Mambo Sita Mwanao Anayohitaji Kuyasikia
PICHA: houstonpress.com |
Watoto wadogo ni watu kamili wenye hisia kama sisi watu
wazima. Hata kama wakati mwingine hawawezi kusema wazi wazi, ukweli ni kwamba akili
zao ni kama dodoki linalonyonya kimya kimya yale wanayoona tukiyasema na kuyatenda.
Unaweza, kwa mfano, kusema jambo dogo kwa mtoto tena bila kumaanisha lakini jambo hilo likawa sumu itakayoharibu kabisa maisha ya mwanao. Unaweza kuwa na nia njema ya kumlazimisha kufanya kitu fulani sahihi kabisa, lakini kwa sababu hujaweza kuelewa na kujali hisia zake, jambo hilo likakosa nafasi kwenye moyo wa mtoto.
Unaweza, kwa mfano, kusema jambo dogo kwa mtoto tena bila kumaanisha lakini jambo hilo likawa sumu itakayoharibu kabisa maisha ya mwanao. Unaweza kuwa na nia njema ya kumlazimisha kufanya kitu fulani sahihi kabisa, lakini kwa sababu hujaweza kuelewa na kujali hisia zake, jambo hilo likakosa nafasi kwenye moyo wa mtoto.
Jukumu letu kama wazazi ni kuwasaidia watoto kujenga mtazamo sahihi wa maisha utakaowasaidia kuwa na mtazamo chanya na maisha, kujiamini na hata kuwa na nguvu ya kufanya mambo makubwa katika maisha kadri wanavyokuwa.
Katika makala haya, nimechagua mambo sita ninayoamini mtoto akiyasikia kwa mzazi wake anajenga mtazamo chanya na maisha yake.
‘Ninakupenda’
Unaweza kumpa mtoto vitu vingi, lakini
kamwe huwezi kumpa mtoto upendo utakamzidi. Unapokuwa na tabia ya kumwambia
mwanao mara kwa mara kuwa unampenda unamfanya ajione anathaminika. Kuthaminika
ni hitaji la msingi la kila mwanadamu.
Mwambie mtoto mara kwa mara kwamba
unampenda. Mtoto akishaamini wewe mzazi wake unampenda atakuwa mtu mwenye
ujasiri na furaha. Moyo wake utachangamka na atakuwa na utulivu. Bila kuwa na
uhakika na upendo wako wewe mzazi wake, mtoto hukosa utulivu wa nafsi. Moyo
wake utakuwa na ombwe. Hatajiamini.
Achana na yale mawazo kuwa ukimpenda
sana mtoto unamdekeza. Unaweza kumpenda mtoto na bado ukawa na msimamo
kuhakikisha anafanya kile anachotakiwa kukifanya.
‘Wewe ni fahari yangu’
Watoto, kwa kawaida, wanapenda kuwa na
uhakika kuwa wao ni watu wa maana. Ndio maana mara nyingi wanafanya vitu kwa
lengo la kusifiwa na wazazi wao. Huo sio udhaifu bali hitaji la msingi la
nafsi. Mtoto anayeamini wazazi wake wanajisikia fahari na yeye mara nyingi
anakuwa na mtazamo chanya na nafsi yake. Moyo wake unashiba na tabia zake
zinatulia.
Hata kama hukubaliani na mengi
wanayoyafanya, wajibu wako ni kuonesha unatambua juhudi wanazozifanya kufikia
malengo fulani. Usiwe na matarajio makubwa mno kiasi kwamba mtoto anajikuta
muda wote yuko kwenye shinikizo.
Kama ni kwenye masomo, usisubiri awe wa
kwanza ili umtambue. Mpongeze kwa kila hatua anayopiga kwenye uelekeo sahihi.
Kama ni tabia fulani, usisubiri awe mkamilifu ili umtambue. Tambua kila
badiliko dogo jema analolionesha.
‘Nisamehe
nimekosea’
Wakati mwingine sisi kama wazazi
hatupendi kuonekana huwa tunakosea. Ingawa tunapenda watoto wajifunze kuomba
msamaha pale wanapokesea, hatuwi tayari kuwa mfano wa kukiri makosa na kuomba
msamaha.
Mtoto anahitaji kusikia ukikiri makosa
yako. Hupotezi mamlaka yako kwa kumwambia mtoto kweli umekosea. Unapokubali
kuwa umekosea, unapanda mbegu njema ya kuomba msamaha. Ukimwambia mwanao
nisamehe, unamwonesha kuwa na wewe ni binadamu unayeweza kukosea na atakuamini
zaidi.
Sambamba na kumwomba msamaha, unahitaji
kujenga tabia ya kumsamehe. Mtoto anapokukosea, onesha mfano wa kuachilia. Kosa
lisiwe sababu ya kuvunja uhusiano wako na mwanao.
‘Ninakusikiliza’
Binadamu tunapenda kusikilizwa.
Unapoongea na mtu asiye na tabia ya kukusikiliza unajisikia vibaya. Unajiona
huna thamani kwake. Hali hii inapoendelea kwa muda mrefu, inaweza kufanya ukawa
na wasiwasi na vile ulivyo. Unaanza kujidharau.
Ndivyo ilivyo hata kwa watoto wetu.
Pamoja na udogo wao, wanapenda sana kujua kuwa wanasikilizwa. Kumsikiliza mtoto
kunagusa moyo wake kwa sababu anajisikia unajali na kumheshimu kama binadamu timamu.
Kusikiliza maana yake ni kumpa muda na masikio
yako na kumpa usikivu. Pia kumsikiliza mtoto ni pamoja na kuvumilia mawazo yake.
Badala ya kutoa maelekezo ya nini afanye muda wote, unaweza kumpa nafasi ya
kusema mawazo yake hata kama unadhani hayana mantiki.
Ikiwa kuna haja ya kumrekebisha na
kumwelekeza, fanya hivyo kwa upendo baada ya kuwa umemsikiliza. Mtoto
anayelelewa kwenye mazingira kama haya hujenga tabia ya kuwa mkweli, kujiamini
na kufanya maamuzi.
‘Unawajibika’
Umewahi kukutana na watu wanaopenda
kubebesha wengine lawama hata kwa makosa yao wenyewe? Wapo pia wavivu lakini
wenye tabia ya kuwalalamikia na kuwakosoa wale wanaojaribu kufanya kitu. Watu
hawa hawajajifunza kuwajibika.
Mtu mwajibikaji, kwa kawaida, anajua
kile anachotakiwa kukifanya. Unapokuwa mwajibikaji hutegemei watu wengine
wafanye badala yako; hutafuti mtu wa kumlaumu mambo yanapokwenda mrama; huogopi
kufanya maamuzi na kuwajibikia maamuzi yako.
Mfundishe mtoto uwajibikaji kwa kujenga
tabia ya kuongozwa na malengo anapofanya majukumu uliyompa. Pale anaposhindwa
kufikia malengo, au hata pale anapokosea, mwajibishe na aone matokeo ya kutokufikia
malengo aliyonayo.
Pia, mpe mtoto fursa ya kufanya maamuzi
yanayomhusu. Usimfanye awe mtu anayesubiri kuambiwa nini cha kufanya kila
wakati. Pale anapohitaji mawazo, msaidie bila kummnyang’anya uhuru wake.
‘Ukiwa
na bidii utafanikiwa’
Nimeshakutana na watu wengi wanaoamini
mafanikio huja kwa muujiza. Wanafikiri kufanikiwa ni bahati na ‘kismati’ hivyo
ili ufanikiwe lazima uombewe au basi upate msaada wa ‘nguvu za giza.’ Mawazo
kama haya yamefanya watu wengi watumie muda mwingi kudanganyika kuliko kufanya
kazi.
Nimefuatilia maisha ya watu wengi
waliofanikiwa. Jambo moja liko wazi. Wanafanya kazi kwa bidii na kujituma.
Hawasubiri kusaidiwa, hawasubiri muujiza utokee. Muujiza wanaoujua wao ni
kujifunza mambo mapya na kuchukua hatua.
Tunahitaji kuingiza mawazo haya kwa
watoto wetu. Hakuna mafanikio yanayopatikana kwa njia za mkato. Mtoto ajue bila
kufanya kazi kwa juhudi na maarifa hawezi kufanikiwa.
Kadhalika, ni vyema mtoto ajue kuwa
Mungu amempa kila anachokihitaji kupata mafanikio kulingana na uwezo wake.
Kilicho muhimu na cha maana ni yeye kuelewa ulipo uwezo wake na aufanyie kazi. Mtoto
akiwa na nidhamu ya maisha itakuwa rahisi kwake kupata mafanikio anayoyahitaji
sasa na baadae.
Maoni
Chapisha Maoni