Lugha ya Ubabe Hupunguza Ushawishi Wako
Niliwahi kusoma barua ya
mfanyakazi mmoja kwa bosi wake. Ingawa alikuwa na madai ya msingi aliyoyaelekeza
kwa mkuu wake huyo wa kazi, kwa maoni yangu, alikuwa ametumia lugha isiyo na
staha. Kwa kufikiri kuwa maneno aliyokuwa ameyatumia yangepunguza ushawishi
wake, nilimshauri angebadili lugha kuifanya iwe rafiki zaidi. Hata hivyo, hakukubaliana
na maoni yangu. Miezi michache baadae, barua ile ilimgharimu kazi.
Wengi wetu huchukulia kirahisi
suala la lugha. Tunafikiri kwa sababu tunazo hoja na tunafahamu kile tunachokitetea
ndio ukweli wenyewe, basi tuna hiyari ya kutumia lugha yoyote. Hatujali
kuchagua maneno ya kusema. Tunasahau kuwa maneno yetu yana athari kubwa katika
mawasiliano kama ilivyotokea kwa mfanyakazi yule.
Lakini ukweli wa mambo ni kuwa
lugha, mbali na ujumbe, hubeba hisia. Kuna maneno ukimwambia mtu hata kama una
hoja hatakuelewa. Nakumbuka siku moja nilimsikia mkubwa wa ofisi mmoja akitoa
maelekezo kwa watu waliokuwa chini yake. Nilishangaa. Mkubwa yule, pengine
shauri ya mamlaka yake, aliongea kama mtu anayezungumza na watoto wadogo ambao,
hata hivyo, nao wanastahili heshima. Nilifikiri ilikuwaje mtu anaweza kuwakosea
adabu watu anaotarajia ndio watekeleze maagizo yake.
Kwa upande mwingine
nilimwelewa. Mkubwa huyu, kama wengi wetu, aliamini ubabe una nasaba na
ushawishi. Kwamba ili watu watambue madaraka yake, ilikuwa ni lazima kwake
kuwafokea na kuwatisha. Inaelekea kwa uelewa wake, aliamini vitisho na kelele
vingesaidia kuongeza ushawishi wake. Alichosahau, mkubwa huyu, ni kwamba lugha
ya ubabe hupunguza ushawishi.
Pengine unajiuliza ushawishi
maana yake ni nini? Ushawishi ni uwezo wa kumfanya mtu mwingine, kwa hiyari
yake mwenyewe, akubaliane na mtazamo wako. Maana yake ni kwamba unapofanikiwa
kubadilisha mawazo ya mtu mwingine bila kumlazimisha hapo unakuwa umeweza
kumshawishi.
Katika jamii yetu, mambo kadhaa
yanaweza kuongeza ushawishi wa mtu. Mosi, maarifa. Mtu anayeaminika kuwa na
taarifa sahihi –au ujuzi na uzoefu wa jambo fulani, anakuwa na uwezekano mkubwa
zaidi wa kuwa na ushawishi zaidi kuliko mtu asiye na maarifa. Mwalimu wa shule,
kwa mfano, ana uwezekano mkubwa wa kuwa na ushawishi kwa wanafunzi wake kuliko
mwanafunzi kwa mwalimu wake. Kinachompa mwalimu nguvu ya kubadili mawazo ya
mwanafunzi wake ni yale maarifa aliyonayo.
Lakini pia, hadhi ya mtu katika
taasisi au jamii. Mtu mwenye nafasi au madaraka katika taasisi, kwa mfano, ana
uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na ushawishi kuliko mtu wa hadhi ya chini. Tunafahamu, kwa mfano, kiongozi wa taasisi
huwa na uwezo mkubwa wa kubadili mitazamo ya wafanyakazi wake kwa sababu tu ya
nafasi aliyonayo. Sambamba na madaraka, hadhi ya mtu pia inaweza kujengwa na uwezo
wa kifedha. Sauti ya tajiri, mathalani, husisika zaidi kuliko sauti ya mtu
asiye na kitu.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa
mtu mwenye nafasi ya kuwa na ushawishi kwa watu akajikuta akikosa ushawishi. Sababu
moja kubwa inaweza kuwa uwezo mdogo wa kuwasiliana vyema na watu. Kama
nilivyotangulia kusema, lugha ina nguvu ya kugusa hisia za mtu. Lugha inayobeba
ujumbe wako ni lazima iguse hisia za mtu. Huwezi kumshawishi mtu anayejisikia
kuonewa na kudhalilishwa hata kama ni kweli unachoongea kina hoja ya msingi.
Jamii yetu, kwa bahati mbaya, imetuaminisha
ubabe na kiburi ndiyo silaha ya ushawishi. Tunafikiri tunapotumia lugha
inayoonesha mamlaka yetu, lugha ya majigambo na ubabe basi tutakuwa na ushawishi
zaidi kwa watu. Tunasahau kuwa majivuno, kiburi na ubabe, mara nyingi ni dalili
za magonjwa ya nafsi yanayohatarisha ushawishi wetu.
Na ilivyo ni kwamba watu
wababe, kisaikolojia, huwa ni watu wanyonge sana ndani yao. Ule udhaifu
wanaojisikia ndani yao, ombwe la nafsi ndani yao, huwafanya watafute namna ya
kuuficha. Maneno ya kujikweza, kejeli na
ubabe mara nyingi hulenga kufunika udhaifu wanaojisikia ndani yao.
Ndio kusema ikiwa tunataka
kuwashawishi watu, kwanza kabisa, tunahitaji kushughulika na udhaifu unaosumbua
nafsi zetu. Tunahitaji kupambana na ombwe la heshima tunalojisikia ndani yetu. Tukifanikiwa
hilo, itakuwa rahisi kutumia lugha ya unyenyekevu na uungwana kwa watu.
Lugha ya unyenyekevu ile inayotambua
nafasi na heshima za wengine. Lugha ya namna hii ndiyo inayoweza kugusa mioyo
yao na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa. Watu hawa wanaopoamini wamethaminiwa
wanakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kukupa nguvu ya kuwashawishi.
Maana yangu ni kwamba badala ya
kutumia lugha zinazowafanya watu tunaowashawishi wajione dhalili, tunahitaji
kujifunza namna ya kuwa wanyenyekevu kwa maneno yetu tukitambua kuwa ubabe
haujawahi kuongeza ushawishi wa mtu katika mioyo ya watu.
Maoni
Chapisha Maoni