinapokosekana, huyo hana tofauti na marehemu Yuda.

Sambamba na manne hayo, ndugu yangu epuka kuwaamini watu kirahisi. Usitoe idhini ya watu kufahamu undani wako. Kikulacho ki nguoni mwako. Usisahau. Mara nyingi watu unaokaa nao, unaocheka nao, unaofuatana nao kila siku, ndio hao hao wanaweza kukugeuka na ukashangaa. 

Chukua tahadhari unapowashirikisha watu mambo yako ya muhimu. Chora mstari usiotakiwa kuvukwa na baadhi ya waungwana hata kama wanaweza kuonekana wana nia njema na wewe. 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?