Tunatofautiana sana...

PICHA: Verastic


Mwanamke, kwa asili yake, anajisikia vizuri kusema matatizo yake kwa mtu wake wa karibu anayemwamini –kama, mathalani, mume wake. Ile tu kujua kuna mwanaume yuko tayari kusikia yanayousibu moyo wake kunamfanya ajisikie salama.


Kutegemeana na aina ya tatizo, mara nyingi, mwanamke anaweza kusema jambo kwa lengo tu la 'kupumua.' Hahitaji kupata 'technical lecture' ya namna tatizo lake linavyoweza kutatuliwa. Hata pale anapohitaji ufumbuzi, nia yake si kukusumbua wewe mwanaume –bali kukuambia kuwa wewe ndiye mtu anayekuamini zaidi. [Kama wewe ni mwanaume mwenzangu, nina hakika unahitaji kusoma sentensi hiyo tena].

Bahati mbaya, mwanaume, kwa hulka yake, hapendi kusikia matatizo hasa yale anayojua hana majibu yake. Ndio maana unapoanza tu kueleza matatizo anaweza kurukia kutoa majibu ya haraka hata kama kiukweli hana majibu sahihi. Mwanaume hufanya hivyo kwa nia njema kabisa ya kulinda heshima yake kwa sababu kwake, kushindwa kutatua matatizo ni dalili za udhaifu.


Hapo ndipo tunapotofautiana kijinsia. Mwanamke anakwambia matatizo yake kwa sababu anakuamini. Usichukulie matatizo yake kama kero. Msikilize. Unapomsikiliza unamhakikishia kuwa yuko kwenye mikono salama ya mtu anayejali, anayesikiliza, anayeguswa na mambo yake. Sijui kama kuna heshima kubwa inayozidi hiyo.


Kwa upande mwingine, wanawake na nyie eleweni akili za wanaume. Kwa mwanaume matatizo yasiyo na ufumbuzi ni sawa na 'uchochezi' unaolenga 'kuendesha mapinduzi' ya mamlaka yake. Unapomweleza mume wako jambo linalohitaji ufumbuzi chukua tahadhari. Kwanza, elewa akili yake haipendi kusikia matatizo hasa yale ambayo anajua fika hawezi kuyatatua. Ndio maana ukimwambia shida mwanaume na ikawa ndani ya uwezo wake, hawezi kujizungusha kama kweli anakupenda. 

Pili, epuka kueleza matatizo mengi mfululizo hasa kama unajua hayuko kwenye nafasi nzuri ya kuyapatia ufumbuzi kwa wakati mmoja. Jaribu kuwasilisha tatizo moja lipate ufumbuzi, kisha leta jingine. Unapoongea mambo mengi kwa wakati moja na yote yanahitaji ufumbuzi, akili ya mwanaume inatafsiri kama unampigia 'kelele.' Si wanaume wengi wana uwezo wa kuvumilia 'makelele.' Ndio maana wengi wao huona ni afadhali washinde baa wakifarijiana kuliko kwenda nyumbani 'kupigiwa kelele.' Kelele zenyewe ni hiyo orodha yako ya matatizo anayotakiwa kuipatia ufumbuzi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3