Elimu Isinoe Ufahamu Pekee, Itufanye Tuwe Binadamu Timamu Wanaojitambua

PICHA: EDUCATION / BUNKIE


BILA shaka umewahi kukutana na mtu unayeamini ni msomi akifanya mambo usiyoyatarajia. Jambo hilo hilo lingefanywa na mtu asiyekwenda shule wala usingeshangaa. Lakini kwa kuwa anayefanya hivyo ni ‘msomi’  basi unakata tamaa na kuhoji, “Hivi huyu naye amesoma? Kama kusoma kwenyewe ndio huku, basi hakuna haja ya kusoma.”

Jamii ina matarajio makubwa na elimu. Kiwango cha elimu anachokuwa nacho mtu kinatujengea matarajio fulani kwake. Tabia ya mtu aliyesoma, kwa mfano, inatarajiwa kuwa bora zaidi ya mtu asiyesoma. Hapa tunazungumzia mambo madogo, lakini ya muhimu, kama vile heshima kwa watu, uwezo wa kuvumilia mawazo tofauti na namna anavyoweza kuwasilisha mawazo yake. Hivi ni baadhi ya viashiria vinavyotumiwa na jamii kupima ikiwa ni kweli mtu ameelimika.

Ingawa ni kweli ubora wa elimu ya mtu unaweza kupimwa kwa uwezo wake wa kuona na kutatua matatizo yanayoikabili jamii, mara nyingi jamii huangalia mambo ya kawaida yanayogusa utu wa watu. Watu wanataka kuona namna gani elimu imemjengea mtu tunu muhiu kama uadilifu, uaminifu, kusema kweli na unyenyekevu zinachukuliwa kwa uzito mkubwa wakati mwingine kuliko fani halisi.

Mtu aliyesoma na bado akawa tapeli, mlaghai, mwenye majigambo, mlevi, mzinzi, hufanya watu wawe na wasiwasi na elimu yake. Mara zote mtu anapoonesha tabia hizi, watu watajiuliza, “Elimu ina faida gani kama mtu anafanya mambo ya kijinga kama haya?” Kwa mukhtadha huu, mabadiliko ya maisha ni kipimo muhimu cha ubora wa elimu aliyoipata mtu.

Kadhalika, jamii inaamini mtu aliyesoma lazima aweze kumudu maisha yake. Usomi wake ni lazima uende sambamba na kuboresha mtindo wake wa maisha. Huwezi, kwa mfano, kusema umeelimika na bado ukabaki kuwa masikini. Katika macho ya jamii, umasikini ni kiashiria cha mtu aliyeshindwa kuelimika. Elimu inatarajiwa ikusaidie kutumia maarifa yako kujipatia/kujiongezea kipato.

Unapokuwa na elimu kubwa lakini huna uwezo wa kubadili changamoto zilizopo kwenye jamii kuwa fursa, watu wanakuwa na wasiwasi na wewe. Wakati mwingine, hali hiyo inafanya jamii iwabeze wasomi kwamba wamepoteza muda mwingi kujifunza mambo ambayo yameshindwa kuwasaidia kuboresha maisha yao wenyewe. Kwa mujibu wa jamii, kushindwa kumudu maisha yako kunaweza kuwa kiashiria cha elimu isiyokidhi haja.

Inawezekana mitazamo hii inawakilisha mtazamo hasi wa jamii dhidi ya elimu. Tunafahamu, kwa mfano, lipo wimbi la kujaribu kuifanya fedha iwe ndio kipimo cha heshima ya mtu. Lakini ni kweli pia kwamba wasomi wenyewe –kupitia namna wanavyoonekana kupitia mchango walionao kwa jamii –ndio  waliochangia kukuza mtazamo hasi uliopo kwa jamii dhidi ya elimu. Kwa kuwa matokeo ya elimu ni sharti yaiguse jamii, ni dhahiri jamii isipoguswa na matokeo hayo, maana yake ni kwamba wasomi wameshindwa kufanya wajibu wao.

Moja wapo ya sababu zinazofanya elimu ishindwe kuwa na manufaa kwa watu na jamii kwa ujumla, ni msisitizo wake kwenye eneo moja tu la taaluma. Tangu mwanafunzi anapoanza darasa la kwanza mpaka chuo kikuu anatarajiwa ‘kuelimika’ kwa kipimo cha kufaulu mitihani. Mzazi anategemea mtoto arudi nyumbani na cheti chenye alama za juu. Wakuu wa elimu wanapozungumzia kupandisha kiwango cha elimu, wanafikiria ufaulu wa mitihani.

Mtazamo huo wa kutukuza taaluma dhidi ya maeneo mengine ya kimaisha unashushwa kwa mwalimu ambaye naye anakuwa hana namna nyingi zaidi ya kufanya kazi ya ziada kufikia matarajio hayo kwa kuhakikisha mwanafunzi anafaulu kwa kiwango cha juu. Mtazamo huu finyu wa elimu, unasahau maeneo mengine muhimu ya maendeleo ya binadamu. Siha nyingine muhimu zinazokuza utu na utimamu wa binadamu kama vile nidhamu, maadili, bidii ya kazi, uaminifu, afya ya akili na mwili, stadi za maisha na ukuaji wa kiroho hazipewi nafasi inayostahili.

Mitalaa yetu inabaki kutushinikiza kuvielewa vitu na pengine kukuza uwezo wa kudadisi mambo kuliko kujielewa na kuwa binadamu timamu. Tunatumia muda mwingi kuyaelewa mambo yanayotuzunguka lakini tunasahau kumfanya ‘msomi’ huyu aingie ndani yake na kujitafakari yeye ni nani na nafasi yake ni ipi katika jamii. Matokeo ya mtazamo huu, ni kwamba wanafunzi wanakazana kupata alama A darasani lakini hawana nidhamu itakayowasaidia kufanikiwa kwenye maisha.

Ni vyema tukitambua kwamba ufaulu mzuri usiokwenda sambamba na kujengwa kitabia hauwezi kuwa na manufaa ya maana. Tunahitaji kuweka msisitizo katika kukuza maeneo yote muhimu kwa maendeleo ya mwanafunzi. Tujenge mfumo thabiti wa kuwalea vijana kimaadili na kiroho ili maarifa wanayoyapata yawasaidie kuwa binadamu wenye tija kwa jamii.


Sera zetu za elimu, kadhalika, zisiishie kuelimisha akili za vijana wetu na kuwaacha hawajitambui wao ni nani na nafasi yao katika jamii. Vinginevyo, elimu itabaki na kazi ya kumwandaa mtu atakayesubiri kuajiriwa ili apate fursa ya kutumia maarifa yake kuiba na kujiletea manufaa yake binafsi. 

Maoni

  1. Sir Christian Bwaya Tunaomba pia Mafunzo yako Uyahifadhi katika Fasihi Andishi (( kupitia Vitabu ))) Nakuelewa sana

    JibuFuta
  2. Sir Christian Bwaya Tunaomba pia Mafunzo yako Uyahifadhi katika Fasihi Andishi (( kupitia Vitabu ))) Nakuelewa sana

    JibuFuta
  3. Yaa nimepata kitu asante sana mwl

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Pay $900? I quit blogging

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Heri ya mwezi mpya!