Mbinu Nne za Kugundua na Kukuza Kazi ya Wito Wako






Umewahi kujisikia unafanya kazi isiyokupa utoshelevu? Unaweza kuwa na kiwango kikubwa cha elimu, kazi nzuri yenye heshima na mshahara mkubwa lakini unajikuta hufurahii kile unachokifanya.


Ingawa moja ya sababu inaweza kuwa uongozi na mazingira mabaya ya kazi, hata hivyo, mara nyingi, tatizo huanzia ndani yetu –kufanya kazi isiyoakisi wito wetu.

Mifumo ya elimu hulenga kutuandaa kukidhi mahitaji ya nje matarajio ya jamii, soko la ajira na mengine yanayofanana na hayo –matokeo yake mifumo hiyo inatuchonga kuwa watu tusiokidhi miito tuliyozaliwa nazo.

Robert Green, mwandishi wa vitabu maarufu vya “Mastery” na “The 48  Laws of Power” anasema elimu ina nafasi kubwa ya kutupoteza. Kadri tunavyoelimishwa na watu waliotuzunguka ndivyo tunavyojikuta “tumekuwa wageni wa nafsi zetu wenyewe.”

Maoni ya wazazi, walimu, marafiki, matarajio ya jamii, mara nyingi, yanatupeleka mbali na wito.  Kwa hiyo, badala ya kuheshimu kile ninachokiita wito, tumefungwa kwenye matarajio ya watu wengine.

Robert Green anasema, “mafanikio yako hayawezi kupatikana nje yako. Unahitaji kujifunza kuangalia ndani yako, ujiunganishe na vile vitu ulivyowahi kuvipenda kabla kujakutana na washauri.” Msikilize Robert Green hapa [Kiingereza].

Ninapozungumza na watu, hasa vijana, ninagundua  watu wengi ni wageni wa nafsi zao kama anavyosema Robert Green. Kazi wanazofanya zimewapeleka mbali na wito wao –yaani hawatumii vipaji na uwezo unaokuza mbegu ambazo ambazo Mwenyezi Mungu ameziweka ndani yao.

Watu hawa, naweza kusema, wamevamia kazi zisizo za wito wao kwa sababu tu zina harufu ya kuwaharakishia mafanikio ya kifedha, umaarufu katika jamii, madaraka na mambo mengine yanayowajengea heshima katika jamii.

Katika makala haya, ninakuuliza maswali  manne ninayoamini yanaweza kukusaidia kurudi ndani yako na hivyo kubaini na kukuza wito wako kupitia kazi unayoifanya.

Kitu gani kinakugusa?

Kila mtu analo eneo la maisha linamvutia kulifuatilia kwa karibu. Kuna kitu ambacho ukikisikia kinazunguzwa mahali moyo wako unasisimka. Unapokuwa kwenye mazungumzo na watu wengine, masikio yako yanasikia kitu hicho hata kama watu wengine hawakisikii. Unanunua vitabu, unafuatilia televisheni na mitandao na karibu kila unachokifanya kinazunguka zaidi kwenye eneo hilo hilo.

Unapoendelea kusoma hapa tayari kuna kitu kinakujia kichwani. Inawezekana ni matatizo fulani ya watu, hitaji fulani unalofikiri jamii yetu inalo au ubunifu fulani unaoamini bado jamii haijauona.

Robert Green anasema, “Mambo yanayotugusa mara nyingi huwa hayabadiliki. Mtoto mdogo anajua kitu gani kinamgusa wakati mwingine vizuri zaidi kuliko mtu mzima. Usidharau mambo haya yanayokusisimua.”

Huenda unaguswa na masuala ya teknolojia; mfumo fulani wa maisha, imani au fikra katika jamii unazofikiri ungepewa nafasi ungezibadilisha. Chochote kile kinachogusa fikra zako, hicho ndicho kinachoweza kuwa wito wako. Ukifanya kazi zinazogusa eneo hilo unaweza kufanya vizuri zaidi.

Unajitambulisha na kitu gani?

Kwa kawaida, kuna vitu tukivifanya vikaleta matokeo fulani tunajisikia fahari. Kila mtu ana eneo lake akilifanya vizuri anajisikia kuridhika.  Kuna watu wanajisikia fahari wanapotetea haki za watu; wengine kufundisha; wengine uandishi; kubuni vitu vipya; kuongoza wengine; kushauri, kuendesha biashara, kutaja kwa uchache.

Kile kinachokuletea ufahari, mara nyingi, utapenda kujitambulisha nacho. Utatumia muda mwingi kukielewa kuliko unavyofanya kwenye maeneo mengine.

Nina rafiki yangu ambaye kila nikikutana naye lazima atazungumzia uharibifu wa mazingira. Dada huyu atazungumza kwa kirefu kwa nini anafikiri siasa za dunia zina athari kubwa kwa mazingira. Ukimsikiliza unaona wazi moyo wake uko kwenye mazingira. Hii ndiyo sifa ya wito wa mtu.

Jiulize, kitu gani ukikifanya vizuri unajisikia fahari? Je, watu wanakusifia na kukutambua kwa kitu gani? Ukiweza kuuoanisha uwezo huo na kazi unayoifanya itakuwa rahisi kupata mafanikio makubwa.

Unayatazamaje mafanikio?

Mafanikio ni dhana pana isiyo na jibu moja. Kila mtu ana namna yake ya kutafsiri kile kinachoitwa mafanikio. Wapo wanaochukulia mafanikio kama uwezo wa kujikusanyia mali. Hawa huridhika wanapokuwa wamefikia kiwango cha kujitosheleza na vitu vinavyowawezesha kuishi maisha mazuri.

Wengine mafanikio yao ni umaarufu. Vitu vinavyowafanya wajulikane ndivyo wanavyovichukulia kama mafanikio. Wengine wanakwenda mbali zaidi. Hawaridhiki na fedha wala umaarufu bali mamlaka. Wasipopata madaraka yanayowapa nguvu ya kuwatawala wengine, bado hawajisikii kufanikiwa.

Pamoja na hao, wapo pia wanaopima mafanikio yao kwa namna wanavyotatua matatizo ya watu wanaowazunguka. Hawa, hawaishii kuridhika na maisha mazuri bali kuona  maisha yao yanagusa watu wengine.

Tafsiri ya mafanikio uliyonayo, ni kiashiria kimojawapo cha wito ulionao katika maisha. Wito wako hutengeneza mtazamo fulani wa mafanikio. Ukiweza kuoanisha tafsiri uliyonayo ya mafanikio na kazi unayoifanya uwezekano ni mkubwa kuwa kufanya vizuri zaidi.

Maamuzi gani unayafurahia?

Kipimo cha juu cha wito ni aina ya maamuzi unayoyafanya. Kuna nyakati unaweza kufanya maamuzi ambayo si kila mtu anaweza kukuelewa lakini wewe mwenyewe ukawa na amani na kile unachokifanya.

Kuna kijana aliwahi kuacha kazi yenye kipato kikubwa ili akafanye kitu alichoamini kinabeba thamani yake. Aliacha kazi ambayo watu wengi wangetamani kuipata na akaenda kuanzisha biashara. Mtu wa namna hii kwa vyovyote anakuwa na wito wa ujasiriamali ndani yake. Ili wito huo ukamilike inakuwa ni lazima afanye maamuzi magumu.

Jiulize, umewahi kufanya maamuzi gani yaliyobadili mwelekeo wa maisha yako? Ikiwa kuna maamuzi unatamani kuyachukua ukiamini yatabadili maisha yako, huo inawezekana ndio wito wako.

Usiogope kufanya makosa

Robert Green anasema, “Watu wengi wanataka njia rahisi, iliyonyooka, isiyo na usumbufu kuwafikisha moja kwa moja kwenye nafasi na mafanikio wanayoyahitaji.”  

Mtazamo kama huu unaweza kukupoteza. Robert Green anashauri, “Usiogope kufanya makosa unapotafuta wito wako. Makosa yanakusaidia kujitambua. Unaweza kufanya kazi nyingi zisizokidhi wito wako lakini zikakusaidia kukusanya ujuzi na kukuza uzoefu wako. Kwa namna hii unakomaa kuuelekea wito wako.”

Maoni

  1. Makala nzuri ndugu Bwaya ninapoisoma leo Jumamosi ya pasaka nikiwa nimepumzika hapa nyumbani nikitafakari mambo machache ya kutujenga kimaisha. Nikweli kwamba asilimia kubwa ya watu tunafanya kazi zinazotokana na career za matarajio wa wazazi, ndugu au marafiki wa wazazi wetu. Umetoa mifano hai ya elimu na kazi tunazosomea. Hii inamfanya mtu kutokufurahia elimu na kazi anazozifanya. Mfano mzuri ni pale ambapo mtu anatumia muda mwingi kufanya shuhuli nyingine anazozifurahia kuliko kazi aliyoajiriwa. Hapa ajira inakuwa “less productive” especially pale ambapo mtu anaogopa kuachana na ajira na kufanya kile anachokifurahia. Na hii inatokana na mtazamo kuwa jamii itanifikiriaje endapo nikiacha kazi yangu ya Engineer na kuanza kuhubiri injili au kulima mbogamboga ? pia kufikiri kwamba kufanya jambo au kazi ya wito ni makosa. Hapo ndipo tunasema usiogope kufanya makosa jenga kipaji chako katika kazi ya wito wako.
    Nimejifunza jambo kubwa katika makala hii. Ahsante

    JibuFuta
  2. Asante sana Gilead kwa kupitia kibarazani na kuweka maoni murua. Natumai Australia mko poa.

    JibuFuta
  3. หนังออนไลน์ ระดับ Premium ได้ที่ Doonung1234 ฟรี ระดับ 4K HD หลากหลายเรื่องมากมาย กับเรื่อง Joker โจ๊กเกอร์ (2019) [ Final ]

    JibuFuta
  4. but for some Muslims, a return to the grand mosque, like the 500 years it has ever been, is their pride.
    ข่าว
    bet2you

    JibuFuta
  5. Yaah nafurahi sana kuona nakala nzuri sana ndugu bwaya

    JibuFuta
  6. Good and interesting

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia