Nafasi ya Mzazi Katika Kukuza Vipaji vya Watoto
Jioni moja, mwanzoni mwa miaka ya tisini, nikiwa darasa la tatu, mama alikuja nyumbani na barua aliyoniambia ilikuwa yangu. Barua hiyo fupi iliyoanza na maneno, ‘Mpendwa mwanangu Christian,’ ilikuwa ndani ya bahasha yenye barua ya mama kutoka kwa baba yangu, ambaye kwa wakati huo alikuwa masomoni.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza
kupata barua niliyoiita yangu. Kabla ya hapo, nilizoea kukaa pembeni mwa mama kumsikia
akinisomea sehemu ya barua yake iliyokuwa na salamu zangu kutoka kwa baba.
Jioni hiyo, bila kutegemea, nikajikuta napanda ngazi na ‘kumiliki’ barua. Sitasahau
nilivyojisikia vizuri. Niliisoma mara kadhaa bila kuchoka.
Kesho yake ilibidi
nimshawishi mama tujibu barua ya baba. Kipindi hicho hapakuwa na namna yoyote
ya mawasiliano isipokuwa kwa njia ya barua. Mama alikubali ombi langu la
kumwandikia baba barua. Ulikuwa ni uzoefu mwingine wa pekee. Nilimtaarifu mambo
mengi ya shule na nyumbani ambayo siwezi kuyakumbuka hivi leo. Huo ukawa ni
mwanzo wa tabia yangu ya kupenda kuandika.
Mazingira ya uandishi
Aliporudi baada ya
masomo, baba alikuwa na tabia ya kukaa mezani akiandika. Meza yake ilijaa madaftari
yaliyokuwa na maandishi mengi. Wakati mwingine alitusimulia yale aliyoyaandika
kwa lugha tunayoweza kuiielewa. Alikuwa akishiriki shindano la uandishi wa muswada
wa kitabu lililoandaliwa na Kituo cha Maandiko Habari Maalum.
Siwezi kukumbuka kitu
gani hasa kilifanya nami, katika umri ule, nipate wazo la kutunga na kuandika
hadithi yangu kwenye daftari dogo. Nafikiri, kama mtoto, niliiga kile nilichozoea
kukiona baba akikifanya nyumbani.
Nakumbuka siku moja
nikiwa nimejilaza sebuleni baada ya chakula cha jioni, nilimsikia baba
akiwasomea rafiki zake ile hadithi yangu. Nilijifanya nimelala na sisikii lakini
nikisikia kila kitu. Siwezi kusimulia nilivyojisikia fahari kuona watu wazima
wakisifia kazi yangu. Nilijifanya kukoroma lakini moyoni nilijaa kicheko cha
ufahari. Nilijisikia fahari kuona baba yangu anatambua kile nilichokuwa nakifanya kama
mwanae.
Bila kujua ilikuwaje,
nilianza kujitambulisha na kile ambacho baba alikifanya karibu kila siku. Baba
yangu ni mpenzi wa maandishi hata leo. Nyumbani kwetu alijaza nakala za
magazeti, majarida na vitabu. Pia, alikuwa na tabia ya kutunza kumbukumbu za
matukio kwenye maandishi. Kwa kuwa nilijipambanua na yale aliyoyafanya, nilianza
kuvutiwa na yale niliyoamini anayapenda. Naamini nilifanya nilichokiona
anakifanya kwa sababu ndicho nilichofikiri kinamfanya ajisikie fahari na mimi.
Kipaji kilichojificha?
Nikiwa sekondari,
maandishi yalikuwa sehemu ya muda wangu mwingi. Sikuchukulia kusoma vitabu kama
adhabu. Nilisoma kama sehemu ya burudani. Nakumbuka siku moja, mwalimu wa somo
la Kiswahili aliyeitwa Kitumbuizi alinishauri nikakuze kipaji changu kwa
kusomea lugha. Sikufikiri nilikuwa na kipaji alichokiona yeye. Marafiki na
wanafunzi wenzangu nao walifikiri ningefanya vizuri kama mwandishi.
Sikukubaliana nao.
Ingawa hatimaye
nilikwenda kidato cha tano kusoma Fizikia, Kemia na Baolojia, nilianzisha
gazeti la shule tulilolibandika kwenye ubao wa matangazo. Mule tuliripoti
matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea mabwenini na madarasani. Ilikuwa kama
sehemu ya burudani ya wanafunzi. Waandishi wenzangu, hivi sasa wengine ni
madaktari.
Sina hakika kama
nilizaliwa nikiwa na mapenzi na maandishi. Nafikiri kukulia kwenye mazingira
yenye harufu ya maandishi kuliumba uwezo fulani ndani yangu.
Nyumbani tulikuwa na
desturi ya kusikiliza hadithi za biblia kila siku jioni. Baba alitenga muda
mfupi kila siku kutusimulia matukio mbalimbali kama yanavyoelezwa kwenye
biblia. Wakati mwingine alitusomea hadithi mbalimbali kwenye vitabu. Kuna
uwezekano mkubwa kwamba mazingira ya namna hii yalichochea kipaji ambacho, hata
hivyo, sikufikiri ningekuwa nacho.
Kuchochea vipaji
Siwezi kukumbuka
nilianzaje kuchora. Sikujifunza kuchora. Uchoraji ulianza bila mimi kuelewa. Nikiwa
darasa la V, nilikuwa na uwezo wa kuchora sura inayomtambulisha mtu
anayefahamika. Niliwachora rafiki zangu, wazazi wangu, walimu wangu, wadogo
zangu pamoja na mimi mwenyewe.
Sijawahi kumwona ndugu
yangu mwingine akichora. Lakini nafahamu wazazi wangu walichochea kipaji hicho.
Baba alikuwa mwalimu wa Jiografia. Mara nyingi nilimwona akichora ramani. Pale
shuleni tulikokuwa tukiishi, alitengeneza ramani ya dunia ardhini kwa kutumia
saruji na mawe. Sehemu zenye bahari ziliwekwa maji, milima ilionekana vizuri na
maandishi yenye majina ya mabara na bahari yalionekana vizuri. Niliiga
alichokifanya shuleni kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi wake. Nilitengeneza
kitu kile kile nyumbani.
Wakati mwingine,
nakumbuka alikuja na tufe yenye ramani ya dunia nyumbani. Nilipata wazo la
kutengeneza kitu kama kile. Nilitumia kibuyu, nyaya, mbao na rangi kutengeneza ‘tufe
ya bandia.’ Sikumbuki nilikuwa darasa la ngapi.
Hiyo ni mifano ya namna
mazingira ya kimalezi yalivyochochea ubunifu na vipaji vilivyokuwa vimejificha
ndani yangu. Mzee hakuwa mchoyo wa pongezi. Wakati mwingi nilichora na kufanya
vitu kwa lengo la kumsisimua mtu niliyejua anajivunia kwa dhati nikifanyacho.
Hiyo, ninaamini, ndiyo hasa ilikuwa hamasa yangu.
Ingawa yeye hakuwa
mchoraji wa picha, aliniwekea mazingira ya kisaikolojia kunifanya nipende
kuchora. Kwanza, alitambua uwezo niliouonesha kupitia ‘michezo’ yangu ya kila
siku. Lakini pia, hakuchukulia ‘michezo’ hiyo kama upotevu wa muda ambao
ningeutumia kujisomea. Kumtia mtoto moyo kufanya kile anachopenda kukifanya kwa
hiyari, kunaibua na kukuza vipaji alivyonavyo.
Kipaji na mafanikio
Sikuweka mkazo kwenye
uandishi na uchoraji kwa sababu niliaminishwa mafanikio yangu yanategemea ufaulu
wa darasani. Nilifikiri kupata daraja la I na kusoma sayansi kungeniongezea
nafasi ya kushindana vizuri kwenye soko la ajira. Pamoja na kuyapata hayo, bado
niliendelea kujisikia kukosa kitu fulani nisichokifahamu.
Nikaanza kujifunza
kuheshimu vipawa vilivyoanza kuchipua tangu nikiwa na umri mdogo. Nikaanza
kuoanisha vipawa vyangu na elimu rasmi. Ingawa kila mtu amezaliwa na uwezo
fulani wa pekee ndani yake, si kila mtu anaujua vipawa vyake. Kipawa ni ule uwezo
wa kufanya kitu ambacho si watu wengi wanaweza kukifanya. Kuna watu, kwa mfano,
wana vipawa vya biashara. Ukiwapa fedha kidogo, wanajua namna ya kuzizungusha.
Wengine, wana vipaji vya ufundi. Hawajasoma sana, lakini wanaweza kutengeneza
vitu ambavyo sisi wengine hata tungefundishwa hatutaweza.
Kipaji, kwa kiasi
kikubwa, ndicho kinachoamua mafanikio ya mtu. Mtu asiyefahamu uwezo wa pekee unaoishi
ndani yake, anaweza kuchukua muda mrefu kufurahia kile anachokifanya.
Bahati mbaya, mfumo wetu
wa elimu hausaidii kujenga vipaji vya watu. Tunachukulia vipaji kama ‘shughuli’
za ziada zisizo na umuhimu. Kama wazazi, tunao wajibu mkubwa wa kuwasaidia
watoto kuibua vipaji vyao na kuvitumia.
umesema vizuri sana.
JibuFuta